Congress itawafukuza wageni Lejiko - Mtemvu
Mwafrika Jumanne Septemba
25, 1962
"AMRI kali kali zinakuja katika serikali ya TANU ya Jamhuri, kwa hiyo ukipigia kura TANU, unajipalia Makaa ya moto yakuunguze kichwani; pia unakaribisha taabu".
Haya yalisemwa na Bw. Mtemvu, Rais wa Congress katika mkutano wa hadhara juzi mjini Dar es Salaam huko Magomeni.
Akasema: Wapiga kura wakiichagua Congress (wala si Mtemvu labda mnayechukiana), bali hutamwona tena Mzungu au Mhindi ndani ya Baraza la Taifa.
Pia watemi watarudishwa katika utemi wao; sheria za wafanya kazi za kugoma iwapo hawafanywi haki zitarejeshwa; na hata marejinoli kamishna na maarea kamishna ambao hivi sasa ni watumishi wa serikali bali ni macheameni wa TANU wataachishwa kazi hizo.
Ukoloni wa ndani
Kuhusu habari za ukoloni wa kisirisiri uliomo serikali na kuitwa Afrikanaizesheni, Bw. Mtemvu alisema katika kila ofisi ya Waziri, yupo Mzungu anayeitwa 'Staff Officer". Je, kazi ya Mzungu huyo ni nini? Kama si kupeleka habari za siri zenu kwao London? (bomoa!!!!!)
Akasema kwamba TANU haiwezi kuondoa mseto kwa sababu uhuru huu usingepatikana ila kwa sababu TANU imeahidiana na Uingereza mseto uwepo.
Vile vile TANU inaona ugumu kuvunja ahadi zake na ndiyo sababu Wazungu chungu nzima pamoja na Wahindi wamejiandikisha kuwa raia wa Tanganyika. Je, watawezaje kuwabagua ndani ya Baraza la Taifa? aliuliza Bwana Mtemvu.
Kamishna aeleza mafanikio ya mkoa
Mwafrika Alhamisi Machi 12, 1964
REGIONAL Commissioner wa Mkoa wa Pwani Bwana Suleiman Kitundu alipokuwa akihutubia mkutano wa Halmashauri ya maendeleo ya mkoa wa Pwani uliofanyika mjini Dar es Salaam majuzi, Kamishna huyo aliieleza komiti hiyo mipango mbalimbali ambayo ilipangwa mwaka jana na imefanikiwa.
Akianza kueleza kwa sehemu mbalimbali alisema kwamba sehemu ya Kisarawe barabara tatu, shule tano za Lower, Primary, nyumba nne, dispensary moja, barabara nane zenye urefu wa maili sabini na tatu na soko moja.
Makadirio ya majengo haya yanakadiriwa kuwa shilingi 47,410 msaAda wa kupata vitu vilivyojengea ni shilingi 9,400.50 na akiba imekuwa shilingi 38,009.
Katika sehemu ya Mzizima shule mbili za Upper Primary, kisima kimoja, madaraja matatu, nyumba mbili za kukaa watu, stoo moja ya ofisi na mabarabara manne yenye urefu wa maili kumi na nne. Fedha za akiba zilifikia shilingi 43,577.88.
Sehemu ya Mafia ni dispensari moja tu ndio ambayo imemalizika na gharama yake ni shilingi 5,110.32 msaada ulitolewa ni shilingi 1,720.92 na akiba imefikia shilingi 3,390.
Bwana Kitundu aliuambia mkutano kwamba sehemu ya Bagamoyo na Rufiji ni lazima ziongeze juhudi zao na kama hazikufanya hivyo ni wazi ziTarudisha maendeleo yao ya uchumi wa mkoa huu.
Regional Commissioner aliwashukuru vijana wa National Service kwa kusaidia kujenga daraja la Mbwamaji na pia alitoa shukrani zake kwa chama cha Dar es Salaam Football Association kukubali kuchezesha michezo ya mpira ambayo imewezekana shilingi 700 kupatikana.
Mpaka sasa mfuko huo wa maendeleo umefikia shilingi 6,000 ambazo zitatumika kwa mipango mbalimbali.
MafunGu mawili ya misaada
yametolewa kwa sehemu ya makao mapya ya Mafia na Mbwamaji. Mafia imepokea
shilingi 500 na Mbwamaji shilingi 722 kutoka mfuko huo.
Aliyempiga mfumaniwa kaachiwa
OMARI bin Musa, kabila Mpogoro aliyekuwa ameshitakiwa kortini huko Magomeni mjini Dar es Salaam kwa sababu ya kumjeruhi vibaya sana Bwana mmoja wa Kihaya aitwaye Dotratios Karema, aliAchiliwa huru jana na Hakimu Bw. Balozi Rehani, kwamba mshitakiwa huyo alikuwa na sababu ya kutosha ya kumwumiza bwana huyo baada ya kumfumania na mkewe.
Hakimu alitamka kuwa mtu yeyote angekasirika na kuchukua hatua aliyofanya mshitakiwa ya kupigana, kama angemkuta mtu mwingine akizini na mkewe.
Alimwonya mshitaki ajihadhari na tabia ya kutembea na wake za wenzake; alimwonya asiwe na makuu ya kujifanya hajui Kiswahili, kumbe wakati wote alipokuwa akizungumza na bibi huyo alitumia Kiswahili.
--
|
|