TAHARIRI
Wenye chuki ni hao waliochoma moto Misikiti
 

KATIKA masiku ya hivi karibuni Nigeria wamepata Rais aliyechaguliwa na wananchi baada ya miaka kadhaa ya kutawaliwa na serikali ya kijeshi. Rais huyo ni Mhe. Olesegon Obasanjo.

Mhe. Rais Benjamin William Mkapa na Mwalimu Nyerere ni miongoni mwa Marais na watu mashuhuri walioshuhudia kuapishwa kwa Rais huyo.

Toka Rais huyo aapishwe hatujasikia vurugu yoyote iliyofanywa na Waislamu walio wengi katika Nigeria kumpinga Rais huyo Mkristo. Isipokuwa tu Wabunge walichelewesha kupitisha Baraza lake la Mawaziri kwa madai kwamba hapakuwa na uwiano stahiki baina ya Waislamu na Wakristo katika Baraza lake.

Baada ya Obasanjo, Mhe. Rais Mkapa alishuhudia pia kuapishwa kwa Rais Bakili Muluzi wa Malawi.

Kufuatia kuapishwa kwa Rais huyo aliye Muislamu baada ya kushinda uchaguzi uliojumuisha vyama vingi vya siasa; Wakristo walio wengi nchini Malawi walichoma moto Misikiti ipatayo ishirini.

Hiyo ilikuwa ni kuonyesha hasira na chuki zao dhidi ya Rais Muislamu.

Habari za vyombo vya habari zilieleza kuwa mashabiki wa chama cha AFORD waliamua kumaliza hasira zao kwa kuchoma Misikiti, nyumba na maduka ya Waislamu kwa kuwa Rais Bakili Muluzi ni Muislamu.

Aidha, habari zaidi zilieleza kuwa mashabiki wa vyama hivyo vinavyoongozwa na viongozi Wakristo wamedhamiria kuwafukuza Waislamu wanaoishi sehemu za kaskazini zenye Wakristo wengi waende kusini kwenye wafuasi wengi wa Rais Muluzi (Taz. Mfanyakazi No. 12204 la Juni 23, 1999).

Pamoja na matatizo ya udini, rushwa, huduma mbovu za kijamii na kuparaganyika kwa uchumi kwa ujumla wakati wa serikali ya awamu ya kwanza, leo viongozi wa awamu hiyo utajo wao ni kama wa malaika au watakatifu wateule.

Awamu ya pili iliwakuta Watanzania wakipanga foleni kutwa kupata robo kibaba ya unga wa njano, wakivaa makata mbuga na kaniki huku daladala ya wakati huo (UDA) ikifanya kazi saa 12 hadi saa 4 asubuhi nakuanzia tena saa 8 mchana hadi saa 12 jioni. Kama ilikuwa unakaa Keko na sa 12.30 jioni ikakukuta Kawe, basi ili usilalae mbali na familia yako ilikubidi uunge mkono Azimio la Arusha (utembee kwa miguu). Jumamosi na Jumapili ndio ilikuwa haramu kabisa kuendesha gari, lengo likiwa kunusuru kichele cha mafuta kilicho kuwa kimesalia.

Haukupita muda mrefu watu wakawa wanachagua mchele madukani, unga na sukari vikapoteza sifa ya kuwa bidhaa adimu. Watu wakahama kutoka kuchomolewa nauli zao mifukoni na wezi kwa kushonana ndani ya UDA baada ya kuisubiri kwa saa nzima; wakaingia kwenye kupandia na kushuka watakako, huku wakibembelezwa "njoo ukae", baada ya kipindi cha mpito cha "chai maharage".

Hiki ndicho kipindi kilichoelezwa kuiharibu nchi mpaka ikadaiwa inanuka. "Nchi inauzwa, Loliondogate, kashfa, udini" ilikuwa ni misemo iliyotawala vyombo vya habari ikishutumiwa awamu hiyo.

Machimbo ya madini (dhahabu na almasi); viwanda vyetu, mashirika ya umma, mbuga za wanyama, mashamba makubwa na NBC ikiwa njiani; vyote hivyo leo asilimia kubwa vipo mikononi mwa "makaburu", Wazungu na Wahindi. Mhe. Rais wetu Benjamin Mkapa hajashutumiwa kuuza nchi!

Pamoja na matukio ya kuuliwa watu Mwembechai, watu kuchomewa moto nyumba zao na wengine kubomolewa kikatili, kashfa yaonekana neno zito lisilojuzu kuhusishwa na lolote kati ya matukio haya.

Wakati Wakristo huko Malawi wanawachomea Waislamu nyumba na Misikiti yao, CCM ambayo imeweka wagombea wote Wakristo katika uchaguzi mdogo wa ubunge, inawakemea wengine waliochanganya wagombea wasilete udini. Aidha inawakemea Waislamu wasitumie Misikiti kufanya kampeni huku ikiwatukana kuwa ni watu wa fujo hasa wakishahongwa vibandiko na kanzu.

Kauli za mara kwa mara za Katibu Mkuu wa CCM Bw. Philip Mangula za kuwashutumu Waislamu zinalenga kuunda makundi ya mashariki wa AFORD na Malawi Congress Party.

Waislamu wa nchi hii wanarekodi ya kujitoa muhanga kuikomboa nchi hii na Watanzania toka makucha ya wakoloni.

Kwa uzalendo wao na kujali umoja wa kitaifa japo waliuliwa pale Mwembechai kutokana na fitna ya Paroko wa Kanisa Katoliki hawakutoa hasira zao kwenye Makanisa na nyumba za Wakristo.

Tunaambiwa kilichotangulia kuchomwa Misikiti Malawi ni kuhamasishwa Wakristo wasikubali kuwa na Rais Muislamu. Leo CCM inapoweka wagombea wote Wakristo halafu ikawashutumu walioweka mgombea Muislamu kwa udini; inawaambia nini Watanzania Wakristo?

Waswahili husema mchuma janga hula na wa kwao. Tusingependa kuonja chungu ya mbegu mbaya inayopandwa na CCM.

Masheikh mnaopenda kupiga mfano wa Najash watanabahisheni mliowaahidi kuwatii na kuwatukuza, kwamba "mambo iko huko" kwao sio huku. Hatuna chuki na mtu ila tunadai kilicho haki yetu. Wenye chuki ni hao waliochoma Misikiti na nyumba za wenzao.

 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook