Na Mwandishi Wetu
UPO wasiwasi juu ya usalama na haki za waalimu na wanafunzi waliohusika katika kutoa taarifa juu ya tukio la wanafunzi kulishwa nguruwe huko Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara.
Baadhi ya wanafunzi na wafanyakazi walioongea na gazeti hili wameeleza kuwa sura iliyokuja kujitokeza baada ya Waislamu kuja juu; kufuatilia kulishwa nguruwe; inaonnyesha hali si shwari tena kwa Waislamu walio jamii ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara.
Kwa hofu hiyo ofisi ya Bakwata Mkoa wa Mtwara imemuomba mkuu wa mkoa afanye taratibu au za kuhamishwa Mkuu wa shule hiyo. Katika barua yake no. MTR/BKT/17/162 kwa Mkuu wa Mkoa Bakwata imesema kwamba ni muhimu Mwalimu huyo ahamishwe kwani "alishindwa kuchukua hatua yoyote baada ya yeye kupata taarifa ya tukio mpaka mkoa ulipoingilia kati" na kusisitiza kuwa "Mkuu huyo wa Shule ameshindwa kumudu madaraka yake hasa katika suala nyeti kama hili."
Aidha ikasema kuwa kumhamisha Mwalimu huyo ni katika "kulinda usalama wa haki za Waalimu na wanafunzi wote waliohusika kutoa taarifa kinyume cha matarajio ya uongozi wa shule".
Siku tisa tu baada ya barua hiyo ya Bakwata kwa Mkuu wa Mkoa; Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana Mtwara, alitoa taarifa ya kusitisha shughuli za Imamu wa msikiti uliopo ndani ya shule.
Katika barua yake na. MGS/D.6/48 ya April 12, 1999 kwa Mkurugenzi wa Africa Muslim Agency, Mkuu huyo wa shule Bi T. Zenda alimtuhumu mwalimu Ali Omar Chilumba kwamba ndiye aliyetoa habari za wanafunzi Waislamu kulishwa nguruwe nje ya mipaka ya shule na hivyo kumhesabu kama mchochezi.
Aidha katika kikao cha Bodi ya shule cha April 1, Mwalimu huyo Mkuu akiwa Katibu wa Bodi alitoa shutuma nyingi dhidi ya mwalimu huyo zikiwemo kuanzisha swala tano bila ya kuzingatia ratiba ya shule; kuanzisha madrasa ndani ya msikiti na kuwaruhusu Waislamu toka nje ya shule kushiriki swala ya Ijumaa na wanafunzi.
Mwalimu Ali Omar Chilumba aliajiriwa na Africa Muslim Agency kuwa Imamu wa Msikiti uliojengwa na taasisi hiyo ndani ya shule.
Historia ya kadhia ya wanafunzi kulishwa nguruwe inaeleza kuwa mmoja wa wafanya kazi wa shule hiyo aliua nguruwe wake akachukua mafuta ya nguruwe huyo akapikia maandazi na kuwauzia wanafunzi.
Wanafunzi wakristo wenye uzoefu na mafuta hayo wakawatahadharisha wanafunzi wenzao Waislamu wakati wengine walishakula maandazi hayo.
Wanafunzi walikuja juu ya habari zikafika mjini, Maimamu nao wakalisemea katika hotuba zao za Ijumaa. Vuguvugu lilipozidi na uongozi wa shule hauonekani kuchukua hatua; Mkuu wa Mkoa ikabidi aingilie kati.
Mkuu wa Mkoa baada ya kuongea na uongozi wa shule aliagiza kuwa nguruwe wote waondolewe katika eneo la shule na kwamba taasisi zote za elimu Mkoani humo zisifuge nguruwe.
Taarifa zisizo rasmi zimeeleza kuwa baada ya mabanda hayo ya nguruwe kubomolewa, nguruwe hao walihamishiwa katika kanisa moja la katoliki mjini Mtwara.
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua kwamba bodi ya shule baada ya uchunguzi wake haikuona uthibitisho kuhusu dai la maandazi kupikiwa mafuta ya nguruwe; kwa hoja kwamba waliohojiwa hawakuweza kueleza tofauti iliyopo kati ya mafuta ya nguruwe na aina nyingine za mafuta ya kupikia.
Aidha Bodi iliona kuwa suala la Swala tano limeletwa kwa wanafunzi wakati halitekelezeki katika mazingira ya Shule Serikali.
Uchunguzi zaidi umeonyesha kuwa Bodi hiyo ilimtia hatiani Mwalimu Ali Chilumba kwa kutokuwa na ushirikiano na Uongozi wa Shule.
Kuhusu madai ya vijana Waislamu
kulishwa maandazi yaliyopikwa kwa mafuta ya nguruwe; taarifa ya Bodi hiyo
imedai kwamba waliolisimamia kwa dhati jambo hilo ni wanafunzi wakristo
na wala sio Waislamu. Na kwamba maoni ya wanafunzi, walimu na wafanyakazi
wengine Waislamu ni kuwa hakuna unyanyasaji wowote dhidi yao unaofanywa
na uongozi wa shule.
--
|
|