Lipumba gumzo la wananchi mikoani
 

Na Mwandishi Wetu
 

WANANCHI wa baadhi ya mikoa nchini wamekuwa na kiu kubwa ya kutaka kumuona na kumsikiliza Mshauri wa chama cha CUF Prof. Ibrahim Lipumba.

Mikoa mitatu iliyotembelewa na mwandishi wa habari hizi gumzo la makundi mbalimbali ya wananchi ni kuhusu Prof. Ibrahim Lipumba.

Mkoani Morogoro mwandishi alishuhudia wazee kwa vijana wakijadili hotuba za Prof. Lipumba na kuhoji lini angetembelea mkoa huo.

Mzee mmoja maarufu mkoani humo ambaye ni mstaafu wa shirika moja maarufu alikutwa na ANNUUR akiulizia kuwasili kwa Profesa Lipumba mkoa wa Morogoro katika moja ya vikao vya wapenzi wa CUF kilichopo katika eneo la stendi katikati ya mji huo.

Wakazi wengi wa mkoa wa Morogoro tangu kuibuka kwa Prof. Lipumba na hotuba zake wamekuwa katika pilika pilika ya kujiunga na CUF huku kadi za chama zikiwa zimezagaa maeneo kadhaa ya mji huo.

ANNUUR ilishuhudia kundi la watu katika eneo la Misufini likingoja kukata kadi za chama hicho.

Mkoani Dodoma hali ni hiyo hiyo ambapo baadhi ya maeneo ya mji huo makundi ya watu yamekuwa yakijadili uwezekano wa CUF kuipiku CCM katika uchaguzi ujao wa Rais.

Mazungumzo makubwa ni juu ya hotuba nzito zinazogusa hali ngumu ya maisha waliyonayo Watanzania hivi sasa ambazo Profesa Lipumba amekuwa akizitoa katika mikutano yake ya hadhara katika maeneo mbalimbali jijini na mikoa ya jirani.

Nako mkoani Kigoma mwandishi wetu anaeleza kwamba wenyeji wa mkoa huo wamekuwa wakimsubiri kwa muda mrefu mtaalam huyo wa uchumi wa kimataifa.

Mazungumzo kuhusu Profesa Lipumba yametawala zaidi maeneo ya Ujiji, Gungu na Mwanga ambamo upenzi wa siasa za mabadiliko umetawala mkoani humo.

Profesa Lipumba amewagusa wananchi wengi kwa umahiri wake wa kuchambua matatizo ya kiuchumi yanayoikabili nchi.

Mvuto wa mtaalam huyo huenda ukawa tishio kwa chama tawala hivi sasa ambacho wananchi wengi wanawaona "vigogo" wake ni mabingwa wa siasa za udhibiti.

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook