Pilika pilika za Uchaguzi Dar:
 
Mgombea wa CCM aonja joto ya jiwe Manzese
 

Na mwandishi wetu

UZINDUZI wa kampeni za Uchaguzi kuziba nafasi za Ubunge zilizowazi katika Majimbo ya Ubungo na Temeke wiki hii, zimeanza kwa vituko kadhaa huku wananchi wa Jimbo la Ubungo wakijaribu kuonesha hasira zao dhidi ya Chama Tawala kwa kumzomea mgombea wake Bwana Venance Ngula.

Katika hali iliyoonekana kuvuruga itifaki ya kiusalama iliyojitokeza eneo la Manzese, kundi la watu lilivamia msafara wa Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na kumsindikiza pole pole kuelekea uwanja wa Ukombozi huku likiimba wimbo uliokuwa na kibwagizo cha Mwinyi mkombozi.

Msafara huo ulipowasili katika uwanja wa shule ya Ukombozi ambako CCM ilikuwa ikizundua kampeni zake na kumtambulisha mgombea wake kwa wananchi wa Jimbo la Manzese, kundi lililokuwa likisindikiza liliendelea kuzunguka uwanja huo huku likiimba wimbo wenye ujumbe kuwa wamechoka na CCM wakitaja tukiola kuuliwa Waislamu Mwembechai.

Huku ratiba ya kampeni hiyo ikiendelea kundi hilo liliendelea kuzunguka uwanja huo na kutoa shutuma mbalimbali dhidi ya CCM na viongozi wake hadi pale polisi walipoingilia kati kujaribu kuweka utulivu mahali hapo.

Kufuatia harakati za wanausalama, watu hao waliondoka kabisa katika eneo hilo huku likiwaacha 'wakereketwa' waliovalia mavazi rasmi wakiwa wamepigwa na butwaa.

Wakati wa kutambulishwa mgombea Bwana Venance Ngula hali ilivurugika zaidi ambapo watu walianza kuzomea na kutawanyika kutoka uwanjani hapo huku wakitoa maneno yalioashiria kutoukubali ugombea wa chama hicho wa kiti cha Ubunge Jimbo la Ubungo.

Awali akizungumza katika kampeni hiyo, Mzee Ali Hassan Mwinyi alimtambulisha kwa wananchi Bwana Venance Ngula, alisema baadhi ya vyama vimesimamisha wagombea wao kwa misingi ya udini.

Aliitaja NCCR kama mfano wa vyama hivyo kwa kumsimamisha Bwana AbdulRazak Atiki.

Vyama vingine vinavyoshiriki katika uchaguzi huo ni pamoja na chama cha CUF ambacho mgombea wake ni Bwana Hussein Mmasi na CHADEMA ambacho kilizindua kampeni zake juzi katika uwanja wa DABCO Ubungo Kibangu na kumtambulisha mgombea wake Bibi Justin.

Wananchi mbalimbali hasa wa mitaa ya Kariakoo na katika vigenge vya kahawa wiki hii kwa siku tatu mfululizo wamekuwa wakibashiri hali ngumu itakayoikabili CCM katika uchaguzi huu mdogo na ule wa mwakani kufuatia mfano wa tukio la Manzese.

Wananchi hao wamedai utendaji wa viongozi wa chama hicho na serikali yake ndiyo wa kulaumiwa kwa kusababisha kwenda hovyo kwa mambo kadhaa.

"Watu si kwamba wanakichukia chama (CCM), mambo ya Mwembechai na hali ngumu ya uchumi ndiyo yamefanya CCM ifike hapa sasa", amedai mzee mmoja katika kikao kimoja maarufu cha kahawa kilichopo mtaa wa Livingstone, Kariakoo.

Kulingana na mazungumzo ya watu sehemu mbalimbali nchini suala la Mwembechai na hali ngumu ya uchumi inayowakabili wananchi huenda zikawa rejea za wapiga kura wengi katika chaguzi zijazo.
 --

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook