Mtume (s.a.w.) ametukumbusha sote kuwa kila mtu ajue kuwa ni kiongozi anayewajibika juu ya wale anaowaongoza na hapana shaka ya kuwepo maulizo ya Allah (s.w.) juu ya uwajibikaji wake juu ya wale anawaongoza kwa mujibu wa Hadith ifuatayo.
Abdullah bin Umar (r.a.) amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: "Kila mmoja ni mchunga (kiongozi) na kila mmoja ataulizwa juu ya wale aliowaongoza. Imam (kiongozi wa jamii) ni mchunga wa watu anaowaongoza na ataulizwa juu yao. Mwanamume ni kiongozi wa familia yake na ataulizwa juu ya watu wa familia yake. Mwanamke ni malkia wa nyumba ya mume wake na watoto na ataulizwa juu yao. Mtumushi ni mchunga wa vitu vya mwajiri wake na ataulizwa juu ya vitu hivyo. Sikilizeni! Hakika kila mmoja ni mchunga (kiongozi) na ataulizwa juu ya wale aliowachunga (aliowaongoza)" (Bukhari na Muslim)
Katika Hadith hii tunajifunza kuwa kila mtu ni kiongozi na kila kiongozi anao wajibu kwa wale anaowaongoza. Katika kipengele hiki tumejaribu kubainisha wajibu wa viongozi wa Kiislamu kama ifuatavyo:
1. Ucha-Mungu
Kwanza, kiongozi ajitahidi kujikurubisha kwa Allah (s.w.) zaidi kwa kuzidisha swala za nawafil, funga za sunnah, kutoa sadaqa kwa wingi, kuomba dua na maghfira kwa wingi ili kupata msaada wa Allah (s.w.). Kwani kazi ya uongozi ni nzito mno inayohitajia sana msaada wa Allah (s.w.). Pia kiongozi wa jamii ya kiislamu anawajibika kuzidisha kusoma Qur'an na Hadith ili aweze kufanya kazi yake kwa kuchunga mipaka ya Qur'an na Sunnah na pia aweze kujipamba na mwenendo mwema uliosisitizwa katika Qur'an na Hadith. Kiongozi wa Kiislamu hana budi kujitahidi kuwa kiigizo kwa ucha-Mungu kwa kutekeleza vilivyo maamrisho yote ya Allah (s.w.) na kujiepusha na makatazo yake yote. Ucha-Mungu ni zana muhimu sana inayomwezesha kiongozi kutekeleza wajibu wake vilivyo.
2. Huruma
Kiongozi awe mnyenyekevu, mpole, mwenye huruma - kuwahurumia wale anaowaongoza na mwenye kuwapendelea lile analolipendelea katika nafsi yake. Kiongozi anatakiwa daima kuwa yeye ni mtumishi wa wale waliomuweka katika uongozi, awaheshimu kama mtumishi anavyomuheshimu bwana wake. Wakati huo huo, kiongozi anatakiwa ajiweke katIka nafasi ya ulezi ambayo hana budi kuwahurumia wale anaowalea. Kiongozi wa Kiislamu daima anatakiwa azingatie usia wa Allah (s.w.) ufuatao:
Naye ndiye aliyekujaalieni kuwa Makhalifa (viongozi) katika ardhi. Na amewanyanyua baadhi yenu juu ya wengine daraja kubwa kubwa ili akufanyieni mtihani kwa hayo aliyokupeni. Hakika Mola wako ni mwepesi wa kuhisabu na hakika yeye ni mwingi wa kusamehe, mwingi wa kurehemu.(6:165)
Kutokana na aya hii tunajifunza kuwa kiongozi anatakiwa mara zote afahamu kuwa wadhifa wa uongozi alio nao ni mtihani kwake. Allah (s.w.) amemuinua daraja na kumfanya kiongozi juu ya wengine ili kumfanyia mtihani kuwa atashukuru neema hiyo aliyotunukiwa na Mola wake kwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo na kuchunga mipaka ya Allah (s.w.) katika kazi hiyo au atakufuru ajipe uungu kwa kuchupa mipaka ya Allah na kuwageuza watumwa wake wale waliomchagua na kumfanya kiongozi wao. Kiongozi anatakiwa awe msaada na rehema kwa wale anaowaongoza na wala asiwe mzigo na tatizo kwa raia zake hao. Mtume (s.a.w.) kila alipowachagua sahaba zake kuwa viongozi wa mahali mbalimbali daima alikuwa akiwausia kuwa watu wa msaada wenye huruma na upole kwa raia zao.
3. Uadilifu
Kiongozi wa Kiislamu anatakiwa awe muadilifu. Kipimo cha kiongozi mzuri ni uadilifu. Kiongozi wa Kiislamu akiwa muadilifu huwa Khalifa wa Allah (s.w.) na akiwa si muadilifu huwa Khalifa wa Shetani. Uadilifu unasisitizwa mno katika Qur'an kama tunavyojifunza katika aya ifuatazo:
Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamia uadilifu, mtoao ushahidi
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi
wenu, au jamaa. Akiwa tajiri au masikini. (4:135)
Na mnapo hukumu baina ya watu, hukumuni kwa uadilifu..... (4:59)
Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu....... (16:90)
Kiongozi muadilifu ni yule anayechunga haki za watu anaowaongoza. Yeye ni mchunga na mgawaji wa haki. Hana budi kuhakikisha kuwa yeye mwenyewe hachukui haki zake mpaka ahakikishe kuwa kila mtu amepata haki yake. Mtume (s.a.w.) aliwaamuru wale aliowapa kazi ya uongozi kuliko watu wengine, wala wasivae kivazi kizuri zaidi, wasifunge milango yao wakati watu wanawahitajia haki zao au wanataka kutoa madukuduku yao.
Kiongozi wa Kiislamu anatakiwa awe muaminifu na mkweli na asithubutu kujilimbikizia mali kwa kutumia madaraka yake ya uongozi. Amir au kiongozi wa juu wa Serikali ya Kiislamu anatakiwa achukue mshahara au posho kutoka kwenye mfuko wa serikali (Baitul-mali) kiasi kile tu kinachotosheleza mahitaji muhimu ya chakula, mavazi na makazi kwa yeye mwenyewe na familia yake. Kiongozi wa Kiislamu anatakiwa akumbuke daima kuwa uongozi katika Uislamu si kitega uchumi kama ulivyo uongozi wa Kitwaghuti. Mtume Muhammad (s.a.w.) ambaye ndiye kiongozi wa Ummah huu wa mwisho na kiigizo chetu kwa mwenendo na uongozi wake bora, aliishi maisha rahisi.
Abu Bakar (r.a.) alichaguliwa kushika uongozi wa Umma wa Kiislamu mara baada ya kutawafu Mtume (s.a.w.), alifuata nyayo za Mtume (s.a.w.) kwa kila kitu. Maisha yake yalikuwa rahisi mno. Umar (r.a.) aliyechaguliwa kuwa kiongozi wa serikali ya Kiislamu baada ya Abu Bakar alifuata vyema nyayo za uongozi wa Mtume (s.a.w.) na ule wa Abu Bakar. Pamoja na kuwa Umar alikuwa kiongozi wa Dola kubwa ya Kiislamu iliyoenea mashariki ya kati yote na kupanuka hadi Spain, aliishi maisha rahisi sana. Umar (r.a.) alikuwa na kawaida ya kuzunguka usiku ili kujua matatizo ya watu wake.
Kinyume chake viongozi wa Kitwaghuti, huchukua madaraka ya uongozi wanaopewa na jamii zao kama kitega uchumi chao kwa ajili ya kujinufaisha wao binafsi. Huifuja watakavyo na humpa yeyote wamtakaye kwa upendeleo mali ya jamii ambayo imepatikana kwa kukung'uta mifuko ya masikini. Muda mfupi baada ya kiongozi wa Kitwaghuti kukabidhiwa madaraka ya uongozi wa ngazi ya juu katika jamii, utamuona ana gari zuri jipya ana nyumba nzuri mpya, ana miradi huku na kule na mabadiliko ya kila namna katika matumizi yake ya kimaisha pamoja na familia yake.
Kama mambo yenyewe ni haya, kwa nini watu wengine katika jamii ya Kitwaghuti wasiupupie uongozi kwa hali na mali au kwa kufa na kupona? Kwa nini mtu aliyeonja uongozi katika serikali ya Kitwaghuti asing'ang'anie kubakia humo kwa gharama yoyote ile? Kwa nini mapinduzi ya mara kwa mara, rushwa na mauaji yasitegemewe katika jamii za Kitwaghuti ambapo watu wanashindania uongozi kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi? Haya yote ni matunda machungu yanayotarajiwa katika jamii kutokana na uongozi uliokosa uadilifu.
Kiongozi muadilifu hana budi kuhakikisha kuwa wanyonge katika jamii wanapata haki zao na wenye mali wanatoa haki za wanyonge. Abu Bakar, katika khutuba yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Khalifa wa kwanza wa Mtume (s.a.w.) alisisitiza:
"Mnyonge miongoni mwenu ni mwenye nguvu katika uongozi wangu mpaka apate haki zake; na mwenye nguvu miongoni mwenu atakuwa dhaifu katika uongozi wangu, mpaka akipenda Allah nichukue haki za watu anazodaiwa..."1
Vile vile ni katika uadilifu
kwa kiongozi kuhakikisha kuwa kila mtu mkosaji anahukumiwa kwa mujibu wa
sharia bila ya upendeleo au uonevu wowote. Kiongozi hatamchelea yeyote
katika kupitisha hukumu. Katika Uislamu watu wote ni sawa mbele ya sharia
na hakuna aliye juu ya sharia hata akiwa Amir (Rais) wa nchi.
Mwanadamu ameumbwa na mahitajio mengi ambayo hana budi kuyapata ili aweze kuishi kwa furaha na amani hapa ulimwenguni. Kwa kuwa mwanadamu ni mchanganyiko wa mwili na roho, pia mahitajio yake yamegawanyika, anamahitajio ya kiroho na kimwili. Mahitajio ya kiroho ambayo humuwezesha mwanadamu kuishi maisha ya utulivu yenye furaha na amani, hupatikana kwa kufuata kwa utii na unyenyekevu mwongozo wa Allah (s.w.) .
Mahitajio ya kimwili kama vile chakula, mavazi, vipando na njia ya uchumi hupatikana kwa kuchapakazi chini ya mazingira yanayotawaliwa na itikadi sahihi yenye kusimamiwa na viongozi wanaozingatia haki itakayo kwa Muumba. Katika Qur'an tunafahamishwa kuwa Allah (s.w.) amejaalia mali anayoichuma mwanadamu iwe ndiyo inayoboresha maisha yake:
"Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambazo Mwenyezi Mungu amezijaalia kwa ajili ya maisha yenu........" (4:5)
Kutokana na aya hii, kuchuma mali si jambo la hiari kwa mwanadamu kwani kwa namna Allah (s.w.) alivyokadiria,maisha ya mwanadamu kwa hapa ulimwenguni hayawezekani pasi na kuchuma. Ni kweli kwamba vitu vyote vilivyomzunguka mwanadamu katika ulimwengu huu vimeumbwa kwa ajili yake kwa ushahidi wa Qur'an.
"Yeye ndiye aliyekuumbieni vyote vilivyomo katia ardhi......" (2:29).
Lakini mara nyingi vitu hivi haviko katika hali ya kutumiwa na mwanadamu moja kwa moja. Bali mwanadamu analazimika kutumia elimu yake, maarifa yake, juhudi zake na vipawa vyake vingine ili ayabadilishe mazingira yake yaweze kumtumikia na kukidhi haja zake. Kwa mtazamo huu Uislamu unatuamrisha kuchuma kama unavyotuamrisha kusimamisha swala, kutoa zakat na kutekeleza Ibada nyingine kama hizi:
" Na itakapokwisha swala, tawanyikeni katika ardhi mtafute adhila za Mwenyezi Mungu na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi, ili mpate kufaulu (62:10)
Tunajifunza kutokana na aya hii kuwa, kuchuma ni wajibu unaompasa Muislam mara tu baada ya kutekeleza Ibada maalum. Hili linabainishwa katika Hadith ifuatayo:
"Abdullah bin Mus'ud ameeleza kuwa Mtume (s.a.w.) amesema: Kutafuta chumo la halali ni faradhi baada yakutekeleza faradhi nyingine." (Baihaqi).
Pia Mtume (s.a.w.) amebainisha wazi ubora wa kujizatiti katika kutafuta chumo la halali kwenye Hadith ifuatayo:
"Miqdam bin Ma'ad Yakrab ameeleza kuwa Mtume wa Allahamesema: Hapana mmoja wenu aliyekula chakula kizuri kuliko kile alichokula kutokana na kazi ya mkono wake mwenyewe. Na Daudi,Mtume wa Allah, alikuwa anakula kutokana na kazi ya mikono yake" (Bukhari)
Kwa upande mwingine Uislamu unalaani uvivu na kuwategemea wengine pasina sababu au dharura maalum kama tunavyojifunza katika Hadith zifuatazo:
"Jubair bin Awam ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema:Mmoja wenu kuchukua kamba na kisha akaja na mzigo wa kuni akiwa amebeba mgongoni mwake na akauuza, na kwakufanya hivyo Allah akailinda hadhi yake, ni bora kwake kuliko kuomba omba watu, wakimpa chochote au wasimpe(Bukhari).
Mpaka hapo tumejifunza kuwa kwa mtazamo wa Uislam, uchumi ndio msingi wa maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni na Uislam umewajibisha kuchuma kwa kila mwenye uwezo. Ni makosa katika Uislam mtu mwenye uwezo na afya kubweteka na kuwategemea wengine katika kikidhi mahitaji yake.
3. Kanuni za uchumi katika Uislamu
Kanuni kuu za uchumi katika Uislam ni:
(i) Kumwamini Allah kuwa ndiye muumba na mfalme wa ulimwengu huu yaani kumtii Allah katika mambo yote.
(ii) Binadamu ni Khalifa wa Allah hapa duniani, hivyo wajibu wake ni kusimamisha amri ya Allah.
(iii)Ili kumsaidia mwanadamu kutimiza wajibu wake kama Khalifa, Allah amemdhalilishia kila kitu katika ulimwengu huu:
"Mwenyezi Mungu ndiye aliyekutiishieni bahari ili humo zipite merikebu kwa amri yake ili mtafute fadhila yake na mpate kushukuru". (45:12)
"Je, Hukuona kwamba Mwenyezi Mungu amevitiisha kwa ajili yenu vilivyomo ardhini........." (22:65)
"Je, Hamuoni kwamba Mwenyezi Mungu amekutiishieni vilivyomo mbinguni na ardhini na anakukamilishieni neemake zilizo dhahiri na za siri?.................." (31:20).
"Yeye ndiye aliyefanya ardhi iweze kutumika kwa ajili yenu. Basi nendeni katika pande zake zote na kuleni katika rizk zake na kwa yeye ndiyo marejeo." (67:15).
Hivyo kuzitumia neema hizo za Allah si dhambi bali ni katika kushukuru:
(iv) Kutokana na wajibu wa Ukhalifa wa Allah, mwanadamu ataulizwa kwa neema alizompatia na atahesabiwa kwazo, ikiwa ni pamoja na namna alivyochuma na kutumia mali.
(v) Kuwa na mali au kutokuwa na mali nyingi au kidogo si dalili ya ubora au udhalili wa mtu. Hali zote mbili ni mtihani. Anachotazama Allah ni nyoyo za watu.
Misingi au kanuni hizo zikithibiti katika moyo wa mtu zinakuwa na athari kubwa sana katika shughuli za kiuchumi za Muislamu.
Kanuni ya kwanza kwa mfano humfanya mtu afuate maamrisho ya Allah na hivyo atafanya kila njia ajiepushe na makatazo yake.
Pili, kwa kujua kuwa yeye ni Khalifa tu atajua yeye si mmilikaji wa hakika, hivyo atafuata maagizo ya huyo aliyempa ukhalifa yaani Allah.
Tatu, atajua kuwa umaskini si kitu cha kukipigania mtu, bali mtu apiganie maisha bora na afya njema na ajitahidi kutumia mali na afya katika kutafuta radhi za Allah.
Nne, kwa kujua kuwa atahesabiwa na Allah anayeshuhudia kila kitu ataendesha shughuli zake za uchumi kwa kumcha Allah.
4. Sera ya uchumi wa Kiislamu
Katika Uislamu utekelezaji wa mambo yote hutegemea zaidi ucha-Mungu wa mtu binafsi na kuogopa kwake kusimamishwa mbele ya Allah na kuhisabiwa, kuliko usimamizi wa vyombo vya dola kama sheria, mahakama, na askari polisi. Hii ni kwa sababu hisabu siku ya kiyama itakuwa kwa kila mtu binafsi. Hapana shaka vyombo vya dola vipo katika Uislamu na vinafanya kazi lakini msisitizo wa utekelezaji wa mambo yote upo katika uadilifu na taqwa kuliko katika kuogopa polisi na mahakama.
Pili, uhuru wa watu binafsi kufanya wanalolitaka ndio kanuni inayofuatwa katika Uislamu. Yaani katika masuala ya uchumi Uislamu umempa uhuru kila mtu afanye lile analiona linafaa. Na serikali ya Kiislamu haitaingilia uhuru wake huo isipokuwa tu pale ambapo haki haitatendeka iwapo uhuru huo hautaingiliwa. Mtume (s.a.w.) amelielezea kwa ufasaha sana suala hili pale alipoyapigia mfano maisha ya watu katika jamii na wasafiri waliomo chomboni baharini:
"Hebu tuchukue mfano wa meli inayosafiri baharini ikiwa imejaza abiria ambao wamekaa katika sehemu zote za chini na juu. Sasa iwapo abiria mmoja aliyekaa katika sakafu hiyo ataamua kujipatia maji kirahisi kwa
kutoboa pale alipoketi na iwapo abiria wengine watamzuia kufanya hivyo (na ni wajibu wa abiria wote walio juu na chini kumzuia) watamnusuru yeye na wao wenyewe na kufa maji. Iwapo watamwacha atoboe basi watazama wote walio chini na juu ya meli" (Bukhari)
Mfano huu unatuonyesha kuwa japo Uislamu unampa kila mtu uhuru wa kufanya alitakalo lakini uhuru huo una mipaka. Iwapo mtu atafanya jambo lisilo la haki basi serikali ya Kiislamu lazima iingilie kati kwa maslahi ya jamii nzima.
Tatu, wajibu mkubwa wa serikali ya Kiislamu ni kusimamia haki na kuzuia dhulma katika maisha ya jamii.
--
|
|