KUHUSIANA na jambo hili hatuna budi kuzingatia kuwa Uislamu si mfumo uliobuniwa na watu bali ni mfumo utokao kwa Allah. Na Wahyi ni haki yenye yakini na ukweli wa milele usiohitaji marekebisho yoyote. Kama tulivyoona huko nyuma tunapozungumzia demokrasia au theokrasia, au ujamaa, ukomunisti, ubepari, nakadhalika. tunazungumzia mifumo iliyobuniwa na watu ambao mawazo yao ni finyu yanayonitajia marekebisho ya mara kwa mara. Hivyo basi itakavyokuwa vyovyote mifumo hii haiwezi kulinganishwa na Wahyi. Maadam haitoki kwa Allah mifumo hiyo ni dhaifu na si mikamilifu. Kunaweza kuwapo jambo moja au mawili mazuri katika mifumo hiyo lakini katika ujumla wake mifumo hiyo ni dhaifu. Ni makosa makubwa kulinganisha Uislamu na demokrasia kwa lengo la kuonyesha kuwa Uislamu ni mfumo mzuri kwa sababu unaona na demokrasia. Ni dhahiri kuwa zipo sehemu chache katika demokrasia ambazo zinakubalika katika Uislamu, lakini Dola ya Kiislamu si sawa na ile ya kidemokrasia.
Kufanana na kutofautiana kwake na Demokrasia
Serikali ya Kiislamu
1. Watu wote wako chini ya Ufalme au utawala wa Allah (s.w.) na kila mtu ameku sudiwa awe Khalifa, wa Allah (s.w.) katika kusimamisha ufalme wake hapa ulimwenguni.
2. Itikadi na sheria zinatoka kwa Allah (s.w.) kupitia kwa Mitume wake.Kila Muislamu anawajibika kutii sheria za Allah na kutii maelekezo ya Mtume. Hakuna aliye juu ya sheria wote wanahukumiwa sawa.
3. Dola ya Kiislamu iko kwa madhumuni ya kusimamisha ufalme wa Allah na kutafuta radhi yake. 4. Kwa ujumla Dola ya Kiislamu iko chini ya mamlaka ya Allah (s.w.) na Mtume wake, na huendesha mambo yake kwa kuchunga barabara mipaka ya Allah (s.w.) na Mtume wake.
Serikali ya kidemokrasia
1. Ufalme au utawala uko chini ya watu walio wengi (popular sovereignty).
2. Itikadi, sheria na sera hutungwa na Wananchi au wawakilishi wao katika bunge au kamati za vyama. Na kiongozi wa juu wa nchi (Rais) amepewa madaraka makubwa ya kuwa juu ya sheria.
3. Madhumuni ya serikali ni kutosheleza mahitaji na matashi ya raia "walio wengi".
4. Dola ya kidemokrasia ina mamlaka ya mwisho na uhuru wa kuendesha mambo bila ya kuwa na yeyote aliye juu yake.
Tafauti kati ya serikali ya Kiislamu na ile ya kidemokrasia
Baadhi ya kanuni za demokrasia zinazokubalika katika Uislamu ni hizi zifuatazo:
(i)Uhuru wa watu kuchagua viongozi wao.
(ii)Kanuni kuwa watu washiriki katika kufanya maamuzi ya kisiasa.
(iii)Haki ya watu kuibadili serikali isiyotekeleza au kutimiza matarajio yao.
Lakini pamoja na kuafikiana na kanuni hizo mfumo wa siasa wa Kiislamu siyo wa kidemokrasia kwa sababu zifuatazo:
Katika demokrasia kauli ya mwisho kabisa ni watu wenyewe. Ndio maana tafsiri maarufu ya demokrasia ni kama tulivyoona katika kurasa za nyuma kuwa ni"serikali ya watu inayoongozwa na watu kwa manufaa ya watu". Hivyo watu ndio wenye kauli au mamlaka ya mwisho. Katika Uislamu mamlaka yote ni ya Allah peke yake. Viongozi na watu wote wanatakiwa wajisalimishe chini ya sheria na amri za Allah.
Aidha, mfumo wa kidemokrasia unaweza kudhulumu haki za wachache kwa sababu haki ni ya walio wengi. Kwa mfano iwapo watu walio wengi ni wa kabila la Wasukuma na watu walio wachache ni kabila la Wamanyema basi Wasukuma wakitaka wanaweza kupitisha sheria kuwa watu wasile dagaa haliyakuwa wanajua kuwa Wamanyema ndicho chakula chao kikuu. Wamanyema wakilalamika Wasukuma watasema hebu tupige kura ili tuone wangapi wanataka dagaa. Kwa sababu Wamanyema ni wachache watashindwa. Wengi wape (demokrasia)!
Katika Uislamu dhulma kama hiyo haiwezi kutokea kwa sababu haki za watu wachache (Minority) zimehifadhiwa katika Qur'an na Hadith,- hivyo Waislamu hata kama ni wengi hawawezi kuwadhulumu Wakristo haki zao, hata kama Wakristo ni wachache kwa sababu Qur'an imewaamrisha wazitekeleze haki hizo. Na Muislamu hawezi kuipinga Qur'an halafu akabakia na Uislamu wake.
Katika nchi ya kidemokrasia hata kama haki za watu wote zitakuwa zimehifadhiwa katika katiba ya nchi bado watu hawawezi kuwa na dhamana kwa sababu hata hiyo katiba yenyewe yaweza kuvunjwa au kubadilishwa.
Serikali ya Kiislamu ni ya ki-Khalifa
Wapo waandishi wa kiislamu walioandika vitabu kuelezea namna Uislamu unavyokubaliana na itikadi za wakati fulani. Katika maandishi yao wamethubutu kutumia lugha ya kuona haya(apologetic language) wakijaribu kuonyesha Uislamu ni itikadi inayooana na itikadi zinazoibuka na kupapatikiwa na wengi duniani. Katika uwanja huu wa uandishi wa kuona haya kukaibuka misamiati kama "Islamic Socialism" yaani ujamaa wa kiislamu, demokrasia ya kiislamu na kadhalika. Haya ni mawazo potofu yenye taathira ya ukafiri ndani yake ambayo waandishi wa kiislamu hivi leo hawana budi kufanya kazi ya ziada kuyapiga vita yatokomee. Kwa hakika Serikali ya Kiislamu si ya kijamaa, kitheokrasia wala kidemokrasia bali ni serikali ya Ukhalifa wa watu wote (Popular vicegerency). Allah amewajaalia watu wote kuwa ni Makhalifa wake hapa duniani, na ufalme ni wake Allah peke yake. Hivyo kama Makhalifa au Manaibu wa Allah hapa duniani binadamu hawana mamlaka wao binafsi bali wajibu wao ni kutekeleza mamarisho ya Allah hapa duniani. Kiongozi na muongozwa wote wana hadhi sawa hakuna aliyejuu ya sheria
Haki ya Serikali ya Kiislamu kuzuia dhulma
Serikali ya Kiislamu inao wajibu na haki ya kuingilia kati ili kusimamia haki na kuzuia dhulma. Ni wakati gani kwa mfano ambapo serikali inaweza kuingilia kati. Allah ndiye aliyeziumba rasilimali zilizopo duniani na hivyo ni wajibu wa binadamu kuzitumia rasilimali hizo kwa manufaa ya watu na kwa ufanisi. Hivyo Serikali yaweza kuingilia kati iwapo rasilimali hizo zitatumiwa kuwadhulumu watu au hazitatumika kwa ufanisi.
Pili, baadhi ya kazi ni haramu katika Uislamu kwa sababu zimefungamana na mambo ya haramu, kama vile kamari, umalaya, uchawi, ulevi n.k. Ni wajibu wa serikali kuona kuwa mambo hayo hayapewi nafasi katika jamii.
Tatu, ni wajibu wa serikali pia kutoa fursa sawa kwa watu wote ya kuendeleza na kuvikuza vipaji vyao kwa kuwapa fursa sawa za elimu na mafunzo. Ni wajibu wa serikali kugharamia elimu kwa ajili ya manufaa ya watu wote. Elimu ni haki ya msingi kwa wanadamu wote.
Nne, ni wajibu pia wa serikali kuhakikisha kuwa hata katika zile kazi za halali kisheria zinafanywa kwa uadilifu pasi na dhulma yoyote. Yaani Serikali ihakikishe mathalani kuwa bidhaa zinazotolewa zimefikia ubora kwa wanaoizalisha, kuona kuwa uadilifu wa kitaalamu unadumishwa, kuona kuwa wafanyakazi wanalipwa mshahara wa haki.
Hata hivyo, Uislamu hauelemei upande mmoja tu wa kumtetea mfanyakazi peke yake wala kumtetea mwajiri peke yake. Wafanyakazi pia wakileta madai yasiyo ya haki ni juu ya serikali kuingilia kati.
Tano, ni wajibu wa serikali pia kuzuia mambo yanayoweza kudhuru watu, kwa mfano kama mtu akijenga kiwanda cha hatari katika makazi wanamoishi watu. Au hata mambo yanayoweza kuwatesa wanyama, kama kuwabebesha mizigo mizito sana hadi wanaanguka na kuvunjika miguu au kufa, au kuwafanyisha kazi kwa mateso makubwa na kutowapa chakula cha kutosha. Hali kadhalika serikali inaweza kwa mfano kuzuia magari au meli iliyopakia abiria au mizigo kuliko uwezo wake kusafiri.
Sita, katika suala la usambazaji wa bidhaa, serikali inaweza kuingilia kati iwapo watu watahodhi vyakula na bidhaa nyingine muhimu kwa lengo la kupandisha bei.
Saba, ni wajibu wa serikali kuweka au kutengeneza miundo mbinu (infrastructures) na kudhibiti, kwa mfano kujenga barabara, madaraja, reli, kusambaza maji ya mabomba, kujenga mitambo ya umeme, simu n.k..
Wakati wa Ukhalifa wake, Ali (r.a.) alimwambia Nahri, ambaye alikuwa mkuu wa jimbo la Misri; usifanye ukusanyaji wa kodi ya ardhi kuwa ndiyo kazi yako kubwa; kazi yako kubwa ni kuiendeleza ardhi hiyo.
Nafasi ya serikali katika ugawaji
Katika suala la ugawaji, wajibu wa serikali ya Kiislamu upo katika maeneo makuu yafuatayo:
(i) Kusimamia utoaji na ukusanyaji wa zaka. Serikali ndiyo yenye wajibu wa kuhakikisha kuwa kila anayempaswa kutoa Zaka anatoa na serikali inasimamia ukusanyaji wake.
(ii) Kutoza na kukusanya kodi iwapo zaka haikutosha.
(iii) Kutoza na kukusanya Jizya (aina ya kodi) kutoka kwa wasiokuwa Waislamu (dhimi) wanaoishi katika dola ya Kiislamu.
(iv) Serikali ya Kiislamu pia inao wajibu wa kuchukua hatua za kupunguza tafauti kati ya maskini na matajiri. Kwa kugawa Zakat na kutoa huduma muhimu bure kwa maskini
5. Uhuru wa kuchuma katika Uislamu
Kwa kuwa kuchuma kwa njia za halali ni wajibu kwa kila mwenye uwezo wa kufanya kazi, hapana budi kila mtu kupewa uhuru kamili wa kutumia juhudi yake na vipawa vyake katika kuchuma kwa njia za halali. Katika Uislamu ni kosa kubwa kwa serikali au Dola kuweka vikwazo vya kuwazuia watu wasitumie vipaji vyao na uwezo wao wote katika kuchuma kwa njia za halali. Kinyume chake, serikali au dola ya Kiislamu ina wajibu wa kuondoa vikwazo vyote vinavyo wazuia watu kutumia vipawa vyao vyote katika kuchuma na inawajibu pia wa kutoa motisha na vishawishi vya kuwavutia watu binafsi au watu waliojiunga katika vikundi wajiingize katika sekta mbalimbali za uchumi kwa juhudi kubwa na maarifa.
Pamoja na uhuru kamili uliotolewa na Uislam wa kuchuma kwa njia za halali kwa kadri ya uwezo wa kila mtu, pia unampa kila mtu haki ya kumiliki kila alichokichuma kwa njia za halali kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:
"Wala msitamani vile ambavyo Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma, na wanawake wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma Na mwombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. (4:32).
Mafanikio katika Uislamu ni kule kulijua lengo la maisha hapa ulimwenguni, kuwa na kumbukizi ya kisimamo mbele ya Mola siku ya hesabu, kuwa na kukinai moyoni na kukiona kila kitu cha ulimwengu huu kuwa ni cha kawaida. Kujitahidi kuyaendea mambo mema bila ya kuchelea chochote na kujiepusha na yale yote yanayoweza kumtoa mtu kumkhasirisha katika maisha yajayo hata kama yana "manufaa" kwa mtazamo wa wengi katika maisha haya. Kujali shida na matatizo ya wengine na kuweza kutoa kwa ajili ya kuwasaidia wengine kwa kadiri ya wasaa uliopo. Kuwa na huruma, mapenzi na bashasha isiyobagua taifa, kabila, nasabu wala ukoo wa mtu. Kutokuwa na chuki, majivuno, kibri, utesi, usengenyji, ulimbukeni, kujiona, kujitukuza au kujidhalilisha na kujitweza kwa yeyote yule anayemulikwa na jua iwe kihali au kimali.
Aliyetajiri wa Nafsi ni yule ambaye fursa yoyote aliyonayo haiwi kero na huzuni kwa wengine bali huitumia mwisho wa uwezo wake kupambana na taratibu potofu na kandamizi zinazotawala jamii yake. Hii ndiyo Dhana ya mafanikio katika Uislamu.
Kinyume chake umaskini wa
nafsi ni kule kutojifahamu na kutojua lengo la maisha katika ulimwengu
huu kwa hiyo ukaishi kwa malengo ya kula, kunywa, kuvaa na kustarehe!
--
|
|