MAKALA YA KIMATAIFA
 
NATO na mgogoro wa Kosovo
 

Na Abdallah Katunzi
 

NI kawaida kwa watu wenye kufikiri, kutathmini, kuchambua mambo ili kuweza kujua undani wa mambo hayo yanayoyachambua. Katika kufikiri huko lazima kuambatana na utoaji wa hoja ambazo ni madhubuti. Na sio kuwaachia watu wengine watutathminie mambo kama vile sisi ni 'watoto'.

Dunia hii ina jamii mbalimbali, lakini jamii hizo ninaweza kuziweka kwenye makundi makubwa mawili, moja ni la wale wanaoufata utaratibu wa maisha ambao ni sahihi na wengine ni wasiofuata utaratibu huu ambao ndio kamilifu.

Kihistoria kundi hili la pili ni kundi ambalo limekumbwa na matatizo mbalimbali lakini si kama yale yaliyolikumba kundi la kwanza. Kwa hiyo basi ni wajibu wa kundi hili kutumia historia yake ili kutathmini mambo mbalimbali na kuonyesha njia ilio sahihi ya kufuatwa, kwani kundi hili ndilo lenye kuwatoa watu kwenye 'giza' na kuwaonyesha sehemu yenye 'nuur'.

Hivyo basi linapata upinzani kutoka kwenye kundi lingine. Katika upinzani huo njia nyingi zinatumika kama vile 'propaganda' mbalimbali kwa leo la kuficha ukweli na kuwaingiza watu kwenye giza na hatimaye kuweka 'dirisha la chuma'.

Kwa hiyo kuficha ukweli ni kutoa hoja ambazo si madhubuti hivyo basi hoja zenye umadhubuti zinahitajika kuondoa hoja hizo 'chovu'.

Baada ya vita ya pili ya dunia mwaka 1945 kiliundwa chombo ambacho madhumuni yake yalikuwa ni kulinda amani duniani baada ya kile cha awali kushindwa kazi hiyo, chombo hicho kilichoundwa ni UNO yaani United Nation Organisation. Chombo cha awali kiliitwa League of Nationa. Kwa ufupi UNO ndicho chombo chenye dhamana ya kulinda amani duniani na si chombo chochote kile.

Baada ya chombo hiki kuundwa, kikaundwa chombo kingine ambacho ni NATO (North Atlantic Trealy Oraganisation). Jumuia ya kujihami ya nchi za Ulaya Magharibi mwaka 1945.

Kuundwa kwa NATO kukapelekea kuundwa kwa chombo kingine chini ya Urusi (NATO chini ya Marekani). Athari yake ilikuwa ni kuibuka kwa vita baridi na falsafa ya migongano. Katika vita hiyo Jumuiya ya kujihami ya nchi za Magharibi chini ya Marekani ziliibuka na ushindi na kupelekea kuisha kwa vita hivyo baridi.

Jumuiya hii ilijumuisha/inajumuisha nchi kama Marekani, Ufaransa, Ubelgiji, Ugiriki, Ujerumani, Italia, Uingereza na kadhalika na ile nyingine ilijumuisha Urusi, Yugoslavia, Romania, Hangari, Poland na kadhalika. Ikumbukwe kwamba Marekani, Uingereza na Ufaransa pia ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama.

Baada ya mauaji ya mwaka huu ambayo yanasemekana kufanywa na Waserbia ambapo Wakosovo kwa mamia waliuawa, mataifa ya magharibi yaliingilia kati mgogoro huo na kujipa vazi la kuwa wasuluhishi, wakaandaa mazungumzo nchini Ufaransa katika mji wa Rambaoulect na Paris, kushindwa kwa mazungumzo hayo kukapelekea mashambulizi ya NATO dhidi ya Yugoslavia.

Baadhi ya mambo ambayo yalikuwemo ni pamoja na kuwapa Wakosovo uhuru wa kujitawala. Mambo hayo yalipangwa na mataifa hayo wakijua kwamba si rahisi kwa Yugoslavia kuyakubali, na kutoyakubali kutatoa ruhusa ya mashambulizi yao.

Ikumbukwe kwamba sababu ya msingi ni kusimamisha fyeka fyeka ya kikabila Kosovo, hivyo kuzuia maangamizi ya binadamu.

Mashambulizi hayo ambayo yamechukua siku 78 yameleta madhara makubwa pamojana hisia mbalimbali miongoni mwa watu.

Mgogoro huu wa Kosovo ni wa ndani kama migogoro mingine (Kosovo ni jimbo la Yugoslavia), lakini cha ajabu ni kwamba NATO chini ya Marekai imeupa kipaumbele kiasi cha kuwafanya watu wakune vichwa vyao. Ifahamike kwamba suala la kusimamisha fyeka fyeka hizi ni la msingi kabisa lakini ifuate utaratibu uliowekwa na unaokubalika na jumuiya za kimataifa.

Swali la msingi hapa ni je NATO inayo ruhusa ya kufanya mashambulizi hayo? Kama ndiyo, hiyo ruhusa imetoka wapi? Na kama siyo kwanini imefanya hivyo bila ruhusa?

UN Charter inaafiki suala kama hilo iwapo kutatokea sababu kubwa mbili, mosi, kujilinda (self defence) na pili kutekeleza maamuzi ya Baraza la Usalama. Yote hayo hayapo katika mgogoro huu!

Ni kweli usiopingika kwamba mashambulizi haya si halali na ni ya mabavu, na hivyo sababu zake vile vile zitakuwa si sahihi. Nasema hivi kwa sababu hatukuona hali kama hiyo nchini Rwanda na kwingineko.

Historia inatuonyesha kwamba hata katika nchi za jumuiya hii, zimewahi kuwa na matatizo hayo. Mfano ipo mingi lakini miongoni mwa hiyo ni wa Uturuki ambapo Wakurdi wana mahusiano mabaya na serikaki yao na wanataka kujitenga. Kiongozi wao Abdullah Ocalan amekamatwa na amehukumiwa kifo. Hispania na kikundi cha Basque, Uingereza na Waairishi (Irish Republican Army).

Pamoja na mifano hiyo ambayo inaweza kuwa migumu kufahamika, tuna mfano wa karibu katika nchi ya Rwanda. Mauaji ya Rwanda yaliyofanyika mwaka 1994 yamepelekea watu zaidi ya laki sita kupoteza maisha yao bila ya hatua zozote za msingi kuchukuliwa ili kusimamisha fyeka fyeka hiyo, achilia mbali wakimbizi. Walichofanya ni kuyabatiza jina The Massacre of the century.

Mbunge mmoja katika Bunge la Uingereza alimuuliza Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje swali kuhusiana na mauaji hayo na hivi ndivyo swali lake lilivyokuwa: Are there two sets of laws for preventing same type of massacre one for the European and another for the Africans? Akiwa na maana ya kwamba je zipo sheria mbili za kuzuia janga, moja inawahusu Wazungu na nyingine Waafrika? (janga -mauaji).

Katika kujibu swali hilo Waziri huyo alisema The are no reasons for stationing British troops in Rwanda not now not in the future! Kwamba hatuna sababu za kuweka majeshi ya Uingereza Rwanda sio sasa wala baadaye! Lakini sasa wamepeleka majeshi yao Kosovo kwa kuwa ipo sababu. Sababu hiyo ni ipi? Je, ni ile ya kuwasaidia Wakosovo ambayo ni kusimamisha maangamizi ya binadamu? Kama ndio, kwani Rwanda hakukuwa na maangamizi ya binadamu? Na kama sio, sababu hiyo ni ipi?

Simon Horgarth, mwandishi kutoka gazeti la Guardian akiandika kuhusu misaada kutopelekwa Rwanda na akasema Rwanda is thousand of miles away you don't know anyone who spirits his holiday in Rwanda. Rwandan people are not like us, they are even more helpless than the Bosnian Muslim!

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Boutros Boutros Ghali akielezea mauaji hayo alisema This is not a defeat for the UN but for the world community as a whole. Wakati wa mauaji ya Rwanda hatukuona majeshi hayo ya kuzuia maangamizi ya binadamu, labda ya kuwaokoa wageni hali ilivyokuwa mbaya!

Wakati fulani David Wilby ambaye ni Air Commodare aliwahi kusema kwamba Yugoslavia inatumia asilimia 70% ya mapato yake (GDP) yaani Gross Domestics Pruduct kwa ajili ya jeshi. Je, sababu inaweza ikawa ndio hii? Au alisema hivyo akiwa na maana gani? Ukweli ni kwamba sababu ilikuwa ni kupunguza nguvu za Yugoslavia na hilo wamefanikiwa. Hiyo ni hatua ya kwanza. Wakati mashambulizi yakiendelea NATO walitoa matakwa yao ambayo waliyaita kuwa ni NATO Five Demands, msemaji wa NATO Jamie Shea aliyaita Unnegotiable Demand, kwamba si ya kujadiliwa bali kutekelezwa.

Baada ya hizo Demand zikaja nyingine zikaitwa kanuni yaani G8 principales. Moja ya maazimio yaliyokuwemo ni kuruhusu jeshi la kimataifa la kulinda amani Kosovo (Kosovo International peace keeping force) yaani KFOR linaloongozwa na Lt. Sir Mike Jackson.

Miongoni mwa kazi za jeshi hilo ni pamoja na kutekeleza maazimio ya Baraza la Usalama ambayo yanasisitiza kunyang'anywa silaha kwa jeshi la Kosovo (KLA). Jeshi yapo makubaliano ambayo yametiwa saini kati ya Sir Mike Jackson na kiongozi wa jeshi la ukombozi wa Kosovo Hashim Thaci. Makubaliano hayo ambayo Sir M. Jackson anayaita 'Unlateral Undertaking' yatatekelezwa ndani ya siku thalathini (3).

Swali la kujiuliza hapa ni yepi madhumuni ya kufanya hivyo? Halafu baadaye iweje? Wanasisitiza kuwa jeshi hilo libadilike na kuwa chama cha siasa baadaye kiunde serikali, wasivae nguo za jeshi hadharani, hizi zote ni njama za kuwapangia utatatibu wao ikiwemo na serikali ambayo itakuwa imetekeleza matakwa ya mataifa hayo 'Puppets government'.

Mwanahistoria mmoja aliwahi kusema na ninamnukuu History teaches us that, in certain circumstances its easy for a stranger to impose his rule on a people, But history equally teaches us that whatever the material espects of that rule, it can't be sustained except by the permanet and organised repression of the cultural life of the people in question, it can only firmly entrench itself if it physically destroy a significant part of the dominated people?

Kazi ya kwanza imekwisha sasa imebaki kazi ya kuwabadilisha Wakosovo. Tusijeshangaa kesho na keshokutwa wakosovo wakawa mahasimu wakubwa wa nchi hizi. Naomba ieleweke kwamba NATO haiwachukii Waserbia bali sera za Slobodan Milosovic, hivyo basi akipatikana kiongozi wanaomtaka akafuata wanayotaka atakuwa rafiki yao, lakini NATO haitakuwa na urafiki na watu wenye utaratibu sahihi wa maisha, hivyo urafiki huu ni ulaghai na unatakiwa kuangaliwa kwa makini sana.

Vipo vikundi au watu wenye tabia kama za NATO hivyo hatuna budi kuwa waangalifu ili tusidanganyike. Kwani hawa wote wana tabia zinazofanana na malengo yanayofanana. Hivyo basi, nini tunajifunza kutokana na mgogoro huu? Ni swali la msingi ambalo tunapaswa kulitafakari, tusiwafanye maadui kuwa rafiki.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook