MAKALA
 
Mteja mfalme, mpiga kura je?
 

Na Abu Kalam
 

MFANYABIASHARA awe mkubwa au mdogo tamaa yake ni kuona bidhaa zake zinanunuliwa. Kadri bidhaa nyingi zinavyonunuliwa ndivyo anavyopata faida zaidi na ndivyo anavyokua kiuchumi. Kwa uhusiano huu mnunuzi ana nguvu dhidi ya muuza nyanya au mchuuzi wa sabuni na mwenye hoteli. Ndio ukaibuka msemo "mteja ni mfalme".

Hivi karibuni ulimwengu umeshuhudia aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel Bwana Benjamin Netanyahu akitolewa madarakani kwa nguvu ya kura. Pamoja na juhudi zake za dakika za mwisho kutosheleza matashi yake ya kukalia kiti kwa kipindi cha pili, lakini nguvu ya wapiga kura haikumruhusu. Si kwa Netanyahu tu lakini kwa kila mwanasiasa mtamani kiti (kupitia kura), wenye uwezo wa kutoa kura wana nguvu.

Kwenye ulimwengu huu wa uchumi huria, mfanyabiashara anachaguo moja tu: Kuwaridhisha wateja wake kwa kila hali ili wasimkimbie. Na kama itatokea bahati mbaya akawakasirisha atachukua juhudi hata kuingia gharama kubwa kuomba radhi. Anafanya hivyo kwa sababu wateja wake wanaweza kuua uhai wake kiuchumi pamoja na umaarufu wake katika jamii.

Inapotokea kinyume chake kwamba mteja akageuzwa pakacha la kujaza kejeli, matusi, dharau na masimango na bado uhusiano wa muuzaji na mnunuzi ukaendelea basi lipo tatizo zito la kutisha. Watu kuwa na macho hawaoni kwayo, kuwa na masikio hawasikii kwayo na kuwa na nyoyo pamoja na akili lakini wanaishi zama za utumwa na akili za kushikiwa. Unacharazwa bakora na kulishwa makombo lakini huthubutu kutoroka kwa Bwana wako. Unatukanwa "hewala Bwana", unadhani kutukanwa ndio ishara ya kupendwa zaidi! Kuwepo kizazi cha aina hii katika wakati huu tukielekea karne ya 21 ni msiba usio na mfanowe.

Tofauti na mfanyabiashara, mwanasiasa anaweza kutumia mabavu na fedha kupata kura.

Mabavu yaweza kutumika kuwatisha watu au kutumia vyombo vya dola kupora kura. Wapiga kura hata wakimpa x% matokeo rasmi yatakuwa Y%.

Fedha pia zinaweza kuhusika kuwanunua wapiga kura na wasimamizi wa kura. Hata hivyo kadri demokrasia na uwazi katika siasa za kitaifa na kimataifa unavyopanuka na kukomaa mabavu na fedha zinapoteza nguvu yake dhidi ya nguvu ya wapiga kura.

Kwa mwelekeo huu ukitamani kura ni lazima ujue na bei ya nguvu ya wapiga kura wako. Bei hapa ni msemo tu lakini kinachokusudiwa ni vipi utawaridhisha wapiga kura wako wakuone unafaa kuliko wengine kama ambavyo mteja aweza kwenda masafa kununua sukari duka fulani kwa vile lililopo jirani pamoja na sukari linauza "stella" na "kuvumbua dhahabu".

Ukiona mtamani kura hajali kuyaangalia yale yanayowakera wenye nguvu ya kura basi yapo mambo kadhaa anayotegemea. Ama wapiga kura hao ni wachache sana kiasi kwamba hata wasipompa wote basi haimuathiri kitu.

Lakini muhimu zaidi anaegemea ujinga wa wapiga kura hao. Kwamba kwa upofu wa watu hao hawaoni nguvu waliyonayo. Huwachukulia kama kambaku lenye mapembe makubwa na kilo nyingi lakini huswagwa na mtoto asiyeweza kubeba japo kilo kumi za nyama.

Kwa ujanja wake katika medani za siasa atawaswaga apendavyo, lakini siku ikifika atawalambisha tamutamu, akawalaghai kwa hili na lile na pamoja na kuwa zipo sabuni nyingi za kuogea akawahadaa na wakakubali kwamba ukiogea nyingine zaidi ya ile yake mizimu itakasirika na mazimwi kuivamia nchi.

Kama ilivyojanga kuwa na wateja wale ni janga na msiba mzito zaidi kuwa na wapiga kura wanaodhaniwa kuwa wajinga wa kiwango hiki. Bora basi iwe ni dhana, lakini itakapokuwa ni kweli nusra itoke wapi tena maana watu wa aina hii labda Mitume ndio wanaoweza kuwaokoa na leo hawaji tena!

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook