MAKALA
 
 
Hamkuwaelewa Masheikh wenu?
 

Na Abu Kalam
 

Imam Ahmad bin Muhammad bin Hanbal
 

IMAM Abu Abdallah Ahmad bin Muhammad bin Hanbal alizaliwa huko Marwa mwezi 20 Rabi-ul-Awwal mwaka 164 A.H. Baba yake Muhammad alikuwa mujahidina aliyesifika wakati akiishi Basra.

Baba yake alihamia Baghdad ambapo alifariki muda mfupi baadae na kumuacha Ahmad bin Muhammad akiwa bado mchanga. Pamoja na uyatima wake; kijana Ahmad alikuwa mwenye akili na akautumia ujana wake wote katika kujielimisha. Alisoma zaidi Hadith na akawa mwanasheria na mtaalam wa Fiqh katika zama zake. Miongoni mwa waalim wake alikuwa Imam Muhammad al-Shafii. Kwa hiyo Imam Shafii na Imam Ahmad Hanbal walikuwa karibu sana. Alimheshimu mwanafunzi wake mashuhuri Hanbal.

Ucha Mungu wa Imam Ahmad

Imam Ahmad Hanbal alikuwa mwanachuoni Mcha Mungu sana aliyejitolea maisha yake yote kusoma na kufundisha Hadith na Fiqh. Kwa Ucha Mungu wake alikataa kufanya kazi serikalini, kwani aliona serikali ilikuwa haiongozwi kwa mujibu wa Qur'an na Sunnah. Zaidi ya hivyo alivunja uhusiano wa karibu na wote wale waliokubali kuwa ndani ya serikali za kidhalimu. Alikataa hata kupokea fedha au chakula kutoka kwa mtoto wake ambaye alikuwa akifanya kazi serikalini. Hata wakati alipokabiliwa na hali ngumu ya uchumi hakukubali kupokea msaada wowote ila kwa kuufanyia kazi.

Katika kipindi cha uhai wa Imam Ahmad waliibuka wanafalsafa waliokuja na falsafa iliyoitwa Mu'tazili. Falsafa hii iliwaita watu wawe huria katika fikra. Walichanganya Imani na Kufr hata kufikia kuleta hoja kuwa Qur'an imetengenezwa tu. Harakati hizi za kuleta kufr ndani ya Uislamu zilitokana na athari za falsafa za Wagiriki zilizowalevya baadhi ya Waislamu wa zama hizo.

Bahati mbaya watawala wa zama hizo nao waliathiriwa na falsafa hizo za Kigiriki na wakataka kuifanya kuwa imani rasmi ya Dola ya Waislamu. Viongozi waliotaka kuisimika imani hiyo ni Khalifah Ma'mun al-Rashid; Mu'tasim Billah na Al-Wathiq.

Imam Ahmad bin Hanbal alikataa kuikubali imani hiyo mpya ya watawala na akaendesha harakati kuipinga.

Khalifa Mu'tasim Billah alitoa amri akamatwe afungwe minyonyoro na kuhamishiwa Tarsus toka Baghdad. Huko alitupwa gerezani na kuteswa sana mpaka viungo vyake vingi vikavunjika.

Imam Ahmad aliachwa adumu amefungwa minyonyoro mizito ndani ya chumba chenye giza gerezani. Pamoja na kuteswa sana ikiwa ni pamoja na kuchapwa viboko mpaka damu zimtoke, Imam Ahmad hakutetereka katika msimamo wake. Msimamo huu wa Imam Ahmad ulimstua Khalifa Mu'tasim. Aliikumbuka Akhera akahofia khatima yake. Aliamuru Imam Ahmad atolewe gerezani mwezi 25 Ramadhan mwaka 221 A.H. na akamuomba msamaha, Imam Ahmad akamsamehe.

Miongoni mwa kazi muhimu alizofanya Imam Ahmad ni kuandika vitabu vifuatavyo: Kitab al-Amal; Kitab al-Tafsir, Kitab al-Nasikh wal-Mansukh na kadhalika. Lakini kazi muhimu zaidi aliyotuachia Imam Ahmad ni kitabu chake Al-Musnad. Ndani ya Al-Musnad; Imam Ahmad ametukusanyia Hadith elfu nyingi. Ulipofika mwaka wa 241 A.H. Imam Ahmad alifariki dunia. Maelfu ya watu wa Baghdad walifurika kumzika.

Hawa ndio Maimamu wakubwa wanne ambao wengi leo tunajinasibisha nao. Bahati mbaya kabisa wengi wamejipa madhehebu kutokana na Maimamu hawa katika namna ambayo inaonekana kana kwamba ni dini nne tofauti.

Maimamu hawa wanne walikuwa wanachuoni Wacha Mungu na waadilifu katika zama zao. Walifanya juhudi kubwa kusoma na kufanya ijitihada kutafsiri na kutoa maoni yao juu ya sheria na masuala mbalimbali ya Fiqh. Ni vizuri tunufaike na matunda ya juhudi na kazi zao; lakini tusigawike wala kubaguana kutokana na maoni tofauti ya Maimamu hao juu ya masuala mbalimbali. Wao wenyewe walisoma pamoja au kusomesha na wakaheshimiana na wakaafikiana kutofautiana katika mambo yasiyo ya msingi bila ya kugombana.

Jambo jingine la msingi la kuzingatia ni kuwa Maimamu hawa walipata mateso makubwa kutokana na misimamo na juhudi zao katika kuusimamisha Uislamu. Walichapwa viboko, walifungwa gerezani na kufungwa minyororo na watawala madhalimu. Zaidi ya hivyo hawakukubali kununuliwa na serikali. Walikataa kabisa kuwa vibaraka wa serikali.

Je; wakati tunafuata Fiqh na Fat'wa zao tunao pia uadilifu kama wao? Misimamo yetu juu ya serikali za kidhalimu ni kama wao? Je; hatununuliwi na serikali na kuifanyia kazi kinyume na maslahi ya Uislamu? Je; tupo tayari kufungwa na kuchapwa viboko kama Imam Ahmad bin Hanbal na Imam Shafii kwa ajili ya Uislamu?

Je; hatubadili khotuba za Ijumaa kwa vila kaswali kiongozi wa serikali au CCM? Je; hatuwakatazi watu kutoa mawaidha Misikitini mwetu kwa kuhofia kwamba watagusia suala la Mwembechai? Je; kweli mliwaelewa Masheikh wenu? 
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook