Si katika kawaida na utaratibu wa Allah kuifanya jamii ibadilike toka hali moja hadi nyingine kwa kuiteza nguvu. Bali watu wenyewe waamue kuibadili. Kwa hiyo jamii iliyojaa dhulma na uonevu, yaweza kubadilika na kuwa jamii ya amani, furaha na uadilifu endapo watatokea waumini wa kweli wakafanya harakati za kuondoa tawala zinazo kaidi maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu.
Hili linapotokea jamii hutoka katika kipindi fulani cha historia na kuingia kipindi kingine.
Kutetea na kulinda maadili
Nadharia za masuala ya jamii zinaeleza kwamba katika historia ya ulimwengu, desturi na ustaarabu wa baadhi ya mataifa, makabila au koo umekuwa chimbuko la maendeleo aliyofikia mwanaadamu hivi leo. Baadhi ya jamii hujitokeza kuwa na vipaji vya kutengeneza mila, ustaarabu na uungwana huku nyingine zikikosa vipaji hivyo. Hali ni hiyo hiyo katika sayansi, falsafa, sanaa na ufundi kwa baadhi ya jamii kutoa mchango mkubwa, nyingine zikiwa watumiaji(consumers) tu wa mila, desturi, ustaarabu na fani hizo.
Hili linajitokeza pia katika kubuni taaluma, mafunzo,ufundi stadi na teknolojia. Jamii nyingine zimeongoza katika kazi za harubu zisizohitaji matumizi makubwa ya akili kuweza kuzitekeleza.
Kwa kuliona hili baadhi ya watu huamini kwamba zipo jamii maalum zenye wajibu wa kuuelekeza mkondo wa historia ya mwanaadamu katika ustaarabu(japo kila jamii ina wake), mila na ubunifu katika elimu au maarifa mbali mbali kama ilivyojitokeza kwa Uajemi ya kale, Misri ya kale , Shamu ya kale, Uyunani ya kale, Urumi ya kale na hivi leo Taifa la Wayahudi na nchi za ulaya magharibi na Marekani.
Kwa sababu hii na ile ya mvuto wa kijamii mara nyingi jamii ambazo haziongozwi na sheria ya Allah, huibuka na nadharia, sera, staarabu,desturi na taratibu ambazo mara nyingi huangusha maadili ya jamii (moral corruption and degenaration). Inapofikia hali hii jamii hunusurika tu endapo watakuwepo waumini watakaosimama kutetea maadili na kupinga sera mbaya.
Historia yatuonyesha kuwa awali Ulaya na Marekani hazikuwa zimeanguka kimaadili kama ilivyo leo. Baadae katika kipindi fulani cha historia wakabuni nadharia na sera ambazo zilichochea uzinzi na ulevi katika jamii. Kwa vile walikosekana waumini madhubuti wa kutetea maadili mema; leo nchi hizo zimezama katika ufuska, ulevi wa kupindukia, mauaji n.k., licha ya kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya vitu. Endapo wangekuwapo waumini wa kutetea maadili mema isingefikwa na kipindi hicho cha historia.
Nchi zinazoitwa za ulimwengu wa tatu hivi sasa zinapiga mbio kutekeleza sera za kudhibiti uzazi na zimeanza kufundisha elimu ya ngono mashuleni. Haya pamoja na mambo mengine huandamana na kampeni za kushawishi matumizi na ugawaji wa mipira ya zinaa(kondomu).
Kwa bahati mbaya wengi wa wanaojiita waumini hawaioni hatari hii. Sera na mipango hiyo ya kuiangamiza jamii inapitishwa na kutekelezwa bila upinzani wowote. Pasipokuwepo harakati za kupinga mfumo wa utawala unaoshajiisha hayo, jamii iwe tayari kushuhudia kipindi cha historia kitakachojaa ufuska na yanayoandamana nayo muda si mrefu.
Na madhara hayo hayataishia kuwaangamiza wakosefu bali hata watu wema wataathirika kwa sababu Mwenyezi Mungu ameyaumba maisha haya katika mtandao wa 'nipe nikupe' ikiwa na maana kwamba wanaadamu hushirikiana kifamilia na kijamii:
"Na iogopeni adhabu ya (Mwenyezi Mungu ya hapa duniani) ambayo haitawasibu peke yao wale waliodhulumu nafsi zao miongoni mwenu (bali itawasibu hata walionyamaza wasiwakataze, bali na wengineo pia); na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu". (8:25)
Migongano na migogoro
Migongano na migogoro (conflicts) kati ya makundi yenye nguvu katika jamii; moja likitaka kuondoa lingine ili kuondoa au kupunguza dhulma na ukandamizaji.
Basi (hao watu wa Taluti) wakawaendesha mbio (hao maadui zao) kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na Daudi akamwua Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa (huyu Daud) ufalme na hikma. (Utume) na akamfundisha aliyoyapenda. Na kama Mwenyezi Mungu asingalizuia watu, baadhi yao kwa wengine, kwa yakini ardhi ingaliharibika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhili (kubwa) juu ya walimwengu wote. (2:251).
Kupitia Mitume na watu wema katika jamii, Allah (S.W.) huwaokoa watu kutokana na mateso wanayoyapata chini ya tawala za kidhalimu. Lakuzingatia hapa ni kuwa nusura ya Allah haiji kama mvua inavyonyesha bila ya juhudi ya mwanadamu. Bali watu wenyewe wanaodhulumiwa wanapaswa kutoka jasho ili kujikomboa. Ndio maana ruhusa ya kupigana ikawepo kwa wale waliodhulumiwa:
"Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa, kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni muweza wa kuwasaidia:Ambao wametolewa majumbani (mjini) mwao pasipo haki ila kwa sababu wanasema; Mola wetu ni Mwenyezi Mungu." Na kama Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu, baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangalivunjwa mahekalu na makanisa na nyumba nyingine za Ibada na misikiti ambamo jina la Mwenyezi Mungu hutajwa kwa wingi: Na bila shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayeisaidia dini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda. (22:39-40).
Na nusura ya Allah itawajia wakiwa katika harakati za kujikomboa:
"Na tutakukalisheni(nyinyi) katika nchi hizi(hizi) baada yao." Watapata haya wale walioogopa kusimamishwa mbele yangu na wakaogopa maonyo yangu."
Na walitafutatafuta, na akashindwa
kila jabari mkaidi(14:14-15).
--
|
|