Wanafalsafa wa kisekula wametofautiana katika kulijibu swali hili. Wako wanaosema kuwa kwa umbile lake mwenendo wa tabia hujisimamia wenyewe. Yaani kama lengo kuu ni furaha basi ni kule kupatikana kwa furaha ndiko kutakakosimamia mwenendo wa tabia ya mtu. Wengine wanasema msimamizi ni kitu wanachokiita "law of practical reason" yaani kanuni zinazooana na hoja za akili. Rai hii inafanana na ile ya kwanza. Wengine wanasema msimamizi ni serikali kwa kutumia askari polisi, mahakama na magereza. Na wengine wanasema msimamizi ni maoni ya watu katika jamii hiyo hiyo (social pressure).
Msukumo wa mwenendo wa tabia
Ama kuhusu swali lihusulo ni kitu gani kinachowasukuma watu kufuata mwenendo fulani wa tabia, wengine wanasema ni katika maumbile ya binadamu kutii na kuheshimu sheria kwamba mwanaadamu ameumbwa kuwa mtiifu(submissive). Hata hivyo tunaona siku hizi watu wanavyoshindana kuvunja sheria. Wengine wanasema kinachomsukuma mtu ni ile hamu yake ya kutaka utimilifu. Na wengine wanasema kinachomsukuma mtu ni kutaka hidaya na kuchukia adhabu (Reward and Punishment). Ni nani anayetoa adhabu hiyo? Wengine wanasema ni dola au serikali na wengine wanasema ni jamii anamoishi mtu.
Itadhihirika wazi kuwa yanayotolewa na wanafaslafa wanaojaribu kusimamisha uadilifu katika misingi ya kikafiri yanapwaya na kutatanisha sana. Hata hivyo haina maana kuwa yote yaliyosemwa na wanafalsafa hawa ni upuuzi usiokuwa na ukweli wowote. Zipo chembe chembe za kweli hapa na pale lakini bila kudhibitiwa na mfumo sahihi hoja zao zinaelea tu angani. Dosari kubwa kupita zote ni zile jitihada zao za kujaribu kulitazama suala la tabia ya binadamu bila kwanza kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.
Mtazamo wa Kiislamu juu ya uadilifu
Ni Uislamu peke yake ndio unaotoa msingi sahihi wa uadilifu. Uislamu unayajibu kwa ufasaha maswali makuu tuliyoyaona. Dosari kubwa iliyomo katika mitazamo ya kisekula (Kikafiri) ni kule kushindwa kuoanisha kwa wakati mmoja msingi madhubuti wa uadilifu wa mtu binafsi na jamii. Kinyume chake katika Uislamu kuna maongozi mapana yanayowezo kutufikisha katika kilele cha ustawi katika kila kipengele cha maisha yetu.
Maswali makuu ya kujiuliza kwanza
Kosa kubwa sana walilolifanya wanafalsafa wa kikafiri kuhusiana na mwenendo wa tabia ya binadamu na uadilifu ni kule kuanza utafiti wao katikati badala ya kuuanzia mwanzo na matokeo yake wamejikuta wamezama katika matope ya utatanishi mkubwa wa hoja. Swali kuu ambalo wao wamelifanya ni la kwanza yaani: Ni kitu gani ambacho dio lengo letu kuu hapa duniani? Hili ni swali ambalo ilibidi lije baadaye kabisa. Swali la kwanza ambalo lazima lijibiwe kkwanza ni: Ni ipi hadhi na nafasi ya binadamu katika ulimwengu huu? Ni upuuzi kabisa kujaribu kujenga mfumo wa mwenendo wa tabia ya binadamu bila kwanza kuamua ni ipi nafasi halisi ya binadamu katika ulimwengu huu. Kwa mfano tuseme ipo nyumba ya vyumba sita Kariakoo, na wewe unataka kuamua juu ya la kufanya kuhusiana na nyumba hiyo. Swali la kwanza halitakuwa niuze au nipangishe? Bali swali la kwanza ni: Nani mwenye nyumba hiyo? Ni ya Shirika la Umma, au ya shangazi au yako binafsi? Ni dhahiri kuwa mpangaji hana uwezo wa kuamua kama nyumba anayopanga auze au aibomowe ila kwa idhini ya mwenye nyumba. Uislamu unaanza swali hili na mafundisho ya Qur-an yameweka wazi kabisa kuwa binadamu ni mja na mtumishi wa Mwenyezi Mungu (abd) na pia ni khalifa wa Mwenyezi Mungu. Vitu vyote anavyoviona na asivyoviona katika ulimwengu huu ni vya Mwenyezi Mungu, pamoja na mwili wake na vipawa vyake vyote ni vya Mwenyezi Mungu, kwamba binadamu anavimiliki kwa dhamana tu.
Mwenyezi Mungu pia amemteua binadamu kuwa khalifa wake na hivyo amempa uwezo na vipawa vya kutumia vyote vilivyomo ulimwenguni kwa manufaa yake. Na katika hili umo mtihani na jaribio kwake. Matokeo ya mtihani huo hayatatangazwa katika maisha yetu ya hapa duniani bali yatatolewa baada ya watu wote kumaliza makazi yao hapa duniani na baada ya mema na maovu yao kujidhihirisha kikamilifu. Ni wakati huo ndipo Mwenyezi Mungu atakapomhisabu kila mtu na kuamua yupi alitimiza wajibu wake na yupi hakutimiza. Na hisabu hiyo haitahusu jambo moja maalum au kipengele fulani tu bali itahusu maisha yake yote ya kibinafsi na kijamii. Itahusu pia vipawa vyake vyote vya mwili na akili na amana au dhamana yoyote aliyopewa juu ya watu au vitu.
Ikiwa hii ndio hadhi na nafasi ya binadamu katika ulimwengu huu ni dhahiri kuwa yeye si bwana bali mtumishi ambaye uwezo na mamlaka yake yana mipaka. Ufalme ni wa Mwenyezi Mungu peke yake, binadamu ni khalifa wake, hivyo njia pekee ya uadilifu inayompasa binadamu ni kutekeleza wajibu aliopewa na Mwenyezi Mungu. Hana uhuru wa kuamua apendavyo upi uwe mwenendo wake wa tabia, bali kipimo cha lipi jema na lipi ovu lazima kichukuliwe kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wajibu wa binadamu ni kutekeleza kwa ukamilifu na uaminifu wajibu na ujumbe aliokabidhiwa. Mwenendo wa tabia za watu hautabuniwa na binadamu bali utachukuliwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumba na Mpangaji wa Sheria. Binadamu hana budi kuishi na kutenda kulingana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Pindi msimamo huu ukikubalika na uhusiano uliopo kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu kueleweka, yale maswali yote makuu manne kuhusiana na mwenendo wa tabia ya binadamu, maswali ambayo yamewatanza na kuwakaganya wanafalsafa wa zama na zama. Yanapata majibu yaliyo wazi na yanayotua akilini.
Majibu yanayotolewa na Uislamu
Pindi mtu akiikubali nafasi aliyopewa binadamu katika Uislamu majibu ya yale maswali makuu manne tuliyoyajadili katika kurasa za nyuma yatakuwa kama ifuatavyo:
(a) Kufuzu mtihani wa Mwenyezi Mungu na kupata radhi Zake ndio lengo kuu la maisha yetu hapa duniani.
(b) Kipimo cha lipi jema au lipi baya katika mwenendo wa tabia ya mtu kinategemea ni kwa kiasi gani jambo hilo linamsaidia au kumzuia kufikia lengo kuu la maisha yake.
(c) Chem chem za kweli anazoweza kuzitegemea binaadamu katika ujuzi wa mema na maovu zinapatikana katika mwongozo alioutoa Mwenyezi Mungu kupitia kwa mitume wake - chem chem nyingine za ujuzi wa mema na maovu zinaweza kutumika tu kama nyongeza na visaidizi lakini siyo badala ya mwongozo wa Mwenyezi Mungu.
(d) Kule kumpenda kwetu na kumcha kwetu Mwenyezi Mungu ndiko kunakokuwa msimamizi wa mwenendo wetu wa tabia.
(e) Na kinachotusukuma kutekeleza maamrisho ya uadilifu na kuyawacha makatazo yake ni mapenzi yetu kwa Mwenyezi Mungu, shauku yetu ya kutaraji kupata radhi Zake, hofu ya machukivu yake na matokeo mema au mabaya yatakayofuata huko Akhera.
Majibu haya yametanzua utatanishi wote uliokuwepo katika majibu yaliyotolewa na wanafalsafa wa kisekula. Si hivyo tu bali pia majibu haaya yamejumuisha vipengele vyote muhimu vilivyokuwemo katika falsafa hizo. Dosari kubwa katika majibu ya wanafalsafa hao siyo kwamba ni ya uwongo mtupu usiokuwa na chembe yoyote ya kweli, la. Dosari kubwa ni kule kuchukua chembe moja ya kweli kuwa ndio ukweli wote. Uislamu ndio unaotoa picha yote kamilifu na ukweli wote na hivyo zile chembe chembe za kweli za wale wanafalsafa zimo ndani pia.
Katika biashara pasiwe na viapo kwani hii ni miongoni mwa kuuza kwa ujanja-ujanja. Bidhaa iliyoapiwa sana na mwenye kuuza, inaweza imhadae mnunuzi aidhanie kuwa ni nzuri zaidi kuliko hali halisi. Mnunuzi atakapogundua baadaye ataona kuwa amedanganywa kwa viapo. Hivyo viapo vingi kwenye biashara,kwa muuzaji au mnunuzi vimekatazwa kwa sababu vina hila ndani yake. Mtume (s.a.w.) ameonya katika Hadith ifuatayo:
Abu Qatada ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Kuwa muangalifu na viapo vingi katika uuzaji, kw asababu japo kuna rahisisha uuzaji, kuna punguza baraka. (Muslim)
Kuapa sana katika biashara kuna hadaa, kwa hiyo wanunuzi wanapogundua kuwa wamedanganywa kwa viapo, na kumbe bidhaa hiyo haikuwa nzuri kiasi walichotarajia, hawatapendelea tena kununua kwa mfanya biashara huyo.
Tatu, katika biashara pawe na uhuru kamili kwa mnunuzi wa kuikataa au kuikubali bidhaa baada ya kuiangalia. Uhuru wa kuikataa bidhaa unaendelea kwa mnunuzi hata baada ya kununua, iwapo atagundua dosari yoyote katika bidhaa hiyo kabla ya kuanza kuitumia bidhaa hiyo. Vile vile muuzaji anayohaki ya kukataaa au kukubali kuuza bidhaa yake kwa bei anayoridhika nayo kabla ya mkataba wa kununua hauja kamilika. Muuzaji hana uhuru wa kuitaka bidhaa irudishwe baada ya mkataba wa kuuza na kununua kukamilika labda kwa mapatano yaliyofanywa katika mkataba wa kuuziana. Kuhusu jambo hili la uhuru wa uamuzi wa muuzaji na mununzi katika kuuza na kununua bidhaa, tunafahamishwa katika hadith ifuatayo kuwa:
Ibn Umar ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema:Mnunuzi na muuzaji kila mmoja katika wao ana uhuru wa mapatano na mwenzake ili mradi tu hawajaachana ila kwa uhuru wa uamuzi wa ununuzi (anaweza akakataa bidhaa hata baada ya kuelewana) (Bukhari na Muslim)
Katika maelezo ya Muslim - wakati mnunuzi na muuzaji wanauziana, kila mmoja katika wao ana uhuru wa uamuzi kutokana na mauzo au manunuzi yake, ili mradi tu wawe hawajaachana au wameuziana kwa mapatano. Kama kuuziana kwao ni kwa mapatano basi kila mmoja atafungika (kulingana na mapatano hayo).
Biashara yoyote itakayoendeshwa kwa kumnyima uhuru muuzaji au mnunuzi, ni biashara haramu ambayo haimnufaishi mnunuzi wala muuzaji. Kutokana na uzoefu wetu tunayaona haya katika mazingira yetu. Ni mara ngapi tumeona watu wakilazimishwa kununua bidhaa wasizozipenda wala kuzihitaji? Kwa mfano utaona mtu akilazimishwa kununua kilo ya unga wa muhogo usiofaa kula kabisa, ili apatiwe kilo ya sukari ambayo ndiyo aliyo na shida nayo. Huu ni uuzaji wa hila na ni uuzaji wa haramu. Kuna mifano mingi kama hii. Uislamu umetoa uhuru kwa muuzaji na mnunuzi.
Kwa ujumla utaona biashara itakayoendeshwa kwa misingi hii ya Kiislamu iliyoelezwa hapa kwa ufupi; ndio pekee biashara halali na ndio pekee yenye kutumainiwa kuleta ushirikiano, umoja, ustawi na amani ya kweli ulimwenguni. Kisiasa na kiuchumi inafahamika wazi kuwa matatizo mengi yanayoukabili ulimwengu katika nyakati zote za historia yanasababishwa na kukiuka misingi ya haki ya biashara na ya uchumi kwa ujumla aliyoiweka Allah (s.w.). Kwa hiyo Waislamu hatuna budi kujua kuwa utatuzi wa matatizo yanayo ukabili ulimwengu ni kusimamisha misingi ya Uislamu katika nyanja zote za maisha, hasa katika nyanja za uongozi na uchumi ambazo ndizo roho ya jamii.
Biashara haramu
Biashara inaweza kuwa haramu kwa namna mbili: Kwanza kwa kutofuata misingi ya halali iliyowekwa na Allah (s.w.). Pili, kuna biashara ambayo moja kwa moja imeharamishwa hata kama misingi ya halali itafuatwa. Kwa maana nyingine kuna biashara ambazo zimeharamishwa katika nafsi yake yenyewe. Katika kipengele hiki tutaorodhesha biashara ambazo zimeharamishwa moja kwa moja katika nafsi yake na hadithi mbali mbali za Mtume (s.a.w.).
(i) Muzabanah
Ni kunufaika kibiashara kutokana na matatizo ya watu wengine. Ni haramu kufaidi shida ya mwingine katika biashara. Uislamu unataka mwenye shida asaidiwe na wala asikandamizwe kutokana na shida yake. Bishara ya Muzabanah imeharamishwa kwa muuzaji na mnunuzi. Uislamu unasisitiza kuwa kinachouzwa na kinachobadilishwa nacho ni lazima kifahamike kwa mnunuzi na muuzaji.
(ii) Mu'awamah
Huu ni uuzaji wa matunda, nafaka, na mazao mengine ya shambani kabla ya kukomaa kiasi cha kufaa kuliwa; na ni haramu kama inavyosisitizwa katika hadithi zifuatazo:
Abdullah bin Umar ameeleza kuwa Mtume (s.a.w.) ameharamisha kuuza matunda shambani mpaka yaive. Ameharamisha kwa muuzaji na mnunuzi (wamekubaliana Bukhari na Muslim). Na katika maelezo ya Muslim: (Mtume) aliharamisha kuuza tende mpaka ziive na nafaka mpaka ziwe nyeupe na zisiwe zenye kudhuriwa tena na madhara mbalimbali:
Jabir ameeleza kuwa Mtume wa Allah ameharamisha kuuza (kwa matunda yangali mtini) kwa kipindi cha miaka, na ameamrisha kungojea kwanza yawe tayari (kiasi cha kutoweza kudhuriwa na chochote) (Muslim).
