Na Mussa Ally, Morogoro
"MOROGORO... mjini kwetu kweli yapendeza mji ulio chini ya milima na mabonde ya mitooo, Moro yapendeza...". Hivi ndivyo msanii mashuhuri nchini marehemu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alivyokuwa akiuelezea mkoa wa Morogoro katika moja ya nyimbo zake kuusifia mandhari yake ya kuvutia.
Hamie Rajab Miiko mmoja wa wasanii wakongwe nchini aliwahi kusema katika moja ya mazugumzo yake na vyombo vya habari huko nyuma kua kama kulikuwa na pepo ya ardhini nchini Tanzania hususan katika miaka ya sitini na sabini basi ni Morogoro.
Mkoa huo uliokuwa na vivutio kadha wa kadha ambavyo ama havipo tena hivi leo, au "vimechuja" ulio mashariki ya Tanzania ukiwa ni wa tatu kwa ukubwa baada ya Arusha na Mbeya.
Una jumla ya kilomita za mraba 73,039 sawa na asilimia 8.2 ya eneo zima la Tanzania.
Morogoro imepakana na mikoa ya Arusha na Tanga kwa upande wa Kaskazini na Kaskazini Mashariki.
Magharibi mwa mkoa huo wenye mji mashuhuri "Mji kasoro bahari" upo mkoa wa Dodoma na Iringa kama jirani zake.
Kusini mashariki ya Morogoro kuna mkoa wa Lindi, wakati mkoa wa Ruvuma ukiunga udugu upande wa kusini. Na mkoa wa Pwani nao ukibembeleza ujirani mwema upande wa mashariki.
Morogoro umebeba Halmashauri moja ya Manispaa na Halmashauri nne za wilaya, ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Kilosa, Kilombero (Ifakara) na Ulanga.
Mkoa huo aidha una jumla ya tarafa 30, kata 137 na vijiji 457, ukiwa na jumla ya watu 1,287,960 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1988. Ongezeko la kila mwaka la watu kimkoa ni asilimia 3.1 katika maeneo ya vijijini na asilimia 8.5 kwenye maeneo ya mijini.
Hii inatokana na idadi kubwa ya watu hususan vijana kuhamia mijini kutafuta kazi, maisha bora na mazingira ya kuridhisha hususan huduma za jamii ambazo ni duni mno katika maeneo ya vijijini ukilinganisha na mijini ambapo 'angalau angalau' kuna uafadhali wa 'kudanganyia toto' au 'kuombea kura' ili wajanja wachache wapate 'kula'.
Mgawanyo kamili wa idadi ya watu katika kila wilaya ni kama ifuatavyo: Wilaya ya Morogoro Manispaa (Mjini) yenye jumla wa kilomita za mraba 66, tarafa moja na kata 15 hadi mwaka 1988 ilikwa na jumla ya watu 154,440.
Morogoro Vijijini ikiwa na kilimita za mraba 19,250, tarafa 10, kata 43 na vijiji 215 ina jumla ya watu 443,1000. Wakati wilaya ya Kilosa yenye ukubwa wa kilomita za mraba 14,245, tarafa tisa, kata 36 na vijiji 132 ina watu 360,940; Wilaya ya Kilombero yenye eneo la kilomita za mraba 14,918 na tarafa tano pamoja na kata 19, vijiji 49 ina jumla ya watu 180,000.
Na wilaya ya Ulanga yenye kilomita za mraba 24,560, tarafa tano, kata 24 na vijiji 61 ina jumla ya watu 149,480.
Idadi halisi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi hadi Desemba mwaka 1985 ilikuwa ni 499,535. Kati yao watu 419,609 au asilimia 84 wakiwa ni wakulima na waliobaki wakiwa ni wafanyakazi wa serikali zote.
Hata hivyo, licha ya ongezeko la watu kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi sasa, sehemu kubwa ya wafanyakazi wa mashamba ya mkonge na miwa iliyokuwa wakikadiriwa kufikia watu 31,970 wamestaafsishwa, kupunguzwa au kuacha kazi kutokana na taasisi zao kufa au kubinafishwa katika kipindi hiki cha kuimba kijamaa kucheza kibepari.
Hadithi ni hiyo hiyo kwa wafanyakazi 19,981 ambao ni watumishi serikalini na mashirika ya umma.
Kinyume chake idadi ya watumishi wa sekta binafsi ambao walikuwa zaidi ya asilimia 35 ya wana Morogoro imeongezeka maradufu baada ya kumeza wafanyakazi wa sekta nyingine waliokumbwa na upepo wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi hadi kufikia idadi inayokisiwa kuwa ni zaidi ya asilimia 50 ya wana Morogoro.
Hadi mwaka 1988 "mji kasoro bahari" (Morogoro mjini) uliorodhesha wakazi 85,968 katika kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi basi anafanya hivyo, chini ya mpango wa kile kilichoitwa na wanasiasa "nguvukazi".
Utafiti wa kina wa mwandishi wa makala hii umegundua kuwa kati yao wafanyakazi wa viwandani na maofisini walikuwa 15,337, wakulima 15,829 na wafanyabiashara 3,984.
Hata hivyo, ongezeko la wakazi wa mji limekuwa kubwa hivi leo, huku watu wenye uwezo wa kufanya kazi ni wengi na wasio na uwezo huo ni wachache.
"Idadi ya wasio na kazi nayo pia imeongezeka maradufu...", Sheikh Ayoub Salum Muwinge, Mwenyekiti wa Mkoa wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania alimweleza mwandishi wa makala hii na kuongeza; "hali hiyo imepelekea ongezeko la vitendo vya uhalifu na hata kwa kiasi fulani kuathiri mazingira, utamaduni, maadili mema katika jamii na amani katika eneo husika kuwekwa kitanzini".
Naye Bw. Juma Mohamed Sultan kiongozi mwandamizi wa Chama Cha Wananchi (CUF) wilaya ya Morogoro Mjini alisema kwamba, mbali na upepo wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi, hali hiyo pia inachangiwa ama na mipango mibovu au sera zisizotekelezeka za maendeleo ya Taifa masikini kama hili duniani.
"Tunashindwa kupanga basi moja kwa moja tumepanga kushindwa", alisema mwanasiasa huyo chipukizi na kusisitiza; "na hali hiyo itatupelekea sehemu fulani ama kutufikisha katika mwisho mbutu".
Aidha, Bw. Sultan alisema kuwa endapo tulipanga vyema, tukashindwa kutekeleza kama tulivyopanga, basi tujihesabu kwamba tunautia umma katika msiba mkubwa. Yote hayo mawili ndiyo hasa yaliyosababisha ongezeko hilo kubwa la wasio na kazi katika Morogoro na hata kitaifa.
|
|