Na Abu Halima Sa Changwa
BIN-ADAM (mtu) ana sehemu kuu mbili katika ukamilifu wake ambazo zinategemeana katika maisha yake. Sehemu hizi ni mwili (body) na roho (soul). Sehemu hizi mbili pamoja zinafanya kile kinachoitwa nafsi. (Nafsi = mwili + roho).
Sayansi inayohusu uzima (ubora) na maradhi ya mwili imejaa duniani na kuna mahospitali mengi na tiba aina anuai za kisasa na kijadi. Ama sayansi inayohusu uzima (ubora) wa roho na maradhi yake imekuwa adimu mno, hasa katika wakati wetu huu tunaoishi, na ndio maana dunia leo ina matatizo mengi ya kimaadili, imejaa ufisadi, dhulma, mauaji na kila uovu. Hata watakatifu wanaoaminika kubobea katika kuwatengeneza (au kuwatibu) watu kiroho wanaonekana kuzidiwa nguvu, na tunashuhudia Masheikh na Maustadh wakipata heshima misibani tu kwa kupewa nafasi za kupiga fat-ha na kuombea dua watu waliokufa, wengi wao wakiwa wamekufa na maradhi tele ya kiroho, baada ya wataalam wa tiba ya mwili kushindwa kuokoa maisha ya marehemu.
Watu wengi sasa hivi husahau kuzilea roho zao na kujali zaidi miili yao tu, labda kutokana na kutojielewa na hususan kutokuelewa kwamba ile sehemu ya roho ni muhimu zaidi kuliko ile ya mwili katika kujenga nafsi.
Tunaweza kuona ukweli wa maelezo haya kwa kuangalia tofauti kadhaa zilizopo kati ya mwili na roho, kama zilivyoonyeshwa katika jedwali lifuatalo.
Mwili
1. Mwili una asili ya udongo.
2 Mwili hutokea kwa kuota ndani ya tumbo la mwanamke baada ya mbegu za uzazi za mume na mke kuchanganyika.
3. Mwili unaonekana na kushikika.
4. Mwili unaathirika na nguvu za uvutano za dunia (gravitational force).
5. Mwili huathiriwa na muda (unazeeka na kuharibika au kufa).
6. Mwili unastawi kwa chakula na maji.
7. Mwili una nguvu au uwezo wa kinishati (kitendaji).
8. Wakati wa mauti ya nafsi mwili hurudi kwenye asili yake, yaani udongoni.
9. Maradhi ya mwili na mateso yake hukoma (huisha) mtu anapokufa.
Roho
Roho inatoka moja kwa moja kwa Allah (s.w.).
Roho hupulizwa ndani ya mwili kwa uwezo wa Allah (s.w.).
Roho haionekani na haishikiki.
Roho haiathiriki na nguvu ya uvutano wa dunia.
Roho haiathiriwi na muda (haizeeki wala haifi).
Roho inastawi kwa ibada na mambo mema.
Roho ina nguvu au uwezo wa kifikra na hutoa msukumo wa kiutendaji kwa mwili.
Wakati wa mauti ya nafsi, roho hurudi kwenye asili yake, yaani kwa Allah (s.w).
Maradhi ya roho na ubaya wake hubaki kwenye roho na kwenda nayo kwa Allah (s.w.).
Baada ya kupitia tofauti hizo za mwili na roho, tunapata picha kwamba ili nafsi itengemae vema, mtu hahitaji sayansi ya matunzo na tiba ya mwili tu pekee, bali pia anahitaji sayansi ya matunzo na tiba ya roho, au kiufasaha zaidi sayansi ya maadili ('ilmil-akhlaaq).
Katika mlolongo wa dondoo
zetu za kisaikolojia tutaangalia maradhi ya aina kwa aina ya roho na tiba
zake InshaAllah.
--
|
|