Na Muhibu Said
KATIKA makala iliyopita tuliendelea kuona udhaifu wa hoja za Bw. Elia Batendi zilizochapishwa katika gazeti hili (rejea AN-NUUR namba 205 uk. 8). Hoja hizo dhaifu alizozitunga ni pamoja na maelezo yaliyo katika kitabu cha Isaya 14:14 aliyodai kayatoa kwa mtaalam wake wa magonjwa ya kinamama, majina ya Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) ya "Baba", "Bwana wa Majeshi"", "Mungu wa Israeli" yaliyo katika vitabu vya kale aliyodai yawemo pia kwenye majina mengine 99 ya Mwenyezi Mungu yatajwayo na Qur'an takatifu na utukufu wa mji wa Yerusalem na mji wa Makka. Katika maelezo ya hoja hii (ya utukufu wa mji wa Yelusalem na mji wa Makka) tuliona kwa uchache, jinsi Nabii Yesu (a.s.) alivyobashiri kuhama kwa utukufu wa dini ya Mwenyezi Mungu kutoka Yerusalem. Endelea...
SAMBAMBA na bishara hizo chache alizozitoa Yesu (kama tulivyoona katika toleo lililopita) juu ya kuondolewa utukufu wa dini ya Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) kule Yerusalemu na mji huo kuachwa ukiwa (rejea Yohana 4:21 na Mathayo 23:37-39), Nabii Yesu (a.s.) hakuacha pia kuelezea ni wapi utukufu wa dini ya Mwenyezi Mungu utakapokwenda baada ya kuondoka Yerusalemu, kama tunavyosoma maandiko yafuatayo:
"...Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake". (Mathayo 21:33-43).
Hapa Nabii Yesu (a.s.) anatuonyesha wazi kwamba baada ya utukufu wa dini ya Mwenyezi Mungu kuondolewa Yerusalemu, utakwenda kwa taifa lingine. Na kwa mujibu wa maandiko ya Biblia (kama tutakavyokuja kuona punde), taifa hilo ni lile litakaloendesha maisha yao kwa mujibu wa sheria za Mwenyezi Mungu na hilo ndilo litakaloendeleza utukufu wa dini ya Mwenyezi Mungu (s.w.t). Uthibitisho wa kuwepo taifa hilo unadhihirishwa na maandiko yafuatayo ya Biblia tukufu:
"Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je, hamwisikii sheria? Kwa maana imeandikwa ya kuwa,Ibrahimu alikuwa na wana wawili, mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi. Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima wa Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri. Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa anatumika pamoja na watoto...". (Wagalatia 4:21-5:1)
Baada ya kusoma na kuyaelewa vizuri maandiko ya vitabu vya Mwenyezi Mungu vya kale, Bwana Paulo anatufafanulia hapo juu kwamba taifa hilo litakaloendeleza utukufu wa dini ya Mwenyezi Mungu ya sheria duniani aliyoisema Nabii Yesu (a.s.) ni lile litakalotokana na mwana wa Bibi Hajiri (Nabii Ismaili a.s.) aliyemzaa kwa Nabii Ibrahimu (a.s.); mwana wa agano la Sinai ya Arabuni, yaani agano la sheria linalotokea Arabuni kupitia (uzao wa) Nabii Ismaili (a.s.) ambaye kama maandiko mengine ya Biblia tukufu yanavyoeleza aliishi katika jangwa la Parani, yaani Makka; Mwenyezi Mungu akawa pamoja naye huko (Parani). (Tazama Mwanzo 21:20-21).
Baada ya mama yake kumtwalia mke kutoka nchi ya Misri (Mwanzo 21:20-21), maandiko ya Biblia yanaonyesha kuwa Nabii Ismaili (a.s) alizaa Maseyidi kumi na mbili (tazama Mwanzo 25:12-16). Katika Maseyidi hao 12 waliozaliwa na Nabii Ismaili (a.s.) mwana wa Hajiri mmoja alimwita Kedari.
Huyu Kedari (mwana wa Nabii Ismaili a.s.) ndiye chimbuko la Nabii Muhammad (s.a.w.) kama uzao wake unavyoeleza na ndiye jina lake hapo zamani ndilo lilitumika kuuita mji mtukufu wa Makka sasa. (Rejea Taariykhul Islaami).
Na kwa hakika Muishmaeli (Ismaili) aliyekuja kuuendeleza utukufu wa dini ya Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) ya sheria duniani kama bishara zile zinavyooelezea, si mwingine yeyote ila maandiko yanathibitisha kuwa ni Nabii Muhammad (s.a.w.) (tazama Qur'an 42:13); ambaye baadaye ndiye Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) akamthibitishia kwamba mji huo wa Makka nao vile vile ni mji wake mtukufu, kama tunavyosoma katika aya ya Qur'an takatifu ifuatayo ambayo ilitajwa pia na Bw. Batendi katika rejea zake hapo juu:
"Bila shaka nimeamrishwa nimwabudu Mola wa mji huu (wa Makka) ambaye ametukuza na ni vyake tu (Allah) vitu vyote na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wanaonyenyekea". (Qur. 27:91)
Kwa uchache, hii ndiyo aya ya Qur'an takatifu inayothibitisha kwamba mji wa Makka nao ni mji uliotukuzwa na Mwenyezi Mungu (Allah/Yehova) wakati wa Nabii Muhammad (s.a.w.). Na kama tulivyokwisha kuona katika toleo lililopita, utukufu wa mji huo (wa Makka) sawa na mji ule mtukufu wa Yerusalemu, hauwakilishwi na kila kilichomo au aliye ndani yake. Utukufu wa mji wa Makka nao unawakilishwa kwa kushushwa kwa dini ya Mwenyezi Mungu (Allah/Yehova) kupitia Nabii wake wa mwisho, Mtume Muhammad (s.a.w.); na kuwepo ndani yake nyumba yake nyingine takatifu (Msikiti na Al Ka'aba Shariyfu). (Rejea Qur'an 95:3; 17:1).
Kwa hakika, huu ndio ukweli wa yakini wa maandiko ya Biblia tukufu na Qur'an takatifu kuhusu utukufu wa miji ya Yerusalemu na Makka; kwamba yote ni miji ya Mwenyezi Mungu yule yule mmoja (Yehova au Allah (s.w.t.) aliyejifunua kwa Manabii wake mbalimbali kwa majina tofauti. Sivyo kama apotoshavyo Bw. Batendi.
Upendo wa Mungu kwa Mayahudi
Bw. Batendi anapinga tena kwamba Yehova si Allah (s.w.t) kwa kusema:
"Mungu Yehova anawapenda Israeli (Yer. 31:3) na atawatupilia mbali iwapo misingi ya dunia itaweza kugunduliwa (Yer. 31:37). Mungu Allah anasema Mayahudi ndio maadui wabaya kuliko wote". (Qur. 5:82).
Kutokana na dai lake hilo juu, kwanza yaonyesha dhahiri Bw. Batendi bado hajaziona aya za Qur'an takatifu zifuatazo zinazoonyesha kwa uwazi upendo wa Allah (s.w.) kwa wana wa Israeli na hivyo kudhihirisha kwamba Allah kwa "kigezo" chake hicho ndiye yule yule Yehova:
"Enyi kizazi cha Israeli (Mayahudi)! Kumbukeni neema zangu nilizo kuneemesheni, na nikakutukuzeni kuliko viumbe wengine". (Qur. 2:47)
"Na (kumbukeni) Tulipokutoeni kwa watu wa Firauni waliokupeni adhabu mbaya; wakiwachinja watoto wenu wanaume na kuwaacha hai wanawake, na katika hayo ilipatikana neema kubwa iliyotoka kwa Mola wenu. Na (kumbukeni) tulipoitenga bahari kwa ajili yenu na tukakuokoeni, na tukawazamisha watu wa Firauni na hali mkitazama". (Qur. 2:49-50)
"Na tukakutilieni kivuli kwa mawingu (mlipokuwa mnakata jangwa kutoka Misri kwenda Sham) na tukakuteremshieni Manana na Salwa: (Tukakwambieni) "Kuleni katika vitu vizuri hivi tulivyokuruzukuni"... Na (kumbukeni khabari hii vile vile:) Tuliposema: "Ingieni mji huu, na humo kuleni kwa maridhawa popote mpendapo, na ingieni katika mlango wake kwa kunyenyekea na semeni "Tusamehe dhambi zetu". Tutakusameheni makosa yenu, na tutawazidishia wema wale wafanyao wema". (Qur. 2:57-58).
Kwa uchache, Aya hizo zote za Qur'an takatifu zinaonyesha wazi kabisa jinsi Allah au Yehova alivyowapenda sana wana wa Israeli kiasi cha kuwatukuza kuliko viumbe wengine duniani.
Pili, Bw. Batendi anatakiwa afahamu kwamba Mwenyezi Mungu kuwapenda Waisraeli si kwa sababu wao ni Waisraeli; hapana! Lakini kama maandiko matakatifu yanavyofundisha, Mwenyezi Mungu ataendelea daima kuwapenda si Waisraeli tu mpaka kiama bali na watu wengine pia, pale watakapomtii Mwenyezi Mungu kwa kufuata maamrisho yake na kuacha makatazo yake, kama tunavyosoma maandiko yafuatayo:
"Itakuwa utakaposikia sauti za BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote duniani, na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako... Lakini itakuwa usipotaka kuisikiliza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kupata. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani". (Kumbukumbu la Torati 28:1-16)
"Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya". (Isaya 1:19).
"... Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Allah ni yule amchaye zaidi katika nyinyi...". (Qur. 49:13)
Kwa uchache, hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyowapenda na kuwaheshimu wana wa Israeli na watu wengine, pale tu watakapomtii na kufuata maagizo yake, na si vinginevyo.
Kwa hiyo Allah/Yehova katika Qur'an takatifu aliposema kwamba Mayahudi (wana wa Israeli) ni "maadui zaidi kuliko watu wengine" (Qur. 5:82), hakukosea kwa kuwa yeye daima ni mkweli (Qur. 4:122; 2 Samweli 7:28).
Ni lazima (Mayahudi) watakuwa wamekiuka maagizo yake na ndio Allah/Yehova (s.w.t.) akawaita kuwa ni maadui.
Uthibitisho mmojawapo kwamba Mayahudi waliasi na hivyo kustahiki kuonekana kuwa ni maadui zaidi kuliko watu wengine, maandiko ya Biblia tukufu na Qur'an takatifu yanaweka bayana ukweli wa shutuma hiyo dhidi yao kama ifuatavyo:
"...Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya Allah, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Basi haya ni kwa sababu ya kuasi kwao na kupindukia mipaka". (Qur. 2:61).
"Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanamu? Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi, na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji; hivyo ije juu yenu damu yote ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemuua kati ya patakatifu na madhabahu. Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye Manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!". (Mathayo 23:33-37).
Kulingana na maandiko hayo juu, tunaona wazi jinsi uasi wa Mayahudi ulivyopindukia kiasi cha kufikia kuua Manabii wa Mwenyezi Mungu. . Ambapo Nabii Yesu (a.s.) kwa kuchukizwa na ukatili wao huo, alifikia kuufananisha "uadui wao" huo (wa kuua Manabii) sawa na majoka. Hapana shaka uasi huo peke yake watosha kuthibitisha kwamba wao ni maadui wabaya zaidi kuliko watu wengine wote duniani, kama aya ya Qur'an takatifu (ya 5:82) aliyoitaja Bw. Batendi inavyoeleza.
Kwa shuhuda hizo, kigezo hiki si hoja ya msingi ya kufanya Allah kuwa ati si Yehova!
|
|