Maoni yetu
Kukusanya ushahidi wa dhulma ni kupoteza wakati bure
 

IWAPO mtu aweza kumfumua binadamu mwenziwe fuvu la kichwa kwa risasi ubongo ukatawanyika ili ampore gari lake, haitakuwa ni jambo la kushangaza tena itakaposikika kwamba kampora mtu kitoweo chake watoto wake wakalala njaa.

Taarifa za vyombo vya habari za hivi karibuni zimefahamisha kwamba Kamati ya Kupigania Haki za Waislamu imemtumia Mh. Rais Benjamin William Mkapa Kanda ya Mauaji ya Mwembechai.

Katika kanda hiyo wanaoonekana polisi wakiwalenga shabaha Waislamu na kuburura maiti zao huku zikisikika sauti zikiamrisha "piga shaba", "piga yule".

Matarajio ya Waislamu yalikuwa kwamba huenda Mh. Rais hakupewa picha halisi na sahihi za tukio lenyewe na pengine kwa ushahidi huo ile mantiki ya kuunda tume na suala hili kufikishwa mahakamani ingeonekana. Katika risala ya Waislamu kwa Mh. Rais, mauaji ya Waislamu Mwembechai yametajwa kama kielelezo kimojawapo juu ya udhalimu na uonevu wanaofanyiwa Waislamu. Kama kielelezo hiki hakiwezi kuisukuma serikali ikaona haja ya kuyazingatia malalamiko haya; ushahidi gani tena Waislamu waonyeshe.

Waislamu damu yao imemwagwa bila ya haki na wanaambiwa hakuna haja ya tume wala suala hili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Katika mazingira haya kwenda mbio kufanya utafiti na kukusanya data ili kutoa ushahidi wa kisayansi kwamba kuna dhulma katika elimu na kutoa vyeo na madaraka ni kujidunisha kusiko sababu. Kama mtu aweza kumwaga damu ya mtu bila kushtuka vipi umdhanie kuwa hawezi kupora haki ya mtu mahakamani. Ugumu uko wapi, kumuua mtu au kumnyima mtoto wake fursa ya kusoma au kupata cheo!

Kuua ni kielelezo cha dhulma iliyokubuhu, leo kuwaambia Waislamu walete vielelezo kuonyesha dhulma dhidi yao katika elimu na uteuzi katika nafasi mbalimbali serikalini ni kuwafanya mwanasesere au wengine huita mdoli. Tunayasema haya kwa sababu tumesikia kuna baadhi ya Waislamu wanafanya utafiti kuonyesha ama kuwepo au kutokuwepo kwa dhulma katika elimu na ajira.

Tatizo hapa si 'data', utafiti na uchambuzi wa kisayansi bali mwelekeo hasi dhidi ya Waislamu na kukosekana kwa nia ya kweli ya kukabiliana na tatizo. Na ndio maana yawezekana kila vikao nyeti vya kichama na serikali vikikutana kutathmini mambo huenda hupambwa na taarifa za ... "tunaendelea kuwadhibiti siasa kali, kupambana na mujahidina na tunaendelea kumsaka Ponda (badala ya Padri Luambano na Bw. Makamba)". Na kila mtu leo anajua 'siasa kali' ni kina nani. Walijisemea Wazungu mpe mbwa jina baya ili upate kumuua!

Taarifa juu ya mlolongo wa matukio nchini Rwanda kutoka mwaka 1959 hadi makubaliano ya Arusha yanawasilisha ujumbe muhimu. Waliokuwa madarakani wakiongozwa na Rais Juvenal Habyarimana hawakuwa tayari kushirikiana na wenzao katika utawala kama ilivyoelekezwa na makubaliano ya Arusha. Waliona kuwapa wengine haki ya kuwemo serikalini ni sawa na kupoteza kile walichodhania haki yao pekee ya kutawala.

Kwa hiyo badala ya kutekeleza makubaliano yale wakachochea chuki kati ya Wahutu na Watutsi. Na walipoweka mikakati ya kuwaua Watutsi hawakusema wanapambana na Watutsi kama kabila bali watu waliowaita siasa kali wenye uchu wa kupora madaraka hata ikabidi kutumia silaha. (Taz: Ubutabera No. 44/31 Agosti 1998 uk. 3).Chuki iliyojengwa kupitia propaganda ilisambazwa na vyombo vya habari iliwapelekea Interahamwe kuua bila ya kushikwa na tone la huruma.

Baada ya mauaji ya Mwembechai serikali ilidai inapambana na wanaohatarisha amani na usalama wa nchi.

Vikao vya Chama CCM vilipoidhinisha jeshi litumike badala ya polisi, ilidaiwa ni kupambana na watu walioandaliwa kuvuruga amani ya nchi wakisaidiwa na mataifa ya nje (Taz: Magazeti ya Mtanzania na Rai).

Lakini miaka mitatu nyuma ilisambazwa sumu kwamba hawa 'Mujahidina' wanataka kuua watu kwa kutia sumu katika matanki ya ulevi, kulipua sehemu za kuuzia ulevi na madanguro. Isitoshe ikadaiwa wameletewa msaada wa silaha zikiwa ni majambia ndani ya makontena. Huko Moshi ikadaiwa Mujahidina wanavinjari kwenye Makanisa na taasisi zake wakiwa na mabomu ndani ya Hijaab.

'Ubutabera' inatufahamisha kuwa kilichotangulia mauaji ya halaiki Rwanda ni kundi la Habyarimana kuchochea chuki na kujenga woga wa kutokuaminiana kwa watu wa nchi moja. Unategemea kitokee nini jeshi iwe ni JWTZ au polisi linapopelekwa kwa watu waliopakwa picha hiyo hapo juu!

Tunazikumbuka kelele za 'Loliondogate' lakini hatusikii 'Mwembechai gate'. Mwandishi mmoja wa habari wakati wa uhai wa Profesa Malima, akidhihirisha chuki yake dhidi ya Profesa alisema, "Lau Profesa Malima angekuwa na mabinti angefanya kila njia awatie mimba lakini 'bahati mbaya' kazaa madume matupu!

Kwa walioutazama mkanda wa mauaji ya Mwembechai watakuwa wamesikia sauti ya kamanda ikisema: "piga shaba, piga yule,yote haya sababu ya ruhsa, kila kitu ruhsa". Kama si chuki haya yanakujaje, na imetoka wapi? Bw mmoja aliyekamatwa hivi karibuni huko Tanga kwa tuhuma za kuwa na kanda ya mauaji ya Mwembechai alisimulia jambo la kutisha kidogo. Mmoja wa askari aliyekuja kuwaangalia mahabusu usiku, pamoja na maneno mengine mengi ya kejeli alimuambia; "Mnajifanya kutaka Uwaziri Mkuu wakati darasa la saba; mnataka kuingia Ikulu kwa nguvu wakati hamkusoma; lakini safari hii mtakoma".

Data gani na za nini wakati mwelekeo wa watu ni huo. Tunawaonea huruma ndugu zetu Waislamu wanaokwenda mbio kukusanya "ushahidi" wa kudhulumiwa kwetu. Wanadhani ushahidi huo wa kisayansi utawasaidia kuondosha kunyanyaswa kwa Waislamu nchini. Dalili zote zinaonyesha wanapoteza nguvu na wakati wao bure. Ufumbuzi wa kweli utapatikana kwa Waislamu kuendelea kuimarisha mshikamano wao ili wayakabili na kuyatatua madhila yanayowakuta kama Waislamu. 
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook