Na Said Rajab
Uchumi wa kibepari tunaojaribu kuujenga utatuletea msiba tusipokuwa makini. Sera inayoongoza uchumi huu ni nguvu ya soko. Biashara yoyote inayoweza kuleta wateja; itapanuliwa soko lake hata kama jamii itaathirika kimaadili. Sifa kuu ya mfumo wa kibepari ni ukosefu wa maadili yanayomjenga binadamu. Kilicho muhimu ni kudhibiti masoko na kuendelea kupata faida nono!
HALI kama hii tunaishuhudia hapa nchini katika biashara nyingi tu. Kila kona utakuta matangazo ya biashara; kwenye magazeti, Radio na Televisheni. Tafsiri yake ni kwamba masoko ndiyo yanayoamua uhai wa biashara. Ili uweze kushindana vyema katika biashara ni lazima uitangaze vya kutosha biashara yako kwa lengo la kudhibiti soko. Hali hii imesababisha wafanyabiashara wajali zaidi uhai wa biashara zao kuliko madhara ya biashara zao kwa jamii.
Nia na madhumuni hasa ya makala haya ni kuzungumzia magazeti, majarida, vitabu na fasihi andishi nyinginezo zinazouzwa nchini zenye sera ya kutangaza aibu za ngono kama mkakati wa kudhibiti masoko yao. Athari gani jamii inapata?
Miaka ya nyuma tulikuwa na waandishi wa vitabu wenye majina wanaokidhi haja ya jamii. Waandishi mahiri kama kina Shaaban Robert, Shafi Adam Shafi, Mohamed Said Abdullah, Penina Mhando na wengineo ambao kwa ukweli kazi zao zimeinufaisha jamii ya watanzania kwa kipindi kile, na zitaendelea kukumbukwa daima.
Kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo waandishi mashuhuri wa vitabu wanavyozidi kutoweka na waandishi uchwara wanavyoibuka. Uwanja wa riwaya umejazwa rundo la fasihi zenye mrengo wa ngono tu! Kulikoni? tunataka kujenga taifa la walevi wa ngono!
Wasomaji wa vitabu na magazeti ya maana wanatoweka taratibu kwa sababu hakuna waandishi wa maana wa kukidhi kiu yao ya ufahamu. Wachapishaji na wachapaji vitabu kama wafanyabiashara, wanaoogopa kuchapisha kazi za waandishi wa haja kwa hofu ya kukosa soko. Hakuna wasomaji wa habari wala riwaya zenye mafao. Ni wachache mno kiasi cha kurudisha faida kwa wachapishaji.
Matokeo yake waandishi wa vitabu na magazeti yenye faida kwa jamii wanakata tamaa kwa sababu ya kukosa soko, na magazeti ya kipuuzi na vitabu vya kiasherati ndiyo yaliyofurika sokoni. Siyo kwa sababu yana faida kwa jamii; bali yanauzika tu. Hii siyo hali ya kujivunia. Kwa namna hii tunajenga taifa la kesho lisilopendelea kusoma mambo ya maana na makini na kupendelea upuuzi wa 'Songombingo'.
Kama tunavyojuwa watanzania ni taifa la watu wenye vipaji mbalimbali. Lakini vipaji vya watu katika kazi za fasihi na uwanja wa habari havitaleta manufaa kwa jamii iwapo havitadhibitiwa kwa kuundiwa sera ya taifa inayofaa. Waandishi wa vitabu, majarida, na magazeti wasiachiwe wakuze vipaji vyao kwa kuupandisha chati 'uasherati' ndani ya jamii yetu. Vipaji vya watu lazima viwe na manufaa kwa jamii na siyo madhara.
Vipaji vya waandishi vielekezwe katika kuijenga jamii mazingira haya yaliweza kuleta waandishi bora walioitangaza nchi hii mpaka nje ya mipaka yake. Waandishi hawakuachwa wajiandikie tu!
Jambo la msingi hapa tusiwaachie waandishi wa habari na vitabu wasukumwe na nguvu ya soko tu. Kwa namna hii hatukuzi taaluma hizi.
Tukiwa wayakinifu zaidi, tutayaondoa kwamba vyombo vingi vya habari na kazi nyingi za sanaa zinafanywa na watu wasiokuwa na vipaji wala taaluma za kutosha. Ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira umesababisha watu wengi wajiingize katika fani ya uandishi wa habari na kazi za sanaa. Watu hawa kwa ukweli siyo waandishi wala wasanii bali ni wababaishaji tu wanaochukulia kazi hizi kama njia ya kujipatia riziki. Ni mahodari sana wa kubuni misamiati ya kihuni na kashifa za ngono ili magazeti yao yauzike. Wanachouza siyo ufundi wa sanaa zao au uzito wa habari wanazoandika bali ni ngono! Iwapo tutakuwa na sera madhubiti dhidi ya waandishi wa wasanii wanaouza ngono badala ya habari, ninahakika watapotea kwa muda mfupi sana. Hakuna wanachoweza kuicheza jamii yetu zaidi ya aibu za ngono!
Kwa kawaida vyombo ya habari, vitabu vya riwaya, mashairi, nyimbo, ngonjera na kadhalika huwa na mwelekeo wa kujenga mila na desturi za jamii inayohusika. Mila na desturi hizi zinapofikia kiwango cha kitaifa huwa utamaduni wa taifa. Na kutokana na utamaduni wa taifa tunaweza kupata itikadi ya taifa. Vyombo vya habari vina uwezo wa kuliunganisha taifa zima katika itikadi, misiba, Sherehe na n.k.
Tunaporuhusu vyombo vya habari vya ngono, kuna hatari ya kuifanya ngono iwe itikadi ya taifa letu. Na matunda yake ni ubakaji, ulawiti, na majanga yatokanayo na hayo. Muda siyo mrefu tutaona mabaradhuli wanaandamana wakidai kukubaliwa na katiba kama ilivyo Ulaya na Marekani. Biashara ya ukahaba itaruhusiwa na makahaba watapewa leseni ili walipe VAT! Tungependa kufika huko?
--
|
|