Na Dkt. Abdallah J. Saffari
MARA nyingi maoni ya shahidi huhitajika kuthibitisha au kukanusha jambo fulani. Hivyo ushahidi wa maoni ya mtaalam wa fani kadha unaweza kutolewa mahakamani mintaarafu ya suala linalobishaniwa.
Kuna aina mbili za wataalam ambao wanaweza kutoa ushahidi. Kwanza ni wale ambao wamepata mafunzo maalum kama vile madaktari, mafundi mitambo, watalaam wa maandishi na wakemia. Pili ni wale ambao ni wajuzi wa fani au mambo fulani kutokana na uzoefu wao tu. Ni kawaida kuwa kabla shahidi mtaalam hajatoa ushahidi wake aeleze alivyoupata utaalam au ujuzi wake (Gathera Njagwara v. R. (1954) 21 E.A.C.A. 384).
Kama ni daktari ataelezea aina ya mafunzo aliyoyapata na mitihani aliyohitimu. Wakati mwingine aina fulani ya uchunguzi wa maoni huweza kutolewa na wataalam wenye kiwango maalum cha sifa tu. Kwa mfano taarifa ya sababu za kifo ni lazima itolewe na daktari, na uchunguzi wa madawa lazima uwe umefanywa na mkemia.
Watu wenye ujuzi kutokana na uzoefu wanaweza kutoa maoni yao katika mazingira fulani fulani (K.h.j). Mfano mzuri ni kuwa mtu yeyote anayeuelewa vyema mwandiko wa mtu fulani anaweza kutoa ushahidi kuhusiana na mwandiko huo hata kama yeye siye mtaalam wa maandishi (F. 49, Sheria ya Ushahidi, i.h.j). Itabidi tu aelezee mazingira ambayo yamefanya auelewe vizuri mwandiko unaohusika kama vile amemuona mhusika akiandika mara kwa mara au amepokea na kusoma hati za mhusika huyo katika shughuli zake za kila siku (F. 49, Sheria ya Ushahidi, i.h.j).
Halikadhalika watu wenye ujuzi wa mila na desturi fulani fulani (F.50(1), Sheria ya Ushahidi, i.h.j) wanaweza kutoa ushahidi wa kitaalam, bila kuthibitisha kuwa walipata mafunzo maalum mintaarafu ya fani hizo.
Ila hakuna wakati ambapo mahakama yatalazimika kukubaliana na maoni ya mtaalam yeyote yule japo awe mjuzi kupindukia. Ni vyema, na si busara kuyakataa maoni ya mtaalam, lakini sio pale ambapo yanaonekana kwamba sio sahihi. Katika shauri la R. v. Agnes Doris Liundi (1980) 1 L.R.T. Na. 107). Jaji Makame alikataa maoni ya mtalaam wa maradhi ya akili Daktari Haule kwamba mshitakiwa alikuwa na maradhi ya akili wakati alipowaua watoto wake watatu.
Maoni ya waandishi wa vitabu japo stadi kiasi gani sio lazima yakubaliwe na mahakama (Donoghue v. Stevenson (1932) A.C. 562, uk. 567).
Utambuzi wa Watu na Vitu
(a) Utambuzi wa Watu
Mara nyingi hutokea ubishi kama mshitakiwa au kitu kinachohusika na mashitaka ni mali ya mlalamikaji au ya mshitakiwa. Hivyo ni muhimu sana kuwa ushahidi wa utambuzi unafanyika vizuri.
Inapotokea mshitakiwa alionekana na mashahidi wengi akitenda kosa ambalo anashitakiwa kwalo kunaweza kusiwe na matatizo hasa ikiwa mashahidi hao wamemfahamu vizuri mshitakiwa kwa muda mrefu. Hata hivyo mazingira ambayo inadaiwa mshitakiwa alionekana akitenda kosa hilo ni jambo ambalo huweza kuleta matatizo makubwa. Ni rahisi kumtambua vizuri mtu wakati wa mchana kuliko usiku. Aidha si rahisi zaidi kumtambua mtu kwa kubaini sura yaani uso wake kuliko kiwiliwili tu au nguo alizovaa.
Pia utambuzi huwa sahihi zaidi kama mtu anayetambuliwa yuko pekee na hakimbii. Hali ya macho ya mtambuzi pia ni muhimu. Katika kesi ya R. v. Mathias Kaondoka na Mwenzake (Shauri maalum la Jinai Na. 58, 1978, Mahakama Kuu, Mbeya (haijachapishwa) shahidi mmoja, Kahwa Hagatwa, mzee wa miaka karibu sabini na tano, ambaye alikuwa baba wa marehemu aliyedaiwa kuuawa na washitakiwa, aliyaeleza mahakama kwamba alimtambua Mathias Kaondoka kuwa ndiye aliyehusika na mauaji ya marehemu mtoto wake. Marehemu alifariki usiku wa tukio hilo wakati nyumba ambamo alikuwa amelala ilichomwa moto kusudi. Shahidi Kahwa Hagatwa aliyaeleza mahakama kuwa wakati amelala usiku wa tukio hilo aliamshwa na kilio cha marehemu mtoto wake. Alitoka kwenye nyumba yake, pamoja na mkewe, wakaelekea kunako nyumba ya mtoto wao marehemu ambayo wakati huo ilikuwa imepamba moto. Na kwamba hatua chache tu karibu na nyumba ya marehemu Kahwa Hagatwa alimwona Mathias Kaondoka amesimama kashika kopo kuangalia moto ulivyokuwa unawaka. Baadaye alikimbia. Mke wake Kahwa Hagatwa naye alitoa ushahidi kutoka kwenye tukio la maafa.
Mashahidi wote hao wawili walidai kumfahamu vyema Mathias Kaondoka kwa vile alikuwa mkwe wao yaani mume wa marehemu mtoto wao. Jaji Samatta aliona muhali kuafiki ushahidi wa mashahidi hao kuwa yule mtu aliyemwona nje ya nyumba wakati wa tukio la mauaji alikuwa Mathias Kaondoka kwa sababu zifuatazo: Kwanza ilikuwa ni usiku wa giza ingawa moto mkali ilitupa miali yake huku na kule. Pili, mashahidi hawakumwona mshitakiwa uso kwa uso. Halafu, jicho la Kahwa Hagatwa lilikuwa bovu. Na ingawa Kahwa Hagatwa mwenyewe alidai kuwa jicho hilo lilikuwa zima kabla ya tukio hilo, mahakama yaliona muhali kuamini kauli hiyo.
Ilikuwa na hakika ya utambuzi katika mazingira yanayofanya utambuzi wa mshitakiwa kuwa mgumu, na hasa mshitakiwa anapokuwa mgeni machoni mwa shahidi anayedai kumtambua, ni vizuri kufanya gwaride la utambuzi. Utaratibu wa gwaride la utambuzi umeelezwa vizuri katika shauri la R.v. Mwango (1936) 3 E.A.C.A. 29).
Kwa muhtasari mambo yafuatayo ni lazima yazingatiwe na msimamizi wa gwaride la utambuzi. Kwanza mshitakiwa ambaye anataka kutambuliwa ni lazima aelezwe nia ya kutekeleza jambo hilo. Na kwamba kama akipenda, anaweza akawa na rafiki au wakili wakati gwaride hilo la utambuzi linafanyika. Pili mshitakiwa awekwe katika mstari wa watu wengi wasiopungua wanane wenye maumbile yanayofanana naye kama vile umri, urefu, na hata rangi (K.h.j). Mtuhumiwa huyo aruhusiwe kukaa sehemu yoyote ile anayopenda katika mstari huo. Na kama kuna mashahidi wa utambuzi zaidi ya mmoja mtuhumiwa aruhusiwe kubadilisha nafasi aliyokuwa amekaa mwanzo.
Masharti mengine yanahusiana zaidi na mashahidi ambao wanatakiwa kufanya utambuzi wenyewe. Ni muhimu mwenye kuendesha, yaani kusimamia gwaride la utambuzi, ahakikishe kuwa shahidi au mashahidi wa utambuzi hawamwoni mtuhumiwa kabla ya gwaride lenyewe. Aidha, waelezwe kuwa huenda wakamwona mtuhumiwa au mshitakiwa ambaye wamguse; asiwaeleze kuwa lazima wamtambue mtu. Na kama kuna zaidi ya shahidi mmoja wa utambuzi, wasiruhusiwe kuzungumza baina yao wakati wa gwaride hilo. Yaani baada ya kila shahidi kukamilisha zamu yake asiongee na wale ambao hawajatekeleza zamu yao. Kama shahidi anataka kumwona mshitakiwa akitembea, kuzungumza, kuvaa au kuvua kofia au kuvaa koti, tai na kadhalika basi aruhusiwe kufanya hivyo ili apate nafasi yakuwa na hakika ya utambuzi anaoufanya. Pengine wakati alipomwona mshitakiwa mara moja tu alikuwa amevaa kofia au alikuwa anatembea. Kuvaa kofia, kutembea au kuzungumza kunaweza kuwa na athari kubwa katika utambuzi kwa vile kila mtu ana namna yake ya kutembea, kuzungumza, yaani sauti na hata kucheka.
Mengine ya kuzingatiwa yanamhusu msimamizi wa gwaride mwenyewe. Haifai awarubuni mashahidi ili wamtambue mtuhumiwa kwa vyovyote vile. Shahidi lazima awe huru na kupewa msaada anaoruhusiwa kumwezesha kutekeleza utambuzi wake kwa usahihi. Ahakikishe kuwa anaandika kumbukumbu iwapo shahidi amemtambua mshitakiwa au la, kila baada ya zamu ya shahidi mmoja. Ili kuwa na hakika ni lazima shahidi amguse mtuhumiwa iwapo amemtambua. Watu wasiohitajika wasiruhusiwe kuwepo katika gwaride la utambuzi.
(b) Utambuzi wa Vitu
Kama vile ilivyokuwa kuwatambua washitakiwa ndivyo ilivyo muhimu pia kuvitambua vitu vinavyohusiana na mashitaka. Kwa bahati mbaya suala la utambuzi wa vitu halipewi uzito unaostahili hasa katika mahakama ya chini. Mara nyingi utambuzi unafanyika kizimbani tu; mshitakiwa anaonyeshwa mali au kitu kilichoibwa na kadhalika na anasema ndiyo hicho hicho. Jambo hili sio sahihi na limesababisha upotevu wa haki. Utaratibu mzuri ni ule ulioelezwa na Jaji Mwakasendo katika kesi ya Fadhili Mohammed v. R. (1974 L.R.T. n.5).
Kwa muhtasari, kila shahidi anayekwenda kutambua mali au kitu kinachohusiana na mashitaka yaliyo mahakamani hana budi kwanza ayaeleze mahakama juu ya alama ambazo zinamfanya aweze kutambua kitu chenyewe. Alama hizo zitaandikwa na Hakimu kama sehemu ya ushahidi wa shahidi huyo. Halafu kitu hicho kitaonyeshwa shahidi ili akitambue rasmi. Katika kufanya hivyo itabidi aonyeshe zile alama alizoelezea kabla. Ni muhimu sana mahakama kuhakikisha shahidi anaonyesha vizuri alama anazodai kuzitambua kitu kinachohusika.
Ushahidi wa Kuambiwa
Ushahidi wa maneno ni lazima utolewe na mtu aliyeshuhudia binafsi jambo linalodaiwa (F. 62, Sheria ya Ushahidi, i.h.j). Kushuhudia ni pamoja na kuona, kusikia, kugusa, kuonja na kunusa. Hivyo basi ushahidi wa kuambiwa haufai kuthibitisha kitu isipokuwa katika mazingira ambayo yataelezwa baadaye kidogo.
Madhumuni ya kutoukubali ushahidi wa kuambiwa ni kuepuka hatari za kupotosha kweli. Mara nyingi sana, kwa sababu mbalimbali, watu hupotosha maana ya mambo waliyoelezwa. Huweza kufanya hivyo kwa kukusudia au kutokukusudia. Kwa mfano mtu anaweza kuamua kutia chumvi maneno aliyoambiwa na mtu mwingine ili kukidhi mradi wake. Pengine anaweza kufanya hivyo kwa nia mbaya tu ya kutaka kumpaka matope mtu fulani. Lakini wakati mwingine mtu hakusudii kupotosha maana ya mambo aliyoelezwa. Inaweza tu kuwa hakusikia au kuelewa vizuri mambo aliyoelezwa na mtu ambaye aliona matukio yenyewe. Na hakika, haiwezekani kumhoji vizuri shahidi kutokana na mambo ambayo ameambiwa na mtu mwingine. Sana sana atakanganyika tu na kutoa ushahidi potofu zaidi bila ya kupenda.
(a) Tamko la Mfaji
Muhimu pia katika mashitaka ya jinai ni ule ushahidi wa tamko la mfaji, yaani maneno ambayo mtu aliyatamka wakati anafariki (F. 34(A), Sheria ya Ushahidi, i.h.j). Masharti yake ni kuwa shahidi anayehusika awe alimsikia marehemu akitoa maelezo kabla ya kifo chake. Na kwamba maelezo hayo yahusiane na mazingira yaliyosababisha kifo hicho (K.h/j.).
Kuruhusu ushahidi wa kuambiwa kutoka kwa aliyefariki kunatilia maanani kweli kuwa sio busara kukataa ushahidi huo kwa vile mtu mwenyewe amefariki. Ila mahakama yataukubali tu ushahidi huo iwapo ni imara, na aghalabu, ingawa sio lazima, mahakama yatapendelea ushahidi huo uungwe mkono na ushahidi mwingine. Yatasita kumtia mtu hatiani kutegemea ushahidi huo pekee mpaka yameridhika na kweli ya ushahidi huo.
La muhimu ni kuona iwapo ushahidi wa marehemu ni wa kuaminika. Na ili kulijibu swali hili mazingira ambayo maelezo au maneno ya marehemu yalitamkwa ni muhimu mno kuzingatiwa. Mambo kama hali ya afya ya marehemu wakati huo, uwezo wake wa kuona (R. v. Mathias Kandoka na Mwenzake, i.h.j) , kusikia, uhusiano wake na mtu anayemtaja kuhusiana na kifo chake, ni baadhi tu ya mambo muhimu kuangalia kwa makini mno. Mathalan katika kesi R. v. Mathias Kaondoka (K.h.j) na Mwenzake mahakama yalitilia mashaka tamko la mmoja wa marehemu kwa sababu hali ya mazingira wakati wa kifo chake au mara tu kabla yake yalionyesha asingemtambua mtu aliyechoma moto nyumba yao na kusababisha vifo vilivyotokea. Kwanza ilikuwa ni usiku mkubwa ambapo inawezekana marehemu (msichana wa miaka kumi na mbili) alikuwa amelala kabla ya kushtushwa na moto.
Pili iliwezekana kabisa kuwa alimtaja mshitakiwa baada ya kumsikia marehemu dada yake akimtaja mshitakiwa huyo. Mbali na yote hayo, marehemu shahidi huyo, alikuwa ni mtoto ambaye ushahidi wake ilibidi uangaliwe kwa makini sana.
Kesi nyingine muhimu ni ile ya Tuwamoi v. Uganda (1967) E.A. 84) ambayo mahakama Kuu ya Uganda yalimtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia. Shahidi muhimu katika kesi hiyo aliyeitwa Nacham, aliyaeleza mahakama hayo kuwa marehemu mama yake alimtaja mshitakiwa kama mtu aliyemwua. Mauaji yenyewe yalitokea usiku wa giza na shahidi mwenyewe Nacham alikiri kuwa yeye hakuweza kuona vizuri usiku huo. Mahakama ya Rufani yaliamua kwamba ilikuwa ni makosa kwa mahakama kuu yaliyosikiliza shauri lile kwa mara ya kwanza kuukubali ushahidi wa matamshi ya marehemu kuhusiana na mtu aliyesababisha kifo chake. Sababu kuu ni kuwa mazingira yaliyokuwepo wakati wa tukio hayakuwa mazuri kumfanya marehemu amtambue aliyemshambulia bila makosa.
Hakika sio rahisi kuelezea kila hali ambayo itasemwa kwa usahihi kuwa kama itatokea basi tamko la marehemu kuhusiana na kifo chake lisikubaliwe. Kila shauri litategemea mazingira yenyewe. Mathalan wakati mwingine mfaji anaweza kumtaja mshitakiwa kuwa ndiye alimwona kwa kuhisi tu kwamba ndiye yeye kutokana na ugomvi wao wa siku nyingi. Kwa mfano katika shauri la R. v. Mathias Kaondoka na Mwenzake (i.h.j) ilithibitika kuwa mmoja wa marehemu alikuwa na uhasama wa muda mrefu na mshitakiwa mmoja, ambaye alikuwa mume wake. Ugomvi wao ulisababisha mfarakano uliomfanya marehemu amtoroke mume wake na kwenda kuishi na wazazi wake. Inawezekana kabisa kuwa mshitakiwa alitoa vitisho vya kumdhuru marehemu kabla ya kifo chake. Lakini vitisho sio kutenda. Pengine mfaji alikuwa anatoa maelezo ya kifo chake kujibu maswali aliyoulizwa na shahidi, au mtu yeyote yule. Katika kufanya hivyo, hasa kama hali yake ya afya au akili ilikuwa sio nzuri, anaweza kutoa majibu yasio sahihi, hasa anapoulizwa maswali ya kumchombeza atoe majibu fulani (K.h.j). Kwa mfano; Nani aliyekupiga panga, Hamisi? Au shemeji yako? na kadhalika. Majibu yanayotolewa yanaweza kuwa ya mkato tu: Ndiyo.
Ili kuepuka hatari zote hizo
zilizotajwa na nyingine zinazoweza kufikiriwa na kutokea, mahakama yamesisitiza
mara nyingi kwamba, japo sheria za bunge hazitaji hivyo, ni bora kupata
ushahidi wa kuunga mkono tamko la mfaji kabla ya kumtia hatiani mshitakiwa
(Pius Jasunga v. R. (1954) 21 E.A.C.A. 331). Yaani tamko la mfaji
pekee lisiwe msingi wa kumtia hatiani mshitakiwa bila ya kuwa na ushahidi
wa kuunga mkono tamko hilo. Lakini iwapo mahakama yanaridhika kuwa kwa
kila hali tamko la marehemu ni sahihi, basi tamko hilo linatosha kuwa msingi
wa kumtia hatiani mshitakiwa.
--
|
|