BARUA
 

Yaliyotokea UDSM yaikumba IDM

Ndugu Mhariri

NIMEKUWA nikifuatilia chaguzi mbalimbali katika vyuo, taasisi za elimu na nchi nzima kwa ujumla. Nilichogundua hasa miaka hii ya karibuni mpaka sasa ni kuwa athari zilizopandikizwa na wapinzani wa Uilamu tangu ukoloni mpaka leo zimekuwa kubwa na zenye madhara juu yetu.

Imefikia hatua ambapo sasa Muislamu anaogopa kugombea kwa kuwa anahisi wale wasio Waislamu hawawezi kumchagua ati kwa sababu yeye ni Muislamu hivyo kutunyima nafasi ya kuiongoza jamii nchini na nje hatimaye kuzidi kumkosesha Muislamu kutoa mchango wake wa kuongoza.

Nikianzia na UDSM, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika uchaguzi wa serikali ya wanafunzi (DARUSO) mapema mwaka huu alitokea kijana mmoja aliyekuwa na sifa zote kabisa za kupata nafasi ya Urais wa DARUSO (Umoja wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) lakini baadaye kushindwa kabisa katika uchaguzi huo, hii ilitokana na uzushi na propaganda zilizopandikizwa kuwa Muislamu huyo alikuwa akifanyiwa kampeni Msikitini.

Hali hii ilipelekea watu wasio Waislamu kumkataa na kumkejeli mgombea Muislamu huyo na hatima yake kupatikana Rais na Makamu wake pia kuwa sio Muislamu kwa taarifa ya Majira asubuhi Redio Tanzania na ripota Fredrick Alex Mtoi mwanafunzi wa mwaka wa pili ambaye ni Mtangazaji wa City Radio mwishoni mwa mwezi wa pili mwaka huu.

Aidha, katika uchaguzi uliofanyika Chuo cha Uongozi wa Maendeleo ya Wananchi Mzumbe -IDM yale waliyoyapata wenzetu UDSM yamewakumba ambapo aliyetarajiwa kugombea Muislamu alizushiwa kuwa alifanyiwa kampeni Msikitini hapo Chuoni na wajahidina wenzake na hivyo kuhadharisha watu wasimpe kura ati kwa kuwa yeye ni Muislamu na hatima yake uchaguzi huo ulifanyika Mei 2, mwaka huu siku ya Jumapili saa 2:30 - 6:30 ambapo Bw. Edward Maghali anayesomea Utawala na ambaye amesomea Upadre na hatimaye kuachana na Upadre huo ndivyo kujiunga na IDM alishinda lakini yeye kama alivyojieleza siku moja kabla ya uchaguzi amesomea seminari ya ndani na nje ya nchi hatukumwita ni mtu wa dini, lakini yule aliye Muislamu kuitwa Mujahidina.

Na kitu kilichodhihirisha ni kwa Rais huyo (Edward Maghali) kuteua baraza lake la Mawaziri ambalo nina imani Muislamu ni mmoja au wawili tu. Je, ameona Waislamu hawawezi kupata nafasi hizo katika Wizara zaidi ya tano? Jee, huu siyo ubaguzi na udini? Yale yale ya PAROLE, kuwabagua Waislamu ndiyo yanayojitokeza. Nadhani hata ngazi za juu kitaifa upo ubaguzi huuwa kutaka Muislamu asipate nafasi (fuatilia uchaguzi mkuu tangu uhuru).

Kwa hiyo ndugu Waislamu mnatambua ni hali gani dhahili mliyojayo vyuoni kwenu chukueni wasaa huu kuunda mbinu za kupata uongozi kwani takwimu zinaonyesha kuwa ni wachache kama hakuna kabisa Waislamu walioshika nyadhifa hizo kubwa katika vyuo vya elimu ya juu.

Na pia changieni kuondoa hisia za kisaikolojia kuitwa mjahidina unaonekana dhahiri bado tuna nafasi yakuwa Makhalifa wa kuiongoza jamii ya watu.

Kikwite Ramadhani,
Morogoro.


Yawe maafikiano ya dhati

Ndugu Mhariri

NINA hamu kubwa ya kupata nafasi katika gazeti lako ili nipate kutoa yalio katika moyo wangu ili mimi na moyo wangu tupate muafaka.

Si jingine bali ni suala lililokuwa Juni 9, mwaka huu, suala hili kwa hakika linahitaji utekelezaji wa hayo yaliokubaliwa, sio kuyakubali tu bali pia kuyazingatia na kuyatekeleza.

Kwani kama itakuwa hakuna utekelezaji basi itakuwa tumepuuza kazi iliyofanywa na Chifu Emeka Anyaoku ambaye ametoka huko alikotoka kuja hapa nchini kuwapatanisha Waislamu wawili ambao walikuwa na uhasama wa kisiasa nao ni Dk. Salmin Amour Juma na Maalim Seif Shariff Hamad.

Kwa hiyo ikiwa utekelezaji wa maafikiano hayo au makubaliano hayo kama ambavyo wengine wanapenda kutafsiri yatakuwa mazuri basi ni dalili tosha ya kuelekea katika muelekeo ulio bora kabisa wa kiuchumi.

Ikiwa mshikamano wa kisiasa wa viongozi hao hautakuwepo basi itakuwa ni sawa na kumimina maji ndani ya pakacha.

Tunautakia kila la kheri muafaka huu. AMIN.

Abeid Rashid Abdallah,
P.O. Box
Dar es Salam,
Tanzania.



Muafaka wa CCM na CUF Zanzibar

Ndugu Mhariri

HAITAKUWA busara kukaa kimya bila kutoa shukrani za ukubwa wa busara za viongozi wa CUF na CCM visiwani Zanzibar kwa kufikia muafaka ambao ni faida kwa Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla.

Kwa kweli ulimwengu unakabiliwa na matatizo makubwa kwa kisingizo sawa na kile kilichokuwa Zanzibar kabla ya kufikiwa muafaka wa kisiasa.

Uturuki, Uingereza na Ireland, Kosovo na Yugoslavia, Somalia, Eritrea na Ethiopia, Sudan, Siera Leone, Guinea Bissau, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Commoro wahusika ni UN.

Hizo ni baadhi ya sehemu ambazo madhara yaliyopatikana katika nchi hizo walio wengi wanayafahamu.

Baadhi ya hasara iliyopatikana ni pamoja na vifo kwa watu ambao ndio wazalishaji wa uchumi katika nchi husika. Vijana, watoto, wazee, akinamama ambao ndio walezi wa kizazi kipya, uharibifu wa mali, madaraja, viwanda na nyumba za kuishi raia na kadhalika ukitathmini hasa hiyo kwa Paundi au Dola ni gharama kiasi gani?

Kwa kuzingatia hayo kwa hili letu kuishia hapa yatubidi tushukuru Mungu na tupongezane kwa dhati.

Ni sisi Shaaban Ambar
Maulid Japhar.



Mahari lazima ilipwe

Ndugu Mhariri

MWENYEZI Mungu amesema katika Qur'an tukufu sura (33:36) kuwa: "Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri wawe an hiyari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotofu (upotevu) ulio wazi (kabisa)".

Kitendo cha mtangazaji mmoja maarufu wa ITV na Radio One kusimama na kutetea hoja kuwa mahari haipaswi kulipwa kimeonyesha jinsi gani Bwana huyo asivyouelewa kabisa Uislamu au labda kutokana na fikra potovu alizoivishwa toka katika kizazi alichokikuta.

Katika kipindi maarufu cha 'MALUMBANO YA HOJA" kilichoruhswa wiki iliyopita kilichokuwa na HOJA ya kuwa Je; mahari kwa wakati wa sasa inapaswa kulipwa au la! Bwana huyo ambaye ni maarufu katika kipindi cha SPOTI LEO na akiwa ni Muislamu alidiriki kusema kuwa mahari haipaswi kulipwa na akapendekeza angalau ianzishwe sera ya wanaume nao walipiwe mahari.

Kitendo cha kujifanya hajui na kutaka kuzigeuza amri za Allah (s.w.) ni upotofu mkubwa.

Allah (s.w.) kasema: "Na wapeni wanawake mahari yao, hali ya kuwa ni hidaya (aliyowapa Mungu). (Lakini hao wake zenu) wakikupeni kwa radhi ya nafsi zao kitu katika hayo (mahari) basi kuleni kwa furaha na kunufaika" (4:4).

Pia Allah (s.w.) kasema: "Na kama mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke (yaani kumwoa mke mwingine na kumwacha huyo wa zamani) na hali mmoja wao (naye ndiye huyo unayemwacha) mmempa mrundi wa mali, basi msichukue chochote je, mnachukua kwa dhulma na kwa khatia iliyo wazi". (4:20)

Kutokana na aya hizo hapo juu napenda kumfahamisha Bwana huyo pamoja na wote wenye mtizamo kama wake kuwa sheria za Allah (s.w.) zilizotajwa katika vitabu hazitakiwi kujadiliwa na kurekebishwa kama unavyoweza kubadili yaliyomo kwenye katiba au vitabu tofauti na Qur'an ili kuweza kupata muafaka.

Ahmed Shamdas,
Dar es Salaam.



Shukurani! Vitabu nimevipata

Ndugu Mhariri

APRILI 28, mwaka huu nimepokea zawadi ya vitabu toka kwa ndugu yangu aliyeko nchini Switzerland (Uswisi) ambaye hakujitambulisha.

Hata hivyo bila shaka ni msomaji wa gazeti la AN-NUUR. Hivyo nimeona nipitishie shukrani zangu za dhati kwake na kuthibitisha kupokea zawadi hiyo.

Kwa barua hii namthibitishia ndugu yangu huyo kupokea vitabu sita (6). Namuomba Mwenyezi Mungu ampokelee sadaka yake na amzidishie mapenzi kwa ndugu zake Waislamu popote walipo duniani. Aamiin.

Sheikh Bernard P. Nyangasa,
P.O. Box 96,
Korogwe.



Wanaojichubua wanamkosoa Mungu, je anayeua anamtengenezea nani?

Ndugu Mhariri

WAKATI Dk. Omari Ali Juma akiwahutubia akina mama wa Kiislamu katika kongamano liliandaliwa na Muslim League aliwatahadharisha akina mama juu ya kujichubua na akawaeleza madhara yake ni kumkosoa Mungu na yule anayemkosoa Mungu makazi yake ni motoni.

Ni maneno muafaka kweli haijuzu kujichubua lakini swali linabakia hapa je, kujichubua na kuua lipi kosa kubwa zaidi? Mungu anasema:

Na mwenye kumuua Muislamu kwa kukusudia basi malipo yake ni Jahannam, humo atakaa milele na Mwenyezi Mungu amemghadhibikia na amemlaani na amemwandalia adhabu kubwa. (Surat An-Nisaa 4:93)

Polisi wameua raia kimya, polisi wameua Mwembechai na umma wote umeshuhudia lakini polisi badala ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu wamesifiwa kwamba wao sio mbwa wa kutupiwa mawe, wengine wakasema hata jiwe lilimuua Goliether.

Je, lipi la kukemewa? Kama ni suala la kujichubua, watu wanaojichubua tunafanya nao kazi asubuhi na na jioni, hivi kosa afanye Miriamu akanywe Fatuma ndio njia sahihi ya kufikisha ujumbe?

Waislamu hatuhitaji kuchaguliwa lipi tulifanye au tulifuate katika Qur'an na hili ngojea mradi Qur'an inasema:

Enyi mlioamini! Ingieni katika hukumu za Uislamu zote wala msifuate nyayo za shetani. Kwa hakika yeye kwenu ni adui dhahiri. 2:208.

Kwa hiyo Waislamu haki zetu sio kusali, kufunga, kutoa zaka, kwenda kuhiji, ila hayo yote yanamuandaa mwanadamu katika kulifikia lengo la funga tupate kuwa wacha Mungu. (Rejea Qur'an 2:183).

Lengo la swala ni kumkataza mtu mambo maovu na machafu kama vile kugawa kondomu katika mikutano au wanafunzi wa shule ili wazini salama. Kwani Mungu anasema lengo la sala ni kumkataza mtu mambo maovu na machafu. (Rejea Qur'an 29:45)

Muislamu anayesali hawezi kufungua maonesho ya Wenge BCBG, wanawake walokuwa uchi wanakata viungo vyao ovyo na asiwafikishie kwamba hilo wanalolifanya siyo sahihi.

Uislamu unatuhimiza kusema tunayoyatenda. Lengo la Muislamu sio kusikiliza sauti ya msomaji bali lengo la kusikiliza Qur'an ni tupate kurehemewa. 7:204 inasema Na isomwapo Qur'an isikilizeni na nyamazeni ili mpate kurehemewa.

Kwanini tusiandae wale ambao wametekeleza Qur'an ipasavyo sio kusoma kama shairi. Mungu ni mjuzi kwa yale tunayoyasema.

Abuu Hafsa,
P.O. Box 16617,
Dar es Salaam.
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook