MAKALA YA UCHAMBUZI
 
Kwani nchi hii ya Wakristo pekee?
 

Na Maalim Bassaleh
 

KWA mujibu wa gazeti moja la kidini linalotoka kila siku ya Jumapili, limeeleza kuwa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imempekekea barua Rais Benjamin Mkapa kuitaka serikali isimamishe mpango wake wa kutaka kujiunga na OIC, kwa sababu nchi hii siyo wa Waislamu pekee. Kama habari hizo ni za kweli basi ni vyema wakaulizwa CCT kwani nchi hii ni ya Wakristo pekee?

TANZANIA ni nchi isiyokuwa na dini, kwa hiyo serikali yake hatakiwi ionekane inapendelea dini moja juu ya dini nyingine au inawanyima haki wale wasiokuwa na dini kwa kuwapendelea wale wenye dini. Lakini kutokana na historia ya nchi hii, wakoloni wote waliwahi kutawala nchi hii mwanzo Majerumani na kisha Waingereza walikuwa ni Wakristo.

Jambo hilo likapelekea Ukristo upewe upendeleo maalum na serikali hizo za kikoloni. Utamaduni wa Kikristo ukawandio unaoufuatwa rasmi na serikali hizo. Jumapili iwe ndiyo siku rasmi ya mapumziko, kwa sababu tu siku hiyo ndiyo siku yao ya kwenda Kanisani. Wala hakuna Muislamu aliyehoji hilo; juu ya kwamba kwa Waislamu siku ya Ijumaa ndiyo siku kuu yao ya wiki. Kwa kuwa watu wamezoea linaonekana kama ni jambo la kawaida tu!

Isitoshe, serikali ya Tanzania huru ilipotaka kuongeza siku nyingine ya mapumziko katika juma ilichagua siku ya Jumamosi ambayo pia ni siku ya ibada kwa Wakristo Wasabato. Waislamu hawakusema neno, na bado wanatakiwa waamini kuwa nchi hii haina dini!

Pili, Wakoloni waliifanya siku ya Krismasi kuwa ni siku kuu ya serikali. Lakini hiyo ni siku ya Kanisa, ndiyo siku aliyozaliwa Yesu, mwanzilishi wa Ukristo. Katika jambo hili hatuwezi kudai kuwa Wakristo wamependelewa, kwa sababu na Waislamu wamepewa na wao mapumziko ya siku ya Maulidi, ambayo ni siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.), kiongozi wa Waislamu.

Lakini bado inaonekana kuwa siku ya Krismasi inapewa kipaumbele mkubwa na serikali kuliko ile siku ya Maulidi. Serikali imekuwa ikigharimia sherehe za Krismasi kwa kuruhusu Wizara, Maidara na Maofisi ya serikali kutumia fedha za walipa kodi kupamba kwa bendera, miti, taa na zawadi mbalimbali, wakati siku ya Maulidi haifanywi shamra shamra za aina yoyote ile. Na hilo nalo limezoeleka; hakuna anayesema kuwa Wakristo wamependelewa. Mradi Waislamu wanatakiwa wakubali tu kuwa serikali haina dini.

Tatu, mwaka mpya unasheherekewa kwa kila aina ya mbwembwe. Ofisi za serikali hupambwa, na tafrija za aina mbalimbali huandaliwa kuukaribisha mwaka mpya. Idara za serikali huchapisha kadi pamoja na kutoa matangazo katika magazeti kuwatakia Watanzania heri ya mwaka mpya. Fedha za umma ndizo zinazotumika kugharimia yote hayo.

Lakini huo mwaka unaosherehekewa namna hiyo ni mwaka wa Kikristo. Unaitwa A.D., kifupisho cha maneno mawili ya Kilatini Anno Dominni yakiwa na maana ya "Mwaka wa Bwana" yaani Mwaka wa kuzaliwa Yesu Kristo". Waislamu wana mwaka wao, unaitwa Hijriya. Mbona basi unapoingia huo mwaka mpya wa Kiislamu hatuoni maofisi ya serikali kupambwa au kufanywa sherehe za aina yoyote ile? Na wala siku ya kuingia mwaka wa Kiislamu haifanywi kuwa ni siku ya mapumziko kama inavyofanywa wakati wa kuingia ule mwaka wa Kikristo. Juu ya hivyo Waislamu wanaambiwa waungame kuwa serikali haina dini.

Kwa kweli kuna mambo mengi yanayofanywa na serikali yanayoupendelea Ukristo waziwazi; lakini kwa vile mambo hayo yamezoeleka sana yanaonekana kana kwamba ni mambo ya kawaida tu. Na kwa vile Waislamu wameyanyamzia kimya yanaonekana mambo ni sawa tu. Lakini jambo la Waislamu kutaka Tanzania ijiunge na OIC, Jumuiya ya Makanisa inalipinga kwa nguvu zake zote.

Wahenga walisema "Ukila na kipofu usimguse mkono, la sivyo mtahesabu nyama ndnai ya bakuli", mbona Jumuiya ya Makanisa Tanzania inajifanya kama haina habari na usemi huo. Inavyofanya siyo kwamba inamzuia mkono tu kipofu bali inataka kumnyima kipofu huyo asile kabisa!

OIC ni taasisi ya Kiislamu inayojishughulisha na kutoa misaada ya kijamii kwa zile nchi zilizo wanachama. Hutoa misaada kwa ajili ya maendeleo ya nchi kama hizo, bila ya kupata faida yoyote ya kidunia. Ingawa taasisi hiyo ina nembo ya Kiislamu, lakini misaada inayoitoa ni ile yenye faida na nchi na siyo na kikundi fulani cha watu. Hujenga barabara, madaraja, vyuo vya elimu, hospitali na mfano wa hayo. Bila shaka barabara au daraja litajapojengwa watapita watu wote, wawe ni Waislamu au wafuasi wa dini nyingine. Ndivyo hivyo hivyo kwa mahospitali, vyuo vya elimu na miradi mingine; watakaofaidika ni wananchi wote bila ya kujali itikadi zao za kidini.

Kwa vile misaada kama hiyo inakusudiwa iisaidie nchi husika ndiyo OIC ikaweka shuruti kuwa uhusiano uwe baina yake na nchi husika na siyo baina yake na kikundi au dhehebu fulani la dini. Imefanywa hivyo makusudi ili nchi inayohusika iwe na kauli ya kupendekeza juu ya aina gani ya mradi wa maendeleo inaoutaka.

Swali la dini halipo kabisa, na wala OIC haiingilii kwa njia yoyote ile mambo ya ndani ya nchi. Pia si lazima nchi inayojiunga na shirika hilo iwe ni ya Kiislamu au iwe na wafuasi wengi wa dini hiyo. Uganda na Mozambique ni mfano mzuri wa nchi wanachama. Nchi hizo mbili zina idadi ndogo sana ya Waislamu. Aidha, viongozi wakuu wa serikali za nchi zote hizo mbili ni Wakristo; lakini bado nchi hizo zimejiunga na OIC. Kwanini Tanzania ambayo ama ina asilimia kubwa zaidi ya Waislamu kuliko dini nyingine yoyote, au ina idadi ya Waislamu wanaolingana na Wakristo isijiunge na OIC ikafaidika na ile misaada inayotolewa na taasisi hiyo?

Kama swali ni kuogopa OIC isiwasilimishe Watanzania wenye kufuata dini nyingine, mbona Uganda na Mozambique tokea zilipojiunga na taasisi hiyo hazijawahi kulalamika kuwa OIC inafanya njama za kutaka kuzisilimisha nchi hizo mbili ziwe ni nchi za Kiislamu?

Swali la Tanzania kujiunga na OIC lilianzia pale serikali ya Zanzibar ilipoamua kujiunga na taasisi hiyo kwa ajili ya kutaka kufaidika na misaada inayotolewa na taasisi hiyo. Mara zikasikika kelele kutoka upande wa Bara, kwenye vyombo vya habari, kutoka kwa viongozi wa Kikristo na hata wanasiasa wakiilaumu Zanzibar kuwa imevunja katiba. Mwalimu Nyerere akalikemea sana jambo hilo na kuishinikiza Zanzibari ijitoe katika jumuiya hiyo.

Zanzibar ikakubali kujitoa kwa shuruti kwamba serikali ya Muungano itafanya utafiti kuona kwamba jee Tanzania ijiunge au la. Kikapita kimya kikubwa bila ya serikali ya Tanzania kueleza kama ililifanyia utafiti suala hilo au imelitia kapuni tu. Katika Baraza la Idd el Fitr mwaka huu, ambalo lilihudhuriwa na Rais Benjamin Mkapa, Waislamu walimkabidhi Rais Risala iliyoorodhesha kero walizonazo Waislamu humu nchini na mojawapo ya kero hizo waliikumbusha serikali juu ya hilo suala la Tanzania kujiunga na OIC limefikia wapi? Tunavyosikia na ndivyo Rais alivyoahidi kuwa suala hilo na yote mengine yaliyowasilishwa kwake yatafanyiwa uchunguzi wa kina na kutafutiwa ufumbuzi wake. Hatuna haja ya kuyatilia wasiwasi maneno ya Mheshimiwa Rais. Tunaamini anafanya hivyo kwa kushauriana na Baraza lake la Mawaziri kama alivyoahidi.

Kinachotushtua na kututia wasiwasi ni hili shinikizo la Jumuiya ya Makanisa Tanzania (CCT) kumwonya Rais asimamishe mpango wa Tanzania kujiunga na OIC, kwa sababu nchi hii si ya Waislamu ni suala la kuvunja katiba, lakini kauli hii ya CCT inatuonyesha kuwa tatizo halikuwa ni uvunjaji wa katiba bali ni la udini!

Bwana Yesu hakukosea aliposema kuwa mtu kabla ya kuangalia kibanzi kilichomo katika jicho la mwenziwe kwanza alitoe boriti lililomo katika jicho lake mwenyewe! Wakati Jumuiya ya Makanisa inaikataza serikali isijiunge na OIC kwa sababu hiyo ni taasisi ya Kiislamu, jee, uhalali wa Tanzania kuwa na uhusiano tena wa Kibalozi na Vatikano Makao Makuu ya Kanisa Katoliki? Waunguja walisibu waliposema "Wafanye wao tu kiambo, tukifanya sisi liwe jambo!"

Kama ni kosa kwa serikali ya Tanzania kuwa na uhusiano na chombo cha kidini basi kosa hilo huwa linathubutu pale chombo hicho kinapokuwa ni cha Kiislamu tu; lakini kikiwa ni chambo cha kikanisa inakuwa si kosa? CCT isitudanganye.

Jumuiya ya Makanisa ya Tanzania inataka serikali ya Tanzania isiwe na uhusiano na OIC na hali ya kuwa taasisi hiyo haijishughulishi na mambo ya kisiasa na wala haiingilii mambo ya ndani ya nchi mwanachama, lakini CCT inanyamazia uhusiano wa Kibalozi uliopo baina ya serikali ya Tanzania na Kanisa Katoliki wakati wakijua kuwa Kansia hilo linaingilia mambo ya ndani ya Tanzania pamoja na siasa za nchi hii.

Kitabu cha Dkt. John C. Sivalon alichokiita "Kanisa Katoliki na siasa ya Tanzania Bara, 1953 hadi 1985" kinathibitisha kuwa Kanisa Katoliki linaingilia siasa za nchi hii. Katika kitabu hicho Dkt. Sivalon anaeleza kuwa uhusiano uliokuwapo baina ya viongozi wa nchi hii na Kanisa Katoliki uliwapelekea viongozi wa Kanisa hilo wawe na nafasi nzuri ya kuongoza maendeleo ya kisiasa hapa Tanzania. (Uk.5).
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook