KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI
 
Sapi achaguliwa tena Spika wa Bunge

Mzalendo Jumapili, Novemba 3, 1985
 

CHIFU Adam Sapi Mkwawa alichaguliwa tena jana kwa mara ya tano kuwa Spika wa Bunge, baada ya kuchaguliwa kwa kura zote 189.

Upigaji wa kura kumchagua Spika wa Bunge ulianza saa 10 alasiri wakati Bunge lilipoketi likiwa Kamati ya Chama ambapo Chifu Sapi alikuwa ndiye mgombea pekee wa nafasi hiyo.

Uchaguzi wa Spika ulifanywa kwa kura ya siri. Katibu wa Bunge ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndugu Elias Kazimoto ndiye aliyesimamia uchaguzi huo.

Baada ya wabunge kupiga kura zao, Ndugu Kazimoto aliwateua Ndugu Amran Mayagila, Mbunge wa Iringa Mjini na Ndugu Masoud Omar Masoud (Mkuu wa mkoa, Kaskazini Pemba) kusimamia kuhesabu kura.

Baada ya kura kuhesabiwa, Ndugu Kazimoto alisema: "kwa mujibu wa sehemu ya 22 ya Kanuni za Bunge, Chifu Adam Sapi amechaguliwa kwa kauli moja kuwa Spika wa Bunge".

Huku akishangiliwa, Ndugu Kazimoto aliwaomba Ndugu Austine Shaba, Mbunge wa Mtwara Mjini na Ndugu Masoud Omar Masoud kumtafuta Spika "popote alipo" ili achukue nafasi yake.

Ndugu Sapi alipelekwa kwenye ukumbi wa Bunge akiongozwa na Wabunge hao wawili huku wakizungukwa na wapiga kura hadi kwenye nafasi yake ambapo alimpa.

Ndugu Sapi ambaye ni mzee anayeheshimiwa kwa jinsi anavyoliongoza Bunge, aliwashukuru wote kwa kumchagua na kuwapongeza kwa kuchaguliwa kwao kuwa Wabunge.

"Mimi nikiwa raia wa Tanzania naona fahari sana kuchaguliwa na naahidi kwamba nitalitumikia taifa kwa uwezo wangu wote", alisema Ndugu Sapi.

Mara baada ya kuapa, Spika wa Bunge alitangaza kuwa Waziri Mkuu, Ndugu Salim Ahmed Salim, ambaye pia ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni ndiye atakayekuwa wa kwanza kuapa akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ndugu Anna Abdallah. Baadaye walifuatia wabunge wengine.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook