Na Mujahid Mwinyimvua
HIVI karibuni vyombo vya habari vimeripoti kuwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tume ya Taifa ya Kuthibiti Ubora wa Vyakula (TUKUTA) vimeazimia kuongeza nguvu zao ili kushughulikia tatizo sugu la kuingizwa vyakula vibovu (sub-standards) nchini.
Gazeti la the African linalochapishwa Jijini Dar es Salaam la Juni 25, mwaka huu limeripoti kuwa rejistra (registrar) wa TUKUTA, Fabian Magoma amesema kwamba mwaka ujao wa fedha TUKUTA itasajili si chini ya asilimia hamsini ya vyakula vyote vinavyoingizwa nchini. Sambamba na hatua hiyo, TUKUTA pia itadhibiti vituo 15 vinavyotumika kuingiza vyakula kutoka nje ya nchi.
Pamoja na hayo, TUKUTA imekiri kuwa uingizaji wa bidhaa za Coca Cola na vyakula vingine kutoka Ubelgiji umepigwa marufuku na serikali kwa sababu bidhaa hizo hazifai kwa matumizi ya binadamu. Bidhaa zilizoko madukani zimeingizwa kwa siri na waingizaji watakaokamatwa watafikishwa mahakamani.
TUKUTA kama walivyoripotiwa na gazeti nililolinukuu awali pia wanasema kuwa, hawamjui anayeingiza Coca Cola na makopo licha ya ukweli kuwa bidhaa hiyo iko madukani. Na juhudi zao za kuwatafuta waingizaji wa Coca Cola zimeshindwa. Kwa hiyo, wanawashauri wananchi kuwa wasinunue bidhaa za vyakula na vinywaji hasa vile vinavyotoka Ulbegiji.
TBS nao kwa upande wake kama ilivyoripotiwa na gazeti la the African (Tanzania) la Juni 29, mwaka huu, inasema kuwa haijachunguza (not tested) bidhaa za Coca Cola na zile za vyakula vingine kutoka Ulaya, lakini kazi hiyo itaanza leo (Juni 29). Pia TBS inajua kuwa bidhaa hizo (za Ulaya) ziko madukani. Kwa hiyo itachukua hatua zinazostahili.
Zaidi ya hayo, TBS imeahidi kuwa kuanzia Juni 29 hakuna chakula wala kinywaji kitakachoingizwa kwenye soko kutoka nje kabla ya kuidhinishwa.
Baada ya rejea ya hapo juu ni vyema sasa tukaingia katika kiini cha makala yetu.
Napenda kuwakumbusha TBS na TUKUTA ambavyo ni vyombo vya umma, kuwa uhai wa wananchi wa Tanzania uko chini ya dhamana yao. Kwa maneno mengine, vyakula na vinywaji ni vyanzo vikubwa vya kuharibika kwa afya ya binadamu na mara nyingine huwa ni vyanzo vya vifo vingi duniani.
Ulaya pamoja na kuendelea katika sayansi na teknolojia lakini hivi karibuni ilitingishwa na kemikali ya sumu inayoitwa 'Dioxin' inayohofiwa kuingia katika kinywaji cha Coca Cola.
Vile vile bidhaa zinazotokana na wanyama (nyama, mayai, maziwa, samaki, kuku n.k.) zinazozalishwa Ulaya hasa Ubelgiji zinahofiwa kuwa na 'Dioxin'. Pamoja na madhara mengine, 'Dioxin' inasababisha saratani (kansa) na kuathiri nguvu za kuzaa.
Tukizingatia maelezo mafupi ya hapo juu, haingii akilini unapowasikia watu (TUKUTA) waliopewa dhamana na serikali ya kulinda uhai wa wananchi kwa kudhibiti ubora wa vyakula na vinywaji, wakisema kuwa kuna vyakula ambavyo mkemia mkuu amethibitisha kuwa havifai kwa matumizi ya binadamu, lakini vipo madukani.
Si hivyo tu bali waliopewa dhamana hiyo pia wanadai kuwa wameshindwa kuwakamata waingizaji wa bidhaa hizo. Maneno haya maana yake ni nini kama siyo kuwaambia wananchi wadhurike na vyakula vibovu.
Kuwaambia wananchi wasinunue vyakula fulani na huku wauzaji wa vyakula hivyo (madukani) huwakamati ni kujidanganya. Hasa unapozingatia kiwango cha elimu ya Watanzania. Kwa mfano ni Watanzania wangapi walisikia wito wa TUKUTA uliowataka kuacha kununua bidhaa za vyakula na vinywaji ambavyo havijathibitishwa (have not been certified).
TUKUTA inajua kuwa bidhaa ambayo haijathibitishwa ubora wake au iliyopigwa marufuku kuingizwa nchini dawa yake (inavyosema sheria) ni kuharibiwa. Kwa nini TUKUTA wanasita kutekeleza sheria hiyo na badala yake wanawaambia wananchi ati waingizaji (Impoters) hawajawakamata? Kwanini isiwakamate wenye maduka?
Kumbukeni uhai wa Watanzania na wageni wetu uko mikononi mwenu. Pia namalizia makala hii pia kwa kuikumbusha TBS: Mmesema kwamba, haitaingia bidhaa sokoni inayotoka nje kabla ya kuithibitisha. Nia hiyo mpya wa TBS na ile ya TUKUTA inapaswa kupokewa na kusubiri utekelezaji wake, na kila mwananchi aliyemakini na maswala ya afya yake na ya jamii kwa ujumla.
Hii ni kwa sababu nchi yetu
katika miaka ya hivi karibuni imekuwa kama dampo la kutupiwa vyakula vibovu
kutoka nje ya nchi.
--
|
|