Na Mwandishi Wetu
KIONGOZI wa Ansaar Sunnah Tanga amedai kwamba kupiga kura katika nchi hii ya Tanzania ni ukafiri kwani kufanya hivyo ni kusaidia kuweka tawala za kitwaghuti.
Alisema kuwa nchi hii inaendeshwa na sheria za kitwaghuti na hivyo kushiriki kuzisimamisha' ni kumshirikisha Allah (s.w.).
Akifafanua kauli yake, Sheikh Salim Barahiyan alitoa mfano wa Bunge la Tanzania linavyotunga sheria kinyume na za Allah na hivyo kumshirikisha Allah.
Aidha aliwashutumu viongozi Waislamu waliomo serikalini akidai kuwa hawafanyi lolote la kuusaidia Uislamu ila kumuasi Allah kwa kufungua Makanisa, 'Club' za pombe na kuleta mabenki ya riba.
Akizungumzia muafaka wa CUF na CCM huko Zanzibar alisema kuwa muafaka huo ni batili kwa sababu ni maafikiano ya kikafiri kwa vile hawakutumia Qur'an na Sunnah. Na kuwashutumu Wazanzibari kuwa hawajaufanyia lolote Uislamu zaidi ya kuudididimiza.
Kuhusu suala la Waislamu kuuliwa Mwembechai Sheikh Salim alisema kuwa suala hilo sasa ni usafiri wa kuwapeleka watu Bungeni (isipokuwa CCM) kwani kila anayetaka kura anazungumzia suala hilo. Alieleza kuwa katika tukio hilo hapakuwa na maandalizi kwani haiwezekani watu wenye mawe wapambane na askari wenye bunduki.
Hata hivyo, hakufafanua ni maandalizi gani na silaha gani Waislamu wangejiandaa nazo.
Awali katika mawaidha yake katika ukumbi wa Mikutano wa shule ya sekondari Thaqafa, Sheikh Salim alihimiza juu ya kumpwekesha Allah (s.w.). Alisema kuwa kuhukumu kinyume na sheria za Allah ni ushirikina na ukafiri.
Mawaidha ya Sheikh Salim Barahiyan yamewaacha hoi wananchi wa Mwanza wasijue nini lengo hasa la ziara ya Sheikh ambayo itakuwa nchi nzima akianzia Mwanza, Shinyanga na Kigoma.
Sheikh Jabir Katura aliyeonekana mwenyeji wa ugeni huo ilibidi atoe ufafanuzi kuwa hawezi kumdhibiti mzungumzaji wala kumpangia la kusema ila wasikilizaji wawe na subira na kuichanganua mada. Hiyo ilikuwa ni kutokana na masikitiko ya watu dhidi ya mtoa mada na viongozi waliomkaribisha.
Waislamu wengi wameitafsiri ziara hii ya Amir Mkuu wa Ansaar Sunnah Tanga kama ishara ya kuanza kwa harakati za madalali wa haki za Waislamu.
Wamesema kuwa ukiwazuia watu kushiriki kupiga au kupigiwa kura ni kwamba unawapa fursa wengine waweke viongozi wawatakao kwa maslahi yao. Na serikali watakayounda ni lazima uitii kama ambavyo Ansaar wanaitii serikali ya CCM leo kwa kuisajili taasisi yao kwao.
Wananchi wengi walioongea na mwandishi wa habari hizi wamesema kuwa wana wasiwasi na ziara ya Sheikh Salim kuwa ni ya kuipigia kampeni CCM.
Wamesema kuwa serikali ya CCM inajua imewadhulumu Waislamu zito ya yote ikiwa Mwembechai. "Kama atapatikana mtu wa kuwashawishi baadhi ya Waislamu wasishiriki kupiga kura 2000 hapana shaka atakuwa ameifanyia fadhila kubwa CCM", alisema Abu Hajra aliyeongea na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake.
Aidha amemtaka Sheikh Salim awaeleze Waislamu huo mpango wake alionao wa kusimamisha serikali isiyo ya kitwaghuti au vipi mahusiano yao yawe na serikali ya kitwaghuti baada ya kuwasusia wasiokuwa Waislamu waunde serikali wenyewe watakavyo yaani wagombee Urais na Ubunge wenyewe pamoja na kujipigia kura wenyewe, kisha Baraza la Mawaziri, Bunge na watendaji wote wa serikali wawe wasiokuwa Waislamu watupu.
"Je, Waislamu wakishasusia kupiga kura kwa vile ni ukafiri; wanaishije na serikali hiyo; je, waisusie waiasi?", alihoji Abu Jahar.
Aidha, baadhi ya Waislamu wameipinga hotuba ya Sheikh Salim kwa maelezo kwamba hata katika jumuiya yenyewe ya Ansaar Tanga ambayo ingekuwa kigezo cha hayo anayoyahimiza kumekuwa na mambo ambayo hayaendeshwi kwa mujibu wa Qur'an na Sunnah.
"Ule mtindo wa kuwa na kadi ya uanachama na asiyekuwa na kadi haruhusiwi kupiga kura wameutoa wapi", alihoji Ustaadh Rajab wa Mwanza.
Habari kutoka Kigoma zimeeleza kuwa Waislamu wanamsubiri Sheikh Salim awaeleze baada ya kuwasusia Wakristo serikali hii ni ipi itakayokuwa serikali yao na namna ya kuipata na yapi yatakuwa mahusiano ya serikali hizo mbili.
Madhara ya Waislamu kususa siasa yameelezwa kuwa ndiyo yaliyopelekea Benazir Bhuto kushinda uchaguzi na kuongoza Pakistan kwa miaka kadhaa kabla ya kuondolewa madarakani kutokana na tuhuma za ulaji rushwa.
Katika chaguzi hizo jumuiya
ya Tabligh nchini humo ilitumika kuendesha kampeni ya kuwazuia Waislamu
kupiga kura. Na huko Pakistan ndiko alikosomea Sheikh Salim baada ya kuacha
kazi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia.
--
|
|