Lipumba asema uchaguzi Dar uwe cheche ya ukombozi
 

Na Mwandishi Wetu
 

IPO haja ya kutoa picha ya mabadiliko mwakani kupitia chaguzi ndogo za Ubunge na kwamba majimbo ya Temeke na Ubungo yawe cheche ya ukombozi wa Tanzania mwakani, Profesa Lipumba amewaambia wananchi.

Akizungumza katika kampeni za jimbo la Ubungo Mshauri huyo wa CUF amesema uchaguzi huo ni kioo cha mabadiliko ya nchi nzima mwaka 2000.

Lipumba aliuambia umati mkubwa wa wananchi wa Mwembechai na Mburahati kwamba hali mbaya ya kiuchumi inayolikabili Taifa haiwezi kuondolewa na serikali ya CCM.

Alisema wakati wananchi wanalia kwa dhiki na hali ngumu, serikali ya CCM inajitapa kuwa hivi sasa hali ya uchumi ni nzuri.

"Akinamama wanauza maandazi mpaka saa saba masinia yakiwa yamejaa hakuna mnunuzi, watu hawana pesa", alisema mwanasiasa huyo ambaye ni mtaalam wa mambo ya uchumi.

Aidha, Profesa Lipumba aliwalaumu Wabunge waliopitisha bajeti ya serikali ya mwaka huu ambayo alisema imeidhinisha shilingi bilioni 3 kukarabati Ikulu.

"Ikulu na Manzese sehemu gani inahitaji matengenezo, bajeti ya serikali ya CCM imetenga shilingi ngapi kutengeneza majimbo inayoomba kura hivi sasa", Profesa Lipumba alihoji huku watu waliokuwa wakimsikiliza wakiwa wameacha midomo wazi kwa mshangao.

Aliwachekesha watu aliposema CCM inawazeesha Watanzania kiasi kwamba ni vigumu kuwatofautisha vijana na wazee.

"Kijana wa miaka 25 anaonekana mzee kwa dhiki ya maisha", alisema.

Kuhusu mikopo na misaada kutoka kwa wahisani alisema serikali ilipokea shilingi bilioni 161 kutoka nje ambazo zilikopeshwa kwa wafanya biashara wakubwa. Pesa hizo hadi hivi sasa hazijalipwa na wafanyabiashara hao badala yake alisema Profesa Lipumba kwamba wamekuwa wakitoa michango kuisaidia CCM.

"Bilioni 161 zingetumika kutengeneza barabara Dar, zote zingetengenezwa pamoja na miradi ya maji", alisema.

Kuhusiana na malipo ya wafanyakazi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Profesa Lipumba alisema tangu jumuiya hiyo ivunjike mwaka 1977 serikali imekwamisha malipo yao.

"Watu walikuwa na mishahara yao kwa mwajiri wao, watu walikuwa na haki zao na mwajiri wao mpaka hivi sasa wafanyakazi hao hawajalipwa", alisema na kuongeza kwamba juu ya wale waliofariki dunia hakuna orodha ya ndugu zao; "kama sio dhulma hii ni nini?"

Alimalizia hotuba yake kwa kuwasisitiza wapiga kura wa Ubungo na Temeke kwamba dhamana yao ni ya nchi nzima hivyo wajione wao ni wakombozi wa Tanzania mwakani.

"Temeke na Ubungo mna kura ya turufu, ikiwa mtasema CCM basi ujumbe huo utafika nchi nzima na mwaka 2000 tutaiweka benchi CCM yote", alisisitiza Profesa huyo ambaye hivi sasa ni changamoto kubwa kwa vigogo wa CCM.

Wakati huo huo, CUF imeijia juu Tume ya Uchaguzi juu ya kile ilichodai kuwa ni ongezeko la shahada mpya za kupigia kura baada ya zoezi la uandikishaji kumalizika wiki hii.

Mabishano makali yameripotiwa kuibuka kati ya CUF na Tume ya Uchaguzi juu ya kujitokeza tuhuma za ongezeko na ununuzi wa shahada unaofanywa na chama fulani katika majimbo ya uchaguzi.

Chama cha CUF kimependekeza mambo kadhaa ya kuangaliwa na Tume hiyo wakati wa uchaguzi.

Mambo hayo ni pamoja na kuwepo orodha ya wapiga kura wa kila kituo nje ya kituo, mawakala wote waweke alama ya vema kwa kila jina la aliyekwisha piga kura na kuwepo kwa orodha ionyeshayo jina, umri, namba ya kuandikishwa na namba ya shahada ya mpiga kura.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook