Na Mwandishi Wetu
MAIMAMU Jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita walishiriki katika semina iliyofanyika katika Msikiti wa Mtambani iliyojadiliwa kwa kina masuala mbalimbali yanayohusu Misikiti na waumini wa dini ya Kiislamu Jijini.
Semina hiyo iliyojumuisha Maimamu na wasaidizi wao kutoka Msikiti zaidi ya 60 jijini iliandaliwa na Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu nchini.
Mada tatu ziliwasilishwa katika semina hiyo nazo ni "Umuhimu wa umoja wa Kiislamu", "majukumu ya Imamu katika jamii" na "wajibu wa kumsaidia Muislamu aliyedhulumiwa".
Akiwasilisha mada ya "Umuhimu wa umoja wa Kiislamu", Amir Swalahuddin wa Markaz Tabligh Fiy Sabiilillah Gongo la Mboto alieleza kuwa umoja wa Kiislamu ni jambo muhimu na zito kwa kuwa linatokana na amri ya Allah (s.w.) mwenyewe.
Aliitanabahisha hadhara ya kuwa umoja ni somo ambalo Waislamu, hususan wa Tanzania, tumelisahau. Na kwamba kutokana na kuupa mgongo umoja, Waislamu nchini tumekuwa wanyonge na madhahili.
Aliongeza kuwa Waislamu wameutupa umoja miongoni mwao kiasi cha kufikia kukubali kugawanywa na adui zao kwa kupewa anuani za kuwatofautisha kama vile "siasa poa", Waislamu wenzetu na kadhalika.
"Tumefikia hadi kupigana matapo juu ya mambo madogo, kama vile katika swala kwa mambo ambayo si sunnah wala faradhi, bali ni mapambo tu", alisema Amir Swalahuddin aliwatanabahisha Waislamu juu ya aya ya Allah (s.w.) iliyobeba ahadi yake kuwa atawapa msaada wale walio pamoja na kuongeza kuwa kwa mnasaba wa aya hii hata makafiri wakishikana kwa dhati katika lao hawatashinda.
Katika kuchangia mada hii ilielezwa na mshiriki kutoka Masjid Mwinyi Magomeni Mapipa kuwa udhalili walionao Waislamu unatokana na kukosa kiongozi wa Waislamu wote. Mtu wa kuwasemea na ambaye akisema wote tutasikiliza.
Mshiriki huyo alieleza pia kuwa taarifa za shughuli za Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu haziwafikii Waislamu wote. Hivyo alishauri kuwa kuwepo na jarida litakalosambazwa nchi nzima ili taarifa ziwafikie Waislamu wote.
Kwa kuongezea, alipendekeza kuwa Kamati ingebuni utaratibu wa kuswali Ijumaa Misikiti mbalimbali kwa kuzunguka ili harakati zake zienee Misikiti yote.
Pia alikubaliana na mtoa mada ya kuwa katika kujenga umoja madhubuti, juhudi zifanywe kuondoa tofauti ndogo ndogo na akapendekeza ya kuwa uangaliwe uwezekano wa kuswali Iddi moja na kuendesha shughuli kama hizo kwa pamoja.
Msemaji huyo aliongeza kwa uchungu kuwa kuna haja kubwa ya kuongeza juhudi za kuyatangaza madhila serikali hii inayotufanyia Waislamu.
Akapendekeza kuwa Waislamu waandae utaratibu wa kuvifuata vyama vya upinzani na kuvipa matakwa ya Waislamu na kitakacho kubali tufanye fungamano nacho na kupewa kura.
Msemaji mmoja akitoa rai kuwa hakuna haja majadiliano marefu, alibainisha ya kuwa utatuzi wa matatizo utapatikana tu kwa kujenga umoja. Hivyo alishauri ya kuwa la msingi ni kujadili namna ya kujenga umoja bila kupoteza muda. Aidha alipendekezwa achaguliwe kiongozi wa Waislamu wa Dar es Salaam.
Sheikh wa Ubungo Kibangu alikubaliana na wazo hilo na akapendekeza jina la Sheikh Juma Mbukuzi Imamu wa Msikiti wa Mujahiduun wa Mburahati Barafu kushika nafasi hiyo.
Baada ya mjadala uliofuatia pendekezo hilo, Sheikh Mbukuzi alipitishwa na washiriki wa semina wote kwa sauti moja kushika nafasi ya kiongozi wa Waislamu wa Dar es Salaam, nafasi ambayo itatambulika rasmi kama "Amir-ul-Muuminina" na Misikiti kadhaa ya Dar es Salaam.
Pia ilikubaliwa ya kuwa atatambulishwa rasmi kwa waumini wa Dar es Salaam katika "Bai-a" ya hadhara itakayo fanyika katika siku itakayopangwa na waandaji wa mkutano huo.
Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu Tanzania ilipewa kazi ya kulitangaza tukio hilo na kumtangaza Sheikh Mbukuzi kama Amir-ul-Muuminina.
'Imamu ana jukumu la kuiongoza jamii'
Na Mwandishi Wetu
KHATIB maarufu Jijini Sheikh Musa Kileo amesema majukumu ya Imamu hayaishii anapotoa salam katika swala na kutia Fat'ha, bali Imamu ana majukumu makubwa na mazito ya kuilea na kuiongoza jamii.
Sheikh Musa aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada katika semina ya Maimamu iliyofanyika katika Msikiti wa Mtambani Jumapili iliyopita.
Alieleza ya kuwa kwa Msikiti katika Uislamu ndio makao makuu ya shughuli zote za jamii, kama vile ibada, elimu, matibabu, vita vya jihadi, usimamizi wa uchumi, sheria, uongozi na maendeleo ya jamii, Imam naye anachukua nafasi yake kutokana na kuwa kwake kiongozi wa kituo hicho muhimu katika jamii.
Alieleza kuwa hadhi ya Imam hivi leo imeanguka kutokana na Maimamu kutoitambua nafasi yao na kujiona ya kuwa wao ni waswalishaji tu.
Alieleza ya kuwa kama mlezi wa jamii, ni wajibu wa Imam kuwajua raia zake na kulijua eneo lake na mazingira yake. Awajue wangapi wenye shida, matatizo, maskini, mayatima, wajane, wasomi na wataalam wa aina tofauti.
Pia awajue wangapi wanaswali, wangapi hawaswali, watoto wangapi, wazee na kadhalika.
Imamu anatakiwa ajue uwezo wa raia zake na aweke mipango ya maendeleo yao na namna ya kutatua shida zao.
Pamoja na hayo, Imamu pia anatakiwa kuyajua maraakiz shaytaan (makazi ya shetani) kama vile mabaa, vilabu vya pombe, makanisa, kumbi za madisko, madanguro na maeneo mengine ya maasi vikiwemo vijiwe vya wavuta bangi na wahuni.
Ajue kuna wahuni wangapi, changudoa wangapi na kwa ujumla kuna wenye mirathi ya maasi wangapi ili ayafanyie mipango ya kuyaondosha.
Katika kuchangia mada Sheikh Omar Bashir aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Mwembechai ambaye sasa ni Imam wa Msikiti wa Farasi, Mabibo alielezea ya kuwa Misikiti mingi ina maradhi ya mifumo mibovu ambayo haimpi Imam hadhi na nafasi yake.
Alieleza ya kuwa katika Misikiti mingi Maimamu "huwekwa" na mabaraza ya wadhamini au zile ziitwazo kamati za Misikiti na huweza kuondolewa wakati wowote akitofautiana msimamo na mabaraza au kamati hizo.
Alieleza ya kuwa Maimamu wengine walio "wekwa" hukhofia kuondoshwa kiasi cha kushindwa kusimamia haki. Hivyo aliwataka Maimam wasiwe na khofu na waseme iliyo haki hata kama hawatodumu katika nafasi hizo.
Ustadh Musa katika mada yake hiyo alisema kuwa mimbari za Misikiti ni lazima zitumike kuikosoa serikali kama vile ifanywavyo na Makanisa katika nchi hii yetu sote.
Alieleza kuwa Misikiti ni lazima iwekeane mipaka ya maeneo yake ili kuleta ufanisi katika shughuli zake. Na akaongeza kuwa Maimam ni lazima wawe na mawasiliano na raia kwa njia mbalimbali zikiwemo vikao vya mara kwa mara.
Sheikh Musa pia alisema Maimamu wasiwabague raia zao kati ya wanao swali na wasio swali na kuwatenga wasio swali. Hao wote ni raia zao.
Naye Sheikh Omar Bashir katika mada yake ya "Wajibu wa kumsaidia Muislam aliyedhulumiwa", alieleza ya kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.) anaichukia dhulma na ameiharamisha juu ya nafsi yake mwenyewe.
Hivyo aliwataka Maimamu nao pia kuichukua dhulma kama Mwenyezi Mungu anavyoichukia dhulma.
Wapewa
tuzo ya Hassan bin Ameir, Zainab al Ghazali
Na Mwandishi Wetu
WANAFUNZI wa shule ya sekondari ya Kiislamu ya Ubungo wamepewa tuzo tofauti kufuatia kufanya kwao vizuri mitihani ya kidato cha nne na sita.
Tuzo walizokabidhiwa wanafunzi hao ni pamoja na zile za juu za Hassan bin Ameir, Zainab Ghazal na tuzo maalum ya shule.
Waliopokea tuzo hizo ni Abeid Abubakar, Wafundi Abdillah, Asina Abdillah na Mwanaidi S. Khamisi
Abeid Abubakar (kidato cha sita) na Wafundi Abdillah (kidato cha nne) walipokea zawadi ya Hassan bin Ameir kwa upande wa wavulana. Wakati ambapo Asina Abdillah (kidato cha sita) na Mwanaidi S. Khamis (kidato cha nne) walipokea zawadi ya Zainab al Ghazal kwa upande wa wasichana.
Mwanafunzi aliyepata zawadi maalum ni Wafundi Abdillah Omar ambaye atasomeshwa bure iwapo atarejea kuendelea na masomo ya kidato cha tano na cha sita shuleni hapo.
Mgeni rasmi aliyekabidhi zawadi hizo katika mahafali hayo yaliyofanyika siku ya Jumamosi shuleni hapo, alikuwa Sheikh Othman Matata ambaye aliwataka vijana hao na wengine waliohitimu vidato hivyo wadumishe maadili waliyojifunza wakiwa shuleni hapo.
Sheikh Matata aliwakumbusha vijana hao kuwa nafasi ya mwanadamu hapa ulimwenguni ni ukhalifa.
Alisema Ukhalifa ni utawala (uongozi) juu ya viumbe na mazingira yaliyomzunguka na kwamba yeyote asiye mwanadamu ni raia chini ya dola (utawala) ya mwanadamu.
Ili kuweza kuwa Makhalifa wa kweli Sheikh Matata alisisitiza kushikamana na mafundisho ya Qur'an ambayo alisema ni mwongozo unaojitosheleza kuweza kuwaongoza wanadamu wote.
Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Saidi Nsigarila aliwataka vijana hao kutokwenda kinyume na lengo la kusoma kwao kama inavyobainishwa na Qur'an.
Awataka wananchi waitumie vizuri fursa ya kupiga kura
Na Said Shariff
IMAM Masjid Mujahiduun Sheikh Juma Mbukuzi amewataka wapiga kura waitumie fursa hiyo ya kupiga kura ambayo hupatikana kila baada ya kipindi kupita. Sheikh Mbukuzi ameyasema hayo Ijumaa Msikitini hapo.
Katika taarifa hiyo Sheikh Mbukuzi amesema kupiga kuwa ni haki ambayo kila mtu mwenye kustahiki anatakiwa aitumie.
Sheikh Mbukuzi amesema jambo la msingi kufahamu ni kuwa kupiga kura ni fursa muhimu isiyotaka kupuuzwa na yeyote kwa sababu kura ndio inayoamua mustakabali wa nchi.
Kutokana na umhimu huo, Sheikh Mbukuzi amesema ni sharti fursa hiyo itumike kikamilifu na kwa uangalifu mkubwa. Fursa hiyo itakapotumika kikamilifu na kwa uangalifu itapelekea mustakabali wa nchi kuwa mzuri na jamii itanufaika.
Lakini Sheikh Mbukuzi amesema
fursa hiyo itakapotumika ovyo itapelekea mustakabali wa nchi kwenda kombo
na kusababisha madhila makubwa kwa jamii.
--
|
|