Uchambuzi/hoja binafsi
 
Yehova na Allah hawapingani
 

Na Muhibu Said

WIKI chache zilizopita chini ya maudhui "Je, Yehova na Allah ni miungu tofauti?", zilibainishwa shuhuda kemkem za Qur'an takatifu na Biblia tukufu zinazothibitisha kwa uwazi kwamba Allah na Yehova ni Mungu mmja kutokana na sifa zake takatifu zilizoelezwa na vitabu hivyo kwa pamoja kulingana.

SIFA hizo za Allah au Yehova, tuliona kuwa ni pamoja na kuwepo mwanzo, Uumbaji, Ukuu, uweza, kutokufanana na yeyote wala na chochote, kutokuonekana, upweke, kutokuzaa wala kuzaliwa, kutokufa, kuokoa, kutokuchangia uungu wake na yeyote wala na chochote, kujua kilakitu, utakatifu, kutokuchoka, kuwa na nafsi moja, kutobadilika badilika, utukufu na kadhalika.

Wakati nikiwa bado njiani kuelekea kwenye hitimisho la maudhui hiyo, alijitokeza Mkristo mmoja aitwaye Bw. Elia Batendi na madai kadhaa.

Bw. huyo alikuja na mafundisho mbalimbali ya Qur'an takatifu na Biblia tukufu pamoja na madai mengine aliyodai kayatoa kwa mtalaamu wake wa magonjwa ya kina mama na kudai kwamba mafundisho hayo yanamuonyesha yeye na wenzake kuwa Allah na Yehova ati wanapingana!

Akadai kwamba ili kumuonyesha (yeye ni wenzake hao) kwamba Allah na Yehova ni Mungu mmoja na hivyo kumaliza kiu yao, madai yake hayo na ya mtaalam wake huyo (kama tutakavyo kuja kuona hapo baadae) yajibiwe.

Hata hivyo, mpaka anaamua kutunga madai yake hayo dhaifu, Mkristo huyo ameshindwa kabisa kuonyesha utofauti wa Allah na Yehova kwa kutumia vigezo vya sifa hizo zilizotajwa hapo juu ambazo kwa hakika ndio vigezo muhimu na vya msingi vinavyoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova na kumdhihirisha Mungu wa kweli. Badala yake akasema:

"Sifa hizi na nyingine nyingi ambazo Mungu Yehova na Allah wanazo na hivyo kuwa ni Mungu mmoja aliyejifunuwa kwa Manabii kwa majina mbalimbali, zimeelezewa vizuri na Bw. Muhibu. Kitu ambacho Bw. Muhibu hakukielezea wazi na hivyo kunifanya mimi na wengine waliokuwa wanafuatilia hoja hizo na kutufanya tuamini kuwa ametuacha na kiu ni kutoelezea kwa uwazi kwa nini miungu hawa wanapingana pamoja na kwamba wana sifa moja. Aidha, Bw. Muhibu anatakiwa avunje hoja za huyo "mtalaam wa magonjwa ya wanawake" kuwa kufanana kwa Yehova na Allah katika sifa zao, siyo hila (Qur'an 3:54). (Rejea ANNUUR namba 205, Uk. 8 chini ya kichwa cha habari: Jehova na Allah: Muhibu bado hujajibu hoja)

Kulingana na maelezo yake hayo juu, Bw. Batendi kwanza anakiri wazi kwamba sifa hizo za Mungu wa kweli zilizobainishwa katika maudhui ile zikidhihirisha Allah na Yehova kuwa a Mungu mmoja zimemkinaisha sawiya, na kwa kupitia sifa hizo hana hoja ya kupinga Yehova na Allah kwamba ni Mungu mmoja aliyejifunua au kujitambulisha kwa Manabii wake mbalimbali kwa majina tofauti.

Na labda jambo la kumsisitiza hapa Bwana huyo na wenzake hasa baada ya kutunga hoja zisizokuwa na msingi ni kwamba, Mungu huyo (Yehova au Allah s.w.) mwenyewe daima hutaka ajulikane kwa sifa zake takatifu (Tazama Isaya 40:28; Qur'an 2:255) na si vinginevyo. Sifa zake hazibadiliki kwa mabadiliko ya wakati wala mazingira (Zaburi 102:24-27; Qur'an 33:62 na kadhalika). Hutopata andiko lolote katika vitabu vitakatifu linalofundisha kwamba Yehova au Allah alibebwa mimbani, akazaliwa akavikwa nguo za kitoto (yaani nepi), akakua, akaona njaa, akaona kiu, akala, akanywa, akaenda choo, akasinzia, akachoka, akapigwa, akasulubiwa, akafa, akafufuka, akawa na ukoo na kadhalika.

Lakini miongozo na mafundisho yake ndani ya vitabu hivyo ndio hubadilika kulingana na wakati mahali na mazingira. Hapo huwezi ukasema mwenye mafundisho hayo siyo Mungu mmoja. Na hilo si katika Qur'an na Biblia tu, lakini limo hata katika Biblia yenyewe.

Kwa mfano, kuna kitu katika Biblia tukufu kiitwacho 'Agano la Kale" na "Agano Jipya" ambamo ndani yake kunaonekana mabadiliko kadhaa ya mafundisho na miongozo ya Yehova. (Tazama Yeremia 31:31-34).

Aidha, katika Agano Jipya tunaona pia jinsi Bwana Yesu (a.s.) alivyokuwa akiharamisha mambo mbalimbali yaliyohalalishwa katika Torati. Kwa mfano anasema:

"Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino, lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakayekushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia". (Mathayo 5:38-40).

Kwa shuhuda hizo chache, hatuoni Wakristo wakisema kwamba ndani ya Biblia tukufu kuna miungu wanaopingana (kama adaivyo Bw. Batendi hapo juu) ambao mmoja kafanya Agano la Kale na mwingine kaleta Agano Jipya; au kuna Mungu aliyemruhusu Nabii Musa na wafuasi wake kulipiza kisasi na kuna Mungu aliyemfunulia Nabii Yesu (a.s.) afundishe kusamehe na kuhurumia pamoja na kwamba (miungu hao) wana sifa moja!

Lakini mambo hayo yanapoonekana kati ya Qur'an na Biblia akina Batendi hukurupuka haraka na kuanza kuhoji uhusiano wa Allah na Yehova kwa kutumia vigezo kama hivyo (vya mabadilko ya miongozo na mafundisho yake (Yehova) mbalimbali aliyoyatoa kupitia vitabu hivyo kulingana na wakati, mahali na mazingira tofauti; hata kama watashindwa kukanusha uhusiano wa 'sifa zao' zitajazwo vizuri na kwa uwazi na vitabu hivyo.

Kwa hali hiyo, Bw. Batendi anapohoji kwa nini miungu hawa (Yehova na Allah) wanapingana wakati ameshindwa kukanusha uhusiano wa sifa zao na hivyo kudhihirika kuwa ni Mungu yule yule mmoja aliyejifunua au kujitambulisa kwa Manabii wake mbalimbali hadi Nabii wake wa mwisho, Mtume Muhammad (s.a.w.), yaonyesha ni jinsi gani Bw. huyo asivyomjua Mungu wa kweli hajaelewa kwa sababu au hajazisoma makala zile kwa akili huru na tulivu na kwa moyo wa kutaka kuelewa ukweli!

Kwa uchache, Allah na Yehova daima hawapingani kabisa kabisa (Rejea Qur'an 42:13). Kinyume chake, kama tulivyoona katika makala zile, wanaopingana ni mungu-mtu wa dini ya Kikristo na Yehova (au Allah) kwa sababu mungu-mtu ni mungu wa kipagani "Zeu" au "Herme" kwa jina lingine "Yesu Kikristo" alilopachikwa na Bwana Paulo. Paulo alipompachikia mungu-mtu huyo (Zeu au Herme) jina la "Yesu Kristo" hakumbadilishia sifa zake, alichombadilishia ni jina tu. Mungu-mtu huyo wa Paulo (Zeu na Herme kwa jina lingine Yesu Kristo) alibakia na sifa zake zote. (1 Timotheo 3:14-16; Wafilipi 2:5-7).

Si hivyo tu, lakini Paulo alikuwa ana makusudi mengine vile vile. Baada ya kumpachika mungu-mtu huyo (Zeu au Herme) jina la "Yesu Kristo", alimwingiza pia kwenye vitabu vya Mwenyezi Mungu (Yehova au Allah s.w.t).

Kwa hiyo, mungu-mtu huyo (Zeu au Herme) kupitia jina la "Yesu Kristo" akavaa vile vile jina la Yehova, lakini kiukweli si Yehova bali ni mungu-mtu (Zeu au Herme) yule yule na sifa zake zile zile. Matokeo yake ni kuwa anayebadilika si Zeu au Herme wala si Yehova. Ni jina tu la Yehova amepachikiwa mungu-mtu Zeu au Herme.

Kwa hiyo, Mkristo akimwelezea Yehova, atakachofanya lazima kitakuwa ni kuelezea sifa za Zeu au Herme kwa jina la Yehova. Lakini Yehova anabaki yule yule mwenye sifa takatifu tulizotangulia kuziona hapo mwanzo.

Sifa hizo Mkristo hawezi akazijua, akazifundisha na akazikubali wakati anapomsimulia mungu-mtu "Yesu Kristo". Akifanya hivyo, basi lazima atakuwa anambatilisha mungu-mtu huyo.

Kwa hiyo, wakati wowote, Mkristo yoyote, si Profesa, si Muinjilisti, si mkereketwa, akiwa anaandika habari za mungu-mtu "Yesu Kristo" atakuwa tu anamwelezea mungu-mtu Zeu au Herme ingawa mwenyewe atakuwa anadhani anamwelezea Yehova.

Kwa hiyo, siku zote Mkristo atakuwa anaona kuwa Allah siye Yehova kwa sababu, kwake yeye Yehova ni mungu-mtu Zeu au Herme; naye siye.

Na hii ndio sababu iliyompelekea Bw. Batendi atunge swali lake lile: Kwa sababu kwake yeye Yehova ni Zeu au Herme, na kwa hali yoyote ile Zeu au Herme si Allah (s.w.t.).

Halikadhalika, Paulo baada ya kuzipachikia ibada za kipagani jina la "Yesu Kristo" aliziingiza pia kwenye vitabu vya dini ya Mwenyezi Mungu (Yehova) kupitia jina hili la "Yesu Kristo" kama ibada halali za dini ya Mwenyezi Mungu (Yehova). Ambapo ibada hizi zote katika dini ya Yehova ni ibada najisi na batili.

Kwa mfano, ibada ya dini ya Kikristo ya Paulo; ya kuua wana kama kafara ya dhambi, ni machukizo na batili katika dini ya Yehova (Zaburi 106:35-38), kupandisha, kutoa, kuagua na kwa ujumla kujishughulisha na pepo ni ibada batili katika dini ya Yehova (Walawi 19:31; 2 Wafalme 21:1-6); Walawi 20:27); Kuwaomba (kuabudu) wafu ni ibada batili katika dini ya Yehova (Kumbukumbu la Torati 18:9-11); kuabudu (kuomba) sanamu ni ibada batili katika dini ya Yehova (Kumbukumbu la Torati 5:8-9) na utabatizo ni ibada ya kipagani (Tazama Biblia ya Wakatoliki, Imprimatur M. Mihayo Archbishop of Tabora February, 1967, kwenye maelezo ya Mathayo 3:6, Uk. 879), ibada kama hiyo ya kipagani ya (ubatizo) ni batili katika dini ya Yehova (Yeremia 10:1-4).

Sasa Bw. Batendi, Mkristo yeyote akiwa anamfananisha Allah ndani ya maandiko ya Biblia tukufu daima lazima atakuwa anafanya hivyo kwa kutumia maandiko ya dini ya Kikristo ya mungu-mtu. Lazima atapitia maandiko ya Bw. Paulo.

Nataka nikukumbushe neno hili kuwa Paulo ndiye muasisi wa Ukristo na yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuandika nyaraka zake. (Rejea Biblia ya Imprimatur, 1967).

Wakati anaandika nyaraka zake, kulikuwako na maandiko ya Agano la Kale na Injili ya Nabii Yesu (a.s.) ambayo Paulo ameiita "Injili ya waliotahiriwa" (Tazama Wagalatia 2:6-8). Zama hizo kulikuwa hakuna maandiko mengine juu ya dini ya Kikristo. Paulo aliichukia sana Injili ya Bwana Yesu (a.s.) na kwa hiyo hakuitumia (Tazama Wagalatia 1:8).

Kwa miaka 36 mpaka 45, maandiko ya Paulo ndio yaliyokuwa maandiko pekee juu ya dini ya Kikristo na kila aliyekuja kuuandikia Ukristo baadaye au alikuwa mwanafunzi wake (Paulo).

Kwa mfano, Luka na Marko hao walikuwa watu ambao walisoma na kutumia nyaraka zake (Paulo).

Ninachokuambia Bw. Batendi na wengine wote, ukiwa unanukuu maandishi ya mwandishi yeyote aliyeandikia Ukristo wa kale; kama vile Wainjilisti wanne na wengine walioandika nyaraka zao na waliofuatia baadaye, wote watakuwa wanaandikia Ukristo wa Paulo. Na kwa hiyo, hawawi ushahidi wa kuthibitisha Ukristo. Watakuwa ama wanamnukuu au wanamsherehesha Paulo.

Kama nilivyosema, Paulo anamfundisha mungu-mtu wa kipagani kwa jina la "Yesu Kristo" na ibada wanazomfanyia ni za kipagani vile vile kwa jina la "Yesu Kristo".

Sasa, chochote kitakachofundishwa katika maandiko juu ya Ukristo kama kinamhusu Yehova basi kitakuwa kinaelezea juu ya mungu-mtu Zeu au Herme kwa jina la Yehova. Kama kinahusu mambo ya ibada, basi kitakuwa kinaelezea juu ya ibada za watu wa mataifa yaani wapagani kwa jina la maandiko ya dini ya Yehova.

Na hiyo ndio sababu kwa nini Bw. Batendi utaona ziko tofauti baina ya Yehova na Allah. Ninyi mnazungumzia dini ya watu wa mataifa yaani wapagani, sisi tunazungumzia dini ya Yehova ndani ya maandiko matukufu, kama mifano uliyoitoa inavyothibitisha.

Lakini itakuwa ni vyema hapa chini tukayatazama tazama tu mafundisho hayo ya Qur'an takatifu na Biblia tukufu aliyoyataja Bw. Batendi katika makala yake hiyo ili tuone kama kweli yanastahili kuwa vigezo vya msingi vya kutofautisha Allah na Yehova. Tutaanza kutazama hoja aliyodai kuwa ameichukua kutoka kwa huyo mtaalamu wake wa magonjwa ya akina mama aliyedai tofauti ya Allah na Yehova kwamba Allah ati ni Mungu wa hila (yaani mdanganyifu) kinyume na alivyo Yehova!

Je, Allah/Yehova ni Mungu wa hila (mdanganyifu?)

Hila au udanganyifu ni shutuma mojawapo miongoni mwa shutuma nyingi ambazo Wakristo (Batendi na mtaalamu wake wa magonjwa ya akina mama) wanamhukumu kuwa nayo Allah (s.w.t.) na wanaitumia kama kigezo cha msingi cha kumtofautisha na Yehova wakidai ati yeye (Yehova) hanayo! Hii (kama tulivyotangulia kuona) ni baada ya kushindwa kuwatofautisha kupitia "sifa zao" takatifu ambazo ndizo vigezo vya msingi vya kumdhihirisha Mungu wa kweli sasa wanaanza kutapatapa. Aya ya Qur'an takatifu wanayoitumia kama kihalalisho cha dai lao hilo ni ile isemayo:

"Na (Mayahudi) walifanya hila; na Allah akafanya hila (zake); na Allah ndiye bora wa kufanya hila" (Qur. 3:54)

Kwa uchache, hii ndio aya ya Qur'an takatifu ambayo akina Batendi wanadai inawaunga mkono katika dai lao kwamba Allah ni Mungu wa hila (mdanganyifu) na kwa hiyo yu tofauti na Yehova asiyekuwa na hila!

Kabla sijazibainisha shuhuda za Biblia tukufu zinazoelezea kwa uwazi "hila" za Yehova na hivyo kudhihirisha uhusiano wake na Allah (s.w.t.) katika "kigezo" hicho, pengine hapa ningeliwafahamisha akina Batendi kwamba waisome Qur'an kwa kanuni zake si kwa vingine wataikosea.

Allah kwenye Qur'an ameweka kanuni ya jinsi ya kuisoma Qur'an, naye anasema hivi:

"Yeye ndiye aliyekuteremshia kitabu. Ndani yake zimo Aya Muhkam ambazo ndizo msingi wa kitabu. Na ziko nyingine Mutashaabihaat. Wale ambao nyoyoni mwao mna upotofu wanafuata zile Mutashaabihaat kwa kutaka kuwaharibu watu na kutaka kujua hakika yake vipi. Na hakuna ajuaye hakika yake vipi; ila Allah. Na wale waliozama katika ilimu husema: Tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu. Na hawakumbuki isipokuwa wenye akili". (Qur. 3:7)

Kulingana na aya hiyo juu, tunachojifunza ni kwamba katika Qur'an takatifu, Allah (s.w.t.) ameweka aya za namna mbili. Kuna aya "Muhkam" ambazo ndizo msingi na ndizo zile ambazo maana zake ni zile zile kama zinavyosomeka hapo zilipo. Kwa mfano:

"Qul Huwa llaahu Ahad": "Sema Yeye Allah ni mmoja (tu). (Qur. 112:1). Maana yake ni hiyo hiyo kama isomekavyo hapo ilipo; kwamba Allah ni Mmoja tu.

Na kuna aya nyingine ni "Mutashaabihaat" ambazo zina maana zaidi ya moja ndani yake. Kwa mfano:

"Innaa nahnu nazzalnaa dhikra wainnaa lahuu lahaafidhuun": "Hakika sisi ndio tulioteremsha hii Qur'an, na hakika sisi ndio tutakaoilinda". (Qur'an 15:9)

Hapo tunaona Mwenyezi Mungu yule yule mmoja anajielezea tena kwa kutumia neno "Innaa nahnu" yaani "hakika sisi", ambalo lina maana ya wingi wa heshima na wingi wa namba. Kwa ujumla lina maana zaidi ya moja.

Kwa mantiki hiyo, jambo ambalo inapasa watu kama akina Batendi walielewe hapa ni kwamba, aya ya Mutashaabihaat daima haitengui hukumu ya aya ya Muhkam. Kwa hiyo neno "sisi" kwenye aya ile ya 15:9 inachukuliwa kwa maana moja tu ya wingi wa heshima na taadhima na popote pale ambapo Allah (s.w.t.) anapotumia neno hilo (sisi). Kwa kuwa aya ile ya Muhkam ya 112:1 imekwishahuumu kwamba Allah ni mmoja tu.

Halikadhalika, tunapoitafsiri Qur'an lazima tujue aya tunayoisoma mbele yetu kuwa ni aya "Muhkam" au ni "Mutashaabihaat" na kutafuta hukumu tu kwenye aya Muhkam tu siyo kwenye aya Mutashaabihaat.

Mtaalam aliyemtaja Bw. Batendi amemtafutia hukumu Allah kuwa ana hila (mdanganyifu) kwa kutumia aya Mutashaabihaat ambalo ni kosa.

Neno "Makra" kwenye aya hiyo 3:54, ambalo mtaalam wa Bw. Batendi amependa kulitumia kwa maana ya hila halisi (udanganyifu) pale linapomhusu Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) ni neno Mutashaabihaat (lenye maana zaidi ya moja ndani ya Qur'an takatifu).

Maana yake moja ni: Mipango inayohusiana na hila (Qur. 3:54), maana nyingine ni mipango tu (Qur. 7:99) na maana nyingine ni kuteta au kusengenya (Qur. 12:31).

Kwa hiyo, neno hilo (Makra) ni Mutashaabihaat na kwa hiyo, hatuwezi kulitumia kulitolea hukumu. Tutafute aya Muhkam tuone je, Mungu anafanya hila (udanganyifu)? (Astaghfirullah!) Jawabu ni kwamba Mungu (Allah/Yehova) hafanyi hila (udanganyifu). (Tazama Qur'an 7:28; 3:26, Zaburi 99:9; Luka 18:18-19).

Kwa hiyo, tafsiri pekee tunayoweza kuitumia kuhusu Allah tunapotafsiri neno "Makra" juu yake lazima iwe "kupanga" tu:.

Kwa hiyo, popote neno "Makra" linapotumika juu ya Mwenyezi Mungu tutasema kwa mfano Qur'an 13:42: "Mipango yote ni yake Allah"; Qur'an 10:21 isomeke: "Allah ni mwepesi wa kupanga"; Qur'an 3:54 isomeke: "Allah ndiye mbora wa kupanga" na kadhalika. Na hivi ndivyo ilivyo katika dini ya Mwenyezi Mungu (Allah/Yehova); siku zote hatumhusishi na ubaya. Kwa mfano, tuisomapo Biblia tunaona nayo inasema:

"Mikaya akasema, sikia basi neno la BWANA; Nalimuona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto. BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatokea pepo, akasimama mbele ya BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa Manabii wake wote. Akasema, utamdanganya, na kuridiki pia; ondoka ukafanye hivyo". (1 Wafalme 22:19-22). (Tazama tena 2 Mambo ya Nyakati 18:18-20).

Hapa tunaelezwa jinsi Yehova zamani (kabla ya Qur'an) alivyokuwa akiunda udangayifu (hila au mpango) wa kuangamizwa Ahabu mfalme fisadi wa Israeli wa zama hizo. Katika dini ya Mwenyezi Mungu, hapo hatuwezi tukamhusisha Yehova na sifa mbaya ya udanganyifu (au hila). Badala yake, neno "kudanganya" hapo juu ya Yehova lisomeke "kufanikisha" na siyo hila au udanganyifu halisi, kama wapotoshavyo akina Batendi.

Mfano mwingine katika Biblia wa tafsiri sahihi ya hila juu ya Yehova, ni kama maandiko yafuatayo yanavyosema hapa chini:

"Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya; kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao. BWANA amejidhihirisha na kutekeleza hukumu; Amemnasa mdhalimu kwa kazi ya mikono yake. (Zaburi 9:15-16)

Hapa tunaelezwa vile vile kuwa hila (udanganyifu) au mitego ya maadui (mataifa) imewanasa wenyewe baada ya Yehova kutekeleza hila au "mipango" yake.

Kwa hali hiyo, si katika Qur'an tu kunakomuelezea Mwenyezi Mungu (Allah/Yehova) kuwa na hila (udanganyifu) kwa maana ya "mipango" au "mafanikio", bali katika Biblia vile vile kunaelezwa jambo hilo. Kwa hiyo "kigezo" hicho cha kina Batendi si cha msingi kinachoweza kutofautisha Allah na Yehova.

Itaendelea toleo lijalo 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook