Na Hassan Omar
KWENYE sehemu ya kwanza ya makala hii, tumeelezea kwa urefu mambo ya msingi ya kuyajua kabla ya kuamua kununua hard disk drive (HDD) mpya na kuiweka kwenye kompyuta yako. Mambo hayo ni pamoja na uwezo halisi wa kompyuta yako wa kuhimili HDD za ukubwa mbali mbali. Pia tulielezea jinsi ya kufahamu kama ndani ya kompyuta imo nafasi ya kuongeza HDD nyingine au la.
Baada ya kuamua aina na ukubwa wa HDD unayoitaka, makala hii inakusudia kueleza hatua za kufuata za kuiweka HDD yako mpya kwenye kompyuta yako. Hatua hizo ni kama zifuatazo:
1. Fungua sanduku la kompyuta ili uweze kuona ndani yake. Kabla ya kuendelea zaidi hakikisha mikono yako haina "static" kwa kugusa sanduku la kompyuta mara kadhaa kwa viganja vyako.
2. Kama unahitaji kuwa na HDD mbili kwenye kompyuta yako, endelea kwenye hatua ya 3. Kama unakusudia kuitoa HDD kongwe na badala yake kuweka HDD mpya, kwanza uchomoe waya wa IDE (IDE cable) uliochomekwa kwenye HDD hiyo, pia uchomoe waya wa umeme (power supply cable) uliochomekwa pia kwenye HDD hiyo. Kisha fungua screws zinazoishikilia HDD kongwe mahali pake na uitoe na kuihifadhi mahali pazuri. Ni vyema zaidi kuitunza kwenye mfuko maalum wa kuhifadhia vifaa vya elektroniki, yaani "anti-static bag".
3. Amua ni sehemu gani ya kompyuta yako ungependelea kuifunga HDD yako. Mara nyingi hii huwa ni sehemu iliyo karibu na mahali zinapofungwa CD-ROM drive na floppy drive. Kabla ya kuifunga, angalia kwenye ncha moja ya HDD yako na utaona kuna soketi mbili: moja iliyo kubwa na yenye pini 40 inajuilikana kama "IDE connector" na nyingine ndogo yenye pini 4, hiyo ni soketi ya kuchomekwa plagi ya waya wa umeme wa ndani ya kompyuta, yaani "power supply cable".
Iangalie vizuri soketi ya pini 40 ili uone pini yenye nambari 1 iko upande gani wa soketi hiyo. Ukiangalia kwa uangalifu unaweza kuiona nambari 1 imeandikwa sehemu ya chini ya HDD, au kwenye baadhi yaHDD huwekwa mchoro unaoonesha ilipo pini hiyo. Kwenye baadhi ya HDD huzionesha pini nambari 2 na pini nambari 40 - upande wenye pini nambari 2 huo ndio pia wenye pini nambari 1. Ni muhimu kujua upande ulio na pini hiyo wakati wa kuchomeka plagi ya waya wa IDE kama itakavyoelezwa hapa chini.
Kabla ya kuifunga HDD mahali pake, utahitaji kuiseti "jumpers" zake kuifanya ama kuwa "master" au "slave". Kwenye baadhi ya HDD, pini za kuchomekwa jumper kuifanya kuwa master zina maandishi "MA" na za kuifanya slave zimeandikwa "SL" na huwa inatumika jumper moja tu.
Kwenye baadhi ya HDD zinatumika jumpers mbili na maelezo ya namna ya kuzichomeka jumpers hizo kuifanya HDD kuwa master au slave kikawaida yanaandikwa juu ya HDD yenyewe. Yasome vizuri maelezo hayo kwani yanaweza kuwa tafauti kwenye HDD mbali mbali hasa HDD za siku hizi.
Unaweza kukuta HDD ina maelezo ya kuchomeka jumper kwa matumizi ya aina tatu ya HDD: single, master, na slave. Utachomeka jumper kwenye sehemu ya single kama IDE cable imechomekwa kwenye HDD hiyo tu peke yake bila ya kuwepo HDD nyengine au CD-ROM drive inayotumia waya huo huo wa IDE.
Kifaa chochote cha IDE (Integrated Drive Electronics), yaani HDD au CD-ROM drive, kutambulikana kuwa "master" au "slave" kunategemea namna jumpers zake zilivyochomekwa. Tafauti na watu wengi wanavyodhani, haitegemei kabisa kifaa hicho umekichomeka kwenye plagi gani ya waya wa IDE. Unaweza kuichomeka "master" au "slave" kwenye plagi ya katikati au ya ncha ya waya huo wa IDE ambao kikawaida huwa na plagi tatu. Inapendekezwa tu kuchomeka HDD kwenye plagi ya katikati kwa sababu mbili kubwa.
Sababu ya kwanza ni kuiweka HDD karibu zaidi ya motherboard ili kupunguza matatizo ya kusafirisha data kwa kasi kubwa kwenye waya mrefu. Data zinazosafiri kwa kasi kubwa kwenye waya mrefu zinaweza kuufanya waya huo kuwa kama antenna inayoweza kuambukiza umeme kwenye vifaa mbali mbali vilivyo ndani ya kompyuta na kuvifanya visifanye kazi vinavyotakiwa. Athari hii inaitwa "electromagnetic interference", kwa kifupi "EMI".
Sababu ya pili ni kuwa, HDD hupewa majina C, D, E, n.k. kwa mpangilio unaotegemea kama HDD ni master au ni slave. Kwanza hupewa majina vifaa vilivyofanywa kuwa master na kisha slave. Kwa mfano, kama kompyuta yako ina HDD mbili, HDD iliyofanywa kuwa master itapewa jina C, na iliyo slave itapewa jina D. HDD ya kwanza kuangaliwa wakati wa kuanzishwa kompyuta ni ile iliyo na jina C.
Kwa sababu hiyo, HDD unayoikusudiwa kuanzishia kompyuta, kwa mfano HDD yenye mafaili ya Windows 95, ni lazima uifanye kuwa master, ukiifanya kuwa slave kompyuta yako haitaanzishika. CD-ROM drives kikawaida huwa za mwisho kupewa kupewa majina hata kama imefanywa kuwa master. Kwa mfano, kama kompyuta ina HDD mbili au, ina partitions mbili za HDD, basi CD-ROM drive itapewa jina E.
HDD inaweza kugawanywa na kuwa na partitions kadhaa. Windows 95, kama tutakavyoona mbeleni, inakuwezesha kutengeneza parition moja inayoitwa "primary partition", na parititon nyingine inayoitwa 'extended partition". Unaruhusiwa kuigawanya extended partition kuwa sehemu kadhaa zisizozidi 26 - sawa na idadi ya herufi za alfabeti ya Kiingereza. Sehemu hizi, kwa kweli, ni partitions halisi zinazojitegemea lakini hujuilikana kwa jina la "logical drives".
Wakati wa kupewa majina, majina hutolewa kwa mpangilio ufuatao: - kwanza hupewa jina primary partition ya HDD iliyofanywa kuwa master na kuungwa kwenye primary IDE channel (yaani primary master),
- kisha primary partition ya HDD iliyofanywa kuwa master na kuungwa kwenye secondary IDE channel (yaani secondary master), - kisha primary partition ya HDD iliyofanywa kuwa slave na kuungwa kwenye primary IDE channel (yaani primary slave),
- kisha primary partition ya HDD iliyofanywa kuwa slave na kuungwa kwenye secondary IDE channel (yaani secondary slave),
- kisha logical drives zote za primary master,
- kisha logical drives zote za secondary master,
- kisha logical drives zote za primary slave,
- kisha logical drives zote za secondary slave,
- mwisho kabisa ni CD-ROM drives.
Partition ya HDD inayokusudiwa kutumiwa kuanzishia kompyuta ambayo hupewa jina C, ni lazima iwe kwenye HDD iliyoungwa kwenye primary IDE channel, HDD hiyo iwe master, na partition hiyo ni lazima iwe primary partition. Kwa maneno mengine , parition hiyo iwe na vipaumbele vyote. Nadhani kwa maelezo hayo, utakuwa umefahamu ni nini haja ya kuifanya HDD kuwa master au slave. Hata hivyo kuwa master au slave hakumaanishi kuwa iliyo slave inaitegemea ile iliyo master - la hasha. hata hivyo, huwezi ukawa kwenye IDE channel moja una HDD mmoja tu na yenyewe ukawa umeifanya kuwa slave. Ukiwa na HDD moja utatakiwa ama kuifanya kuwa master au kwa baadhi ya HDD inakupasa kuchomeka jumper kwenye sehemu ya single.
4. Ifunge HDD kwenye mahali pake kwa kutumia screws. Ukiuangalia vizuri waya wa IDE (waya ulio bapa na wa rangi ya kijivujivu), utaona upo ufito mwekundu kwenye upande mmoja wa waya huo. Chomeka plagi iliyo kwenye waya huo wa IDE kwenye soketi ya HDD yenye pini 40 (yaani IDE connector) kiasi kwamba ufito mwekundu uwe kwenye upande wa pini nambari 1 ya soketi hiyo. Hakikisha plagi zote za waya IDE zimechomekwa vizuri kwenye motherboard, kwenye HDD, na kwenye CD-ROM drive (kama ipo).
Ikiwa unataka kompyuta yako iwe na HDD mbili pamoja na CD-ROM drive, kwanza ni lazima motherboard yako iwe na IDE channels mbili; na pili utahitaji kuwa na waya mbili za IDE - waya mmoja utaungwa kutoka kwenye primary IDE connector iliyo kwenye motherboard, plagi yake ya katikati itachomekwa kwenye HDD ya kwanza, na plagi yake ya ncha itaunganishwa na HDD ya pili; waya wa pili wa IDE utaungwa kutoka kwenye secondary IDE connector na plagi yake ya katikati itachomekwa kwenye CD-ROM drive.
Haipendelewi kabisa kuunganisha HDD na CD-ROM drive kwenye waya mmoja wa IDE, labda uwe huna namna nyingine. Hii ni kwa sababu, kasi ya CD-ROM drive ni ndogo sana ukiilinganisha na kasi ya HDD hasa za siku hizi, na zinapokuwa kwenye waya mmoja wa IDE, zote hulazimika kutumia kasi iliyo ndogo zaidi - yaani kasi ya CD-ROM drive. Matokeo yake, kompyuta yako itafanya mambo kwa kasi ndogo sana.
5. Chomeka kwenye HDD, plagi ya waya wa umeme wa ndani ya kompyuta (power supply cable). Kikawaida waya huo una nyaya nne: mbili nyeusi, moja njano na moja nyekundu, na plagi yake (ambayo ni nyeupe) ina tundu nne. Waya huo utauona ndani ya kompyuta yako ukiwa unatoka kwenye "power supply" - yaani kifaa kinachotoa umeme wa ndani wa kompyuta. Power supply ni kisanduku kidogo chenye feni nyuma yake. Mngurumo wa kompyuta ni kutokana na mzunguko wa feni hilo. Si rahisi kukosea kuichomeka plagi hii ya waya wa umeme kwenye HDD, kwani kuna namna moja tu ambayo plagi hiyo inaweza kuchomekeka kwenye soketi ya HDD inayoafikiana nayo.
6. Kabla hujalifunika sanduku la kompyuta, ingiza disketi ya kuanzishia kompyuta (startup disk) kwenye floppy drive, kisha iwashe kompyuta yako kama kawaida. Mara tu baada ya kubonyeza swichi ya kompyuta, bonyeza kifungo cha Delete au Del au chochote kile kinachokuwezesha kuingia kwenye BIOS (Basic Input/Output System) setup. Itabidi ubonyeze kifungo hicho mara kadhaa mfululizo mpaka utakapoweza kuingia kwenye BIOS setup.
Kutegemeana na aina ya BIOS uliyo nayo, angalia kama kuna sehemu inayokuruhusu kuifanya HDD yako mpya itambuliwe na BIOS. Kwa mfano, kwenye AMIBIOS, kuna sehemu ya AUTO DETECT HARD DISK, ambayo ukiichagua, BIOS itaweza kuiona na kuitambua HDD yako mpya. Hakikisha kuwa imetambuliwa kwa kuangalia kama BIOS imeweza kutoa ukubwa wa HDD yenyewe na namna ilivyofanywa - master au slave. Kama imetambuliwa, chagua WRITE TO CMOS AND EXIT ili uweze kuhifadhi kumbukumbu zote kwenye CMOS. Kama haikutambuliwa, basi ama itakuwa haikuchomekwa vizuri au BIOS yako haina uwezo wa kuhimili ukubwa wa HDD hiyo. Kama kompyuta yako ni ya zamani, inawezekana kabisa ikashindwa kuzitabua HDD kubwa za siku hizi.
7. Kama kompyuta yako imeweza kuanzishika bila matatizo kwa kutumia startup disk, ikimaliza utaona prompt ifuatayo: A> Tumia command FDISK kuweza kutengeneza paritions kwenye HDD yako mpya kama haijafanywa hivyo. Huwezi kuitumia HDD kabla ya kutengeneza paritions kwenye HDD hiyo. Command FDISK utaitumia kama ifuatavyo: A> FDISK Kama FDISK yako ni ya karibuni, kwanza utaulizwa kama ungependa kutumia 32-bit file system ambayo ni vyema kusema YES. Kisha utapata menu yenye mambo (options) yafuatayo:
1. Create DOS partition or Logical DOS Drive
2. Set active partition
3. Delete partition or Logical DOS Drive
4. Display partition information
5. Change current fixed disk drive
Chagua option 1 ili upate menu yenye options tatu kama ifuatavyo:
1. Create Primary DOS Partition
2. Create Extended DOS Partition
3. Create Logical DOS Drives in the Extended DOS Parition
Na hapa utachagua option 1 ili uitayarishe primary partition.
Unaweza kuifanya HDD kuwa na partition moja tu. Lakini hiyo haipendelewi na pengine haitawezekana kama HDD drive yako ni kubwa zaidi ya 2 GB. Ni vyema kuigawanya kuwa paritions kadhaa ambazo kila moja haizidi ukubwa wa 2 GB.
Kwa mfano, kama HDD yako ni ya ukubwa wa 6.4 GB, ni vyema kuwa na primary partition ya ukubwa wa 2 GB, na Extended partition ya ukubwa uliobaki, yaani 4.4 GB. Extended partition utaigwanya kuwa Logical drives tatu: moja ya ukubwa wa 1.5 GB, nyingine 1.5 GB, na ya mwisho 1.4 GB iliyosalia. Kuzitengeneza paritions hizo, utachagua option 1 kuitengeneza primary partition. Ukiulizwa kama unataka kuitumia HDD yote chagua NO, na uendelee kuandika ukubwa wa primary partition kuwa 1500 MB. Kisha bonyeza ESC na uchague option 2 kutengeneza extended partition yenye ukubwa uliosalia, yaani kiasi cha 4.4 GB. Ukibonyeza ESC tena utapa ujumbe:
No logical drives defined Enter logical drive size in Mbytes or percent of disk space [4400]
Hapo utaweka 1500 MB kama ukubwa wa Logical drive ya kwanza, na utaendelea hivyo hivyo mpaka logical drive ya mwisho ambayo huna haja ya kuandika ukubwa wake, badala yake ikubali tu kwa kubonyeza Enter utakapooneshwa ukubwa wa logical drive hiyo. Ikiwa nafasi yote iliyotengwa kuwa Extended partition imetumiwa kutengenezea logical drives, utapata ujumbe:
All available space in the extended DOS partition is assigned to
logical drives. Baada ya hapo bonyeza ESC mara kadhaa mpaka ufike kwenye menu ya kwanza kabisa yenye options 5 kama ilivyooneshwa hapo juu. Ukichagua option 4, yaani Display partition information, utaweza kuziona partitions na logical drives zote pamoja na majina yao. Hakikisha umeandika majina ya drives zote mpya. Ukibonyeza ESC mara kadhaa utatoka kabisa kwenye programu ya FDISK na kompyuta yako itaanzishika tena.
Ingojee mpaka upate tena prompt ifuatayo: A> ili uweze kuzi-format partitions na logical drives zote. Bila ya kuzi-format hutaweza kuzitumia partitions na logical drives hizo.Tumia amri FORMAT kuweza ku-format drives zote moja baada ya nyingine kwa kutumia mfumo huu: A> FORMAT C:
Amri hiyo itai-format drive iliyopewa jina C. TAHADHARI, usije uka-format drive ambayo ndani yake kuna data, kwani ukifanya hivyo data zote zitafutika. Ni muhimu kujua majina ya drives unazozitaka kuzi-format ili usije ukachanganya mambo. Baada ya kumaliza kuzi-format drives zote, utakuwa tayari umekamilisha hatua za kuiweka HDD yako kwenye kompyuta yako. Unaweza kuendelea kuweka programu nyingine kadhaa kadri unavyopenda. 8. Kama kompyuta yako ni ya zamani, unaweza kukwama wakati unapotumia FDISK kutengeneza partitions kwenye HDD yako. Unaweza kuona kuwa ukubwa wa HDD uliotambuliwa na FDISK ni 524 MB tu, wakati pengine HDD yako ina ukubwa wa zaidi ya hapo. Ikitokezea hivyo, ni wazi kuwa hutaweza kuitumia FDISK iliyo kwenye kompyuta hiyo kutengeneza partitions kwenye HDD drive yako. Mbinu ambayo inaweza kusaidia, ni kuiweka HDD yako kwenye kompyuta ya karibuni, na kuitumia programu ya FDISK iliyo kwenye kompyuta hiyo kutengeneza partitions na logical drives kwenye HDD hiyo, kiasi kwamba kila partition au logical drive isiwe na ukubwa wa zaidi ya 524 MB. Muhimu tu kompyuta zote mbili ziwe zinatumia operating system moja - kwa mfano zote ziwe zinatumia Windows 95. Baada ya hapo, ni kiasi tu cha kuiweka kwenye kompyuta yako na kwanza kuifanya itambuliwe na BIOS kwa kutumia hatua tulizozieleza, na hutakuwa na haja tena ya kutumia FDISK kutengenezea partitions kwani tayari zitakuwa zimekwishatengenezwa kwenye kompyuta ya pili iliyotengenezwa miaka ya karibuni zaidi.
Hayo ndio maelezo ya hatua za msingi za kuweka hard disk drive (HDD) mpya kwenye kompyuta. Natumai kuanzia sasa hutahitaji tena kuipeleka kompyuta yako kwa fundi wa kompyuta unapotaka kuongeza HDD kwenye kompyuta yako. Kazi hiyo utaweza kuifanya mwenyewe.
|
|