JIFUNZE SHERIA
 
 
Ushahidi: Maana ya ushahidi
 

Na Dkt. Abdallah J. Saffari
 

USHAHIDI ni namna ambayo inatumika kuthibitisha au kukanusha ukweli wa jambo ambalo linachunguzwa (F.3(1) Sheria ya Ushahidi Na. 6 1967). Maelezo na ikirari za washitakiwa ni ushahidi pia (K.h.j).

Kila anayedai jambo fulani ana dhima ya kuthibitisha kwa ushahidi uliopo. Katika jitihada ya kuthibitisha au kukanusha jambo kuna hatari nyingi ambazo huweza kupotosha kweli na haki. Ili kuepuka au kupunguza tu hatari kama hizo kuna kanuni ambazo budi zifuatwe, na wakati mwingine kutiliwa maanani tu, kabla ya kuukubali au kuukataa ushahidi fulani.

Ushahidi unaokubalika ni ule tu unaothibitisha au kukanusha jambo linalodaiwa kwa mujibu wa sheria (F. 7 Sheria ya Ushahidi, i.h.j). Mathalan ushahidi wa kuambiwa na mtu mwingine, japo ni kweli, haukubaliwi, isipokuwa nyakati fulani fulani kama vile katika kuthibitisha sababu ya kifo cha mhusika kutokana na kauli yake mwenyewe (F.34(a), Sheria ya Ushahidi, i.h.j); au ushahidi unaounga mkono maelezo ya shahidi fulani (F.166, Sheria ya Ushahidi, i.h.j. Pia angalia Rex v. Mohammed Allui (1942) 9 E.A.C.A. 72).

Mtu ana fahamu tano kuu; kuona, kusikia, kugusa, kuonja na kunusa. Aina zote hizo huweza hutumika katika kuthibisha au kukanusha kweli ya jambo linalobishaniwa (F.3(1) na 62, Sheria ya Ushaihdi, i.h.j). Kwa mfano: Hamis ameshitakiwa kwa kuchoma nyumba kwa kukusudia. Juma anaweza kuwa alimwona Hamis akichoma nyumba hiyo. Au anaweza kuwa alisikia harufu ya mafuta ya taa kabla ya kulipuka moto uliounguza nyumba hiyo; au anaweza kuwa alimsikia Hamis akipanga kuichoma nyumba hiyo. Aina zote hizo za fahamu zina uzito katika kuthibitisha kosa hilo la uchomaji nyumba.

Hali ya akili ambayo shahidi anaielewa pia huweza kuwa ushahidi (F.3, Sheria ya Ushahidi, i.h.j). Kwa kawaida shahidi anaweza kuthibitisha au kukanusha ukweli mintaarafu ya hali ya akili yake mwenyewe lakini sio ya mtu mwingine (Sarkar on Evidence, Toleo la 12, Sarkar and Sons Ltd., Calcula, 1971 uk. 21).

Hali ya akili ya mtu inaweza kuthibitishwa kufuatana na mwenendo au kauli yake binafsi. Hivyo basi shahidi anaweza kudai hana akili timamu kwa kauli yake mwenyewe. Lakini hawezi kusema kwa uhakika kuwa mtu fulani hana akili timamu isipokuwa kama anatoa maoni ya kitaalam, mathalan daktari, au anafahamu mwenendo wa mtu huyo ambao unathibitisha utovu wa akili timamu.

Hivyo basi katika kurasa zinazofuatia tutajaribu kuonyesha kanuni muhimu mintaarafu ya ushahidi.

Ushahidi wa Maneno na Hati

Jambo linalochunguzwa huweza kuthibitishwa kwa ushahidi wa maneno au maandishi. Mfano: Jambo linalobishaniwa ni iwapo John alikuwepo Arusha wakati ambapo kosa analoshitakiwa nalo lilipotendeka. Rafiki yake Juma ambaye yuko Arusha anaweza kusema kwamba alimwona John Arusha tarehe inayodaiwa. Au Shaaban, rafiki yake mwingine John aliyeko Tanga, anaweza kuonyesha barua ambayo John alimwandikia kuwa alikuwa Arusha wakati huo unaodaiwa. Ushahidi wa Juma mintaarafu ya jambo hilo ni wa maneno ambapo ule wa Shaaban ni wa hati.

(a) Ushahidi wa Maneno

Kila jambo isipokuwa hati lazima lithibitishwe kwa ushahidi wa maneno (F.62, Sheria ya Ushahidi, i.h.j).

Kwa kweli sehemu kubwa ya ushahidi hutolewa kwa maneno maana hata pale ambapo hati zinahusika ushahidi wa maneno pia hauwezi kuepukika.

Masharti makubwa ya ushahidi wa maneno, na hata ule wa hati, ni kama ilivyogusiwa awali: Kuwa lazima utokane na njia tano za fahamu, yaani kuona, kusikia, kugusa, kuonja na kunusa. Kwa mfano mtu anaweza kuwa amesikia harufu ya petroli hata bila ya kuiona petroli yenyewe. Au anaweza kutambua kitu kwa kukipapasa tu, bila ya kukiona na kadhalika.

(b) Ushahidi wa Hati

Hati huweza kuwa ndiyo ushahidi wa msingi kuthibitisha jambo fulani. Katika makosa ya wizi, mathalan, hundi au hati za malipo hutolewa mahakamani kama vielelezo kuthibitisha mashitaka yanayodaiwa. Barua, taarifa za wataalam na aina nyingi za hati ni mifano tu inayoonyesha umuhimu wa ushahidi wa maandishi, yaani hati. Kuna hati za binafsi kama nyaraka za marafiki au ofisi za watu binafsi. Na ziko hati za jumuiya kama vile nyaraka za idara za serikali na mashirika.

Kila inapodaiwa kuwa kuna hati yenye ushahidi kadha basi ni lazima nakala halisi ya hati hiyo itolewe mahakamani (F.66, Sheria ya Ushahidi, i.h.j). Lakini hutokea nakala halisi ya hati inayohusika haipatikani kwa sababu imeibwa, imepotea, imeungua au kwa namna yoyote ile ya kuaminika hati hiyo haiwezi kupatikana. Badala ya hati hiyo halisi nakala ambayo imetokana na hati hiyo inaweza kutolewa mahakamani (F.67(1), Sheria ya Ushahidi, i.h.j), Inapokuwa hata nakala ya hati halisi haipatikani basi ushahidi wa maneno wa mtu ambaye aliyasoma maandishi yanayodaiwa kuwemo katika hati inayohusika yanaweza kutolewa (F.65(E), Sheria ya Ushahidi, i.h.j).

Aidha, nakala za hati halisi zinaweza kutolewa mahakamani bila kuthibitisha kuwa zimepotea au kuharibika ikiwa nakala halisi yenyewe imo mikononi mwa mtu ambaye hawezi kuja mahakamani, kwa mfano yuko mbali, au iwapo mtu mwenye hati hiyo hawajibiki kutoa ushahidi mahakamani kutokana na wadhifa wake kama vile Rais wa Jamhuri au Afisa wa Ubalozi. Au iwapo nakala halisi yenyewe haiwezi kuletwa mahakamani kutokana na hali yake. Au iwapo mtu aliye na hati inayohusika anakataa kuitoa mahakamani kusudi tu.

Kabla hati za jumuiya hazijatolewa kama vielelezo mahakamani ni lazima ionyeshwe kuwa hati hizo zimethibitishwa kuwa sahihi na maofisa wanaohusika. Kwa mfano kumbukumbu za mwenendo wa mashauri yote pamoja na hukumu zake huthibitishwa na mahakama kuwa ni sahihi.

Hati inaweza kutumika kama ushahidi mahakamani kwa kutolewa ili itambuliwe tu na shahidi anayehusika au kutolewa kama kielelezo halisi. Kwa mfano upande wa mashitaka au utetezi unaweza kumwita mtaalam wa maandishi na kumwuliza iwapo anaitambua hati inayohusika. Baadaye hati hiyo inaweza kutolewa mahakamani rasmi kama kielelezo cha kuthibitisha maelezo yaliyomo ndani ya hati hiyo.

Kabla ya hati kutolewa mahakamani kama kielelezo mahakama yatamwuliza mshitakiwa au wakili wake iwapo wanapinga hati hiyo kutolewa kielelezo. Hati inaweza kupingwa isitolewe mahakamani kwa sababu nyingi. Moja ni kuwa labda haitimizi masharti ya kisheria. Kwa mfano taarifa za wataalam wa picha ni lazima ziwe zimeandikwa kwa namna inayoelezwa katika Sheria ya Mwenendo wa Jinai (F.202 na Jedwali ya Nne ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai Na. 1, 1985). Hivyo zisipoafikiana na sharti hilo haziwezi kutolewa kama kielelezo. Au hati ya jumuia inayohusika inaweza kuwa haikuthibitishwa na afisa anayeweza kufanya hivyo (Fungu la 86, la Sheria ya Ushahidi linalihitaji hati za jumuia zote zithibitishwe na maofisa wanaohusika kabla ya kutolewa kama vielelezo). Au hati inayohusika inaweza kuwa haina saini ya mhusika au ina saini ambayo inatatanisha, na kwamba, inawezekana ikawa sio ya mhusika. Na kadhalika.

Kutolewa mahakamani kwa hati inayodaiwa haina maana mshitakiwa anakiri yaliyomo, yaani ukweli wa hati ile. Hati hiyo inaweza kuwa halisi lakini ina taarifa za uongo mtupu, au za makosa ya wazi au ya kujificha. Hivyo kila upande unaohusika na kesi una haki ya kumhoji aliyetayarisha hati inayohusika kuthibitisha usahihi wake. Na kama inavyoelezwa hapo baadaye, mahakama yana wajibu mkubwa mno katika kutekeleza jambo hilo. Hati ya uongo haina maana. Mwisho wa shauri itakuwa ni wajibu wa mahakama kuamua kuikubali hati hiyo kuwa ina ushahidi wa kweli, wote, au baadhi yake au kuukataa kabisa.

Ushahidi wa Moja kwa Moja na wa Mazingira

Ushahidi wa moja kwa moja unaweza kuwa na maana mbili: Kwanza ni ule ambao unathibitisha jambo moja kwa moja kutokana na hakika yake. Kwa mfano ushahidi wowote ule unaoshuhudia tukio fulani ni wa moja kwa moja kinyume na ule ambao unaweza kuthibitisha tukio hilo hilo kwa kuunganisha vipande vipande vya ushahidi. Pili, ni ule ushahidi unaotolewa na mtu aliyeona, kunusa, kuonja, kusikia na kugusa bila ya kuambiwa na mtu mwingine. Ushahidi wa kuunganisha vipande vipande ili kuthibitisha jambo fulani ndiyo wa mazingira. Ni muhimu kuzingatia hapa kuwa hata ushahidi wa mazingira sharti uwe wa moja kwa moja.

Ushahidi wa moja kwa moja, kama ni wa kweli, ndio bora kushinda ule wa mazingira kutokana na hakika yake. Lakini ushahidi wa aina hiyo ni nadra sana, hasa katika hatua ya sasa ya maendeleo ambapo mbinu za utendaji wa makosa ya jinai zimekuwa za kutatanisha sana kiasi cha kuwakanganya hata wapelelezi stadi. Mathalan mara chache mno mshitakiwa atakamatwa akiiba, kuua na kadhalika.

Mbali na uchache wa ushahidi wa moja kwa moja, ushahidi huo una athari kubwa ya kupotoshwa, pengine kwa makusudi tu. Sababu unategemea kauli ya mtu mmoja au hata wengi kufuatana na jinsi walivyoona ushahidi unaohusika mintaarafu na tukio kadha. Mashahidi huweza kununuliwa au hata kurubuniwa tu kusema uongo. Hivyo ushahidi wa mazingira ni bora zaidi kwa sababu unaepuka athari za kupotoshwa kwa kukusudia. Lakini nao, kwa vile ni wa kuungaunga, ni lazima viungo vyake viweze kuwa imara kukamilisha kitu kizima. Yaani mazingira ya ushahidi huo ni lazima yawe hayana shaka. Katika shauri la Simon Musole v R (Simon Musole v. R (1958) E.A. 715 uk. 716) Rais wa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki Jaji Keneth O'Connor, alionya kuwa katika shauri ambalo linategemea ushahidi wa mazingira pekee mahakama yasimtie hatiani mshitakiwa mpaka yameridhika kuwa ushahidi huo wa mazingira hautii shaka juu ya hatia ya mshitakiwa (K.h.j).
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook