MAKALA
 
Hamkuwaelewa Masheikh wenu ?
 

Na Abu Kalam
 

Imam Muhammad Idris al Shafii:
 

IMAM Shafii alizaliwa mwaka 150 A.D. huko Gaza katika ukanda wa Pwani wa bahari ya Meditteranean. Yeye ni wa kabila la Quraish.

Akiwa bado kijana, Imam Shafii alihifadhi Qur'an na kitabu cha Imam Malik al-Muwatta. Alisoma elimu ya sheria ya Kiislamu toka kwa Mwanachuoni mashuhuri na Mufti wa Makka Muslim bin Khalid al-Zanji. Baada ya kifo cha Khalif; alikwenda Madina ambapo alisoma kwa Imam bin Anas na Imam Malik. Wakati Imam Malik anafariki tayari Imam Shafii alikuwa ashavuma ndani ya Arabuni na kwingineko kwa ujuzi wa elimu ya sheria ya Uislamu kwa ujumla.

Kufanya kazi serikalini

Kutokana na elimu na uadilifu wake, Imam Shafii aliteuliwa kufanya kazi serikalini. Hata hivyo hakudumu kwani kwa uadilifu na utendaji wake wa kazi kwa haki aligongana na wakuu wa serikali wasiotaka haki.

Alikamatwa na kuhamishiwa Iraq akiwa amefungwa minyororo kwa shutuma kuwa anafanya uchochezi dhidi ya serikali. Huo ulikuwa mwaka 187 A.H (803 A.D.) wakati wa utawala wa Harun al - Rashid. Baadaye aliachiwa huru kwa kuonekana hana hatia. Alibakia kwa muda Baghdad akisoma chini ya wanafunzi wa Imam Abu Hanifah. Alifanya safari kadhaa kuendesha darsa Makka na akapata wasikizaji wengi akiwemo Imam Ahmad bin Hanbal ambaye wakati huo alikuwa anasoma Makka.

Pamoja na kuwa alikuwa na maoni ya Kifiqhi tofauti na yale ya Imam Malik na Hanafi aliwaheshimu na kuthamini juhudi na mchango wao. Hakujenga kundi la Shafii dhidi ya Maimamu wengine kama ambavyo baadhi ya Masheikh hufanya hivi leo.

Maimamu ambao tunajinasibisha nao hivi leo wao walikuwa wamoja katika Uislamu. Pale walipokuwa na maoni tofauti katika ufahamu wa baadhi ya mambo walikubaliana kutofautiana, wakazikubali tofauti zao, lakini wakabaki kuwa wamoja walioshikamana katika dini ya Allah.

Kazi kubwa ya kufundisha na uandishi Imam Shafii aliifanyia Misri katika mji wa Cairo ya leo. Huko alizungukwa na wanafunzi na wanachuoni toka sehemu mbalimbali. Walisoma na kuandika kila alichosema Imam Shafii. Imam Shafii alikuwa na kawaida ya kuwaamrisha wanafunzi wake kusoma kwa sauti kila walichoandika ili apate kusahihisha.

Kazi muhimu zaidi za Imam Shafii ambazo zinaendelea kutoa mchango mkubwa katika elimu ya Fiqh na sheria ya Kiislamu ni Kitab al-Umm na Kitab al-Risalah Fi-Usul-al Fiqh (al-Risalah). Imam Shafii alifariki na kuzikwa Cairo mwezi Rajabu mwaka 204 A.H/20/1/820 A.D. karne 4 baadae ulijengwa mnara mkubwa katika kaburi lake.

Wengi wa Masheikh wa ukanda huu wa Afrika Mashariki hujinasibisha na Imam Shafii. Masheikh hawa huzikubali fat'wa zake kiasi cha kutengeneza dhehebu kwa jina lake.

Lakini Imam Shafii alifuata sunnah ya Mtume (s.a.w.) ya kuwa mkweli, muadilifu na asiyenunulika kwa bei yoyote mbele ya haki. Mtume (s.a.w.) hakutaka cheo cha kupewa na madhalimu. Halikadhalika Imam Shafii hakupatana na viongozi wa serikali wasio waadilifu.

Leo Masheikh wetu wanaojinadi "Sisi Shafii" huona fahari kuteuliwa au kusimikwa kwa nguvu ya dola kuwa viongozi wa Waislamu. Huona fahari kuitwa wakapewa maelekezo yaliyo kinyume na matakwa ya Waislamu. Huona fahari kuwa Makuhani wao. Historia haina kumbukumbu ya Sheikh yeyote aliye mcha Mungu, muadilifu na mkweli ambaye alipendeza mbele ya watawala wasiomtii Allah (s.w.) na Mtume wake.

Ndio hapo tunajiuliza Masheikh hawa walio maswahiba wa viongozi wa serikali, waliwaelewa Masheikh wao?

Mamantilie wanalalamika wanavyodhalilshwa na vyombo vya dola, Masheikh hawa kimya!

Wamachinga wanaporwa vitu vyao na kunyanyaswa, Masheikh kimya! Wananchi wanalalamika kodi zimezidi wakati hakuna huduma baadhi ya Masheikh ndio kwanza wanakusanyana kwa wakubwa kunywa chai na wengine kuleta ngonjera za Ikhtilaf za Jumuiya na taasisi.

Serikali ikichoma nyumba Nzasa au polisi wakiua pale Mwembechai hutawasikia kufunua mdomo. Ngoja wasikie Ansaar Sunnah watatangulia kuswali Idd au watasema Maulid Bid'a. Hapo ndipo ummah utajua kwamba wapo na aya na Hadith wanazijua.

Je; Masheikh hawa wamewaelewa Masheikh wao?

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook