Na Dkt. Abdallah J. Saffari
SHAHIDI anaweza kuonyesha kuwa kauli ambayo anaitoa mahakamani kama ushahidi aliwahi kuitoa kwa mtu mwingine kabla ya hapo. Kufuatana na kanuni ya kawaida ya ushahidi, ushahidi wa mtu ambaye tamko hilo lilitolewa kwake kwa mara ya kwanza ni wa kuambiwa kwa vile yeye binafsi atakuwa hakushudia jambo hilo.
Lakini fungu la 166 la sheria ya ushahidi (Sheria Na. 6, 1967) limeruhusu ushahidi wa aina hiyo upokelewe sio kuthibitisha ukweli wa yale ambayo yamo kwenye tamko hilo bali tu kudhihirisha kwamba tamko hilo lilitolewa kabla.
Hekima ya kanuni hii inatokana na hulka ya binadamu ya kutaka kuelezea tukio muhimu kwa mtu anayeonana naye kwanza au kwa mamlaka yanayohusiana na upelelezi wa shauri kama hilo. Hivyo basi iwapo baada ya tukio muhimu shahidi atakaa kimya bila kusema au kutoa taarifa kwa mtu ambaye anaweza kusaidia upelelezi wa jambo hilo, inatia wasiwasi sana juu ya mwenendo wa mtu huyo. Hivyo maelezo atakayoyatoa baadaye yanaweza kutiliwa mashaka. Mfano mzuri ni wa masuala ya utambuzi. Iwapo shahidi Z alimwona mshitakiwa N akichoma nyumba, katika mazingira ya kawaida, atakwenda kutoa taarifa hiyo kwa askari wa usalama au mtu yeyote yule mwenye mamlaka ya upelelezi wa tukio hilo, au kusaidia tu katika kutatua tukio hilo. Akikaa kimya tuhuma itakuwa kabla hakuwa na hakika ya yale aliyoyaona. Ikiwa atatoa taarifa au kauli kwa namna iliyoelezwa hapo juu itadhihirisha ushahidi wa yale aliyoshuhudia. Kama ni hivyo basi sio busara kumkataza mtu aliyepewa taarifa hiyo kwa mara ya kwanza asitoe ushahidi mintaaraf ya suala hilo kwa kusudi la kuthibitisha tu kwamba kauli ya shahidi Z ilitolewa na hivyo kuimarisha hakika yake. Ikiwa taarifa ilitolewa kwa maandishi, hati hiyo inaweza kutolewa mahakamani na aliyeipokea, na kama kauli ilitolewa kwa maneno tu, basi yule aliyeelezwa atatoa ushahidi juu ya tamko hilo (Rex v. Mohammed Allui (1942) 9 E.A.C.A. 72).
Ushahidi wa Tabia
Ushahidi unaoonyesha kwamba mshitakiwa ni mtu mwenye tabia mbaya haukubaliwi (F.56, Sheria ya Ushahidi, i.h.j) isipokuwa katika mazingira ambayo yataelezwa baadaye. Kanuni hii ina madhumuni ya kutowarubuni mahakimu kuamini kwamba madhali mshitakiwa ni wa tabia na matendo mabaya basi atakuwa anahusiana na mashitaka ambayo yanamkabili wakati huo. Kwa mfano mshitakiwa anakabiliwa na shitaka la wizi, basi sio sahihi kuruhusu na kuukubali ushahidi kuonyesha kwamba alikuwa ameshapatikana na hatia ya wizi wa aina nyingine kabla ya hapo. Baadhi ya watu huamini kuwa mtu mwenye tabia fulani mbaya basi haiachi. Kwa hali hiyo Hakimu au Jaji anaweza kuathiriwa na ushahidi wa tabia mbaya ya mshitakiwa hata kabla ya kutenda kosa lile analoshitakiwa nalo kwa wakati uliopo.
Hata hivyo ushahidi wa tabia mbaya dhidi ya mshitakiwa unaweza kutolewa katika mazingira matatu tofauti. Kwanza, iwapo mshitakiwa mwenyewe anadai, na ametoa ushahidi kuthibitisha kwamba ni mtu mwenye tabia nzuri (K.h.j.). Pili, ushahidi huo unaweza kutolewa kuthibitisha kwamba matendo yaliyosababisha mashtaka dhidi ya mshitakiwa hayakutoka kwa bahati mbaya yaani ajali, bali alikusudia (K.h.j). Kwa mfano X amewapiga ndugu wawili A na D katika siku tofauti: A tarehe 5/5/1995, halafu akampiga D tarehe 15/5/1995. X akashitakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa la kumshambulia A. Halafu anashitakiwa tena kwa kumshambulia D. Sasa katika shitaka hili la mashambulizi dhidi ya D ushahdi unaweza kutolewa kuonyesha X alikuwa na nia, na alikwishatamka kuwapiga ndugu hao A na D.
Au tunaweza kuangalia mfano mwingine. T ameshitakiwa kwa kuchoma nyumba ya N, halafu tarehe nyingine alichoma shamba la N huyo huyo. Ushahidi wa kuchoma nyumba ya N, japo unaonyesha vitendo vya uhalifu dhidi ya T, unastahili kutolewa na kukubaliwa kuonyesha kwamba T alilichoma shamba la Na kwa kukusudia.
Tatu, ushahidi wa tabia mbaya (hususan makosa ya zamani) unakubalika kuyafanya mahakama kukadiria aina ya adhabu ya kutoa. Kwa kawaida mshitakiwa mwenye kumbukumbu ya makosa ya zamani yanayofanana na kosa ambalo amepatikana nalo na hatia kwa mara nyingine tena, hupewa adhabu kali kuliko mkosaji wa kwanza.
Ushahidi wa kuunga mkono
Imeelewa kwamba ushahidi wa mazingira unahitaji vipande vipande vingi vya ushahidi kuthitibisha shitaka linalodaiwa. Kwa upande mwingine ushahidi wa moja kwa moja unaweza kuthibitisha shitaka bila kuungwa mkono na ushahidi mwingine wa nyongeza wa moja kwa moja au wa mazingira. Kwa kawaida ushahidi wa moja kwa moja hauhitaji kuungwa mkono na ushahidi wa nyongeza ili kuthibitisha shitaka isipokuwa pale ambapo ushahidi huo ni dhaifu mno au sheria inaelekeza hivyo.
Kutokana na mazoea ya muda mrefu mahakama hupendelea aina fulani fulani za ushahidi ziungwe mkono na ushahidi wa nyongeza. Ushahidi wa mtoto, yaani mtu asiyezidi umri wa miaka kumi na nne, mathalan, ni ushahidi wa aina hiyo ( John Makin na Sarah Makin n. Attorney General (1894) A.C. 57). Wasiwasi ni kwamba mtoto chini ya miaka kumi na nne anaweza akatoa ushahidi usio wa kweli kutokana na sababu nyingi tu kama vile kusahau, kufundishwa, woga na kadhalika.
Ushahidi wa mshirika ni mfano mwingine. Mshirika ni mtu ambaye amemsaidia au kumwezesha mshitakiwa katika kesi inayohusika kuweza kutenda kosa analokabiliwa nalo. Wanaopokea mali ya wizi huku wakijua hivyo ni washirika wa wezi wenyewe. Tafsiri nzuri zaidi ilitolewa katika Wanja Kamau v. R. (1966) EA 501) ambapo ilielezwa kwamba mtu ambaye anaridhika na kosa linalotendwa au anashindwa tu kutoa taarifa ya kosa hilo sio mshirika lakini ushahidi wake lazima uangaliwe kwa tahadhari. Iwapo mtu huyo alikuwa anaafikiana na utendaji wa kosa hilo ushahidi huo hauna thamani, sawa na ule wa mshirika. Iwapo mtu huyo alikuwa hajali, yaani amepuuka tu kutendeka kosa hilo, ushahidi wake lazima uangaliwe vizuri sana kabla ya kukubaliwa. Bali endapo mtu huyo aliuwa na hofu tu wakati kosa hilo linatendeka, hakuna sababu ya kutoutilia maanani ushahidi wake.
Kwa jumla mshirika ni mtu ambaye hana msimamo na aghalabu huweza kusema uongo kujiepusha na lawama ya kutenda kosa linalodaiwa. Yafaa izingatiwe hapa kwamba upande wa mashitaka ndio huamua nani wa kumshitaki na yupi wa kumwachia. Pale ambapo ushahidi ni dhaifu au hauwezi kupatikana kabisa isipokuwa kwa kumfanya mmoja wa washirika wa kosa kuwa shahidi, upande wa mashitaka hautasita kufanya hivyo. Mfano mzuri ni katika makosa ya kupokea mali ya wizi. Mara nyingine mnunuzi wa mali ya wizi huelewa kuwa mali hiyo imeibwa. Enzi ile ya hali mbaya ya uchumi Tanzania ilisababisha ukosefu mkubwa wa vifaa muhimu kama spea za magari na kadhalika, au hata vyombo vya muziki, mnunuzi aliweza kuelewa mapema kwamba bidhaa anayotaka kununua ni ya wizi. Pengine huagizia aletewe bidhaa ya wizi kukidhi shida yake.
Hakika mnunuzi huyo ni mshirika wa wizi uliotendeka, na wakati mwingine ameuchochea utendeke kwa kuwa tayari kanunua bidhaa anayoihitaji huku anajua kwamba kwanza itabidi iibwe, kwa mfano betri ichomolewe kwenye gari la shirika au serikali, ndipo aletewe yeye. Au tuchukue mfano wa kosa la kuzinga na maharimu. Aghalabu kujamiiana ni kitendo cha hiari baina ya bwana na bibi. Wakati maharimu wawili wanapojamiiana inaweza kusiwe na ushahidi mzuri zaidi ya ule wa mmoja wa wazinzi maharimu hao. Hivyo upande wa mashitaka utaamua yupi ashitakiwe na yupi atoe ushahidi ili mhalifu atiwe hatiani.
Katika mifano yote hiyo miwili ya washiriki kosa, ni sawa kabisa kuukabili ushahidi wa washirika hao kwa tahadhari kubwa mno na kuukubali pale tu inapokuwa salama kufanya hivyo.
Iwapo kuna washitakiwa wawili mintaarafu ya kosa moja kila mshitakiwa ni mshirika wa kosa linalodaiwa. Hivyo ni busara ushahidi wa mshitakiwa mmoja dhidi ya mwenzake uangaliwe kwa makini kwa kuhofia hatari ya kusukumiana lawama ili kujiepusha. Mara nyingine mshitakiwa anaungama kutenda kosa analoshitakiwa nalo. Anaweza asiishie kosa hilo. Katika hali kama hiyo ni lazima ushahidi wa maungamo wa mshitakiwa huyo uungwe mkono na ushahidi mwingine wa nyongeza (F.127 (4), Sheria ya Ushahidi, i.h.j. Angalia pia Kibangey Arap Kolil v. R. (1959) E.A. 92. Pia Erukana Kyakulagira v. Attorney General (1959) E.A. 152; Oloo v. R. (1960) E.A. 86; Gabriel Maholi v. R. (1060) E.A. 159; Nyasani Bichana v. R. (1958) E.A. 190. Mshitakiwa hawezi kutiwa hatiani kwa uzito wa maungamo ya mshitakiwa mwenzake bila ya kuungwa mkono kwa ushahidi huo.
Zamani ushahidi wa makosa ya zinaa hasa kubaka, kwa kawaida ulihitaji kuungwa mkono (Wanja Kamau v. R (1966) EA 501 sasa angalia F.127(7) Sheria ya Ushahidi, i.h.j). Sharti hili limedaiwa na baadhi ya watu kwamba linadhalilisha hadhi ya wanawake. Hatuhitaji kuingia katika mjadala huo unaoweza kutufikisha mbali kwa hivi sasa. Isipokuwa daima imethibitika, hivyo kuzidi kuhofiwa, kwamba baadhi ya wanawake huafiki kufanya mapenzi na kujamiiana na wanaume baadaye husingizia kwamba walilazimishwa kufanya hivyo na wanaume wanaoshitakiwa. Sababu za kusingizia zaweza kutokana na mambo mengi mathalan kutolipwa ujira wa kufanya mapenzi; au nia tu ya kujitoa lawama mbele ya watu (hasa kwa wanawake walioolewa au walio chini ya uangalizi wa wazazi wao) na kadhalika (K.h.j).
Nyakati nyingine mwanaume anaweza akaamini (kutokana na baadhi ya mila) kwamba mwanamke anajitia kukataa kujamiiwa naye kama bidaa tu. Hivyo nguvu anazotumia mwanaume huyo zinaweza kuwa za kawaida tu ili kumshawishi au kumtoa haya msichana ambaye anaamini huenda ataonekana malaya iwapo atakubali kujamiliwa bila ya kukataa.
Kuna mlolongo wa mifano mingine ambapo inaweza kuwa vigumu kuthibitisha kwa hakika iwapo mwanaume alimjamii mwanamke bila ya ridhaa ya mwanamke huyo. Ndiyo maana ilionekana kauli ya mlalamikaji mwanamke bora iungwe mkono na ushahidi mwingine wa moja kwa moja au wa mazingira. Ushahidi huo unaweza kuwa kelele zilizopigwa na mwanamke, alama za matumizi ya nguvu maungoni mwa mwanamke na mwanaume, kuchafuka au kuchanika kwa nguo za wote au mmoja wao, kutoa taarifa ya kosa mapema iwezekanavyo na kadhalika.
Mbali na aina za ushahidi zilizoelezwa hapo juu ni busara pia kuukubali kwa tahadhari ushahidi wa mtu mwenye maslahi na matokeo ya kesi fulani. Shahidi anaweza kuwa na uhasama na mshitakiwa hivyo akataka kumtokomeza mshitakiwa gerezani kulipiza kisasi. Au anaweza tu kuwa anahofia mshitakiwa akiwa nje anaweza kumdhuru, hivyo atatoa ushahidi wa kumkandamiza afungwe. Katika kesi moja ya mauaji Iringa, 1981, mahakama yaliupuuza ushahidi wa shahidi mmoja wa mashitaka kwa vile aliogopa mshitakiwa akitoka angeweza kulipiza kisasi cha kuzalishwa mkewe na shahidi huyo. Kwa upande mwingine shahidi anaweza kutoa ushahidi wa uongo kumwepusha na hatia rafiki au ndugu yake.
Na pale ambao shitaka ni
kubwa mno na ushahidi ni wa mtu mmoja ni busara kuuangalia ushahidi wa
mtu huyo kwa makini mno. Imekwishaelezwa awali kuwa kwa kawaida idadi ya
mashahidi sio hoja katika kuthibitisha shauri. Muhimu ni uzito wa ushahidi
wao. Hivyo kila shauri huangaliwa kufuatana na mazingira yake. Pale ambapo
mashahidi wengi walishuhudia tukio ni bora kuwaita kadhaa kuthibitisha
tukio hilo. Kutofanya hivyo kunaweza kutia wasiwasi kuwa mashahidi wengine
ambao wangeitwa wangetoa ushahidi tofauti na ule wa shahidi mmoja aliyeitwa
kwanza.
--
|
|