Wajizatiti kujenga msikiti
 

Na Abu Zubeir - Dodoma

WAISLAMU wa kijiji cha Veyula nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, wameanzisha utaratibu wa kuchanga fedha kwa ajili ya kujenga Msikiti mpya, aidha wanawaomba Waislamu wote kushiriki katika kutoa Sadaka ili kufanikisha ujenzi wa Msikiti huo.

Kaimu Katibu wa Msikiti huo Ustaadh Amr Juma alitoa taarifa hizo pale alipotembelewa na mwandishi wa taarifa hzi hapo kijijini (Veyula). Ustaadh Juma alisema wamejiwekea jitihada za makusudi, ikiwa ni pamoja na nguvu kazi na utaratibu mwingine ni kuchangishana kila mwezi 200/- ustaadh Juma alisema katika kijiji chao kuna kaya 70 za Waislamu ambapo ni wastani wa Waislamu 350

Akielezea hali halisi ya Uislamu kijijini hapo Ustaadh Juma alisema idadi ya Waislamu ambao wako mstari wa mbele katika majukumu ya Dini ni ndogo sana, aidha ni katika nyakati maalum ndiyo Waislamu wengi hujitokeza kama misiba na maulid, kauli ya Ustaadh Juma ilithibitishwa na mwandishi wa taarifa hizi kuona Msikiti huo ambao ni mdogo sana lakini haukujaa kabisa.

Ustaadh Juma pamoja na takwimu hiyo ndogo alisema katika masuala ya michango Waislamu wa Kijijini hapo wanaiheshimu na kwa hatua hiyo waliyoianzisha wataweza kufanikisha ujenzi wao.

Hata hivyo Ustadh Juma anawaomba Waislamu wa Dodoma kutoa michango yao ya fedha taslim au vifaa vya ujenzi kufanikisha shughuli za Ujenzi wa Msikiti huo.


Sheikh Zuberi awataka vijana wasimamishe Uislamu

Na Abu Zubeir, Dodoma

VIJANA wa Kiislamu nchini wametakiwa kuacha malumbano badala yake wawe chachu ya kuhuisha Uislamu na kutekeleza majukumu yao ya kutafuta elimu.

Hayo yalitamkwa na Sheikh Ahmed Zuberi wakati akiwahutubia wanafunzi wa Chuo cha Ufundi (VETA) cha mjini Dodoma hivi karibuni.

Sheikh Zuberi aliwataka vijana hao kuwa waelekeze jitihada zao katika kutafuta elimu ili wawe watetezi wa haki za Kiislamu tayari kutekeleza masuala ya ibada katika maeneo yao ya shule na kushiriki kikamilifu katika uvaaji wa hijabu kwa wanafunzi wa kike.

Sheikh Zuberi akiwa kama mgeni rasmi katika uzinduzi wa tawi la Umoja wa Vijana wa Kiislamu (UVK) chuoni hapo, alisema kuwa ufunguzi wa tawi hilo uende sambamba na mikakati na miundo mbinu ya kueneza da'awah kwa wanafunzi wa Kiislamu.

Aidha, aliwasisitiza vijana kuyapa kipaumbele masuala ya elimu zote mbili, aliwaambia nafasi yao ya kupigania Uislamu utapatikana pale kwa kupata elimu zote mbili, elimu za mazingira na ya kiroho (dini).

Vijana hao pia walitakiwa pia waijenge miili yao kiafya na kufanya mazoezi kwani hayo yapo katika mafunzo ya Mtume (s.a.w.).

Sheikh Zubeir alimalizia nasaha zake kwa kuwataka vijana wa Kiislamu wawe mfano bora katika jamii, aidha, aliwaomba wajiepushe na tabia mbaya kama za ujihusishaji wa madawa ya kulevya, mavazi yasiyokubalika katika Uislamu na uhudhuriaji wa vikao vya madisko na utazamaji wa sinema au video zenye kuonyesha tabia za Kimagharibi ambazo haziendi na sheria za Allah (s.w.).


Meya wa Tanga atoa nasaha kwa mashirika ya Kiislamu
 

Na Abu Abdullah, Tanga

MASHIRIKA ya Kiislamu nchini yametakiwa kupanga miradi yao huku yakizingatia maendeleo ya kilimwengu ya karne ya 21.

Nasaha hizo zilitolewa na Meya wa Mji wa Tanga Bwana Kisauji hapo Ijumaa Juni 4, mwaka huu wakati wa ufunguzi wa shule ya msingi inayomilikiwa na Africa Muslim Agency (AMA) kwenye kijiji cha Pongwe nje kidogo ya mji.

Katika risala yake ambayo ilisomwa kwa niaba yake na Naibu Meya Sheikh Ali, Meya wa Tanga aliikumbusha AMA kuwa Tanga ina maeneo mengi na wakazi wa aina tofauti, hivyo ifanye juhudi kutoa msukumo wa kielimu kwenye kila eneo.

Alikumbusha juu ya udhaifu wa kiuchumi wa wakazi wengi wa Tanga na hivyo kuyataka mashirika ya Kiislamu kutilia maanani suala hilo pia, wakati wakipanga viwango vya ada za shule.

Pamoja na kujenga shule za msingi na sekondari, Meya aliyataka mashirika hayo yasisahau kujenga vyuo vya ufundi ili kwenda sambamba an karne ijayo na akaahidi kutoa kila ushirikiano, vile vile kuingilia kati popote patakapokuwa na vikwazo.

Sherehe hizo za ufunguzi zilihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa AMA kutoka Damman Sheikh Mohammed Khamis pamoja na Mkurugenzi wa Elimu Tanzania Sheikh Ramadhani Breima na viongozi wengine kadhaa.


Tawi la Ansaar Muheza kujenga sekondari
 

Na Kassim Billo, Tanga

TAWI la Taasisi ya Ansaar Muheza Tanga likiongozwa na Sheikh Amir K. Kiroboto lina mpango wa kujenga shule sekondari kwa ajili ya vijana wa Kiislamu wanaomaliza shule za msingi na kukosa nafasi katika shule za serikali.

Sheikh Kiroboto alieleza haya katika kikao cha mkutano mkuu wa mwaka wa taasisi ya Ansaar uliofanyika hivi karibuni mjini Tanga.

Sheikh Kiroboto ambae alisikilizwa kwa makini na wajumbe waliohudhuria katika mkutano huo wa mwaka, alisema kuwa tawi lake limepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha mwaka uliopita wa 1998 kwani waliweza kununua shamba la michungwa ambalo tayari hivi sasa mazao yake yameanza kuuzwa na kuleta fedha ambazo zinasaidia mipango ya maendeleo ya tawi hilo.

Sheikh huyo alisema kuwa japokuwa wahujumu wa maendeleo wameanza kuwapinga kuwa kupita nyumba hadi nyumba lakini wao wamesimama imara kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu kwamba ndie mlinzi wao.


Waalimu Waislamu Same wapata mwamko mpya
 

Na Mwandishi Wetu

WAALIMU Waislamu wa shule za msingi mjini Same wamechukua azma kutumia ujuzi wao na nafasi yao kama waalimu kuufundisha Uislamu kwa watoto mashuleni.

Aidha, waalimu hao wameazimia kutumia muda wao zaidi hasa siku za Jumamosi na Jumapili katika kuusoma na kuujua Uislamu.

Waalimu hao wamepata mwamko huo mpya baada ya kuhudhuria semina ya ufundishaji wa elimu ya dini ya Kiislamu mashuleni iliyofanyika Same Juni 1 na 2 chini ya uongozi wa mwalimu A. Mmbagha.

Katika semina hiyo waalimu walielekezwa namna ya kutumia minhaji na rejea zake.

Kwa kupatikana kwa vitabu vya rejea, waalimu hao wameeleza kwamba itarahisisha zoezi la ufundishaji na hivyo wakatoa pongezi zao kwa taasisi zinazoshughulikia uandishi na uchapishaji wa vitabu hivyo.

Ili kufanikisha na kuboresha zoezi la ufundishaji waalimu hao wamewahimiza wazazi wawanunulie watoto wao vitabu hivyo vya elimu ya Kiislamu kwa shule za msingi.


Songea Waswali chini ya ulinzi wa Polisi
 

Na Mwandishi Wetu, Songea

Imeadaiwa kwamba waumini wa Masjid Nur mjini Songea wiki iliyopita waliswali Ijumaa chini ya Ulinzi wa Polisi ikihofiwa kuzuka vurugu msikitini hapo.

Mwandishi wa habari hizi alibaini askari wako na sawa na wale wasio na eneo la msikiti huo wakati wote wa kipindi cha swala.

Uchunguzi wa mwandisih wa habari hizi uligundua kwamba chanzo cha hali hiyo ni taarifa iliyopelekwa kituo cha polisi na baadhi ya wazee mashughuri katika siasa.

Awali kabla ya tukio hilo palitokea hali ya kutoelewana baina ya uongozi wa msikiti, baadhi ya wazee na waumini waliokataliwa kuondolewa Muumini aliyekuwa akihutubu kila Ijumaa.

Imedaiwa khatibu huyo aliondolewa kufuatia hotuba yake ya hivi karibuni iliyo chambua dhana ya ya Shirki katika Uislamu. 
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook