UTUME si jambo lisilojulikana katika dini za Kiyahudi na Kikristo. Katika Uislamu, utume umepewa hadhi na umuhimu mkubwa na wa kipekee kabisa. Kutokana na maelekezo ya Uislamu, Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu kwa lengo takatifu ambalo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu na kuishi kwa kufuata mafundisho na muongozo itokayo Kwake. Mwanadamu angewezaje kujua wajibu wake kwa Mwenyezi Mungu na lengo la kuumbwa na kuishi kwake hapa ulimwenguni bila ya kupata mwongozo sahihi na ulio wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu?
Kwa mujibu wa maelezo ya Qur'an, Nabii Isa alitumwa kwa wana-Israel tu, na alithibitisha umuhimu wa kuitekeleza Torati iliyofunuliwa kwa Nabii Musa (a.s.) na pia alibashiri habari njema ya kuletwa kwa Mtume wa mwisho baada ya yeye kuondoka.
"Na Isa mwana wa Mariam aliwaambia wana-Israel kuwa 'mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu', naisadikisha torati iliyonitangulia na kuwabashiria habari njema ya kuja kwa Nabii mwingine atakayenifuatia, ambaye jina lake ataitwa Ahmad-yaani msifika sana" (61:6).
Hata hivyo, wengi kati ya Wayahudi, waliyakataa mafundisho yake na hivyo kupanga mikakati ya kumuua. Na kwa imani yao walidhani kuwa walifanikiwa kumsulubu na kumuua, lakini kwa mujibu wa maelezo ya Qur'an, ni kwamba Mwenyezi Mungu alimuepusha na suluba na mauaji hayo ila wao hawajui. Pia kuna aya ndani ya Qur'an yenye kumaanisha kuwa Nabii Isa atarudi tena ulimwenguni na kwamba wakatihuo ataudhihirishia ulimwengu yale yote waliyokuwa wakimsingizia na hapo itabidi Wakristo na Wayahudi wamfuate na kumuamini kama wafanyavyo Waislamu (kwa kumtakasa na yale waliyokuwa wakimhusisha nayo kama kuwa eti ni mwana wa Mungu au kuwa eti yeye ndiye Mungu mwenyewe, kuwa eti alisulubiwa, akifa na akafufuka) kabla ya kufa kwake. Maneno haya puia yanathibitishwa na kauli (hadithi) za Mtume Muhammad (s.a.w.).
Mtume wa Mwenyezi Mungu na wa mwisho, Nabii Muhammad (s.a.w.) alizaliwa bara la Arabuni katika karne ya 6. Hadi kufikia umri wa miaka 40, jamii ya watu wote wa Makkah walimfahamu tu kuwa ni mtu mkamilifu na mwenye tabia njema kabisa (kuliko watu wote) na hivyo walimpa sifa itokanayo na tabia yake na kuwa ni "mkweli na mwaminifu - Al Ameen". Hata yeye biansi katika ujana wake, pamoja na kuwa na sifa za tabia tukufu, hakujua kuwa hata siku moja ataweza kuwa Mteule wa Mungu na hivyo kuweza kubeba jukumu zito la kuupokea ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Hata hivyo alikuwa kwa tabia yake akichukizwa na taratibu za watu wa Makkah za kupenda kuyaabudia masanamu. yeyey aliwachukulia watu wale, kuwa wasioweza kuzitumia akili kwani hakuyaona masanamu kuwa na uwezo wowote wa kudhuru au kuponya. yeyey katika fikra zake alikuwa na imani ya kuwepo Mungu mmoja tu na ambaye ndiye aliyeumbwa vitu vyote na ambaye ndiye ambaye angeweza kuponya au kudhuru (dhana ambazo kumbe zilikuwa ni sahihi). Na alipofikisha umri wa maiak 40, ndipo alipofunuliwa rasmi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwamba ujumbe wake ni kwa watu wote na yeye ni mjumbe wa mwisho, hakutakuja tena mjumbe mwingine baada yake. ujumbe wake uliweza kuhifadhika katika kumbukumbu ya kichwa chake na hata katika kumbu kumbu za vichwa vya wafuasi wake na pia kuweza kuandikwa na kuhifadhiwa katika magome ya miti, mbao, ngozi, juu ya mawe, n.k. kuanzia wakati wa maisha yake kama Mtume wa Mwenyezi Mungu na hadi leo hii umeweza kusomwa na jamii za watu wote ulimwenguni.
Hivyo, Qur'an kama tuliyo nayo siku hzi ni ile ile kama ilivyofunuliwa kwake Mtume Muhammad na hakuna hata herufi moja iliyopata kubadilishwa kwani Mwenyezi Mungu mwenyewe ameahidi kuilinda na kila aina ya uzushi au hujuma. hivyo, Qur'an imebakia kuwa ni Kitabu muhimui chenye mwongozo sahihi kwa maisha ya watu wote na kwa nyakati zote. Na pia humtaja Mtume Muhammad kama mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu.
Bishara za kutokea kwa Nabii Muhammad
DALILI za kutokea kwa Nabii Muhammad (s.a.w.) zinapatikana katika bishara za Manabii waliomtangulia na hasa katika hao waliopewa vitabu vitakatifu vinavyojulikana kwa watu wengi ambavyo ni kitabu alichohubiri Mtume Musa ambacho ni Torati na Injili, kile alichohubiri Mtume Isa (Yesu) ambavyo katika jambo hili limetolewa ushahidi pia na Qur'an tukufu, Kitabu alichohubiri Mtume Muhammad (s.a.w.). Na hivyo kwanza tunafahamishwa na Mwenyezi Mungu katika Qur'an kwamba:
"Waambie (ewe Muhammad) kuwa: Mwanaoje iwapo Qur'an hii yatoka kwa Mwenyezi Mungu nanyi mnaikataa, na hali shahidi (Mtume Musa) miongoni mwa wana wa Israel alishuhudia juu ya kuletwa Mtume mwingine mfano wake naye akaamini hayo, lakini ninyi mnyafanyia kiburi haya (awaambiayo). Basi, hakika Mwenyezi Mungu haongozi watu madhalimu". (46:10)
Mtume Muhammad alibashiriwa na Mtume Musa (a.s.)
"BWANA akaniambia, wametenda vema kusema walivyosema: Mimi (Mungu) nitawaondokeshea Nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe (Musa), nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, mtu asiyesikiliza (asiyeyatii) maneno yangu atakayosema yule (Nabii) kwa jina langu, nitalitaka kwake. Lakini Nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina la miungu mingine, nabii yule atakufa". (Kumbukumbu la Torati 18:17-20)
Miongoni mwa Wayahudi na Wakristo kuna watu wanaofahamu vizuri funuo za zamani, na ambao wakiisoma Qur'an pia wanapata uthibitisho wa vitabu hivyo vilivyopita, juu ya kutokea kwa Mtume Muhammad (s.a.w.). Na wanakubali kuwa Uislamu ni utekelezaji wa Torati ya Mtume Musa mwenyewe.
Vile vile Mtume Muhammad katika zama zake za uenezaji wa neno la Mungu, kulikuwepo na Wayahudi na Wakristo waliomsikiliza sana na kumuona kuwa yeye ni Mtume au Nabii wa Mungu aliyebashiriwa katika vitabu vitakatifu vya zamani na wao kuukubali Uislamu kama ulivyoenezwa na Mtume Muhammad (s.a.w.).
Mtume Muhammad pia alitabiriwa na Nabii Isa (Yesu)
Tunakumbushwa kwanza na Mwenyezi Mungu katika Qur'an kwamba ni kweli Mtume Muhammad alitabiriwa pia na Mtume Yesu (a.s.):
"Na kumbukeni Isa bin Mariam aliposema: Enyi wana wa Israel mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu ili niisadikishe kwenu Torati iliyokujieni kabla yangu, na kuwatolea habari njema ya Mtume atakayekuja baada yangu, ambaye jina lake ataitwa Ahmad'. Lakini (huyo Ahmad) alipowafikia na kwa ishara zilizo wazi kabisa walisema: Huu ni udanganyifu (uwongo au uchawi) ulio dhahiri". (61:6)
Ahmad (Muhammad) maana yake ni 'aliye na sifa za pekee' na katika Kigiriki mwenye sifa hizi huitwa 'Periclytos'. Na wasomi wengi wanakubali kuwa katika msemo halisi wa Yesu kulikuwepo na (bishara ya Mtume Muhammad kwa) jina hasa la Ahmad yaani mwenye sifa kama: Rehema kwa viumbe vyote (21:107). Mwenye huruma sana kwa waaminio (Qur'an 9:128).
Nyongeza:
Katika vitabu vya Injili vilivyoandikwa na Wainjilisti waliokubalika, kuna aya nyingi zinazothibitisha kuwa Nabii Isa (Yesu) alitumwa kwa ajili ya watu wake (Waisrael) tu na sio kwa watu wote wa ulimwengu. (Angalia Mathayo 5:17; 10:5-6 na 15:24-26).
Ishara zilizo wazi kutokea Nabii Muhammad (s.a.w.)
Mtume Muhammad alibashiriwa kwa njia nyepesi. Kwanza, alipodhihiri alionyesha ishara nyingi (kuwa yeye atakuwa ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu). Katika muda wote wa maisha yake alipigana na kushinda kila aina ya ubaya (uovu).
Pili, bila ya kujifunza kutoka kwa mtu yeyote, Mtume alitokea kuwa ni kijana mwenye busara na hekima kubwa sana kushinda watu wengi, kiasi cha kuaminiwa na kuombwa ushauri wa mara kwa mara na kuweza kutatua migogoro mbalimbali katika maisha ya watu. Na baada ya kupewa Utume rasmi, katika mahubiri yake aliweza kuzilainisha nyoyo za watu hata zile zilizokuwa ngumu (kufuata amri za Mungu) na kuziimarisha madhubuti nyoyo za wale waliokuwa wanyonge na kustahili msaada wa wengine.
Kutokana na matendo pamoja na mahubiri yake, watu wengi waliweza kugundua na kuuona uwezo wa Mwenyezi Mungu jinsi unavyofanya kazi. Lakini wapinzani, wao waliona ya kuwa ni uchawi mkubwa na wa dhahiri.
Tabia ya Mtume Muhammad
Mtume Muhammad (s.a.w.) aliipitia (experienced) kila hali ya maisha. Hivyo, kila funzo alilofundisha alilipitia katika maisha yake. Kwa mfano, alikuwa mtoto yatima kwani wazazi wake wote wawili walifariki wakati yeye alipokuwa bado mtoto mdogo sana. Alipitia hali ya ujana, na alipokua alifanya kazi za biashara. Alikuwa kwanza maskini na baadaye akawa tajiri na kuweza kuwaajiri watu (watumishi) wengine. Alioa, alizaa watoto, alifiwa na wapenzi wake wa karibu kama wake zake, watoto wake, ndugu na rafiki zake. Pia alikuwa jemadari wa vikosi vya waumini walipokuwa wakipambana mara kwa mara na wapinzani na baadaye alikuwa mfalme, mtawala na kiongozi mkuu wa dola ya Kiislamu kabla ya kifo chake.
Kutokana na kupitia hali mbalimbali za maisha yote haya ambayo ni ya kibinadamu, basi ndiyo maana anakuwa mfano (kiigizo chema) mwema kwa watu wa hali za maisha tofauti tofauti. Na katika mafundisho yake hata jambo dogo namna gani hakuliacha. Hata namna ya kusalimiana, kula, kulala, kutembea, kuishi na majirani na watu wa dini tofauti na kadhalika yote aliyafundisha. Ndiyo maana sifa hizi zinakuwa (Ahmad-periclytos) maalum kwa ajili yake tu na ambaye pia ana sifa ya kuitwa Mustafa yaani aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa kiongozi mkuu wa Manabii wote na wa mwisho, kwamba hatakuja tena Nabii mwingine baada yake atakayeleta sheria mpya kwa wanadamu kwani sheria zimeishakamilishwa na Mwenyezi Mungu kama alivyotaka ziwe, tokea kwa Nabii Adam, Nuhu, Ibrahim, Musa, Daudi hadi kwa Isa (Yesu) na kwa mwisho wao Mustafa Mtume Muhammad (s.a.w.).
Nao Uislamu unatambua na
kuamini sheria kama zilivyoletwa katika vitabu vya Manabii waliotangulia
kama walivyokwisha tajwa. Ila kufuatana na mahitaji ya nyakati, Mwenyezi
Mungu alikuwa anazifanyia marekebisho (ammendments) mwenyewe kwa kuwatuma
Manabii wake baada ya muda ulioukadiria, na kwa taratibu hadi alipoona
kuwa sasa ameikamilisha na kuiweka katika mfumo ilio nao katika Uislamu
wa sasa, kama ulivyohubiriwa na kufundishwa na Mtume wa mwisho Muhammad
(s.a.w.). Na hii linaufanya Uislamu kuwa na tafsiri ya mfumo mzima wa maisha
unaofuata maelekezo ya Mwenyezi Mungu.
--
|
|