Sehemu ya hotuba ya Sheikh Mkuu wa Bakwata Sheikh Hemed bin Jumaaa huko Ikwiriri katika Baraza la Maulid Juni 26
 

"Sinabudi nimshukuru Mheshimiwa Waziri (Frederick Sumaye). Ninakushukuru sana kukubali kujibu wito wetu. Pamoja na wingi wa Shughuli zako na kazi zako umethamini wito wetu na umekubali kuhudhuria pamoja na sisi kwa hiyo nakutakia kila la kheri na kukuambia ahsante sana.

La pili napenda nikuhakikishie na kukutuliza mawazo na moyo wako kukuambia usistushwe hata kidogo na habari unazoziona au kuzisikia ndani ya magazeti juu ya kukuarifu wewe. Kwa kweli zisikustushe, hata kidogo kwa sababu hazina msingi wowote.

Tulia moyo wako usiwe na wasiwasi wowote wala hakuna lolote. Bakwata na Uongozi wake uko pamoja na wewe, uko pamoja na serikali yake, uko pamoja na uongozi wa serikali yake bega kwa bega isikustue hata kidogo hayo.

.....Naamini umeyasikia (maneno ya magazeti) lakini hayakukushtusha kwa ajili ya ushujaa wako na ushupavu wako. Endelea kuwa na hali hiyo Insha-Allah utaallah.

Bakwata Msingi wa Katiba yake ni Qur'an na hadith za Mtume (s.a.w.). Mtume ametuambia kwamba tuwapende viongozi wetu wa Serikali. Wajibu wetu kuwatii, kuwaheshimu na kuwatuza. Mafanikio yetu ni kuihishimu serikali yetu na kuheshimu uongozi wake.

Na Mtume (s.a.w.) anatuambia yeyote anayetokana na twaa ya kiongozi wake ..... akamwepuka, akafa anakufa kifo cha kijinga.

Qur'an haikujenga chuki yoyote baina ya sisi na wasio kuwa Waislamu. Kuhudhuria kwako hapa si sawa na kuhudhuria msikitini na sisi iko ruksa mtu asiyekuwa Muislamu akiruhusiwa na Muislamu kuingia ndani ya msikiti ili aone wanafanya nini Waislamu ndani ya msikiti.

Ule Uhusiano baina yetu na wao Mwenyezi Mungu ameeleza waziwazi ndani ya Qur'ani, kwamba hakuna uadui baina yetu sisi, na wao. Mwenyezi Mungu anatuambia:

"Hakika utawakuta walio maadui zaidi kuliko watu (wengine) kwa Waislamu ni Mayahudi na wale mushirikina (wasiokuwa na kitabu), na utawaona walio karibu kwa urafiki na Waislamu ni wale wanaosema: "Sisi ni Wakristo" (hayo) ni kwa sababu wako miongoni mwao wanavyuoni na wachao Mungu, na kwa sababu wao (Wakristo) hawatakabari; (wakiijua haki huifuata)." (Qur. 5:82)

Kitareikh (historia) nyinyi nyote mwajua kwamba, maswahaba waliposilimu Makka wakaudhiwa kweli kweli na kusumbuliwa na Makuraysh. Mtume si aliwaambia wahame wakaenda Habash,

Na katika Al-Habash famaliku Najash naye ni Mkristo.

Jamani si walikaribishwa kwa uzuri kule wakapokewa mpaka baadae ndio wakarudi makwao.

Chuki hizi zajengwa kwa nini. Watu wayaingilia mambo kwa jazba bila ya msingi wowote, basi tu."
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook