Na Dkt. Abdallah J. Saffari
MOJA ya kanuni adhimu ya utoaji haki ni kwamba mtu yeyote yule asiadhibiwe bila kupewa fursa ya kujitetea. Jambo hili limesisitizwa na kufuatwa katika mifumo mingi ya utoaji haki pamoja na mahakama ya jadi ya nchi kadhaa za Kiafrika. Mathalan Waganda wanao msemo kwamba usiridhike na maelezo ya msichana bila ya kusikiliza yale ya Mvulana (Kilala v Mwanza District Council 1973 L.R.T. n.19). Hekima ya jambo hili ni dhahiri.
Tuchukue mfano mdogo tu ambapo mtoto ametumwa dukani na kukawia mno. Anaporejea, mzazi anamrukia kwa adhabu ya makofi pamoja na maneno makali bila ya kumwuliza mtoto yule kwa nini amechelewa kiasi kile. Baadaye mtoto anasema ilibidi atembee mwendo mrefu kutafuta kitu alichotumwa kwa vile maduka yote ya jirani yalikuwa yahana kitu hicho, ama yamefungwa. Pengine pia sio vizuri kumlaumu mtu aliyevunja ahadi bila ya kumtaka aeleze sababu za kushindwa kufanya hivyo; huenda alishikwa na ugonjwa wa dharura; au katika dunia hii ya harakati, alitiwa mbaroni kwa sababu nyingi tu za kuaminika.
Unaweza ukafikiria na kupata mifano mingine mingi tu ambapo adhabu na lawama zimetolewa bila ya haki kwa vile wahusika hawakupewa fursa ya kusikilizwa, yaani kujitetea.
Kujitetea kwa kweli ni kutoa maelezo kwamba mtu hastahili lawama au adhabu kutokana na shutuma au mashitaka dhidi yake. Maelezo hayo ya utetezi sio lazima yawe kweli ilimradi tu yawe yanaweza kuwa kweli ya kuaminika kuweza kutia shaka ya maana dhidi ya mashitaka yaliyopo. Katika kukamilisha lengo hili mtu anaweza kutoa maelezo ya ushahidi binafsi, kuita mashahidi wake, au anaweza kuwakilishwa na mtu mwingine kumtetea.
Umuhimu wa kuwakilishwa na mtu mwingine unaweza kutokana na sababu nyingi. Mtu anaweza kuwakilishwa na rafiki yake kwa sababu tu ana uwezo wa kuzungumza vizuri mbele ya watu, kipaji cha kuhoji na kuupembua ushahidi, au kutokuwa na woga, yaani imara na thabiti. Lakini njia inayofahamika zaidi ni ile ya kuwakilishwa na wataalam wa sheria, yaani mawakili.
Mawakili
Haja ya kutetewa na mawakili imeelezwa na sheria, mahakama na kamati mbalimbali za sheria hapa nchini na nje ya mipaka yake. Jaji mmoja Mwingereza, mstahiki sana, Mwinyi Denning, alipata kusema kuwa: "Sio kila mtu ana uwezo wa kujitetea mwenyewe. Hawezi kuonyesha udhaifu wa mashitaka wala kuonyesha ubora wa hoja zake. Inaweza kuwa sio bingwa wa kuzungumza, au ana wasiwasi au pengine hana wepesi wa maarifa. Anaweza akashindwa kuwahoji mashahidi wake au hata wale wa upinzani. Haya yanatendeka na kuonekana kila siku (Pett v Greyhound Racing Association Ltd. 1969 1 Q.B. 125 uk. 132).
Mwinyi huyo aliendelea kusema: "Hakimu humwambia mhusika: 'Unaweza kuuliza swali lolote lile'. Badala ya kufanya hivyo mhusika hutoa hotuba. Ili haki itendeke anastahili kuwa na mtu wa kumsaidia kuzungumza. Na nani awezaye kutekeleza wajibu huo vyema kuliko wakili aliyeelimishwa katika taaluma hiyo? Hivyo naona kwamba pale ambapo hadhi ya mtu au uhai wake umo mashakani sio tu ana haki ya kujitetea kwa mdomo wake. Pia anayo haki ya kutetewa na wakili au rafiki yake (K.h.j.).
Hapa Tanzania kifungu cha 310 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai kinaeleza kuwa kila mtu anayekabiliwa na mashitaka ya jinai katika mahakama yoyote yale, isipokuwa mahakama ya Mwanzo, ana haki ya kutetewa na wakili. Na majaji wengi wamelipa jambo hilo uzito unaostahili kama inavyoonekana katika mashauri ya Almasi Kalumbea v R. (Shauri la Jinai Rufani Na. 175, 1978, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mbeya) vile vile Hezekiel Martha v R (Shauri la Jinai la Rufani Na. 132, 1978, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mbeya). Katika mashauri yote hayo mawili Mheshimiwa Jaji Samatta alisema kuwa ni makosa makubwa mno kwa mahakama kuyapuuzia maombi ya mashitakiwa kutaka kutetewa na wakili. Kuendelea kusikiliza shauri na kutoa hukumu katika mazingira kama hayo kumesababisha mashauri kusikilizwa upya hata rufani za washitakiwa kuruhusiwa kama ilivyokuwa katika mashauri hayo mawili yaliyorejewa punde hapo juu.
Mawakili hawaruhusiwi kuendesha au kutetea mashauri katika mahakama ya Mwanzo (F.33 Sheria ya Mahakama ya Mahakimu Na. 2, 1985) kwa vile mahakimu wa mahakama hayo hufuata taratibu za uendeshaji mashitaka na ushahidi tofauti kidogo na zile za mahakama ya juu yake. Zaidi ya hayo kuna imani kuwa kutokana na elimu yao ya chini katika fani ya sheria mahakimu hao wanaweza kukanganywa zaidi kuliko kusaidiwa na mawakili katika utekelezaji sheria iwapo mawakili hao wataruhusiwa kubishana kwenye mashauri mbele yao. Hata waendesha mashitaka, ambao kwa kawaida ni askari polisi, hawaruhusiwi kuendesha mashauri mbele ya mahakama ya mwanzo (K.h.j). Hata hivyo kwa kutilia maanani sana umuhimu wa kutetewa na wakili, mahakama yataruhusu ombi la mshitakiwa la kutetewa na wakili na kuhamishia shauri linalohusika katika mahakama ya wilaya au ya Hakimu Mkazi.
Wakati mwingine kumekuwa na imani miongoni mwa baadhi ya watu kuwa mawakili ni wadanganyifu, laghai na wanatafuta fedha kwa maneno matupu. Kweli ni kwamba mawakili ni maafisa wa mahakama. Ni lazima wawe wamehitimu shahada za sheria na kufaulu mtihani wa uwakili. Kuna sheria mahsusi zinazoangalia utendaji kazi wao.
Mtu yeyote ambaye anafikiri kuwa mwenendo wa wakili fulani sio mzuri anaweza kupeleka malalamiko yake kwa Kamati ya Mawakili (F.10. Sheria ya Mawakili Sura 341, Sheria za Tanzania. (Kama lilivyobadilishw na sheria Na. 39. 1969). Wakili huyo ataitwa kujitetea mbele ya Kamati hiyo na akishindwa kufanya hivyo ataadhibiwa na hata kunyang'anywa shahada ya uwakili (F.13, Sheria ya Mawakili, i.h.j).
Miaka michache iliyopita Kamati ya Kuhakiki Mfumo wa Sheria nchini ilisisitiza kuwepo kwa huduma za mawakili katika uendeshaji wa mashauri na utekelezaji wa sheria (Taarifa ya Kamati ya Kuhakiki Mfumo wa Sheria Tanzania. Mchapaji wa Serikali, Dar es Salaam. 1980).
Hata hivyo, wakili sio shetani anayeweza kufanya mauzauza na kushinda kila shauri analolitetea. Isipokuwa wakili mzuri ni nyenzo kubwa katika kutafuta kweli na utekelezaji sahihi wa sheria katika shauri linalohusika.
Kinadharia wakili hutetea na kuendesha yale mashauri ambayo anaamini yanastahili kuendeshwa naye ili haki itekelezwe. Hivyo iwapo anaamini mteja wake hana haki katika shauri linalohusika inashauriwa aache kulishughulikia (Georgis P.T., Law and Its Administration in A One party State, Wahariri Kassam Na James, E.A.L.B. Nairobi, 1968).
Badala yake amshauri mteja huyo juu ya msimamo wa sheria katika mazingira ya shauri lake. Kama inawezekana akiri shitaka na kuomba kupunguziwa adhabu badala ya kuchukua miezi au hata miaka kuendesha shauri ambalo kiushahidi ni dhahiri mwisho mteja huyo atapatikana na hatia kama alivyoshitakiwa. Njia nyingine sahihi ni kumpa hiari mteja atafute wakili mwingine anayeweza kulisimamia shauri lake kwa moyo mmoja.
Kwa bahati mbaya hali halisi inaonyesha mawakili kadhaa wana mwenendo wa kukubali kuyasimamia mashauri ambayo wanaelewa wazi kuwa mshitakiwa anayo hatia. Kwa kufanya hivyo wanajitoa katika mkondo wa kutekeleza sheria na haki. Badala yake wanavutiwa na haja ya fedha ambazo zitapatikana kutokana na kuliendesha shauri hilo. Tabia hii yastahili kuepukwa kadiri inavyowezekana. Bora wakili asimamie yale mashauri ambayo anaamini kwa akili na moyo wake wote kuwa ni halali kufanya hivyo ili kutekeleza haki.
|
|