MASHEIKH na waheshimiwa wanapokuwa na agenda zao hupenda sana kutaja kisa cha Mfalme Najash na Waislamu waliohajiri kwenda Habash.
Lakini sifa kuu ya Mfalme Najash iliyomuathiri Mtume (s.a.w.) hata awaambie Waislamu dhaifu wahajir kwenda Habash, haikuwa ukristo wake, bali uadilifu wake. Aliwaambia Nendeni huko yupo mfalme ambaye katika ufalme wake hamdhulumu yoyote. Kama suala lilikuwa ukristo zilikuwepo tawala nyingi za kikristo wakati huo tena zilizokuwa karibu zaidi na Makka kuliko Habash.
Na Maqureish walipowafitini Waislamu kwa Najash kwamba wanamtukana Yesu na mama yake; "Kata kichwa, piga mshale na huyo ongeza" haikuwa ndilo jibu la Serikali ya Najash. Iliwaita Waislamu na kuwauliza; "Je; imekuja habari yoyote juu ya Masihi katika dini yenu"! Surat Mariam ikawa ndio jibu.
Je, katika serikali yetu hii ya uwazi na ukweli, nani angalau mjukuu wa Najash!
Makaburu katika Enzi zao pamoja na siasa zao za kibaguzi, hawakuamrisha kina Ahmed Deedat wapigwe risasi au hata kuwekwa rumande kwa madai ya wachungaji kwamba wanamtukana Yesu. Na Ahmed Deedat Mwenyewe anasema Afrika Kusini ni Bahari ya Ukristo!
Wako watu wanaolaaniwa kwa ukatili wao kwa kudiriki kumuua mtu na kumchuna ngozi. Laana hiyo huwaendea pia wale ambao humuua mtu kwa kumvisha tairi wakamchoma moto baada ya kumponda kwa mawe na matofali.
Pamoja na laana nzito nzito wanazoshushiwa watu hawa lakini wakitiwa mbaroni hawapigwi risasi papo hapo. Hushukia polisi kisha mahakamani. Hapo ndipo itathibitishwa kama waliua au la na kwanini. Ndio maana wale, walioua Mbeya wakachuna ngozi hawajauliwa bado wako rumande wakisubiri kesi zao.
Si wote katika wauaji wanaochuna ngozi au kuchoma moto au pengine kumtoboa macho marehemu. Wengine huwalenga shabaha baada ya kupokea amri, piga shaba' 'Piga yule' - kisha huzipiga virungu na kuzitukana maiti zao wakasema "Pumbavu; hiki ndicho mlikuwa mkitaka", wakafukia damu kwa mchanga na kuzirusha maiti ndani ya gari.
Mtu ukishamuua kama utaikata maiti yake masikio ndio uifukie au ukaamua maiti yake uitupe baharini haileti tofauti yoyote kwa maiti. La muhimu kumuua. Manyanyaso mengine yote yatakayofuatia baada ya kuudhulumu uhai wake hayana maana yoyote.
Ndio maana wakati watu wengine huwazika maiti wao; Baniani wakwao huwachoma moto, wala hawalaaniwi kwamba wanafanya unyama.
Kila kiongozi wa serikali na vyama vya siasa leo haoni kukamilika uongozi wake kama hajakemea na kulaani wachuna ngozi. Kila Mbunge anayesimama Bungeni kutoa hoja au kuchangia hoja basi awali ya yote atalaani aliyemua mtu na kumchuna ngozi.
Tungependa tuungane na Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania wote kulaani kitendo hicho cha kinyama na kuitaka serikali ichukue hatua kali kabisa.
Lakini mwaka jana Waheshimiwa Wabunge walipopelekewa habari za Mwembechai ambapo yaliyofanyika pale ilikuwa pamoja na kuuliwa Waislamu kwa kupigwa risasi; wote walishangilia. Walipiga meza na miguu ikadunda sakafu kama ilivyokawaida yao wanapolifurahia jambo.
Kama kuwalaani wauaji ni wauaji wote. La msingi ni kuua si namna ya kuitendea maiti.
Na Waislamu wote leo ukiacha wale vibaraka wataraji 'Pepo' ya dunia kutoka kwa viongozi wa siasa, huona taabu kukaa katika hafla iliyohudhuriwa na ye yote kati ya walioshangilia kuuliwa kwao.
Hakuna Muislamu anayemchukia Mbunge; Waziri au kiongozi yoyote wa serikali kwa ajili ya dini yake. Lakini lile doa jeusi walilojitia kwa kushangilia kuuliwa kwa Waislamu.
Waziri Kivuli wa Wizara ya Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa akichangia hoja ya Mh. Kingunge Ngobale Mwiru katika Bunge la Bajeti linaloendelea Dodoma alitoa tuhuma nzito nzito kwa serikali na baadhi ya watendaji wake. Huku akitaja majina ya watu na vyeo vyao, alitoa madai jinsi watu hao walivyofanya hujuma lakini wakalindwa na Serikali kuu.
Naibu Spika Mh. Philip Marmo aliingilia kati kwamba si uadilifu kuwataja watu ambao hawawezi kuja Bungeni kujitetea. Lakini jingine Muhimu ni kwamba kwa vile hoja za Mbunge huyo ziliegemea taarifa rasmi za Mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali na kamati ya Bunge husika na Masuala hayo; Mh. Marmo alisema kwamba bado hayo ni maoni ya kamati na tuhuma tu; vyombo husika vya kisheria (Mahakamani) havijathibitisha.
Lakini Bunge hili hili lilipoletewa taarifa za Mwembechai - mantiki ya watuhumiwa kujitetea haikuonekana wala ile hoja ya msingi kwamba hizi ni tuhuma ambazo Mahakama haijathibitisha haikuhitajika.
Waziri Mkuu Mh. Fredrick Sumaye kama kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni akapongeza hatua zilizochukuliwa na polisi na wabunge wakamshangilia!
Swaleh kapigwa risasi ubongo ukamwagika baada ya kufa anaambiwa 'pumbavu' Mnashangilia! (Ezekiel)? Kauliwa huko Mbeya wote mnalaani. Salamu gani mnatupa.
Tunadhani salamu zenu zimeeleweka ndio maana Waislamu wanawaomba angalau msiwatoneshe.
Wakiwaona kwenye hafla zao wanamkumbuka Ustadh Swaleh akigaragara chini akirusha miguu na kukoroma baada ya kupigwa risasi.
Wakiwaona kwenye hafla zao wanamkubuka Mzee Chata akiteseka gerezani bila ya matibabu na lishe.
'Mkivamia Maulidi zao mnawatia simanzi wakimkumbuka kijana aliyepigwa risasi mgongoni, maiti yake ikawa imelalia dimbwi la damu. Vipi umpongeze aliyefanya kitendo hiki halafu uwe na uso na ujasiri wa kukaa na wafiwa katika karamu zao na hafla zao tukufu!
Kweli yahitaji Mtu jasiri, kama alivyojisemea Sheikh Hemed bin Jumaa, Muft wa Bakwata.
Qur'an inatuambia kuwa: "Hakika utawakuta walio maadui zaidi kuliko watu (wengine) kwa Waislamu ni Mayahudi na wale mushirikina (wasiokuwa na kitabu), na utawaona walio karibu kwa urafiki na Waislamu ni wale wanaosema: "Sisi ni Wakristo" (hayo) ni kwa sababu wako miongoni mwao wanavyuoni na wachao Mungu, na kwa sababu wao (Wakristo) hawatakabari; (wakiijua haki huifuata)." (Qur. 5:82)
Aya hii masheikh hupenda sana kuisoma katika hafla zenye kubarikiwa na viongozi wa serikali au wanapotumwa kazi. Lakini hiyo sio aya pekee inayowahusu wakristo na Mayahudi. Zipo hizi zifuatazo:
"Enyi mlioamini! Mkiwatii baadhi ya wale waliopewa kitabu, watakurudisheni kuwa makafiri baada ya Uislamu wenu". (Qur. 3:100)
"Enyi mlioamini! Msiwafanye wasiri wenu watu wasiokuwa katika nyinyi: Hao hawataacha kukufanyieni ubaya. wanayapenda yale yanayokudhuruni. Bughudha (yao juu yenu) inadhihirika katika midomo yao. Na yanayofichwa na vifua vyao ni makubwa zaidi. Tumekubainishieni dalili (zote) ikiwa nyinyi ni watu wa kufahamu".
"Oh! Nyinyi mnawapenda (maadui zenu hao), hali wao hawakupendeni! Nanyi mnaamini vitabu vyote (chenu na vyao). Na wanapokutana nanyi husema, "Tumeamini". Lakini wanapokuwa peke yao wanakuumieni vyanda kwa uchungu (wa kukuchukieni). Sema: "Kufeni kwa uchungu wenu (huo); hakika Mwenyezi Mungu anayajua (hata) yaliyomo vifuani."
"Ikikupateni kheri huwasikitisha. Na ikikupateni shari wanaifurahia. Na kama ninyi mkisubiri na mkamcha Mungu hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua vizuri yote wanayoyatenda." (Qur. 3:118-120)
Hizi pia ni aya za Mwenyezi Mungu na anawaonya wanaochagua aya za kusema na kuzifumbia macho nyingine kwa kusema.
"...Je! Mnaamini baadhi
ya kitabu na kukataa (baadhi yake)? Basi hakuna malipo kwa mwenye kufanya
haya katika nyinyi ila fedheha katika maisha ya dunia; na siku ya kiama
watapelekwa katika adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafirika
na yale mnayoyatenda". (Qur. 2:85)
--
|
|