Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi katika gazeti lako la AN-NUUR ili nitoe yangu machache kuhusiana na hotuba ya Sheikh Mkuu aliyoitoa katika Baraza la Maulidi Juni 26, mwaka huu huko Rufiji mkoa wa Pwani.
Kwanza katika hotuba yake amesema kwamba BAKWATA inaongoza kwa misingi ya kufuata kitabu kitakatifu cha Qur'an na Hadithi za Mtume (s.a.w.), hilo si sawa, na kama kweli BAKWATA inafuata Qur'an mbona katika hotuba yake kuna mambo ambayo hayaendani na Qur'an (yaani Qur'an inayakataza mambo hayo).
Mfano suala la Waislamu kumkataa mtu asiyetenda haki kuwa mgeni rasmi katika hafla ya Maulidi au hafla yoyote ya kidini, kwa kweli suala hili analifumbia macho na kuwabeza Waislamu wanaopinga suala hilo.
Na baya zaidi amefikia kumtoa hofu Waziri Mkuu asiwe na wasiwasi kana kwamba Qur'an imehalalisha suala hili. Napenda kumkumbusha Sheikh Mkuu katika suratul-Muntahinah aya ya 1-2: Enyi mlioamini msiwafanye maadui zangu na maadui zenu kuwa marafiki mnaowapelekea habari zenu kwa ajili ya urafiki hali ya kuwa wameshakanusha haki iliyokujieni... (mpaka mwisho wa aya).
Sasa kwa hali hii Mufti anapinga aya hii? Au anataka kuwapendezesha viongozi wa serikali kwa maslahi yake na kupotosha maslahi ya dini? Au atubainishie maadui aliowataja Mwenyezi Mungu katika aya hii ni maadui gani.
Kuhusu suala lake la kumkaribisha mtu asiye Muislamu ndani Msikiti, na kusema kwamba inafaa Mwenyezi Mungu (s.w.) anasema katika suratul-Tawba aya 27-28: "Enyi watu ambao mlioamini, hakika watu mushrikina ni najisi, wasiukuburie Msikiti mtukufu wa Makka baada ya mwaka wao huu, kama mkiogopa umaskini kutokana na kwamba wao wanakusaidieni, atakutajirisheni Mwenyezi Mungu, hakika fadhila zake atakapotaka, katika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mno, mwingi wa hekima".
Na hii ilikuwa katika mwaka wa tisa tokea Mtume kuhama na Sayidina Ally alikuja kuwasomea watu wa Makka mwaka wa kumi. Je, hii si aya ndani ya Qur'an yenye kupinga jambo hilo? Au haoni?
Sasa nataka awaweke wazi Waislamu na kauli zake hizo alizozitoa katika baraza la Maulidi. Ukiondoa hizi aya kuna aya nyingine nyingi ambazo zimepinga kauli zake.
Mfano Suratul Baqarah aya 119-120 Mwenyezi Mungu anasema: "Hawatokuridhia wewe Muhammad Mayahudi na manaswara mpaka ufuate mila zao, sema ya Muhammad kuwaambia hakika uongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uongofu na kama ukifuata matamanio yao baada ya kukujia yale ambayo katika ilimu hutakuwa na mlinzi wala wa kukunusuru".
Sasa kipi kinachomfanya Sheikh Hemed ajipendekeze kwa watu hao. Ni kwamba hawatomridhia mpaka aingie katika unaswara akitaka. Wakati umefika kwa Sheikh Hemed bin Jumaa arejee kwa Mwenyezi Mungu na kuwacha kuwabeba kwa kuwaridhisha watu hao. Ilhali ya kuwa watu hao wanaudhalilisha Uislamu, kwani akumbuke haukuwa uhai wa dunia isipokuwa ni pambo la kupita.
Maneno M. Ally,
Dar es Salaam.
Vatican ruksa, OIC kulikoni?
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi katika gazeti letu hili ili nieleze wasiwasi wangu nilioupata kufuatana na tamko lililotolewa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwenda kwa Rais Benjamin Mkapa likihusu OIC.
Mwenyezi Mungu (s.w.) anasema: "Hawatakuwa radhi juu yako Mayahudi wala Wakristo mpaka ufuate mila yao..." (2:120). Tunaelewa wazi kwamba haiwezekani Allah (s.w.) aseme neno na lisitimie, lazima tu kweli wake utadhihirika, sasa hivi au baadaye.
Nimesoma gazeti moja la kidini litolewalo kila wiki kwa lugha ya Kiswahili (siyo ANNUUR) toleo No. 068 la Juni 20-26, mwaka huu likimtahadharisha Mhe. Rais Mkapa kwamba serikali lazima iwe makini na isitishe mipango ya kujiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu (OIC).
Kufuatana na taarifa hiyo ambayo gazeti hilo lina nakala yake inadai kama serikali ilivyokwisha ona hapo awali kuwa kujiunga na Jumuiya ya Waislamu (OIC) kunaweza kuleta mgogoro wa kikabila na kijamii, tunatoa wito kwa serikali isitishe jitihada zozote za kujiunga na jumuiya hiyo.
Katika sehemu nyingine taarifa hiyo inasema: "Kwa kuwa nchi hii ina raia wa dini kubwa mbili, Ukristo na Uislamu, haitakuwa haki kwa serikali yetu kujiunga na OIC ambayo ni taasisi ya kidini.
Sasa maswali ambayo nafikiri CCT wangeyajibu ni Je, ubalozi wa Vatican unawakilisha nchi gani? Na kama unawakilisha taasisi ya kidini upo wapi uharamu wa OIC? Tulipojiunga na Vatican kulikuwa na dini kubwa ngapi?
Katika maelezo ya taarifa ya CCT niliyonukuu hapo juu kuna hoja ambazo Waislamu wanafaa kuzichunguza. Kwanza kwa maelezo ya Serikali ilivyokwishaona hapo awali" hapa tunafaa kujiuliza ni wakati gani serikali iliona OIC haifai?
La pili, kuzua mgogoro, je kuna mgogoro gani utakaozuka kwa sababu ya OIC. Kumekuwepo kwa ubalozi wa Vatican kumezua mgogoro gani?
Ramadhani Amri L. Nkobokobo,
Magomeni,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NI masikitiko makubwa hapa wilayani na kwingineko nchini kuona tatizo hili likijitokeza pahala pengi pa kazi kana kwamba semina zinazoendeshwa na Wizara zetu mara nyingi zinatowa mafunzo ya kufuja mali ya wananchi walio wanyonge, maskini badala ya kufundishwa namna bora ya kuhifadhi mali hizo kwa njia ya kubana matumizi.
Jambo la kushangaza ni kwamba: Hivi inawezekana Madiwani wote, wasiwe na sauti ya kulinda fedha za wananchi wao waliowachagua? Au inawezekana madiwani wote kuidhinisha fedha zitakazotolewa bila ya utaalamu? Au bila kukitathmini kinachoombewa fedha na watendaji wao?
Tunauliza, je, serikali baada ya kutuma maodita kufanya mahesabu na kugundua fedha zote hizo zimeidhinishwa na waheshimiwa madiwani bila ya utaalamu, serikali imechukuwa hatua gani dhdi yao? Au madiwani hawashtakiwi?
Tunaomba wafikishwe mahakamani mar moja au wasimamishwe uongozi pamoja na DED. Vinginevyo tusikatwe makato kwa faida ya wachache.
Sharifa Manjelu,
Newala, Mtwara.
Ndugu Mhariri
NIMEKUWA nikifuatilia kwa makini msururu wa makala zenye kichwa kilichopo hapo juu ambazo zilimalizika kwenye toleo Na. 200 la gazeti lako hili tukufu. Pamoja na maelezo yaliyotolewa na mwandishi Hassan Omar, ningependa kuongeza maelezo yafuatayo:
Unapotaka kununua kompyuta kwanza la msingi kujiuliza kuwa hiyo kompyuta itakuwa ni ya kazi gani, na kama ni matumizi ya binafsi kama kutumia word processing yaani software za kuchapa barua, hadithi, maelezo ya aina yoyote na kadhalika kununua kompyuta ya kawaida ambayo haitohitaji mambo mengi.
Vitu muhimu kujua wakati wa kununua kompyuta ni:
Processing Chip. Pia uangalie aina ya chip na uwezo wa chip yaani (Mhz). Aina ya chip ziko nyingi kwa mfano zilizotengenezwa na Cyrix, Intel, ADM, n.k. Ukipata kompyuta yenye precessor ya aina ya Inter Pentium II au ya karibuni zaidi Pentium III basi ni bora zaidi kwa kuwa ndio inayoongoza na bila shaka ni ya bei ghali zaidi.
Processor ikiwa kubwa (ukubwa wa hapa sio kimacho bali uwezo wa kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja na kwa muda mfupi mfano 200, 233, 266, 300, 333, 350, 400, 450 Mhz) na ndio kompyuta itakuwa na nguvu na uwepesi wa kufanya kitu kwa haraka zaidi. Ufanyakaji kazi wa processor pia inategemea na RAM.
RAM, yaani Random Access Memory hii ni sehemu ambayo mafaili yanawekwa kwa muda kwa ajili ya kufanyiwa kazi. RAM inafupisha muda wa processor kuanza kutafuta mafaili ambayo unayahitaji katika hard drive au hard disk. Ram iko kati ya processor na hard drice, kwa hiyo RAM huwa ni ya kwanza kuzungumza na processor, na kwa hivyo, kama unatafuta faili lako basi inachukuwa muda mfupi kwa processor kulipata iwapo litakuwa kwenye RAM badala ya hard drive. Kwa hiyo RAM ikiwa ina uwezo mkubwa wa kuhifadhi na ndio uwepesi wa processor kufanya kitu.
Hard drive nayo inachangia. Ikiwa hard drive ina nafasi kubwa ya kutunza mafaili ndio vizuri kwa kompyuta kufanya kazi vizuri na kutunza mambo mengi pamoja na kuongeza software. Hard disk/drive ni sehemu ya kuhifadhia kila kitu (mafaili ya data pamoja na software ambazo zitarekodiwa kwenye kompyuta).
Angalia kompyuta sasa iwe na hard drive ya ukubwa wa 2 Gigabytes, chini ya hapo hutaweza kuitumia kuhifadhia mafaili makubwa makubwa.
Mambo mengine madogo madogo ndio kama hiyo sound card, graphics card, CD-ROM, DVD-ROM, Zip Drive, n.k.
Omar A. Baalawy,
U.S.A
Ndugu Mhariri
NIKIWA kama mtu wa Linux Community (Jumuiya ya watu wanaotumia Linux) nimefurahishwa sana na makala ya mwandishi Hassan Omar iliyotolewa kwenye gazeti lako tukufu toleo Na. 201, inayoelezea hii Operating System ambayo imetokea kuwa tishio kwa kampuni ya Micro$oft inayoonekana kuthamini pesa zaidi ya kitu chochote. Lakini katika historia ya kuanzishwa kwa hii Linux nimeona kuwa kuna kasoro kidogo.
Mwandishi ameeleza kuwa hii ilikuwa moja ya project ya shujaa Linus Torvalds alipokuwa shuleni. Nilisoma kwenye baadhi ya sites kwenye Internet na walikuwa wanaelezea kuwa mwaka 1991 shujaa Linus alinunua PC yake na ilikuwa imekuja na Operating System za Windows na MS-DOS ambazo yeye binafsi alikuwa hajazipenda na wakati ule UNIX ilikuwa aghali sana (hata hivi sasa) kwa hiyo alishindwa kumudu kununua UNX.
Kwa uchungu huu akaamua kuwa ataandika mwenye version yake ya UNIX. Akaandika sehemu ya kwanza na kuiweka kwenye Internet na kuomba msaada kutoka kwa ma-programmer wengine. Hapa chini ndiyo ulikuwa ujumbe wake wa kwanza kuwaarifu wengine kuhusu hii Operating System yake mpya ambayo sasa inatamba duniani! Ujumbe huu pia unachukuliwa kama mwanzo wa Linux:
..."Hello everbody out there using minix- I am doing a (free) operating syestem (just a hoby), won't be big and professional like gun) for 386 (486) AT clones"...
Tafsiri:
..."Nawasalimu nyote mnaotumia minix - Ninatayarisha operating system (ya bure) kwa ajili ya kompyuta za 386 (486) (kwa kujifurahisha tu, haitakuwa kubwa na yenye hadhi kama gnu)"...
Hayo maandishi ya kwenye mabano si yangu ila yake mwenyewe shujaa Linus. Pia katika kuelezea Linux Operating System mwandishi amesahau kutaja sifa moja muhimu sana ambayo operating system zingine hazinayo nayo ni kuwa Linux ni Open Source Code Operating System, yaani kiini cha code yake kiko wazi kwa watu wote na mtumiaji anaweza kuibadilisha na kuifanya ifanye kazi kwa mujibu wa mahitaji yake, tofauti na Operating System zingine kama za hao Microsoft.
Ni hayo tu nilikuwa nataka kueleza.
Akhsanteni,
Wako katika Linux Community,
Salim Khatri, Oklahoma,
U.S.A.
|
|