BARAZA LA MAULID MORO
 
Msiogope kudai haki zenu - Sheikh Mbukuzi
 

Na Mussa Ally, Morogoro
 

MGENI rasmi katika Baraza la Maulidi lililofanyika katika Msikiti wa Kiwanja cha Ndege mjini hapa Sheikh Juma Mbukuzi ambaye pia ni Amir wa Waislamu Dar es Salaam amewataka Waislamu kote nchini kutowagopa watawala katika kudai haki zao badala yake wamwogope Mwenyezi Mungu.

Akizungumza katika Baraza hilo mapema wiki hii, Sheikh Mbukuzi alisema kuwa woga unahatarisha maslaha ya Waislamu naUislamu nchini.

Sheikh huyo pia aliwekawazi kuwa yale yote yanayowatokea Waislamu wa Tanzania hivi leo ni kwa sababu tu wamegoma kutenganisha dini na siasa pamoja na uchumi katika maisha yao ya kila siku, kiasi cha maadui wa Uislamu kuwaita kuwa ni wenye msimamo mkali.

"Wanachotaka maadui wa Uislamu nchini ni kwa Waislamu wa Tanzania kutenganisha dini na siasa pamoja na uchumi, Waislamu wa aina hiyo ndiyo wanaowapenda na kuwaita kuwa ni Waislamu waungwana", amesema Sheikh Mbukuzi huku akisoma waraka wa Kadinali Pengo (alipokuwa Askfu wa Dar es Salaam) kwa watendaji wake Parokia kutilia nguvu hoja yake.

Naye Ustaadh Musa Kileo aliwataka viongozi wa Misikiti kote nchini waendeshe sensa ya Waislamu katika maeneo yao, ili kuwawezesha kutengeneza miundo mbinu ya maendeleo yao katika eneo husika.

Aidha, akawatanabahisha Waislamu kuwa makini na mada zinazoundwa na makafiri ili kuwashughulisha huku wao wakisukuma mbele mambo yao.

Muhadhiri mwingine Ustadh Salim Khamis wa Dar es Salaam katika madai yake "Nini Mtume alituachia kama urithi" katika Baraza hilo, alisema kwamba urithi pekee Mtume (s.a.w.) aliowaachia Waislamu ni Qur'an na Sunnah na si vinginevyo. Hivyo, aliwataka Waislamu waishi kwa mujibu wa Qur'an.

"Kwa Waislamu kuwacha mwongozo aliowapa Mwenyezi Mungu na kufuata miongozo iliyotungwa na wanadamu wenzao, ni sawa na kutoka kwenye nuru ya matumaini mema na kuingia katika kiza cha maangamizi".

Wengine waliozungumza katika hadhara hiyo tukufu ya Uzawa wa Mtume (s.a.w.) ni pamoja na Sheikh wa Baraza Kuu Mkoa Sheikh Ayoub Salum Muwinge aliyehimiza mshikamano miongoni mwa Waislamu, Katibu wa Baraza hilo mkoa Sheikh Ahmed Mabira aliyetoa changamoto kwa Waislamu wa mkoa huo kuandaa utaratibu wa kuwa na Amiri mmoja kama wenzao wa Dar es Salaam, Sheikh Zakaria wa Dar es Salaam aliyewahimiza Waislamu kuwa watu wa vitendo zaidi kuliko nadharia na Ustaadh Juma Ramadhani pia wa Dar es Salaam aliyewausia Waislamu wawe na msimamo thabiti katika vita dhidi ya dhulma na ukandamizaji vinavyofanywa na serikali ya CCM dhidi ya Waislamu nchini.

Aidha, baraza hilo lilitoa tamko kwamba kwa kuwa Waislamu nchini wamedhalilishwa, kunyanyaswa na kunyonywa na serikali ya CCM kiasi cha kutosha basi wakati umefika wapewe haki zao na suala hilo lisilo na mjadala ni la lazima sio ombi.

Pia wameitaka serikali ya CCM kuwachukulia hatua wale wote waliohusika kwa njia moja au nyingine na mauaji ya Mwembechai, na si kuwasaka wasiohusika.

Mapema katika hafla hiyo, Kamati ya Kutetea haki za Wanawake wa Kiislamu Tanzania iliwataka kinamama wa Kiislamu nchini kujifunga vibwebwe kuondoa dhulma kwa njia ya boksi la kura ili kuondoa utawala mbovu unaondesha dhulma na ukandamizaji dhidi yao.

Kwa kuanzia kamati hiyo iliwaasa wanawake hao washiriki kikamilifu kuleta mabadiliko ya uongozi katika serikali za mitaa na vijiji, kupitia chaguzi zake zitakazofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Wakati huo huo, Waislamu wa Msikiti wa Kiwanja cha Ndege mjini hapa wametoa tathmini yao ya maendeleo katika Baraza hilo.

Akitoa tathmini hiyo, Mwenyekiti wa Msikiti huo Bw. Shomari Mtogo alisema kwamba hivi sasa wameanza ujenzi wa shule ya watoto wadogo na msingi.

Hadi sasa mradi huo umekwishagharimu jumla ya shilingi 4,272,500 toka katika michango ya waumini wa Msikiti huo. Hatua iliyobaki itagharimu jumla ya shilingi milioni 9.7.

Hivyo, Bw. Mtogo aliwaomba Waislamu popote walipo kusaidia mradi huo kwa hali na mali ili kuleta mapinduzi ya kweli kitaaluma katika jamii hiyo.


Wanawake wa Kiislamu wamtaka Mufti apumzike
 

Na Mwandishi Wetu

SHEIKH Mkuu wa Bakwata, Hemed bin Juma ametakiwa kujiuzulu nafasi aliyonayo ili kulinda heshima yake na Waislamu hapa nchini.

Ushauri huo umetolewa na kongamano la wanawake lililokutana mwanzoni mwa wiki katika Msikiti wa Taqwa Mwanyamala Jijini.

Kongamano hilo liliandaliwa kufuatia hotuba ya Sheikh Hemed aliyoitoa katika Baraza la Maulidi lililofanyika Ikwiriri wilayani Rufiji.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake Taifa Bi. Fatma Lazaro alimuomba Sheikh Mkuu apumzike kwa kuwa umri wake umepea hali inayoweza kumkosesha udhibitifu wa masuala mbalimbali yanayojitokeza katika ulimwengu huu.

Bibi huyo aliwaomba ndugu wa karibu, jamaa na wapenzi wa Sheikh Mkuu wamsisitize kuchukua uamuzi huo.

Wanawake wengine waliopata fursa ya kuongea katika kongamano hilo walielezea kuchukizwa na tabia iliyojengeka hapa nchini kwa viongozi wa serikali kuteka nyara hafla za kitaifa za Waislamu kupitia Bakwata.

Wamesema tabia hiyo inathibitisha madai ya Waislamu kwamba Bakwata ni chombo kilichoundwa na serikali kuwadhibiti Waislamu.

Hotuba ya Mufti Hemed Ikwiriri sehemu kubwa ilishutumu habari zilizoripotiwa na gazeti hili kuhusu kupingwa Waziri Mkuu Bw. Frederick Sumaye kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Maulidi wilayani Rufiji.

Sheikh Mkuu alizieleza habari hizo kuwa hazikuwa na msingi na zilitawaliwa na jazba na kijicho hivyo alimtaka radhi Waziri Mkuu kwa fedheha kutokana na taarifa hiyo.

Hata hivyo, hakuwa Sheikh Hemed wala Waziri Mkuu Bwana Frederick Sumaye katika hotuba zao aliyeweza kukanusha ukweli kwamba mauaji ya Mwembechai yalipongezwa badala ya kulaaniwa.


Maulid yasheherekewa kwa ulinzi mkali
 

Na Mwandishi Wetu

SHEREHE za Maulidi ya Mtume (s.a.w.) zilizoandaliwa Ikwiriri mwishoni mwa wiki iliyopita zilifanyika huku kukiwa na ulinzi mkali wa makachero waliotawanywa sehemu mbalimbali za eneo hilo.

Mbali na ulinzi wa kawaida kwa ajili ya viongozi wa juu wa nchi, uwanja wa Msikiti ulizungukwa na utitiri wa maaskari waliokuwa wakipita na kukagua hiki na kile muda wote wa shughuli hiyo.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia tukio moja ambapo watu ambao hawakuweza kufahamika waliingia nyumba moja iliyojirani na Msikiti Mkuu baada ya kuangaza huku na kule walitoka bila ya kuzungumza na yeyote.

Kona zote muhimu ya kuingilia uwanja wa Msikiti huo zilikuwa na watu waliokuwa makini kuchunguza tukio. Makachero hao wengine wakiwa wamevalia kanzu na vibandiko walizunguka hapa na pale hali iliyosababisha hofu kwa waumini waliohudhuria 'sherehe' hiyo.

Tukio jingine ambalo halikuwa la kawaida ni lile la kupokewa kwa mgeni rasmi katika mkesha Dk. Omar Ali Juma ambapo akinamama waliovalia sare ya khanga iliyokuwa na maandishi ya TANU na Afro Shirazi walipamba upokezi huo.

Kwa upande mwingine waandalizi wa shughuli hiyo, walikuwa imara kuhakikisha ratiba haitoi nafasi kwa "wakorofi" kama ilivyojitokeza mwaka jana wilayani Bagamoyo.

Makundi ya Twariqa yaliamriwa kuwa mbali na mahali walipoketi wageni rasmi tangu siku ya mkesha na wakati wa Baraza la Maulidi.

Udhibiti huo ulionekana kuzua malalamiko yaliyopelekea baadhi ya waumini kususia shughuli hiyo kwa madai kwamba haikuendeshwa Kiislamu na kwamba hawakupata kuyaona mambo hayo katika Maulidi zilizopata kufanyika.

Hata hivyo wengine walionyesha kufurahia kuwaona viongozi wa kitaifa waliohudhuria sherehe hiyo.

Nasaha zilizotolewa ni pamoja na zile za Makamu wa Rais ambaye aliwataka Waislamu wajiepushe na migogoro inayoweza kusababisha vurugu hatimaye kuvunja amani na utulivu nchini.

Mufti Hemed aliwataka Waislamu wawe wapole na wavumulie taabu wanazozipata.

Naye Waziri Mkuu Mhe. Frederick Sumaye akizungumza katika Baraza la Maulidi siku ya pili, aliwataka Waislamu wamuige Mtume (s.a.w.) kivitendo.

Aidha aliwataka walaani mauaji yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Mbeya ambapo watu wawili waliuawa na kuchunwa ngozi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu hakugusia kabisa mauaji ya raia Waislamu yaliyofanywa na polisi katika Msikiti wa Mwembechai Jijini Dar es Salaam. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook