JAALIA mtu akukate mkono wako kisha akurejeshee vidole halafu aone kakusaidia! Au akuvunje mguu halafu akupe gongo au bakora uchechemelee halafu ajigambe kuwa kakufadhili!
Mwanafunzi Chuki Athumani alipigwa risasi mwaka jana katika tukio la Mwembechai ambapo Waislamu kadhaa waliuliwa.
Taarifa rasmi ya serikali ilidai kwamba mtoto huyo alipigwa risasi kwa vile alikutwa na makaratasi ya uchochezi.
Lakini serikali hiyo haikueleza kilichotangulia nini; kupigwa risasi au kukamatwa na makaratasi hayo. Lakini pia mpaka leo makaratasi hayo hayajafikishwa mahakamani
Chuki Athumani risasi aliyopigwa ilivunja sehemu ya mfupi eneo la kifuani ikawa kipande cha mfupa kinakandamiza mishipa ya fahamu katika uti wa mgongo (Spinal cord).
Hiyo ilikuwa ni kwa mujibu wa uchunguzi wa awali na hivyo maelekezo yalikuwa kufanyika uchunguzi zaidi ambao ingepelekea kuondolewa kipande hicho cha mfupa kisiendelee kukandamiza mishipa ya fahamu. Kilichoendelea ni kuwa mtoto huyo alifungwa pingu kitandani na watu kuzuiliwa kumwona.
Gazeti la Nipashe la Februari 18, 1998 lilieleza kwamba wauguzi walishindwa kumpeleka Chuki Athumani kwenye chumba cha uchunguzi kwa sababu kafungwa pingu kitandani.
Gazeti hilo lilitoa picha inayowaonyesha wauguzi hao wakiwa hawana la kufanya ila kumtizama tu mgonjwa wao kwa jicho la huruma.
Kilichofuatia ni Chuki kupooza na kupoteza kabisa fahamu katika sehemu zake za chini na akawa hapewi tena matibabu yoyote ya tatizo hilo la msingi.
Lakini pamoja na kupooza huko akaendelea kufungwa pingu na huku ndugu na jamaa zake wakizuiliwa kukaa naye kumpa msaada.
Matokeo yake mifupa ikakaribia kuwa nje kutokana na madonda yaliyotokana na kukosa msaada wa kuhudumiwa akiwa na hajandogo na kukalia sehemu moja muda mrefu.
Wakati wauguzi wanashindwa kumtibia Chuki kwa kufungwa pingu na wakati anaendelea kukatika madonda kwa kukosa msaada, serikali iliibuka na dai kwamba wapo vijana waliofundishwa kuleta vurugu na ilionekana vijana hao ni hatari sana kiasi kwamba risasi za moto za polisi zisingetosha tena ila zitumike zile za jeshi la wananchi (Tazama gazeti la watu makini Mtanzania No. 706 la Februari 20, 1998 na gazeti la nguvu ya Hoja, Rai No. 225 la Februari 19, 1998). Na maamuzi haya kuelezwa kuwa yalifikiwa katika vikao vilivyoendeshwa chini ya Uenyekiti wa Rais Benjamin William Mkapa.
Hapana shaka kwa hatari hiyo iliyodaiwa kuwepo Chuki akaendelea kufungwa pingu na kuota madonda. Tusingetarajia huruma kwa mtoto huyu kutoka serikalini kwa vile ishasema hakuna cha "mswalie..." lakini ni usalama gani ungehatarishwa na mtoto huyu aliyepooza?
Kama suala pekee ni usalama wa nchi; mtoto chini ya miaka 18, kisha kapooza hatari gani angeliletea Taifa hata ikalazimika afungwe pingu bila ya huruma bila kujali kwamba atakosa matibabu?
Miezi minne baada ya Chuki kupooza na huku akiendelea kufungwa pingu; gazeti hili lilihoji; "Ni kitu gani hasa serikali inanufaika iwe ni kisiasa au usalama wa nchi kwa Chuki Athumani kuteseka hospitalini akiwa kapooza miguu huku akiwa bado kafungwa pingu. Manufaa gani hasa serikali inapata kwa Chuki kuota vidonda kwa vile kafungwa pingu na hana mtu wa kumsaidia kumgeuza na kumbadili nguo mara kwa mara kama hali yake inavyohitaji!
Manufaa gani hasa serikali inapata kwa Chuki kuendelea kukosa matibabu stahiki, zaidi ya kujenga hisia kwamba kuna watu wanafurahi Waislamu wakiteseka.
Usalama gani wa nchi hii mtoto huyu wa umri wa miaka 17 anahatarisha hata afungwe pingu pamoja na kupooza kwake kutokana na risasi alizopigwa na polisi wa serikali!
Usalama gani wa serikali hii anauhatarisha! Kwamba mtoto huyo wa miaka 17 kaonekana hatari sana anatengeneza pengine mabomu ya kuua au kupindua serikali!
Hata kama ni jambazi lililoua, si anatibiwa kwanza akipona ndio umshitaki! Hata kama mwisho wake, itakuwa kuhukumiwa kunyongwa! Huu ndio utaratibu duniani kote".
Walikuwepo watu walioona huruma wakataka kumpeleka mtoto huyo nje akatibiwe. Taasisi moja ya Kiislamu ilishaanza kufanya mawasiliano na Wizara husika pamoja na kuandaa taratibu za kufungua 'Account' benki ya kupitishia michango. Mipango hiyo ilivia kwani wenye fedha zao walitishwa na wakaogopa.
Awali serikali ilikuwa imedai kwamba suala la Mwembechai lina harufu ya siasa na kwamba Balozi za nje zinahusika. Lakini baadae serikali ikadai kwamba ni wafanyabiashara na ikawaonya.
Wakati huo huo mfanya biashara mmoja akawa anasota rumande kwa kutuhumiwa kwamba alikuwa anawapa misaada wanaotuhumiwa "kuhatarisha amani".
Kwa mazingira hayo hakuna tena aliyethubutu kusaidia matibabu ya Chuki nje ya nchi. Japo wasamaria wema waliendelea kumnunulia asali ambayo kwa Tawfiiq ya Allah (s.w.) ndiyo iliyoponyesha vidonda.
Zimetujia habari kwamba serikali ama ina mpango au tayari ishamnunulia Chuki pikipiki ya tairi tatu (Motorcycle) japo hajakabidhiwa. Vyanzo vyetu vingine vya habari vimedai kwamba kipikipiki hicho kishasajiliwa na kupewa No. TZN 7431.
Awali wauguzi na madaktari walipotaka kumtibia Chuki alifungwa pingu kitandani na pengine kwa bahati isiyotarajiwa ikawa mwenye funguo za pingu hapatikani anapohitajika.
Watu wakapiga kelele afunguliwe pingu na atibiwe serikali nayo inazidisha vitisho vyake. Je, nia ilikuwa afikie hatua hii? Leo ndio serikali inazindukana kwamba naye ni binadamu mwenye kuhitaji kutendewa haki na usalama wa maisha yake kutohumiwa?
Baada ya kupewa kibaskeli aendee wapi, akacheze mpira kama zamani, aendee shule, aendee Kariakoo shimoni kuuza dagaa na pilipili hoho au afanye nini sasa kwa maisha yake baada ya kupooza!
Lakini huyu katiwa kilema
cha maisha bado anapumua. Na wale waliouliwa je? Damu yao ndio imemwagwa
bure bure tu!
--
|
|