Na Mwandishi Wetu
JUMANNE wiki hii Waziri Mkuu Mheshimiwa Frederick Sumaye alitoa kauli maalum bungeni kuhusiana na kile alichokiita tabia iliyojitokeza hivi karibuni ya wananchi kufanya matendo yenye muelekeo wa kuhatarisha amani nchini.
Aidha, Waziri Mkuu alidai wananchi hao wamethubutu hata kupambana na vyombo vya dola ambapo mwisho wa vurugu hizo yamekuwa yakitokea mauaji nayotokana na polisi "kujitetea" dhidi ya mashambulizi yanayoelekezwa kwao.
Waziri Mkuu aliongeza kusema kuwa baadhi ya wananchi wamejitokeza hata kuwatetea wahalifu wanapoandamwa na vyombo vya dola hali iliyowafanya maaskari kutumia silaha na hata silaha za moto!
Waziri Mkuu alitetea hatua hizo za watendaji wa vyombo vya dola kwa "hoja" kwamba na ni binadamu kwa hiyo wasingekuwa tayari kuhatarisha maisha yao.
Kadhalika, Mheshimiwa Sumaye alizungumzia kampeni za uchaguzi mdogo katika majimbo ya Temeke na Ubungo kwa kusema baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa vikifanya matendo ya hatari kama vile kubeba jeneza lenye picha ya Rais, jambo ambalo yeye ameliita la kashfa na uchuro kwa kiongozi wa nchi.
Huku akishangiliwa na Wabunge wa CCM waliokuwa wakipiga miguu chini na ngumi juu ya meza, Waziri Mkuu alionya kwamba serikali isingekuwa tayari kuvumilia hali hiyo na ili kudhibiti uwezekano wa kutokea vurugu ya uchaguzi wa majmbo hayo, alisema serikali ilikuwa ikiandaa kuweka ulinzi mkali.
Hii ni mara nyingine Waziri Mkuu kusimama Bungeni kutoa matamshi ya vitisho na kuunga mkono hatua za polisi zinazoonekana kukiuka sheria na haki za binadamu.
Mara ya kwanza ni mwaka jana wakati akiakhirisha kikao cha Bunge, ilikuwa ni baada ya kutokea kadhia ya Mwembechai.
Yapo maswali kadhaa yanayoweza kuulizwa kuhusiana na matamshi haya ya Waziri Mkuu.
Lakini la msingi hapa ni ule ukweli kwamba Waziri Mkuu kazungumza yasiyokweli na hii imekuwa ni desturi kwa viongozi wetu wa juu.
Kueleza yasiyo sahihi ni kujaribu kujenga mazingira au kutoa picha isiyo yenyewe isli kuhalalisha hatua fulani inayokusudiwa kuchukuliwa au iliyokwishachukuliwa ambayo ama ni ya kinyama au haipendezi katika hali ya kawaida.
Huko ni kukiuka haki na uadilifu ambako mara zote huwa kiini cha vurugu na mifarakano katika jamii.
Serikali inapokosa uadilifu lazima itegemee fujo na ghasia kutoka kwa raia.
Alipokuwa akitoa mfano ya jinsi wananchi wasivyoheshimu vyombo vya dola, Mheshimiwa alitaja mkasa uliotokea eneo la Mtoni Jijini ambapo watu wawili waliuawa na polisi kwa kutuhumiwa kuwa ni majambazi sugu.
Waziri Mkuu alisema mauaji hayo yametokea baada ya wananchi kujaribu kuwatetea "wahalifu" hao wasidhibitiwe na vyombo vya dola. Akasema jaribio hilo ndilo lililopelekea askari kujitetea kwa kurusha risasi ovyo na kusababisha vifo vya watu hao!
Lakini wakati Waziri Mkuu akitoa maelezo hayo juu ya mkasa huo nadhani wakuu wa vyombo vya dola walikuwa wakiuma vidole kwani taarifa zao zinaonyesha kuwa watu hao waliouliwa hawakuwa majambazi na ilishatoka amri ya Kamanda wa Polisi Mkoa kwamba askari waliohusika wafikishwe mahakamani kwa kuwa wanakabiliwa na shtaka la mauaji.
Ni dhahiri kuwa hapa pana maswali kadhaa ya kujiuliza lakini la msingi ni kuwa maelezo ya Waziri Mkuu hayakuwa sahihi. Kinachosikitisha zaidi ni kule kushangilia kuliko kuwa kunafanywa na Wabunge wa CCM.
Waziri Mkuu anatoa kauli ambayo inatishia wananchi, Wabunge wanachekelea!
Ni yale yale ya Mwembechai, watu wanauawa kama paka Wabunge wanapongeza.
Kwa mwenendo huu wa kutosema
kweli na kushabikia dhulma, nchi itadumu vipi katika amani na utulivu?
--
|
|