ZAMANI ukiwa na kiunga chako cha minazi ndio tajiri na ndio Mwinyi. Kadri mtu alivyokuwa na mashamba makubwa ya miwa, pamba, katani au kahawa ndivyo alivyozidi kuwa tajiri.
Zama hizo zilipita utajiri ukahamia kwa wenye kumiliki migodi na wenye viwanda vya kutengeneza magari na mashine nzito nzito.
Leo matajiri wakubwa zaidi duniani sio wenye mashamba ya mikorosho wala wenye migodi ya almasi, ni wenye kumiliki sayansi na teknolojia yake pamoja na mfumo wa habari na mtandao wake.
Mwenye kiunga chake cha minazi lau atabakia na mawazo ya karne ya 19 kwamba mashamba makubwa na kuwa na watumishi wengi ndio utajiri, atakuwa juha.
Mpaka miaka ya 1930 ili mtu wa Bara ajue udhu wake ilibidi aende Unguja, Mombasa au Tanga. Vinginevyo aletwe mwalimu toka masafa ya mbali.
Zama hizo zilipita waalimu wakawepo kila kona ya nchi. Lakini ufundishaji ukawa ni ule wa kutafsiriwa vitabu vya Kiarabu. Huwezi kujua udhu mpaka uweze kutamka "Furudhul-udhui sitatu", huwezi kufunga mpaka utamke "nawaitau swaumu ghada". Kwa lile la udhu huwezi kulijua mpaka ukae kitako na utulie kwa Sheikh yaweza kukuchukua mwezi mzima hujamaliza mlango wa udhu na hivyo hujajua kutawadha.
Leo dakika tano tu zatosha kumfanya mtu hata yule aliyesilimu leo ajue kutawadha au kufunga. Mwalimu mwenye taaluma ya ufundishaji hatampotezea mwanafunzi wake muda kumfasiria "Babu Maja', 'Risala na Safina'. Bali vitabu hivi atavitumia kama rejea kuandaa somo.
Rejea hizo hizo leo zimefasiriwa katika lugha mbalimbali. Aidha, Qur'an na Hadith za Mtume (s.a.w.) navyo vimefasiriwa na kutolewa maelezo na ufafanuzi mwingi na wataalamu mbalimbali.
Tunaishi katika ulimwengu wa teknolojia ambayo imewezesha tafsiri mbalimbali za Qur'an na vitabu vyote vikubwa vya Hadithi kuingizwa kwenye kompyuta.
Atakayetambua kwanza kwamba unahitaji birika la maji, kata au bomba kumuelekeza mtoto wa leo namna ya kutawadha na wala sio kumkaririsha "Risalatu jamiya" huyu ndiye atakayedumu na Usheikh wake.
Lakini atakayedhania kwamba watu hawawezi kujua masharti ya kuswali mpaka wakae kitako waitikie "Dhwahir Sheikh" huyu hana tofauti na Mwinyi wa viunga vya minazi.
Hata hivyo, heri ya mwenye viunga vyake kwani mtu ukishamiliki shamba ndio umemiliki hawezi kumiliki mtu mwingine shamba hilo wakati huo huo. Litabakia lako pekee.
Si elimu. Watu wote kijijini, mtaani au mkoani kwako waweza kuwa na elimu uliyo nayo kwa wakati mmoja.
Sheikh atakayedhania elimu ni kiunga cha minazi, jahazi la kuvulia samaki au kundi la ng'ombe hatoisha kukwaruzana na waumini kwa dhana yake kwamba hawajui kwa vile hajawamegea.
Sheikh huna sababu leo ya kugombana na waumini kwamba hawaleti watoto Madrasa ya kupiga dufu na kughani aya za Mwenyezi Mungu wakiwa wamekalia majamvi.
Wahamasishe waumini watoe michango, waunde kamati za wataalamu, wajenge shule safi za awali kwa watoto. Watoto waje kwenye madrasa wakiwa na sare safi na saa nne wapate uji safi madrasa ziwe safi yenye madawati. Wafundishwe kumjua Mola wao; Akhlaq alif be, a e i o u na mbili jumlisha tatu.
Sheikh, Mwinyi mzito wa akili asiyeliona hili heshima yake itaporomoka kila uchao na mikwaruzo baina yake na waumini haitokwisha.
Waislamu tumefunzwa adabu
tuwaheshimu Masheikh wetu, lakini pia tumehimizwa tukumbushane na kupeana
nasaha. Na hii ni kwa mkubwa na mdogo. Tupeane nasaha njema ili sote tuelekee
njia moja kwa manufaa ya ummah.
--
|
|