MASHAIRI

Enzi Na. 1

Bure mnazuzuka, enzi ni kama maua,
Hayakawi kunyauka, hili ninachanganua,
Chini yakapukutika, mwisho wake hivyo hua,
Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

Maua hunawirika, vizuri yakachanua,
Lakini kubadilika, kupo likawaka jua,
Mwisho yakaja toweka, kana kwamba hayakua,
Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

Msije kughafirika, kudhani zake hatua,
Ni za kudumu miaka, sivyo hivyo nachambua,
Mara hali hugeuka, yakesha nafafanua,
Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

Ole kwenye mamlaka, msije kujifutua,
Enzi mliyoishika, yaweza kujifungua,
Juu mkaporomoka, hadi chini mkatua,
Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

Mwembechai hekaheka, mambo mmeyatibua,
Watu mlivyowafyeka, utadhania mabua,
Bado Ponda mwamsaka, ni mambo ya kushtua!
Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

Itakuja kufutika, enzi mliyochukua,
Nyinyi zidini mahoka, tutakuja washushua,
Mtu cho huanguka, kufumba na kufumbua,
Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.

Mpanda ngazi hushuka, usemi huu murua,
Kiingiacho hutoka, mzima huja ugua,
Enzi huja huondoka, jueni msiojua,
Enzi ni kama maua, hayakawi kunyauka.
 

“Ni Mkonikoni wa Washairi”,
Abdallah Ahmad Seif (Ngoma Imara),
S.L.P 1786,
Mtaa wa Airport - Dodoma “Jimbo la Kati”.


Kuzaa na kuzaliwa (Kinyale)
 

Yeye wa tangu na tangu, mwanzo mwisho Yeye hana
Mmoja Mwenyezi Mungu, katu mshirika hana
Muumba nchi na Mbingu, na vyote vilojazana
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi kaepukana.

Mfanowe hana Mungu, kiumbe akafanana,
Si watatu kwenye mbingu, baba, roho, wala mwana,
Yangalizuka majungu, sheria kufarakana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi kaepukana.

Halali hachoki Mungu, hasahau Subhana,
Mjuzi wa mambo chungu, yote yalofichikana
Kwenye ardhi na mbingu, hanaye wa kushindana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi kaepukana.

Mlezi Mwenyezi Mungu, atulisha Maulana
mtandazaji mawingu, mmvua zanyesha mwanana,
Minanasi na mikungu, miembe inashonana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi kaepukana.

Kaumba Mwenyezi Mungu, Sura kutofuatana,
China, Mwarabu, Mzungu, rangi zisizofanana,
Kabila za ulimwengu, kilugha zinapishana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi kaepukana.

Razaku Mwenyezi Mungu, Mgawaji kwa mapana,
Atupa pweza na changu, bahari wazaliana,
Michuzi yajaza chungu, Samaki wanoneana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi kaepukana.

Muweza Mwenyezi Mungu, sifaze ni nyingi sana,
Nemaze kwako na kwangu, tele zimerundikana,
Kuhesabu kwa mafungu, idadi yashindikana,
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi kaepukana.

Beti nazifunga pingu, mwisho ninatulizana,
Nawapisha na wezangu, sitaki kusema sana,
Waseme sifa Mungu, wazame wendo kwa kina’
Kuzaa na kuzaliwa, Mwenyezi kaepukana.
 

Idd S. Kikong’ona
Morogoro


Tubadili Tabia
 

1.Bismillahi jalali, usopungukiwa fani,
Mjuzi wa kila hali, umekosa mpinzani,
Kwa mujibu wa Rasuli, Akhera na duniani
Tuzibadili tabia, Ukimwi Una hatari.

2. Ukimwi una hatari, nami asoutambua,
Unaondoa kiburi, Mbishi kuangamia,
Mwisho wake ni kaburi, shimoni kukufukia,
Tuzibadili tabia, Ukimwi una hatari.

3. Ukiukwaa jamani, sio kama malaria,
Haitofaa (Quinini), (Fansidal) nawambia,
Utazidi kuwa duni, muda mrefu ugua,
Tuzibadili tabia, ukimwi una hatari.

4.Tajiri na maskini, wote ni sawa jamani,
Nafuu hawaioni, maradhi ni namba wani,
Kwa pamoja ni sandani, Jenezani kaburini,
Tuzibadili tabia, ukimwi una hatari.

5. Dini kuishikamana, Salama tutaipata,
Zinaa tukaachana, Ndoa hadhi zikapata,
Kondom siyo maana, Vijidudu vinapita,
Tuzibadili tabia, Ukimwi una hatari.

6. Mwenye dini anatisha, itikadi kuishika,
Ana msimamo tosha, kwa jambo lenye mashaka,
Huwezi mshurutisha, mpira ni uhakika,
Tuzibadili tabia, ukimwi una hatari.

7. Bali dini atajali, zinaa ataepuka,
Kukurubia muhali, kitabuni imetoka,
Ataipitia mbali, Haitaweza mfika,
Tuzibadili tabia, Ukimwi una hatari.

8.Kwa herini nawaga, shikeni wenye imani,
Nasema bila Uoga, siyomimi Qur’ani,
Abishae kama boga, Hajawa mtu jamani,
Tuzibadili tabia, Ukimwi una hatari.
 

Said Khamisi Mkama
C/o Zuberi Mtemvu
P.O. Box 65
Sweet Cooner
Mtwara


Tuweni na Istiqama
 

Naanza kwa jina lake, Mola Muumba dahari,
Hakika yeye yupweke, kwa hili lilafakari,
Hakuna mfano wake, ila huu mashuhuri,
Lazima tuwe wakweli, yapasa Istiqama.

Pili natoa salamu, kwale wangu wa linu,
NOLO aliye hitimu, na wengine nifahamu,
NinakiRi muhamu, si kuwa ime hasimu,
Lazima tuwe wakweli, yapasa Istiqama.

Istiqama lazima, kama wewe ni mkweli,
Akina baba na mama, lazima tuyakubali,
Ni kauli ya Karima, siwe na nafsi mbili!
Lazima Istiqama, kama wewe Muumini.

Achana na unafiki, Muislamu wewe vipi!
Mbona hutambuliki, biskuti au pipi?
Kuku au mishikaki, bora sema sasa kipi?
Achana na unafiki, lazima Istikama.

Elfu mbili nafika, lazima kuhamasisha,
Vibudu vilivyo chuka, achana navyo si hasha,
Tafuta kisicho chuka, kilicho ndani ya kasha,
Lazima tuwe wakweli, Istiqama ni njema.

Lililopita sindwele, sasa tungange lijalo,
Sio tupige kelele, tulishike sasa hilo,
Hakuna tena sumile, chakua ulitakalo,
Kama wewe umuumini, lazima Istiqama.

Hapa na keti uchani, kwanza nataka pumua,
Ilah Mola Manani, utupe nyingi afyaa,
Na pia tupe afweni, kama tumodhamiria,
Lazima tuwe wakweli, tuweni na Istiqama.

Rashidi N. Moh’d (Mdabi)
S.L.P. 55105
Dar es Salaam
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook