MAKALA YA UCHAMBUZI
 
Mnyama mwenye namba '666' ni nani?
 

Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

KATIKA kitabu cha ufunuo wa Yohana (13:18) ametabiriwa mnyama ambaye idadi ya herufi za jina lake itakuwa 66. Wataalamu wa Biblia (wanatheologia) wamekhitilafiana katika aya hiyo. Wakatoliki wanasema ni Kaisari (mfalme) Nero aliyewauwa Petro na Paulo na kuwatesa sana wanafunzi wa Yesu (a.s.). Wasabato wanasema ni viongozi wa Kanisa Katoliki (ma-pope). Lakini dunia ilipata mtafaruku mkali baada ya wataalamu fulani kugunuda kuwa, majina "EURO", "US DOLLAR" na "BILL CLINTON" nayo yanaleta idadi ya 666 kwa kutumia kanuni fulani.

Kabla ya kusema wazi ni nani kati ya hao ni "mnyama" mwenye namba "666", kwanza niweke sawa mambo mawili yafuatayo: Kwanza tujue kuwa kitabu cha Yohana ni kitabu cha unabii (ufunuo). Hivyo haiwezekani kukifasiri kwa kutumia elimu za kibinadamu (Taz. 2 petro 1:20-21). Kwa hiyo ni rehma za Allah (s.w.) (Roho mtakatifu) ndizo zinawezesha mtu afasiri unabii au ufunuo (Taz. 1 korintho 2:10-16). Wanatheologia kwa kukosa Roho matakatifu, ndio maana wanaweweseka ovyo. Kitu cha pili ni kuwa, siku zote Mwenyezi Mungu anawasiliana na watu kwa lugha na misamiati inayoeleweka kwa wakati huo. Aidha kujipa jina fulani au utukufu fulani, havikufanyi uwe na jina au utukufu huo (Taz,. Yohana 8:31-47, Mathayo 3:7-9, ufunuo 3:1-3 n.k.). Hivyo maneno "mashahidi wa Yesu", "mwana kondoo", "wafuasi wa Yesu", "Kristo" nk. yanayojitokeza katika ufunuo wa Yohana, yanatafsiri tofauti kabisa na hii inayotolewa na viongozi wa kanisa. Wafuasi sahihi wa Yesu (a.s.) ni wale wanaofuata mafundisho sahihi ya mtume Yesu (a.s.) kama asemavyo "Na uzima wa milele ndio huu, wakujua wewe, mungu wa pekee wa kweli na (Mtume) Yesu kristo uliyemtuma" Yohana 17:3. Hivyo watu wanaofuata mafundisho yanayosema, "Mungu ana nafsi tatu", "Yesu ni Mungu" nk. Sio wafuasi wa Yesu, bali ni wafuasi wa hao walioanzisha itikadi hizo akina Yustino Shahidi, Athanasio, mpagani Kaisari Constantino na Kaisari Theodosio. Rejea makala yangu "SSiri ya Miujiza" katika AN-NUUR na.175. Kwa hiyo tafsiri sahihi ya sasa ya "wafuasi wa Yesu" ni Waislamu. Na "mashahidi wa Yesu ni Waislamu waliouwawa wakipigania Uislamu au kwa kudhulumiwa tu.

Mnyama - Ufunuo 13:1-18

Kila kitu kinatambulika kwa sifa zake na vitendo vyake. Jina pekee haliwezi kuthibitisha mtu au kitu. Kwani mara nyingi majina hufanana au hubadilishwa au kubadilika. Hivyo katika makala hii sitajihangaisha na utafiti wa majina kama hao wanatheolojia waliofilisika kielimu wanavyofanya. Hapa nitafafanua sifa zilizotajwa katika ufunuo ili kila msomaji mwenye akili zilizotulia aone mwenyewe ninani mnyama huyo.

Kwanza tujue "mnyama" huyu amepata kutoka wapi madaraka hayo makubwa. Kama inavyoeleweka, hadi sasa dunia iko chini ya miliki ya Shetani (Taz. Yohana 12:31, 16:11; 1 Yoh 5:19 nk). Hivyo naye mnyama amepewa mamlaka hayo na shetani, yaani "Joka". (Taz. Ufunuo 13:1-10, 12:7-9). Kwa hiyo "Mnyama" huyo ni Wakala wa Shetani duniani. Hivyo atafanya juhudi zote kinguvu, kiushawishi nk. ili wanadamu wamwasi Mwenyezi Mungu na wamtii Mkubwa wake (Shetani).

Sifa za Mnyama

(1) Atasifiwa, atatiiwa na kuogopwa na watu wote duniani. "...Dunia yote ikamstaajabia mnyama yule. Wakamsujudu yule joka (Shetani -kufanya maasi) kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama (yaani wakamtii na kumuogopa kupita kiasi), wakisema, ni nani afananaye na mnyama huyu?" (Uf. 13:3-4).

(2) Wakuu wa dola (marais, wafalme, masultani nk.) wote watamtegemea yeye na kumpa mamlaka na nguvu zao za kidola. Hivyo watatawala kwa kufuata apendavyo "mnyama". Kwa hiyo watakuwa mawakala wa mnyama katika nchi zao. Kwa hiyo nao watakuwa mawakala wa "Joka" (Shetani). "... Na zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme (watawala) kumi, ambao hawajapokea ufalme bado, lakini wapokea mamlaka kama wafalme muda wa saa moja pamoja na yule mnyama. Hawa wana shauri moja, nao wampa yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao: (Uf. 17:12-13).

(3) Mnyama huyu ili kufanikisha kaziyake vizuri, atasaidiwa na "Manabii" wake wa uongo wakifanya "miujiza" mikubwa itakayowalazimisha wanadamu wamtii mnyama. Yaani mtawala huyo (mnyama) atakuwa na wanasayansi (manabii wa uongo) watakaofanya miujiza mikubwa ya kisanyansi, ikiwa ni pamoja na kutengeneza makombora (moto) yatakayotupwa toka angani (mbinguni). "... Naye (Nabii wa uongo) afanya ishara kubwa, hata kufanya moto (kombora) kushuka kutoka mbinguni (angani) uje juu ya nchi mbele ya wanadamu." (Uf. 13:11-13).

(4) Kutokana na nguvu anazopewa na wanasayansi (manabii) na kiuchumi, dunia yote itajinyenyekeza kwake (itamsujudia). Mtu au dola itakayokataa kujinyenyekeza kwake itapigwa na kuuwawa. "(Nabii wa uongo) akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauwawe." (Uf. 13:15). Hivyo dunia nzima ikawa haiwezi kufanya jambo lolote bila kuwa na utambulisho (chapa) kuwa nchi au mtu huyo anafuata utaratibu wa maisha autakao mnyama (Demokrasia). Au hata kama hafuati demokrasia (chapa), lakini lazima akubaliane na matakwa ya mnyama ja apate idhini ya mnyama yaani "hesabu jina lake". "... tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake" (Uf. 13:16-17).

Nadhani mpaka hapo msomaji tayari umeshamnyooshea mtu kidole. Naomba usifanye hivyo. hebu endelea na sifa hii ifuatayo:

(5) Atasema maneno machafu na ya kufuru dhidi ya Mwenyezi Mungu. Yaani atafanya dharau kubwa kwa vitu vilivyotukuzwa na Mwenyezi Mungu, pamoja na utaratibu au kanuni zilizoamriwa na Mwenyezi Mungu "Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni." (Uf. 13:6). Hapa nitoe mfano hai mmoja. Mtume (s.a.w.) amesema, "Mwenyezi Mungu (s.w.) amesema, mwezi wa Ramadhani ni mwezi wangu." na katika hadithi nyingine amesema "Mwenyezi Mungu anasema .......... saumu ni yangu mimi". Sasa rejea mwanzoni mwa Ramadhani ya mwaka huu ambako Bill Clinton aliipiga Iraq kwa makombora aliyoyaandika hivi, "Here is a Ramadan present from chao Rickendero" (Yaani. Hii ni zawadi ya mwezi wa Ramadhani toka kwa mharibifu wa halaiki). Maandishi yanaendelea kusema, "The boys in they will say hellow and goodby" (yaani. Vijana wa huko Iraq watasema karibu kombora kisha watakuwa kwaheri - watakufa). Angalia An-Nuur na. 183 ya Januari 8-14, 1999 uk.8 Sasa ndugu msomaji linganisha zile hadithi Quds na hizo "zawadi" za Clinton kwa Waislamu (wafuasi wa Yesu) wa Iraq.

Kahaba Mkuu - Ufunuo 17:1-7

Ili tujue kwa uhakika zaidi nani ni "Mnyama", lazima tumjue pia nani ni "Kahaba mkuu". Kwani mnyama" na "kahaba" wanafanya kazi moja pamoja, na wanaishi pamoja (nchi moja). ufunuo unasema "... Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi, ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo wa uasherati wake." (Uf. 17:1-2). Tafsiri ya "kahaba" ni hii ifuatayo: "Na yule mwanamke uliyemuona ni ule mji mkubwa, wenye ufalme (madraka) juu ya wafalme wa nchi" (Uf. 17:18). Tafsiri ya "maji mengi" ni hii, "Kisha akaniambia yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa, na makutano na mataifa na lugha". Uf. 17:15). Na "ulevi wa uasherati wake" ni zile athari zinazotokea wakati wa ushirikiano wa mji huo mkubwa na nchi nyingine duniani (uzinifu). Hivyo tukionesha tafsiri hizo tunaona kuwa, kabaha ni mji mmoja mkubwa na maarufu ambao utakuwa na madaraka ya kupanga utaratibu wa kuendesha dunia. Na kuwa nchi na taasisi zote za kimataifa zitakuwa na mwakilishi (balozi) katika mji huo, ili kuthibitisha nchi au taasisi iko chini ya uamuzi wa mji huo. Kwa lugha nyepesi ni kusema, "kahaba" ni mkao makuu ya umoja wa mataifa.

Ama "ulevi wa uasherati wake", ni ile mikakati michafu inayopangwa katika mji huo, ambayo inasababisha dunia nzima iharibike (ilewe). Mikakati hiyo ni kama, utaratibu wa maisha (demokrasia), mpango wa uzazi (condom nk), sheria na kanuni, kasumba na ustaarabu wa mji huo, kama vile, mavazi, mitindo ya nywele, muziki, starehe mbalimbali kama vile ngono huria, vinywaji - ulevi nk. Hivyo kwa kuwa dunia nzima "italewa" mambo hayo, mtu ambaye "hajalewa" ataonekana ni msaliti. Hawa watakuwa wachache sana, lakini watakatifu sana mbele ya Mwenyezi Mungu kwani wamevumilia mateso makubwa kwa kukataa kumtii (kumsujudia) mnyama.

Ufunuo unaendelea "Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu na kwa damu ya mashahidi wa Yesu" (Uf. 17:6). Kama nilivyosema mwanzoni kabisa kuwa, "mashahidi wa Yesu" ni Waislamu waliouawa wakipigania Uislamu, (dini ya Yesu a.s.) au waliouwawa kwa kudhulumiwa na kuonewa bila kosa lolote au kufanya chochote cha kidini. Hawa ni watoto, akina mama, wazee, viwete nk. Hivyo aya ya Uf. 17:6 inamaanisha mauaji ya mujahidina (watakatifu) na mauaji ya wasio na hatia. Kwa hiyo "ulevi" wa kahaba ni yale "mawenge" ya umoja wa mataifa yanayotokana na oparesheni za kuangamiza Waislamu walizozipanga na kuzitekeleza. Hivyo kutokana na "ulevi" (mawenge) huo umoja wa mataifa badala ya kusuluhisha migogoro duniani, ndio unachochea zaidi.

Kuangamizwa kwa mnyama na Kahaba

Baada ya dadili zote nilizozitaja kuonekana wazi, na kujulikana nani ni mnyama na nani ni kahaba, inachofuatia ni kuangamizwa kwa mnyama na kahaba. Aidha watawala na dola zote zilizomtii mnyama zitaangamizwa pamoja naye. Maangamizi yanatangazwa rasmi katika Ufunuo 18:1-3. "Baada ya hayo naliona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake. Akalia kwa sauti kuu, akisema, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza; kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake."

Kisha yanafuatia maombolezo na masikitiko toka kwa nchi zote na watu wote waliofaidika kwa utaratibu wa "mnyama" na "kahaba". Tazama Uf. 18:9-24.

Wakati waovu duniani wakiomboleza, malaika, watakatifu na viumbe vyote mbinguni wanashangilia na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Tazama ufu. 19:1-9. Maneno wayasemayo ni pamoja na "... Haleluya; wokovu na utukufu na nguvu zina Bwana Mungu wetu. Kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake." (Uf. 19:-12). Pia wanawahimiza wachamungu walioko duniani nao washangilie. "Sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi ikisema, msifuni mungu wetu, enyi watumwa wake wote, ninyi mnaomcha, wadogo kwa wakuu" (Uf.19:5). Sababu kuu ya shangwe hiyo mbinguni na duniani (wacha Mungu tu) ni kuwa, sheria za binadamu (za shetani) zimefutwa pamoja na utawala wao. Badala yake imesimama dola iliyo chini ya Mwenyezi Mungu mwenyewe (Sheria za Kiislamu). "Nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikasema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, AMEMILIKI" (Uf. 19:6).

Kisha oparesheni ya uangamizi inaanza ikiongozwa na mtu aitwaye "mwaminifu na wa kweli", akisaidiwa na majeshi toka mbinguni (uwezo na nguvu za Mwenyezi Mungu - Roho mtakatifu). Tanzama Ufunuo 19:11-21. Hata hivyo "Mnyama" akisaidiwa na mataifa yote yanayomuabudu (yanayofaidika kwake), watajaribu kupigana na majeshi ya Mwenyezi Mungu (mujahidina), lakini watashindwa vibaya kisha "Mnyama" na viongozi wote waliomsaidia watakamatwa na kusulubiwa misalabani. (Tazama Uf. 19:19-20). Aidha watu wote wa dini zote (Waislamu na wasio Waislamu), watakaomsaidia "mnyama" kwa hali yoyote ile, nao wataangamizwa (Taz. Uf. 19:17-18).

Hatimaye Dola ya Mwenyezi Mungu inasimama duniani kote na shetani anaondolewa kabisa kwa muda wa miaka elfu (mrefu). (Uf. 20:1-3). Hivyo mujahidina nao wanapata nafasi ya kutawala dunia yote. "Kisha nikaona viti vya enzi (utawala), wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu (uongozi - madaraka); nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake (mtawala anayemtii mnyama), wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai wakatawala pamoja na kristo miaka elfu." (Uf. 20"4). Tafsiri ya aya hii ni kuwa, utawala wa dunia utakabidhiwa kwa wale mujahidina (wanaharakati) walioteswa, kuudhiwa na kunyanyaswa kwa kuhubiri ukweli (ushuhuda) juu ya Yesu (a.s.), kupigania dini ya Mwenyezi Mungu (Uislamu) nk, pamoja na wote waliokataa kumtii mnyama. Hivyo wanapata heshima na ubora wao ("...Wakawa hai") wanaostahili, wakitawala pamoja na kiongozi wao mkuu aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu (Khalifa - Kristo) kwa muda mrefu sana. Naona nifafanue wazi hapa kuwa neno "waliokatwa vichwa", halimsanishi watu waliouwawa katika harakati za dini, bali walioteswa, walionyanyaswa, waliodharauliwa au usumbufu wowote kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu (Uislamu). Wanaharakati waliouwawa kabisa hawatafufuka kama isemavyo aya ya tano. "Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu." Yaani hawa watafufuka baada ya utawala wa kidunia uishe (mwisho wa dunia)." Ufufuo" uliotajwa katika aya ya nne ni uhuishaji dini. Hivyo baada ya kuhuishwa dini na utawala wa Mwenyezi Mungu ukasimama barabara, watakaoingia motoni (jehannamu) watakuwa wale tu madhaifu sana kiroho kama aya ya sita inavyosema, "Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili (Jehannam) haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa mungu na wa Kristo (mtawala wao mkuu) nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu." Ufuno juu ya mwisho wa dunia Unaanzia katika Ufunuo 20:7 hadi 22:

5. ("miaka elfu" = Dolaya Kiislamu itadumu kwa muda mrefu sana).

Mwisho nawaleza wanaharakati wote na watu wote wasiopenda uchafu waislamu na wasio Waislamu kuwa, oparesheni hii ni ya kuondoa uchafu kwa kumwangamiza "mama wa uchafu" (mnyama) na sio ya kusilimisha watu kwa nguvu. Utaratibu wa kusilimisha watu unabaki pale pale kama ulivyowekwa na Mwenyezi Mungu (s.w.). Hikma, mawaidha mema na mijadala mizuri. Na inabaki kuwa ni hiyari ya mtu kukubali au kukataa Uislamu (Taz. Kur. 2:256, 13::11, 10:108 nk.).

Aidha tujue kuwa, japo oparesheni hii imepangwa na Mwenyezi Mungu (s.w.), lakini watekelezaji wakuu ni sisi binadamu,japo msaada mkubwa utatoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.) mwenyewe. Pia tujue wazi kuwa, itatubidi tutumie nguvu nyingi sana (akili, ujuzi, mali nk). "Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari akisema, kama hivi, kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli, mji ule mkuu, wala hutaonekana tena kabisa" (Uf. 18:21). Hivyo tujiandae ipasavyo. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook