ALLAH (S.W.) anastahiki kupewa nafasi ya kwanza na ya juu ya Utii wa mwanaadamu kwa sababu yeye ndiye Muumba na Mmiliki pekee wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo - vidogo na vikubwa na vinavyoonekana na visivyoonekana. Yeye ndiye Mfalme wa kweli mwenye uwezo juu ya kila kitu asiyehitajia msaidizi au mshirika yeyote katika kuuendesha ufalme wake. Ufafanuzi wa ufalme wake tunaupata katika Qur'an. Hebu tuzingatie aya zifuatazo:
Hakika Mola wenu ni Allah aliyeziumba mbingu na ardhi kwa nyakati sita. Kisha akatawalia juu ya arshi yake. Huufunika usiku kwa mchana ufuatiao upesi upesi; (na huufunika mchana kwa usiku ufuatiao upesi upesi). Na ameliumba jua, mwezi na nyota (Na vyote) vimetiishwa kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba (ni kwa Allah) na amri zote ni zake. Ametukuka kweli kweli Allah, Mfalme (Rabbi) wa walimwengu wote. 7:54) (Mwenyezi Mungu) ambaye ni wake (pekee) ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuzaa mtoto wala hana mshirika katika ufalme (wake) na ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo (chake)(25:2)
Allah (s.w.) amekiumba kila kitu kwa lengo na akakiwekea utaratibu (sharia) madhubutri utakaokiwezesha kuwepo, kubakia na kufikia lengo lake. Hivyo ili kiumbe chochote kibakie hakina hiari ya kutii sharia za Allah (s.w.) alizokiwekea. Hizi ni sharia za maumbile (natural laws) ambazo hata miili yetu inazitii bila hiari. Allah (s.w.) anatutanabahisha:
Je! wanataka dini isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu, na hali kila kilichomo mbinguni na ardhini kinamtii yeye kipende kisipende? Na kwake watarejeshwa wote.(3:83)
Aya hii inamtanabahisha mwanaadamu kuwa pamoja na kwamba amepewa uhuru na uwezo wa kujiamulia utaratibu wa maisha na kujiwekea sharia zitakazo muongoza katika kuendesha maisha yake ya kijamii, kwanini asitumie uhuru wake kwa busara kwa kuamua kufuata utaratibu au sharia za kuendesha maisha ya kijamii (social laws) alizoziweka Allah (s.w.) ambazo zinalandana na sharia za maumbile zinazofuatwa na kila kilichomo mbinguni na ardhini pamoja na mwili wake wenyewe. Je, mwanaadamu atakapo amua kujitiisha katika utaratubu wa maisha kinyume n aule aliomuwekea Muumba wake; Maisha ya upinzani wa kijinga yatamfikisha wapi mwanaadamu kama si katika matatizo ya kijamii ya kila namna na maangamivu? Mwanaadamu mwenye akili na busara ni yule anayemtii Muumba wake ipasavyo kwa kuitikia wito wake ufuatao:
Basi uelekeze uso wako katika dini iliyo sawa sawa - ndilo umbile Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu, (yaani dini hii ya Kiislamu inawafikiana bara bara na umbo la binaadamu). Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe vya Mwenyezi Mungu. Hivyo ndiyo ilivyo haki, lakini watu wengi hawajui. (30:30)
Kwa nini Mtume (s.a.w) achukue nafasi ya pili ya utii?
Ilivyo ni kwamba, Allah (s.w.) katika utaratibu wake wenye hikima, hawasiliani na kila mwanaadamu bali amewateua wajumbe wake miongoni mwa wanaadamu kufikisha ujumbe wake kwa wanaadamu wote na kuwafundisha kwa matendo namna ya kuutekeleza katika kuendesha maisha yao ya kila siku kwa mtu binafsi na kwa jamii kwa ujumla. Wajumbe hawa ni Mitume ambao walifunuliwa na Allah (s.w.) namna ya kuiongoza jamii katika njia anayoiridhia ambayo ndiyo pekee inayomfikisha mwanaadamu katika lengo la kuumbwa kwake kwa furaha na amani. Mitume wa Allah (s.w.) wamethibitishwa kwa walimwengu kwa kuwaambatanisha na dalili mbalimbali na pia amewateremshia vitabu kutoka kwake ambavyo ni mwongozo kamili wa maisha ya mwanaadamu na ni vyenye kutoa hukumu baina ya watu kwa uadilifu.
Kwa hakika tuliwapelekea Mitume wetu kwa dalili wazi wazi na tukaviteremsha vitabu na uadilifu pamoja nao, ili watu wasimamie uadilifu...... (57:25)
Mtume wa Allah (s.w.) ni tofauti na viongozi wa kawaida ambao huongoza kwa kutumia fikra na jitihada za kibinaadamu ambazo mara zote huathiriwa na udhaifu mwingi alio nao mwanaadamu. Mwanaadamu wa kawaida anaathirika sana na mazingira yake, matashi yake na ufinyu wa elimu yake. Kutokana na udhaifu huu si lazima kila atakaloamua liwe sahihi na lenye manufaa kwa jamii. Lakini Mitume hawaongozi kwa fikra na matashi yao, bali huongoza kwa ufunuo (Wahyi) kutoka kwa Allah (s.w.) ambaye ni mjuzi wa kila kitu mwenye habari ya mambo yote. Allah (s.w.) anatuthibitishia hili katika Qur'an:
Naapa kwa nyota zinapoanguka kwamba mtu wenu (huyu Nabii Muhammad) hakupotea wala hakukosa, wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake). Hayakuwa haya anayosema ila ni Wahyi (ufunuo) uliofunuliwa (kwake). Amemfundisha (malaika) mwenye nguvu sana. (53:1-5)
Hivyo mwanaadamu hawezi kufuata njia ya uongofu anayoiridhia Allah (s.w.) ambayo ndiyo pekee yenye kumuwezesha kupata furaha na amani katika maisha yake hapa ulimwenguni pasina na kumtii Mtume wa Allah (s.w.). Qur'an inatubainishia:
Mwenye kumtii Mtume amemtii Allah........ (4:80)
Sema (ewe Muhammad): ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni; Mwenyezi Mungu atakupendeni na kughufirieni dhambi zenu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye maghfira mwenye rehema. Sema: Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume(wake). Na kama mkikengeuka (Mwenyezi Mungu atakutieni adabu). Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi Makafiri. (3:31-32)
Masharti ya kuwatii viongozi
Viongozi au wenye mamlaka (Ulul-Amr) waliokusudiwa katika Qur'an (4:59) ni viongozi wa aina zote na wa ngazi zote katika fani zote za jamii ambao huielekeza na kuiongoza jamii kwenye kuliendea lengo la maisha. Qur'an haituamrishi kumtii kila kiongozi au kila mwenye mamlaka juu yetu kwa sababu si kila kiongozi anawaongoza vyema walio chini yake na kuwaelekeza kwenye kufikia lengo la maisha yao. Kuna viongozi wengine wanawatoa watu wao kwenye maisha ya furaha na amani na kuwatumbukiza kwenye maisha ya matatizo na huzuni. Viongozi tunaoamrishwa na Allah (s.w.) kwa kuwatii ni wale tu Waislamu ambao ni wacha Mungu wanaoongoza kwa mujibu wa Qur'an na Sunnah. Viongozi hawa tulioamrishwa kuwatii hawako juu ya sharia bali nao wako chini ya sharia ya Mwenyezi Mungu sawa na wale wanaowaongoza. Wako tayari kukosolewa na kurejeshwa kwenye Qur'an na Sunnah endapo watateleza kidogo katika kufanya kazi yao. Viongozi wa namna hii ndio pekee tunaoamrishwa tuwatiii kwani ndio pekee wanaotuongoza katika njia iliyonyooka:
Mwenyezi Mungu ni mlinzi (kiongozi) wa wale walioamini
Huwatoa katika giza na kuwaingiza katika nuru .......(2:257)
Kinyume chake, Waislamu tumeamrishwa tusiwatii viongozi wanaowaongoza kwa miongozo mingine kinyume na Qur'an na Sunnah. Inasisitizwa katika Qur'an:
Na usiwatii makafiri na wanafiki wala usijali udhia wao, na mtegemee Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi. 33:48)
"............ wala usiwatii wale ambao tumezighafilisha nyoyo zao wakafuata matamanio yao, na mambo yao yakawa yamepita mipaka (yaani makafiri). (18:28)
Tukiwatii viongozi hawa kinyume na mwongozo wa Allah (s.w.) tutakuwa tumewafanya miungu yetu na kuangukia kwenye shirk. Tumekatazwa kuwatii hawa kwa sababu watatuelekeza kwenye maovu na kuacha maadili mema ili tu wakidhi matashi ya nafsi zao.
Na (wazazi wako) wakikushurutisha kunishirikisha na (yale) ambayo huna elimu nayo, USIWATII, lakini kaa nao kwa WEMA hapa duniani. shika njia ya wale wanaoelekea kwangu kisha marejeo yenu ni kwangu, hapa nitakuambieni mliyokuwa mkiyatenda. (31:15)
ILI KUJIPATIA maendeleo ya kiuchumi katika zama zote mwandamu anahitaji rasilimali za kumwezesha kufikia azma hiyo.Miongoni mwa rasilimali kuu (natural resources) ni zile zinazohusiana na ardhi na kilimo, maji, bahari na uvuvi, na wanyama.Kwa mujibu wa Uislamu rasilimali hizo ni neema za Allah (S.W.).
(a) Rasilimali za ardhi na kilimo:
"Na katika ardhi muna vipande vinavyoungana (na kuzaa kwake namna mbalimbali) na muna mabustani yamizabibu, na mimea mingine, na mitende ichipuayokatika shina moja na isiyochipua katika shina mojaVyote vinanyweshelezwa (vinamiminiwa) maji yale yale;na tunavifanya bora baadhi yake vyengine katika kula(katika utamu). Hakika katika haya zimo ishara kwa watu wanaotia mambo akilini". (13:4)
(b) Rasilimali za maji na mvua:
"...na unaiona ardhi imetulia kimya lakini anapoyateremsha maji juu yake, inataharaki na kukuwa nakuotesha kila namna ya mimea mizuri." (22:5)
"Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka Mawinguni. Kisha akayapitisha (chini kwa chini)yakawa chemchem katika ardhi, tena akaotesha kwayo mimea ya rangi mbali mbali (na sura mbalimbali........"(39:21)
(c) Rasilimali za bahari na samaki:
"Mwenyezi Mungu ndiye aliyekutiishieni bahari ili humo zipite merikebu kwa amri yake, na ili mtafute fadhila yake na mpate.kushukuru". (45:12)
"Na yeye ndiye aliyeitiisha bahari ili humo mule daima kitoweo kipya (samaki) na mtoe humo mapambo mnayoyavaa. Na utaona merikebu zikipasua humo, ili mtafute fadhila zake (kwa kufanya biashara) na ili mpate kushukuru." (16:14)
(d) Rasilimali za wanyama:
"Na (pia) amewaumba wanyama. Katika hao mnapata (vifaavitiavyo) joto na manufaa (mengine); na wengine mnawala".
"Na mnaona raha mnapowarudisha jioni na mnapowapelekamalishoni asubuhi."
"Na (wanyama hao pia) hubeba mizigo yenu kupeleka katikamiji msiyoweza kuifika isipokuwa kwa mashaka na taabu.Hakika Mola wenu ni Mpole sana (na) Mwenye rehema nyingi""Na (amewaumba) farasi na nyumbu na punda ili muwapande na (wawe) mapambo.Na ataumba (vipando vyengine) msivyovijua". (16:5-8)
Muhutasari wa aya hizo juu ya rasilimali unapatikana katika aya ifuatayo:
"Yeye ndiye aliyekuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi"(2:29)
Wajibu wa kufanya kazi
Uislamu siyo tu unawahimiza watu kufanya kazi kwa bidii na kutokuwa wavivu bali kufanya kazi ni Ibada. Kila jambo lenye manufaa kwa watu binafsi, familia, jamii (n.k) laweza kuhesabiwa kuwa ni Ibada kwa Allah yakitimia masharti mawili; usafi wa nia (Ikhlasi) na kutenda jambo kwa kuzingatia mipaka ya sheria ya Kiislamu. Hivyo kazi ni Ibada. Kufanya kazi ni wajibu alionao mtu mbele ya Allah.
Qur'an inawahimiza Waislamu kutenda kazi nzuri zenye manufaa nao katika eneo lolote ile:
"Na sema: Tendeni mambo (mazuri). Mwenyezi Mungu atayaona mambo yenu hayo na Mtume wake na Waislamu. Na mtarudishwa kwa mjuzi wa siri na dhahiri;naye atakwambieni (yote)mliyokuwa mkiyatenda" (9:105).
Katika aya hii Mwenyezi Mungu amefungua milango kwa watu kutenda mambo yote mema katika eneo lolote la uchumi au siasa na yeye ataliona na atalilipa.
Uchaguzi wa kazi
Uislamu umempa mtu uhuru wa kuchagua kazi yoyote aipendayo maadam kazi hiyo ni ya halali kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Na ni wajibu wa serikali ya Kiislamu kuhakikisha kuwa watu wanapata fursa ya kufanya kazi wazipendazo. Watu watafanya kazi kwa mujibu wa vipaji vyao, kwani Mwenyezi Mungu amewajaalia watu vipawa mbali mbali:
"Na amewanyanyua baadhi yenu juu ya wengine daraja kubwa ili akufanyieni mtihani kwa hayo aliyo kupeni" (6:165).
Kila mtu anafanyiwa mtihani kwa neema au kipawa alichopewa. Katika maisha yetu ya kila siku wanaadamu ni viumbe wanaotegemeana kila mmoja ananufaika kwa kazi ya mwenzake. Daktari atamhitaji Muashi kumjengea nyumba yake na Muashi atamhitaji Daktari kumtibu maradhi yake n.k. Katika Uislamu kazi hutegemea uwezo tu, hakuna kazi zilizotengwa kwa ajili ya watu wa ukoo au kabila au nasaba fulani.
Tafauti ya malipo
Qur-an inatambua kuwepo kwa daraja tofauti za kiutendaji miongoni mwa watu katika jamii. Inatambua kutofautiana vipaji, uzoefu na utaalamu kati ya watu hivyo inakubali kutofautiana kimapato na kimalipo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii.(Islamic Economics: Theory and practice(A comperative study) by M.A.Manna.
Tafauti ya mapato au malipo ipo kwa sababu ya utendaji, uwingi au ubora wa bidhaa zilizozalishwa au huduma. Ni halali kwa mtu aliyetengeneza mashati kumi kumzidi kipato yule aliyetengeneza matano. Au yule aliyetengeneza kitu bora lazima amzidi yule aliyetengeneza kitu duni na vivyo hivyo aliyetoa huduma bora zaidi.
Aidha tafauti ya mapato pia ni halali iwapo kutokana na muda mrefu wa mafunzo baadhi ya kazi zikilinganishwa na nyingine. Kwa mfano ikiwa mtu ataajiriwa kufuta mavumbi katika madirisha ya ofisi atahitajia siku moja tu ya kuelekezwa namna ya kuifanya kazi hiyo. Lakini mtu akiajiriwa kutengeza madirisha hayo atahitajia muda mrefu zaidi katika kujifunza useremala. Hawezi kuelekezwa kwa siku moja tu halafu akaweza kuunda dirisha. Hivyo malipo ya mfutaji na mtengenezaji wa madirisha hayawezi kuwa sawa. Malipo yao yakiwa sawa basi watu wanaweza kuzikwepa kazi zinazohitaji mafunzo ya muda mrefu kama udaktari, usanifu majengo, uhandisi (n.k.) na kukimbilia zile zenye mafunzo ya muda mfupi kama utarishi, uhudumu, kufagia ofisi n.k.
Aidha, malipo hayatakuwa halali iwapo shughuli anayoifanya Muislamu ni faradhi. Kwa mfano: Si halali kwa Imamu kupokea mshahara kwa ajili ya kusalisha swala za faradhi, si halali kupokea malipo kutokana na kumfanyia kazi maskini, n.k.
Hifadhi ya wafanyakazi
Uislamu pia umeweka taratibu za kuhifadhi haki na maslahi ya wafanyakazi. Kwanza kila mfanyakazi lazima awe na mkataba (contract) na mwajiri wake. Mkataba huo uweke wazi malipo yake na kazi yake na makubaliano yao mengine. Mkataba huo ni bora uwe kwa maandishi lakini waweza pia kuwa kwa mdomo. Mwenyezi Mungu ameagiza katika Qur'an kuwa watu watekeleze kikamilifu ahadi zao za halali.
"Enyi mlioamini tekelezeni wajibu......." (5:1)
Katika Hadith iliyosimuliwa
na Bukhari, Mtume (s.a.w.) amesema kuwa miongoni mwa watu watatu ambao
Mtume (s.a.w.) atawakataa siku ya Kiyama ni yule anayemwajiri mfanyakazi
halafu asimpe haki zake. Katika Hadith nyingine amesema; Mlipeni mtu mliyemuajiri
kabla ya jasho lake halijakauka. Mradi wa Hadith hii ni kuwa mtu asicheleweshewe
malipo yake. Kama mapatano ni kila wiki au kila mwezi n.k. basi muda huo
ukifika tu mtu alipwe. Vivyo hivyo kwa mfanyakazi malipo ya kazi yatakuwa
ni halali iwapo atatimiza kipimo walichoafikiana na mwajiri kwa mshahara
huo. Kutegea kazi humfanya mtu achukue sehemu ya malipo isiyo haki yake.
Kwa hiyo, kipato kinachotokana na kazi iliyotegewa kimechanganyika na kipato
cha haramu. Uislamu unamtaka kila muumini awe mwaminifu na muadilifu katika
kazi baada ya kupatana na kukubaliana na muajiri.
--
|
|