CHAKULA NA LISHE
 
Virutubisho kwenye matunda
 

MATUNDA ni moja ya chakula muhimu kwa mwanadamu. Hata hivyo, matunda pekee siyo mlo kamili kama baadhi ya watu wanavyoelewa. Kwa maneno mengine ili uwe na afya nzuri lazima ule matuda na vyakula vingine kama vile nyama, mahindi, maharage, samaki, mboga mboga, karanga na kadhalika.

Makala hii inalenga kuonesha kwa ujumla virutubisho (nutrients) vinavyopatikana katika matunda ili watu wafahamu na kuamini kuwa matunda pekee siyo mlo kamili, na hatimaye waweze kula vyakula vya aina mbalimbali.

Kwanza, watu wanatakiwa wafahamu kuwa sehemu kubwa (75 - 95%) ya matunda ni maji. Hata hvyo, maneno haya hayamaanishi kuwa maji siyo kirutubisho cha maana. Kama tunavyojua kuwa maji ni kitu muhimu sana kwa afya ya binadamu. Isitoshe zaidi ya asilimia 55 ya mwili wa mwanadamu ni maji. Ila ninalokusudia kuonesha hapa ni kuwa mwili lazima upate virutubisho vyote muhimu kwa afya nzuri.

Pili, matunda mengi yana kiasi kidogo sana cha protini. Hata hivyo baadhi ya matunda kama vile Avokado (Ovacado) na Olive yana kiwango kikubwa cha mafuta (yanafika 40%).

Tatu, matunda yanaviwango tofauti vya wanga na sukari. Kwa mfano ndizi mbichi zina wanga kiasi cha asilimia tatu (3%) na sukari asilimia 1.2. Lakini ndizi mbivu zinakiwango kikubwa cha sukari.

Matunda mengine maarufu Tanzania ambayo yana kiwango kikubwa cha sukari ni kama vile tende kavu (63.9%). Epo (11.8%); Black Currents (63.1%), embe (15.3%), machungwa (8.5%), mananasi (11.6%), pasheni fruti (6.2%) na kadhalika.

Nne, matunda ni chanzo kikubwa cha vitamini C. Hata hivyo, matunda yaliyokaushwa au yaliyotengenezwa na kuwa katika hali ya unga, yana upungufu mkubwa wa vitamini C. Hii kwa sababu vitamini hiyo ni rahisi kupotea wakati wa utengenezaji wa matunda kiwandani au hata nyumbani. Ila kama vitamini itaongeza makusudi.

Tano, matunda ni chanzo kizuri cha nyuzi nyuzi za kilishe (dietary fibres). Matunda yenye kiwango kikubwa cha nyuzi nyuzi na pia yanafahamika Tanzania ni kama vile Pasheni fruti (15.9%), tende (8.7%), Currents (8.7%).

Kama tulivyowahi kuona katika makala zilizopita, nyuzi nyuzi za kilishe ni muhimu sana kwa afya zetu. Kwanza, zinasaidia kumfanya mtu apate choo kikubwa mara kwa mara. Yaani zinaondoa tatizo la kukosa choo kikubwa (constipation).

Pili, zinasaidia kunyonya sumu ambayo inaweza kuwepo kwenye utumbo. Sumu hiyo inaweza kuwemo tumboni kutokana na chakula tunachokula au imezalishwa na vijidudu vilivyomo katika utumbo wa mwanadamu.

Zaidi ya virutubisho hivyo tulivyoviona hapo juu, matunda pia ni chanzo cha madini ya aina mbalimbali. Madini yana kazi nyingi katika mwili wa mwanadamu.

Sasa napenda kuhitimisha makala hii kwa kusisitiza kuwa matunda ni chanzo kizuri cha baadhi ya virutubisho na hasa vitamini C. Lakini lazima tule vyakula vingine ili tuweze kupata virutubisho tunavyovikosa katika matunda.

Mfano wa vyakula hivyo ni aina mbalimbali za nyama (halali), maharage na jamii yake, ulezi, mboga mboga, maziwa, asali na kadhalika. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook