Na Yassin Sadik
VIONGOZI wa Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania BAKWATA juzi walianza kufanyia kazi zao 'uhamishoni' katika eneo la Upanga Magharibi nyumbani kwa mkubwa mmoja wa baraza hilo ili kupanga mashambulizi ya kukomboa ofisi zao zilizowekwa chini ya ulinzi siku ya Jumamosi na Waislamu wanaopendelea mageuzi ndani ya BAKWATA.
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari jana utokana na tukio hili la aina yake hapa nchini, umeonyesha kuwa zaidi ya Masheikh 20 na viongozi wa BAKWATA wa mikoa yote ya Tanzania bara ambao walikuwa mjini Dar es Salaam kusubiri jawabu la kuonana na Rais Ali Hassan Mwinyi baada ya mkutano wa Morogoro juu ya kusakamwa BAKWATA, walionekana kufadhaika na wengine wakijadili majaliwa ya uongozi wa Waislamu.
Huko Kinondoni yaliko makao makuu, waandishi wa habari walikuta kundi kubwa la Waislamu wanaendelea kuchunga milango yote ya ofisi na majengo mengine, ikiwemo nyumba ya Sheikh Mkuu huku magari yakiwaletea vyakula na huduma zinazostahiki.
Ulinzi wa aina hiyo umewekwa pia katika ofisi ya BAKWATA mkoa wa Dar es Salaam iliyoko kona ya mtaa wa Agrey na Lumumba, na pia Alharamain ambako huko palikuwa panalindwa kwa doria kali.
Baadhi ya waliokuwa wanadhibiti ulinzi wa shule hiyo ni kati ya walimu 14 waliofukuzwa shuleni hapo mwezi Oktoba mwaka jana kwa kile kilichoelezwa kuwa hawakuelewana na Mkuu wa Chuo kuhusu maslahi na mikataba ya kazi.
Mmoja wa maofisa walioonekana kusimamia mipango ya kuchukua uendeshaji wa ofisi za BAKWATA aliwaeleza waandishi wa habari jana hiyo kuwa watakuwa tayari kulegeza msimamo wao ikiwa viongozi wawili wa makao makuu watatangaza kujiuzulu wenyewe. Viongozi hao aliwataja kuwa ni Alhaj Suleiman Hegga ambaye ni Kaimu Makamu Mwenyekiti na Alhaj Mahami Rajabu Kundya ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu.
Kwa mujibu wa ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini viongozi hao inadaiwa wanaendesha chombo cha Waislamu kama kampuni ya mtu binafsi au kambi ya jeshi.
Alipoulizwa kuhusu hatua waliyochukua baada ya kukamata maofisi ya BAKWATA, msemaji huyo alieleza kuwa "vinginevyo tumeshaiomba serikali iwaondoshe watu hao wawili kwa ajili ya usalama na amani ya Taifa hili, isimamishe katiba ya BAKWATA ya 1984 na hapo hapo Sheikh Mkuu awajibike kwa kufumbia macho maovu, dhulma, dharau na madhambi yanayofanywa na watendaji wake dhidi ya Waislamu wa nchi hii kwa zaidi ya miaka 15 sasa.
Juhudi za kumpata Sheikh Mkuu Hemed bin Jumaa bin Hemed zilishindikana jana ili kupata maelezo yake juu ya mgogoro huu maana inasemekana kuwa siku moja kabla ya tukio hilo alihamisha familia yake iliyokuwa inaishi karibu na Makao Makuu ya BAKWATA na hivyo kila akitafutwa huambiwa "yuko Tanga".
Mwenyekiti wa jumuiya hizo za Kiislamu ambazo inadaiwa zimeungana kuchukua nafasi ya BAKWATA Sheikh Salum Khamis alieleza kuwa katiba ya kuendesha baraza hilo jipya imepitishwa Jumamosi walipokutana Waislamu wa nchi nzima, na tayari imeshawasilishwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ili kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Alipoulizwa juu ya kuvamia ofisi za watu, ofisa mwingine ambaye naye aliomba asitajwe jina alidai kuwa "hata hao wakubwa wawili (Hegga na Kundya) wanaong'ang'ania uongozi hawakukabidhiwa baraza hilo bali walifanya hila na ujanja kwa siri na kutangaza ghafla kuwa wametwaa madaraka, na makabidhiano (kama yapo) yalifanyika baada ya kuwatimua wenzao maofisini.
Mpaka sasa ni miezi 18 Waislamu hatujaitwa kuelezwa walikabidhiwa nini, kitu gani kimepungua au kuongezeka, makosa gani yaliyowapelekea kuwaondosha wenzao na maendeleo gani yamepatikana, hivyo tumechoka kutapeliwa na watu ambao hata serikali iliwatimua kwa kujifanya maarufu kumbe wabadhilifu", alieleza huku akionyesha uchungu.
Mpaka sasa kila upande unadai kuwa umepeleka taarifa zake Ikulu na kuomba maamuzi ya Rais Mwinyi juu ya purukushani za uongozi imara wa Waislamu.
Wakati gazeti hili linakwenda mitamboni polisi waliendelea kufanya doria kwenye maeneo hayo ili kuhakikisha usalama wa wananchi. Hata hivyo wafanyakazi wa makao makuu na mkoa wa Dar es Salaam walionekana nje ya ofisi zao wakisubiri hatima ya patashika za ukubwa.
WAZIRI wa Mambo ya Nchi za Nje Ndugu Benjamin Mkapa aliwasili mjini Khartoum jana akiwa na salamu kutOka kwa Rais Nyerere kwenda kwa Rais Jaafar Nimeiri wa Sudan, Shirika la Habari la Sudan (SUNA) limeeleza.
Shirika hilo limesema kwamba,
salamu hizo zitaimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili, pia zitafafanua hali
ya hivi sasa katika Afrika Mashariki, lakini halikutoa maelezo zaidi.
--
|
|