Pepopunda (Tetanus)
PEPOPUNDA ni ugonjwa hatari sana unaosababishwa na sumu (toxin) inayozalishwa na vijidudu viitwavyo Clostidium tetani au Tetanus bacilli. Ugonjwa huu una sifa ya kuwa na maumivu makali yanayoambatana na kukaza misuli kwa ghafla.
Vijidudu Tetanus bacilli vyaweza kuishi tu sehemu isiyo na hewa ya Oxygen hivyo mara nyingi huishi ndani ya (tumbo) fuko la kuhifadhia uchafu la wanyama kama ng'ombe.
Vijidudu hivyo vikitoka pamoja na kinyesi hujijengea koti (spores) ili viweze kuishi katika hali ngumu. Na vyaweza kukaa katika udongo uliochafuliwa na kinyesi cha ng'ombe.
Mtu hupata ugonjwa wa Tetanus Spores za Tetanus bacilli zitakapoingia mwilini kwake kupitia majeraha. Majeraha machafu yanayofanya aerobic bacteria wazaliane kwa wingi hutoa fursa kwa Clostridium tetani kukua kwani aerobic bacteria humaliza hewa iliyopo.
YAFUATAYO ni majeraha ambayo yanaweza kusababisha Pepopunda. Majeraha yanayosababishwa na kuchomwa na misumari, miiba au vibanzi, majeraha ya seng'enge zenye miiba a matundu yanayodungwa kwa sindano chafu. Mengine ni majeraha ya kisu au risasi na majeraha yanayosababishwa na kuumwa na wanyama hasa mbwa na nguruwe.
Sababu za Pepopunda kwa watoto wachanga:
Iwapo kitovu cha mtoto kitakatwa kwa kutumia chombo ambacho hakikuchemshwa na kuwekwa katika hali ya usafi, na iwapo kitovu kitakatwa mbali sana na mwili basi upo uwezekano wa vijidudu vya Pepopunda kumshambulia mtoto.
Dalili za Pepopunda:
1. Jeraha lenye usaha - hata hivyo, mara nyingine sio lazima jeraha lionekane.
2. Maumivu na shida ya kumeza.
3. Kinywa kukaza ikifuatiwa na kucheza misuli ya shingo na sehemu nyingine za mwili.
4. Mikazo ya ghafla yenye maumivu kuanzia kinywani na kutapakaa mwili wote. Ukimgusa mgonjwa mistuko hii ya ghafla inarudia. Aidha mwanga na kelele husababisha mshtuko huo.
Kwa watoto wachanga dalili ya kwanza ya Pepopunda hutokea kati ya siku tatu hadi kumi tangu kuzaliwa. Mtoto analia kutwa na hawezi kunyonya. Mara nyingi kitovu ni kichafu au kina dalili za kutunga usaha. Hali hii hufuatiwa na kinywa kukaza kisha dalili nyingine. Ni lazima tiba ianze mara moja baada ya kuona dalili ya kwanza. Pepopunda huua tena haraka.
Namna ya kumsaidia mtu mwenye dalili za pepopunda
Kwanza ni kuangalia kama ana jeraha. Jeraha lisafishwe kwa sabuni na maji ya moto na uchafu wote kama usaha, miiba uondolewe. Kama hydrogen peroxide inapatikana basi inyunyiziwe.
Mgonjwa apigwe sindano ya procaine penicilin na kurudia kila baada ya masaa 12. Kwa watoto wachanga wadungwe sindano ya Cystalline penicilin.
Aidha, mgonjwa adungwe Tetanus antitoxin unit 40,000 hadi 50,000 au Human immune globulin unit 5,000. Ili kuzuia mikazo ya ghafla adungwe phenobarbitone au valium. Mgonjwa asiguswe wala kunyanyuliwa. Aidha mwanga na kelele viepukwe. Njia ya hewa iwekwe wazi kwa kunyonya makamasi puani na kinywani na kama anaweza kumeza apewe chakula bora cha maji maji kidogo kidogo mara kwa mara.
Nusu ya wagonjwa wa Pepopunda hufa hata katika hospitali zilizo bora. Kwa hiyo kukinga ndio njia ya salama na uhakika zaidi.
Zindiko (Vaccination) ni njia bora sana ambapo watoto na watu wazima ni lazima wachanjwe dawa ya kinga.
Majeraha yote ni lazima yawekwe katika hali ya usafi na yatibiwe mara moja. Na iwapo mtu kapata jeraha na haja zindikwa atumie Penisilini kisha sindano ya tetanus antitoxin.
Kwa watoto wachanga, vyombo
vinavyotumika kukatia kitovu ni lazima vichemshwe na kuwekwa mahali pasafi
kabla ya kutumiwa. Aidha kitovu kikatwe karibu na mwili na kiwekwe katika
hali ya usafi na ukavu.
--
|
|