MASHUJAA WA KIISLAMU
 
Je, unamfahamu Majza-ah-Ibn Thawr as-Sadusiy?-2
 

Mambo yakaanza kuharibika kwa upande wa Waislamu ambao walikuwa wakisuburi nje ya ngome wakijaribu kuingia ndani ya ngome ya Tustar. Wafursi walikuwa wakiwamiminia mishale na kuwauwa askari wa Kiislamu. Kila wakati askari wa Kiislamu alipojaribu kuupanda ukuta wa ngome wale maadui waliokuwa kwenye doria juu ya ukuta walishusha vyuma aina ya ndoao tena vya moto sana hivyo kumchoma au kuwachoma Waislamu waliokuwa wakijiribu kuupanda ukuta. Wengi waliunguzwa hadi wakafa. Jeshi la Waislamu likamuelekea Allah na kumuomba kwa Ikhlaas awaondoshee madhila na taabu na awape ushindi dhidi ya maadui wao na maadui wake Allah. Endelea...

SIKU moja Gavana wa Basra ambaye ndiye alikuwa Amiri Jeshi wa vita hivi, akaamua kuupanda ukuta wa ile ngome. Wakati anajiandaa mara mshale ukachoma ardhini karibu na miguu yake. Alipoutazama ule mshale akaona kijibarua kimechomekwa. Akainama na kuuhukua mshale ili apate kuona kilichomo ndani ya karatasi ile. Kijibarua kiliandikwa hivi:

"Ninaamini enyi watu wa Uislamu. Mimi ninajiombea amani, usalama, na hifadhi juu ya nafsi yangu, mali yangu na familia yangu na wale watakaonifuata mimi. Nikihakikishiwa hilo basi badala ya hifadhi hiyo (kwa kulipa ihsani hiyo) nitwaonyesha njia ya kuingia ndani ya ngome ya mji huu".

Abu Musa akajibu barua ile kwa kukubali mpango huo na akamrushia majibu hayo yule askari aliyekuwa juu ya ukuta wa ngome kwa kutumia mshale. Yule askari baada ya kusoma majibu yale kwa kutambua ukweli na uaminifu walionao Waislamu, askari yule akaamua kuwaamini Waislamu na hivyo kutekeleza yale aliyoahidi yeye.

Usiku ulipoingia akajipenyeza ili aonane na Abu Musa. Walipokutana, huyu askari akaanza kumueleza sababu zilizomfanya achukue uamuzi wa kuomba hifadhi kutoka kwa Waislamu. Alisema hivi:

"Sisi ni watu wenye heshima kutoka katika ukoo wetu. Hormuzan amemuuwa kaka yangu mkubwa na akachukua fedha zake na familia yake iliyobakia akawaweka jela, yeye ananijengea uadui mimi pamoja na familia yangu. Ninahisi maisha yangu yamo hatarini. Nitakapokuongozeni katika njia ya siri zitakazowapeleka hadi ndani ya Tustar. Kwa ajili hiyo ninahitaji mtu mmoja, hodari, jasiri na awe ni askari mahiri kuliko wote na vile vile lazima awe muogeleaji mzuri".

Abu Musa Al-Ash'aree akataka ushauri kutoka kwa Majza-ah-akimmuliza kama alimfahamu mtu ambaye atakuwa na sifa zinazohitajika na yule askari.

"Mimi ndiye huyo anayehitajika", akajibu Majzah-ah. Basi hapo Abu Musa bila kusita akampa jukumu hilo na akamtaka ahifadhi vizuri njia ya kuingilia na wakati atakapokuwa ndani apeleleze wapi alipo Hormuzan lakini asichukue hatua yoyote.

Majza-ah na yule askari wakaondoka usiku ule ule hadi kwenye pango la chini ya ardhi ambalo liliishia kwenye mto ambao unaingia katika ule mji. Njia katika pango hili lilikuwa ana sehemu fulani, hivyo kuwafanya wapite bila ya taabu. Na baadhi ya sehemu zilikuwa ni finyu na za hatari sana na hapo hapo wakihitajika kuogelea huku mto ukiwasukuma kule wasikotaka kuelekea.

Baada ya kuogelea kwa shida zote hizo na kwa kipande kirefu mara wakatokea mjini Tustar. Yule askari akamuonyesha Majza-ah mahala ambao Hormuzan alikuwa amejificha. Bila ya kufikiri mara mbili Majza-ah akaelekeza mshale upande aliko Hormuzan ili amuue. Mara akakumbuka maelekezo ya Abu Musa ya kwamba asichukue hatua yoyote ile. Akaurudisha upinde wake pole pole na akautoa mshale pangoni na akageuza pole pole akinyata kurejea kwa wenzake.

Siku ya pili Abu Musa alichagua watu mia tatu ambao walikuwa askari wenye ari na subira na ambao walikuwa waogeleaji wazuri kuliko waliobakia miongoni mwao na akamchagua Majza-ah kuwa ni kiongozi wao kisha akawaaga. Kundi hili likawaambia wenzao waliobaki kuwa wakisikia ukelele wa "Allahu Akbar" basi hapo ndio iwe kufa na kupona kwa kuanza mashambulizi.

Majza-ah akawaamuru watu wake waondoshe nguo nzito na wavae zilizo nyepesi na vile vile waache silaha zao zote isipokuwa upanga wa kila mmoja wao ambao walitakiwa kuufunga kiunoni. Njia iliyokuwa ikiwakabili ilikuwa ngumu na ya hatari, hivyo walihitajika wawe wepesi kadri iwezekanavyo ili wasizamishwe kutokana na maguo mazito pamoja na silaha zingine.

Iliwachukua masaa mawili kuogelea katika mto ule hatari wakipita kwenye mapango yenye kiza kikubwa. Waislamu hawa wakimfuata kiongozi wao Majza-ah ambaye alijitahidi sana kupambanua njia licha ya kiza kama hicho.

Hatimaye walipofika Majza-ah alisimama na kulikagua kundi lake. Hapo akagundua kuwa wanajeshi wake wamebaki themanini tu, na waliobakia wapatao mia mbili na ishirini wamekuwa wamezama!

Haraka haraka wakatoa panga zao na kwa ghafla kabisa wakawapiga panga wale walinzi wa milango na kuwaua wote. Waislamu wakaifungua ile milango ya kuingilia huku wakipiga Takbeer. Wenzao waliokuwa nje ya ngome wakaitikia Takbeer hizo. Wanajeshi wa Kiislamu wakamwagika kuingia ndani ya mji kama vile mto uliofurika unapopasua matuta ya kingo zake.

Wakiwa na hamu ya kupigana na maadui zao baada ya kuwazingira kwa muda mrefu likaanza pambano kali sana huku pande zote zikipata kipigo ambacho kiliacha wengi kuwa maiti. Vita hivi vilikuwa vya aina yake kwa ukali, ingawa ni mara chache kusikika katika historia ya Kiislamu.

Majza-ah akamtafuta Hormuzan katikati alipomuona na akafanya haraka kumfuata lakini tahamaki zogo la watu akampotea. Akatokeza tena na Majza-ah akamrukia. Wakapambana wao wawili tu kwa kutumia panga zao. Wakapigana vikali sana hadi kila mmoja akainua panga lake na kupig pigo la mauawaji. Pigo la Majza-ah likakosa wakati pigo la Hormuzan likampata Majza-ah akanguka akafa ili hali akiridhika kwa ushindi Allah aliowapa Waislamu kupitia kwake.

Vita vikaendelea kwa muda mfupi na Waislamu wakalishinda jeshi la maadui na Hormuzan akatekwa ambaye alichukuliwa huku akiwa na pingu akiwa amevaa taji lake, majoho na vishale vyake vya thamani vikiwa mabegani mwake. Walimpeleka katika hali hiyo hadi kwa Khalifa amuone. Wanajeshi wa Kiislamu wakamletea habari njema Khalifa Umar Ibn Khattab za ushindi dhidi ya jeshi la Makafiri na hapo hapo wakampa habari za kusikitisha za kifo cha askari wake shujaa Majza-ah Ibn Thawar. Sahaba ambaye Waislamu wachache wamepata kusoma historia yake.

Imeandikwa na Alia Amer kwa lugha ya Kiingereza. Imetafsiriwa na Sherally Hussein.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook