Moto wa siasa wawaka Dar
 

Na Mwandishi Wetu

MOTO wa siasa za upinzani umelikumba Jiji la Dar es Salaam ambapo hivi sasa mrindimo wake unaelekea kuvishughulisha vyombo vya dola, ANNUUR imegundua.

Ubebaji wa jeneza wenye kuashiria kukizika Chama Tawala, hotuba zenye mchomo na shamrashamra za Kosovo, Chechnya, Nato na Usama bin Laden zilizotanda katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Ubunge zinaonekana kuwakosesha usingizi watendaji wa serikali na vigogo wa Chama tawala.

Makundi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya Jiji hususan majimbo ya Temeke na Ubungo yamekuwa yakijadili siasa za nchi kwa mtazamo wa mabadiliko.

Mwandishi aliwakuta vijana katika "kijiwe" kimoja eneo la Ubungo ambacho hufahamika kwa jina la Brunei, wakitathmini hali yao ya maisha chini ya utawala wa miaka 38 wa serikali ya CCM.

Baadhi ya watu waliohojiwa na gazeti hili kuhusiana na mwamko huo wa kisiasa wamesema kiini kikubwa ni hotuba za Mshauri Mkuu wa Chama cha CUF Profesa Ibrahim Lipumba ambazo huchambua hali ya Watanzania kiuchumi na kuonyesha jinsi serikali iliyopo madarakani ilivyoshindwa kuwajibika kwa kupindi chote cha uongozi wake.

Uchunguzi wa ANNUUR umeonyesha kwamba vijana kwa wazee, wanawake kwa wanaume ambao hivi sasa wanaonekana kuunganishwa na istilahi za makabwela na wanyonge, wameyageuza maeneo ya Manzese, Mwembechai, Tandale, Mburahati na Temeke kuwa kambi zinazojadili mabadiliko ya uongozi nchini yenye lengo la kuboresha kile wanachokiita hali mbaya ya maisha inayowakabili.

Haki na usawa kwa wote, asiyetaka haki aende "Butiama", aelimishwe, "anywe sumu" ndio nyimbo zinazoonekana kutawala siasa za upinzani Jijini.

Mtaalam mmoja wa masuala ya jamii ameufananisha muelekeo huu wa kisiasa unaoanza kupenya taratibu miongoni mwa Watanzania na ule uliowashwa na waasisi wa itikadi ya kijamaa karne iliyopita ambao kwa maandiko na hotuba waliamsha mapambano baina ya makabwela na wale walioonekana kuwa ni mabwanyenye.

ANNUUR ilishuhudia maelfu ya watu katika maeneo ya Mwembechai na Temeke wakiimba kwa sauti kukikana Chama tawala huku mioto ikiwashwa kuashiria 'kumekucha' wako njiani kuelekea 'ukombozi'.

Kwa upande mwingine chama tawala hakionyeshi kuikubali demokrasia hii inayoelekea kutishia himaya yake.

Viongozi wa chama hicho na serikali yake wanaonekana kutaharuki ambapo mara kadhaa wamekuwa wakitoa matamshi ya shutuma na vitisho dhidi ya vyama na wapiga kura wasiowakubali.

Katibu Mkuu wa CCM Bwana Philip Mangula aliwashutumu watu waliosemekana kutumia Misikiti kutaka kuvuruga uchaguzi ambapo alidai kuwa kanzu na vibandiko vimekuwa vikigawiwa kushawishi wapiga kura.

Zito la yote ni matamshi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bibi Rita Mlaki yaliyowataka wapenzi wa CUF kusitisha shamrashamra zao zinazoandamana na ubebaji wa jeneza lenye kuashiria kukizika chama tawala.

"Hii ni dharau kwa serikali na ni uhuni. Tunalaani vitendo hivyo vya kumtukana Rais na chama tawala na tunasema serikali italishughulikia suala hilo kwa mujibu wa sheria. Serikali ipo na ina uwezo huo", vyombo vya habari vimemkariri Bibi Mlaki kusema hayo na aliongeza; "Nazungumza kama serikali na sio mwana CCM wala Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM".

Matamshi hayo yalitafsiriwa kama ni hatua ya kuvinyima uhuru vyama vya upinzani.

Vyombo vya dola kufuatia kauli hiyo vinaelekea kuitikia wito ambapo kwa siku tatu mfululizo vimekuwa vikimimina maaskari wa kawaida na FFU katika mikutano ya CUF.

Ni maoni ya wananchi wengi kwamba upo uchanga kwa viongozi katika kuzielekea pilikapilika za medani ya siasa za upinzani.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook