Mafundisho ya Qur'an
 
 
Mabadiliko ya kihistoria kwa mujibu wa Qur'an
 

KWA mujibu wa mafundisho ya Qur-an mabadiliko ya kihistoria huwa na upendeleo maalum kwa watendao mema:

"Kwa hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wale wanaomcha, na wale wafanyao mema."(16:128).

Kihistoria aya hii imeshuka wakati ambapo mapambano baina ya waumini na makafiri Makka yameuma. Waumini pamoja na juhudi za kuijenga jamii na kuibadili hatua fulani ya historia yao, hupata msaada kutoka kwa Muumba wao. Kwa hiyo kama watu wataamini, wakajivika ucha Mungu, wakasimamisha haki na uadilifu, lazima msaada wa Allah utakuwa upande wao na watakuwa washindi na watawala. Hii ndio ahadi ya Allah:

"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri, kuwa atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwako kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia dini yao aliyowapendelea na atawabadilishia amani baada ya hofu yao."(24:55)

Kwa upande mwingine watu waliomuasi Mwenyezi Mungu hawapati upendeleo wowote zaidi ya kutegemea uwezo wao wa kibinadamu. Jambo lingine la kuzingatia ni kile wanachokiita wanahistoria wa kiislamu kama"selectivity of the historical process" kwamba historia huchuja na kuhifadhi yaliyo mema kwa jamii, na yale yaliyo machafu hata kama yatastawi kwa muda hatimaye hutoweka:

Ameteremsha maji kutoka mawinguni. Na mabonde yakapitisha maji kwa kadiri yake. Na mafuriko ya maji yakayachukua mapovu yaliyo juu ya maji. Na katika wanavyoyeyusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo (kama dhahabu au fedha, huja) povu vile vile. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyotoa mfano wa haki na batili. Basi lile povu linapita kama takataka tu basi; lakini vile vinavyowafaa watu vinakaa katika ardhi. hivindivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mfano. (Kuwa huenda ubaya ukapata nguvu lakini mwisho wake hupotelea mbali. (13:17)."

Njama, mauaji, vitisho, mbwembwe na vishindo vya wanaoupinga na kuupigia kelele Mwongozo wa Allah yamelinganishwa na povu la maji wakati wa mafuriko ambalo punde tu hutoweka:

Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya matata (kabisa) katika ardhi (hiyo) wala hawakusuluhisha (jambo ila kuharibu tu).

Wakasema: "Apianeni kwa Mwenyezi Mungu (ya kwamba) tutamshambulia usiku yeye (Saleh) na watu wake, kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona maangamio (yake wala) ya watu wake na bila shaka sisi ni wa kweli kwao.

Basi wakapanga vitimbi (vyao); na sisi tukapanga mipango (yetu, tukapangua vitimbi vyao) na hali ya kuwa hawana habari.

Basi angalia ulivyokuwa mwisho wa vitimbi vyao, tuliwaangamiza pamoja na watu wao wote.

Basi hizo nyumba zao tupu, (ni magofu tu hamna mtu) kwa sababu ya dhuluma yao; bila shaka katika haya muna mazingatio kwa watu wanaojua.

Na tukawaokoa wale walioamini na waliokuwa wakimcha (Mungu). (27:48-53)

Katika aya hizi Mwenyezi Mungu anatufahamisha mabadiliko yaliyotokea katika Taifa la kale lililoitwa Thamudi. Watawala wa Thamudi waliunda kamati maalumu (NEC au System) ilivyokuwa ikipanga vitisho, propaganda na mauaji dhidi ya watu wema walioongozwa na Nabii Saleh. Kamati hii ya watu tisa ilidumu muda mrefu kuwafanyia madhila waumini, hata hivyo aya zinatufahamisha kuwa hatimaye msaada wa Mwenyezi Mugu ukawa upande wa waumini na madhalimu wakaangamia.

Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, na hali hamjajiwa na mfano wa (yale yaliyowajia) wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka na madhara na wakatetemeshwa sana hata Mitume na walioamini pamoja nao wakasema: "Nusura ya Mwenyezi Mungu itafika lini?" Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu iko karibu. (2:214).

Madhalimu wa zama zote mila yao ni moja. Hupanga njama, propaganda na mauaji ya siri dhidi ya watu wanaoonekana kuhatarisha maslahi yao. Hivi leo watu wengi huuawa chini ya mtandao huo ambapo baadaye hutolewa maelezo kufunika unyama uliofanywa. Maelezo kama "ameuawa na watu wasiojulikana, alipigwa risasi kwa bahati mbaya akidhaniwa jambazi sugu, alikuwa akisakwa na polisi kwa kufanya uchochezi ambao ungesababisha kuvurugika kwa amani, amekufa ghafla kutokana na shinikizo la damu na vile vile kukimbilia kutoa pole kwa wafiwa na kueleza sifa kemkem za marehemu na kadhalika". Yote haya ni namna ya kujaribu kuudanganya umma kuwa hapakuwa na mipango mibaya dhidi ya mtu au watu hao. Pamoja na vitimbi hivi mwishowe madhalimu hushindwa na haki husimama.

Athari ya muda(Time-factor) katika Historia

Mabadiliko ya kihistoria hayatokei ghafla katika jamii ni mrundikano wa pole pole wa vijisababu na visababisho (A slow accumulation of causes) ambavyo baadaye huzaa mabadiliko makubwa. Hivyo huchukua muda mrefu mpaka athari yake kuonekana:

Na wanakuhimiza ulete adhabu lakini Mwenyezi Mungu hatavunja ahadi yake; na kwa hakika siku moja kwa Mola wako ni kama miaka elfu mnavyohisabu nyiye. Na (watu wa) miji mingapi niliyowapa muda, na hali walikuwa wakidhulumu? Kisha niliwatia mkononi na kwangu ndiko marudio. (22:47-48).

Pamoja na uovu atakaokuwa anafanya mwanadamu, Mwenyezi Mungu humpa muda wa kutosha, ambapo kama ni wa kurejea basi atakuwa ametanabahi. Lakini akizidi kuzama kwenye uasi adhabu ikija hakuna makimbilio wala msamaha haukubaliki tena.

Na Mola wako ndiye Mwingi wa Msamaha, Mwenye rehema. kama angewatesa kwa sababu ya yale waliyoyachuma, bila shaka angewapa adhabu upesi upesi. Lakini wanayo miadi ambayo hawatapata makimbilio yoyote ya kuepukana nayo. (18:58).

Na lau Mwenyezi Mungu anawatesa (upesi) watu kwa sababu ya maasi yao, asingalimwacha hata mnyama mmoja juu ya ardhi; lakini anawaakhirisha mpaka muda uliowekwa. Na unapofika muda wao hawawezi kukawilia saa moja wala hawawezi kuutangulia. (16:61).

Kusambaratika kwa Jamii

Mwenyezi Mungu hailetei miji au jamii maangamizi hali ya kuwa watu wake ni watenda mema. Aidha jamii haiangamizwi kama haijafikiwa na muonyaji kuwaonyesha muongozo sahihi wa maisha:

... Mola wako hakuwa wa kuiangamiza miji kwa dhulma, hali wenyewe wameghafilika (hawakujiwa na mitume wa kuwaonya). (6:131).

Na Mola wako si wa kuangamiza nchi kwa dhulma tu na hali watu wake ni watendao wema. (11:117).

Sababu za kusambaratika na kuangamizwa kwa jamii ni udhalimu, uonevu na ukandamizaji. Jamii ikishastawisha mizizi ya uonevu, udhalimu na ukandamizaji basi hatima yake ni kuangamizwa:

Na mingapi tuliiharibu katika miji iliyokuwa ikidhulumu. Na tukawaumba baadaye watu wengine. (21:11).

Na miji mingapi tuliiangamiza, na iliifikia adhabu yetu usiku au katika wakati wa adhuhuri walipokuwa wamelala. basi hakikuwa kilio chao ilipowafikia adhabu yetu isipokuwa kusema: Bila shaka sisi tulikuwa madhalimu. (7:4-5).

Aidha, Qur'an inatubainishia kuwa utajiri, maisha ya anasa na mamlaka huwa na kawaida ya kuharibu maadili ya jamii kama pana uchache wa imani ya Allah. Vile vile Qur-an inatufahamisha kwamba mataifa yamekuwa yakiangamia kutokana na si tu kutokufanya mambo mema bali pia kuyanyamazia au kulinda maovu na waovu:

Na iogopeni adhabu ambayo haitawasibu peke yao wale waliodhulumu nafsi zao miongoni mwenu( bali pia itawasibu walionyamaza wasiwakataze); na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.(8:25).

Qur-an inasisitiza kwamba kushika madaraka kwa watawala waovu katika jamii mbali mbali vipindi vyote vya historia na watu kuwakubali watawala hao kwa mtindo au mfumo wowote ule, ni sababu nyingine ya kuporomoka kwa mataifa:

"Na tumeiangamiza miji mingapi iliyojifaharisha juu ya maisha yao! Hayo maskani yao yasiyokaliwa baada yao tena ila kidogo tu hivi, na sisi tumekuwa warithi." (28:58).
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook