Na Mwandishi Wetu
WAZANZIBARI wiki hii wamekubaliana kurejea katika mahusiano ya zamani huku viongozi wazito wa nchi wakishindwa kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Mbele ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Chifu Ameka Anyaoku, wananchi hao waliafikiana kuishi kwa kufuata misingi ya haki na kuheshimu demokrasia.
Wengi walitazamia jambo zito la mwafaka wa pande mbili zilizokuwa na mgogoro uliotishia "episode" kama ya Rwanda, ungeshuhudiwa na viongozi wazito wa nchi hii.
Hata hivyo, hali haikuwa hivyo Juni 9 (juzi) mwaka huu wakati wa kutiwa saini muafaka huo mjini Zanzibar.
Hakuwepo mwasisi wa Muungano ambaye pia ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, hakuwepo Rais wa nchi, vigogo wengine wa CCM wala Marais wastaafu wa Zanzibar.
Watu wengi walionyesha kushangazwa na hatua ya viongozi wa juu kutohudhuria jambo hilo la kihistoria ambalo wengi wamelieza kuwa limeepusha shari ya mauaji yaliyoinyemelea sehemu moja inayounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wadodosaji wa mambo wameeilezea hali ya viongozi wakuu wa nchi kutohudhuria muafaka kwamba imeitia dosari Tanzania mbele ya nchi za Jumuiya ya Madola.
Wamesema kama hazipo sababu za msingi kwa viongozi hao kushindwa kuwepo siku hiyo, watakuwa wameweka mashaka makubwa kwa wananchi hasa ikizingatiwa kwamba siku chache zilizopita Baba wa Taifa na Rais Benjamin Mkapa walikuwa miongoni mwa watu walioshuhudia kuapishwa kwa Rais mpya wa Nigeria Jenerali Obasanjo.
Kwa mujibu wa wanasiasa; muafaka wa CUF na CCM Zanzibar umeweka matumaini mapya kwa Wazanzibari kuweza kusimama pamoja kutetea maslahi ya nchi yao.
Wananchi wa Zanzibar kwa umoja wao wana mambo yanayowaunganisha ambapo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekuwa wakiyadai muda wote wa Muungano licha ya tofauti zao za kisiasa. Mambo hayo ni pamoja na haki ya kuwa na serikali yao kamili na kujitawala kama Taifa huru.
Wananchi wengi wa Zanzibar wameuchukulia muafaka huo kama ni mwanzo wa safari ndefu na nzito ya kuirejesha nchi yao katika utamaduni wa asili wa" Zanzibar ni njema anaetaka na aje".
Hata hivyo, wananchi hao wameonyesha wasiwasi kwamba huenda juhudi zao za kuleta umoja wa kitaifa zikakwamishwa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi yao.
Wamesema siku ya muafaka wamejifunza mengi ambayo hapo kabla hayakuwa wazi kwa wengi hasa waliokumbwa na wimbi la ushabiki wa vyama.
Baadhi ya vijana walisikika wakidai kwamba sasa wamewajua "wachawi" wanaoroga umoja, amani na maendeleo ya nchi yao.
Vijana wengi wa Kizanzibari walioko vyuoni na mashuleni siku nzima ya juzi walikaa madarasani huku mioyo ikiwa imeelekezwa Zanzibar na wengi walionyesha nyuso za shauku na furaha.
Wazanzibari wengi wamedai kutosahau katika kumbukumbu zao kushindwa kuhudhuria viongozi katika muafaka huo huku baadhi ya ya viongozi hao wakiwa maarufu katika usuluhishi wa migogoro ya kimataifa.
--
|
|