(iii) Hablul-Habalah
Kuuza kilicho tumboni kabla hakijazaliwa. Kwa mfano kuuza mimba ya ng'ombe, mbuzi, kondoo, ngamia, n.k. ni haramu. Tunafahamishwa katika hadithi ifuatayo:
Ibn Umar ameeleza kuwa Mtume Mtukufu ameharamisha mauzo ya Habalul-Habalah; na ni uuzaji waliokuwa wakiufanya watu majahili. Mtu alikuwa akinunua ngamia mpaka ngamia jike ashike mimba na mpaka hicho nacho katika tumbo la uzazi kiwe na mimba (Bukhari na Muslim).
Jambo linalosisitizwa katika hadithi hii ni kwamba imeharamishwa kuuza mimba kwani ni jambo ambalo halina uhakika kabisa. Ajuaye na mwenye uhakika wa kuzaliwa au kutozaliwa kilichomo tumboni ni Allah (s.w.) peke; yake. Kwa hiyo uuzaji wa mimba ni uuzaji wa pata-potea.
(iv) Uuzaji wa bidhaa kabla hazijamfikia mnunuzi ni haramu. Ununuzi au uuzaji hauhusiki mpaka mnunuzi ashuhudie bidhaa anazouziwa. Hivyo ndivyo tunavyofahamishwa katika hadithi ifuatayo:
Ibn Abbas ameeleza: Katika mauzo aliyoyaharamisha Mtume (s.a.w.) ni mauzo ya chakula mpaka yawe mikononi mwa mnunuzi... (Bukhari na Muslim).
Msisitizo wa hadithi hii ni kwamba mtu asiuze kitu ambacho hajakishuhudia machoni mwake au machoni mwa mwakilishi wake.
(v) Uuzaji wa bidhaa njiani kabla ya wauzaji kufikisha bidhaa sokoni. Wakati mwingine wafanya biashara hufanya ujanja kwa kuteka nyara bidhaa njiani kabla hazijaingia sokoni ili kuwaghilibu na kuwapumbaza wauzaji ambao hawajajua bei halisi ya bidhaa ile sokoni.
Ununuzi wa namna hii ni ulanguzi na umeharamishwa katika Uislamu kama inavyosisitizwa katika khadithi zifuatazo:
Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Usimfuate mfanya biashara wa nafaka mkakutana naye njiani kabla (ya kuingia sokoni). Na akanunua kutoka kwake-atakapoingia sokoni na kujua hali halisi ya soko ana haki ya kukataa mauziano ya awali. (Muslim). (Bukhari).
Ibn Umar ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Usikutane (usiteke nyara) bidhaa njiani mpaka zitakapofikishwa sokoni. (Bukhari na Muslim).
Kununua bidhaa iliyonunuliwa na mwingine kwa kulipa bei kubwa zaidi au kwa sababu nyinginezo ni haramu kama inavyobainishwa katika hadithi zifuatazo:
Ibn Umar ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Hapana mapatano ya atakayenunua kitu yatayofanyika baada ya mwenzake kununua na hapana atakayemchumbia ambaye ameshachumbiwa na mwenzake (ndugu yake) mpaka apate ruhusa kutoka kwake (huyo aliyeanza kupatana bei au aliyeanza kuchumbia).(Muslim).
Kinachosisitizwa katika hadithi hii ni kwamba, Muislamu haruhusiwi kununua bidhaa iliyonunuliwa na mwingine. Mara nyingine kwa sababu ya husuda au uroho, matajiri huweza kuwashawishi watu wenye uroho kama wao wakaamua kuvunja mkataba wa mauzo uliofanyika hapo awali ili apate bei kubwa kwa huyu mteja aliyejitokeza baada ya mauzo kwa yule mteja wa kwanza.
(vi) Kuuza maji au majani ambayo mtu hakuyagharamikia chochote imekatazwa katika hadithi zifuatazo:
Jabir amesimulia kuwa Mtume
wa Allah amekataza (ameharamisha) kuuza maji ya asili (Muslim).
--
|
|